Mungu tunamtwisha mizigo isiyomstahili

Balozi wa China hapa nchini, Dk. Lu Youqing, amesema kama kweli Watanzania wanataka kuondoka kwenye lindi la umasikini, waige kile kilichofanywa na nchi yake. Amesema China ya miaka 50 iliyopita ilifanana kwa kila hali na Tanzania ya wakati huo, ambayo imegoma (imegomeshwa) kubadilika. Imeendelea kuwa hivyo hivyo licha ya rasilimali nyingi.

Maneno ya Balozi Lu si mapya. Si mageni kuyasikia. Hivi karibuni rais wetu alizuru Japan, Malaysia na mataifa mengine ya Asia. Akaona hao waliokuwa wenzetu miaka hiyo, namna walivyotuacha mbali kimaendeleo. Bado tunakumbuka alivyoulizwa swali kwanini Tanzania ni masikini licha ya rasilimali ilizonazo. Jibu lake likawa, “Hata mimi sijui”.

 

Kwenye makala yangu ya wiki iliyopita nilisema wanaoifanya nchi hii isitawalike, si Chadema wala wapinzani wengine wa kisiasa, bali ni Serikali yenyewe ya CCM. Nilijaribu kueleza namna viongozi na watumishi wetu walivyokosa maadili. Nilizungumzia ujangili unaofanywa na askari wetu kwa kushirikiana na watu wenye mamlaka makubwa serikalini.

 

Nashukuru Mungu kuwa kabla wino haujakauka, kumekamatwa majangili ambao ni maofisa wa Jeshi la Magereza wakiwa wameua twiga, mbuni na wanyama wengine wasioruhusiwa kuuawa kwa mujibu wa sheria zetu.

 

Kitu cha maana kilichofanywa na jeshi hilo ni kuwafukuza kazi mara moja. Kwetu sisi wahifadhi, tunasema adhabu hiyo pekee haitoshi. Wanastahili adhabu kali zaidi kwa sababu wakiachwa watamaliza wanyamapori wetu.

Nikirejea kwenye hoja ya Balozi wa China, ni ajabu na kweli kwamba Tanzania tuna rasilimali nyingi, lakini tumebaki kwenye lindi la umasikini. Nami sioni kwa mwenendo huu wa kila mtu kula kwa urefu wa kamba yake, kama Tanzania inaweza kupiga hatua mbele.

 

Ukiwauliza wataalamu wetu wa uchumi na wanasiasa waeleze sababu zilizoyafanya mataifa kama China, Malaysia, Korea Kusini na mengine katika Asia yapige hatua kubwa mbele, majibu wanayotoa ni mepesi. Moja ya majibu hayo ni kwamba mataifa ya Magharibi – Ulaya na Marekani – yamewekeza sana katika mataifa hayo! Kwa hiyo wanataka na sisi Tanzania tukaribishe wawekezaji wengi ili tuweze kutoka hapa tulipo.

 

Haya ni majibu mepesi kwa sababu Tanzania ni kama pakacha lililotoboka. Usitarajie pakacha la aina hii likajaa hata kama maji yote ya ziwa yangewekwa humo. Kuna mahali tunakosea.

Kuna jambo kubwa tusilotaka kulizungumza na pengine kulitekeleza kwa dhati. Jambo hilo si jingine, bali ni la kupambana na wimbi la wezi wa mali za umma, wala rushwa na watumiaji wabaya wa ofisi za umma.

 

Rushwa katika China na hayo mataifa mengine, ni kitu kinachopigwa vita kwa nguvu zote. Juzi tu, Waziri wa zamani wa Reli, Liu Zhijun, alihukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya rushwa. Pamoja na adhabu hiyo inayoweza kubadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela, Mahakama imeamuru mali zote za Liu zitaifishwe. Hii ndiyo China isiyokuwa na mchezo na viongozi wala rushwa na watumia vibaya madaraka.

 

Tanzania ni pepo ya wala rushwa na wafujaji wa mali za umma. Tanzania ukipata kazi serikalini au katika shirika la umma, usipoiba, unaonekana mjinga! Unachekwa.

 

Watu wanaomba kazi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) si kwa sababu wana uwezo kitaaluma, bali ni kwa sababu sehemu hiyo ndiyo njia ya mkato kwa kijana aliyehitimu chuo mwaka mmoja uliopita, kuajiriwa na kutajirika ndani ya miezi sita tu!

 

Tanzania kijana haombi kujiunga Jeshi la Polisi kwa sababu kazi hiyo ipo kwenye “damu” kama walivyo ndugu zangu wa Mkoa wa Mara, bali ni kwa sababu akiwa polisi anajua atatajirika haraka kwa kubambikia kesi, kushirikiana na magenge ya majambazi au atahakikisha anasimamia usafirishaji magendo.

 

Katika Tanzania kijana anasoma awe mwanasheria, si kwa sababu ana wito wa kuwatetea wanyonge na wasiokuwa na sauti, bali aweze kuwa wakili wa majahili yanaoingia nchini kwa jina zuri la wawekezaji. Atahakikisha anasoma sheria ili siku moja awaongoze wawekezaji kwenda kutwaa ardhi ya makabwela kwa kilemba cha kuwapa huduma za jamii.

 

Fikiria, anakuja mtu anauziwa ekari 500 za miti – mali ya kijiji – kwa ahadi ya kujenga chumba cha darasa au kiofisi cha kijiji. Mikataba inasainiwa kwa baraka za hawa hawa Watanzania waliosomea sheria. Hawapo kwa ajili ya kuwasaidia masikini wanaonyanyaswa.

 

Nchi yetu ndiyo unaweza kumkuta mtu yuko radhi kuuza nyumba yake ili aweze kuukwaa udiwani. Anajua akishakuwa diwani, basi maeneo yote ya wazi, vikiwamo viwanja vya kucheza watoto, yatauzwa. Kwake huyo, udiwani ni upenyo wa kufikia kilele cha maisha bora. Hana habari wala hasumbuliwi na kero zinazowakabili wananchi katika eneo au Taifa lake.

 

Tanzania ndipo mahali ambako watendaji wa Serikali wakishasikia ujio wa wageni, wanajaa furaha, si kwa sababu ya kuwapokea na kuwakarimu vema, bali kwa sababu wanakuwa na hakika ya kuongeza nyumba au gari jingine! Tumekuwa Taifa la mission town.

 

Kwa kuheshimu uhuru wa Mahakama, sipendi kuingilia mashauri yanayoendelea huko, lakini historia inaonesha kuwa watuhumiwa wakuu wa ufujaji mali za umma na matumizi mabaya ya madaraka, wamekuwa wakipeta. Wanaliibia Taifa, wanakamatwa, wanafikishwa mahakamani, wanapewa hukumu za kawaida, baadaye wanatoka wanaendelea kula maisha kama kawaida.

 

Naomba radhi kwa hili, lakini niseme wazi kwamba kesi nyingi zinazoendelea katika Mahakama mbalimbali nchini, ni kiini macho tu. Mwisho wa siku sidhani kama kutakuwapo adhabu ya kuwafanya majizi wengine waogope. Kesi nyingi zinafutwa kwa sababu za ki-technicalities. Masikini anakoseshwa haki yake kwa technicalities.

 

Ndugu zangu, haya niliyojaribu kuyasema hata kama yapo China, Korea Kusini au Malaysia, basi ni kwa kiwango cha chini kabisa.

 

Sisi kama Taifa kamwe hatuwezi kuendelea kama nchi yetu inageuzwa kuwa pepo ya wezi na watumia madaraka vibaya. Nchi haiwezi kuendelea kwa kuwa na polisi, askari magereza na wanajeshi majangili.

 

Imepata kusemwa mara nyingi kwamba uzalendo na haki ni vitu muhimu sana katika maendeleo ya Taifa lolote. Lakini uzalendo hauwezi kujengwa na masikini pekee, wakati majizi na watumia madaraka vibaya wao wakijiweka pembeni. Uzalendo unajengwa kwa watu wote kuishi kwa haki na usawa.

 

Sasa umeibuka mtindo wa sisi wenyewe kuharibu mambo katika nchi yetu, kisha tunawahimiza viongozi wa kidini na waumini kuongeza sala ili Taifa lisiangamie. Wanasiasa wanahubiri udini, nchi inachafuka, sasa wanataka tuliombee Taifa!

 

Tunamdhihaki Mungu. Sisi wenyewe tuvunje mihimili ya amani, halafu tumwombe atuepushe na zahama ya machafuko? Hilo linawezekana kweli? Tumeamua kumtumia Mungu kama jawabu la mkato la kukwama kwetu kimaendeleo. Tuna nchi nzuri, watu wa kutosha, ardhi tele, madini ya kila aina, makaa ya mawe, gesi, mafuta, wanyamapori wasio na idadi, maziwa, bahari, mito, mabonde, milima, hali ya hewa murua. Tumeshindwa kuutumia utajiri huu, sasa tunamtaka Mungu atukomboe. Huyu Mungu atupe nini zaidi ya hivi? Yaani asafishe shamba, alime, asihe, apalilie, avune, aandae chakula, atuite mezani, bado tumwombe atuwekee chakula midomoni? Tuache dhihaka jamani.

 

Tunashangilia misaada ya wawekezaji kama vile mwenyeji mpuuzi ambaye ana kila aina ya chakula ndani ya nyumba yake, lakini anashangilia peremende anayoletewa na mgeni! Anapopewa hiyo peremende anamshukuru kweli kweli huyo mgeni kwa kumwokoa asife njaa!

 

Sisi wenyewe tumekaribisha bodaboda bila kuhakikisha kwanza vijana wanaoziendesha wanakuwa na mafunzo mazuri ya udereva. Ajali zinatumaliza. Walemavu wanaongezeka. Tunaacha kuona wapi tumekosea, badala yake tunahimizwa tuendeshe sala ili Mungu aliokoe Taifa letu. Tumeamua kujiaminisha kwamba ajali hizi ni mapenzi ya Mungu, ilhali ukweli ukiwa kuwa haya ni matokeo ya uzembe wetu wenyewe. Hatukufanya maandalizi wakati tukiruhusu vyombo hivi.

 

Tumeamua kuwasujudia wawekezaji wanaotuletea madawati na kutujengea matundu ya vyoo, huku wao wakibeba utajiri wa madini na rasilimali nyingine. Tunawasumbua watoto wengi kwa kuwaimbia wawekezaji nyimbo za shukrani kwa misaada ya vyoo! Mkuu wa Wilaya anapewa msaada wa matairi mawili ya gari, anashukuru hadi anakaukiwa mate mdomoni!

 

Haya yanafanyika katika Taifa ambalo Serikali na vyombo vyake vya dola vimejifaragua kwa kujifanya haviwajibiki kuwabana wezi wa mali za umma na wanaotumia vibaya madaraka. Bado naamini kwamba Balozi Lu ni miongoni mwa watu wachache wanaofaa kuwapa semina elekezi Watanzania. Tumwite, atoke hadharani atuambie China wakiwakamata wezi wa mali za umma wanawafanyaje?

 

Atueleze hao wasafirisha na wauza mihadarati ambao ni sumu kwa nguvu kazi ya Taifa (vijana) wakikamatwa, adhabu yao ni ipi? Atueleze kiongozi yeyote wa umma anayetumia ofisi kujinufaisha yeye mwenyewe, ndugu na rafiki zake, akibainika anapata nini? Balozi Lu atueleze kama kwao askari wa umma ndiyo wanaoongoza ujangili.

Atufumbue macho ili tujue kama kwao mtu au watu wanaweza kuibua mahekalu kama uyoga na wasiulizwe wapi walikopata fedha.

 

Tumwulize Balozi Lu atueleze kama kweli siri ya maendeleo ni kuwaruhusu watu kuvunja sheria kwa kisingizio cha demokrasia. Balozi huyu atuthibitishie kama kweli omba-omba tunayoifanya licha ya utajiri mwingi tulionao, ndiyo njia sahihi ya kufikia maendeleo kama waliyonayo wao.

 

Ndugu zangu, tuna sababu zote halali za kuhakikisha tunabadili mfumo wetu. Mabadiliko yanapaswa yaanzie kwa mtu mmoja mmoja hadi kwa Taifa zima. Tudhamirie kuondokana na mfumo huu ambao unamfanya kila mmoja kujiona ana haki ya kuiba.

 

Tunapojadili mambo haya tunapaswa kutazama haki za pande zote mbili. Kama ilivyo kwa wanaopinga adhabu ya kifo, vilevile wawepo watu wanaowatetea wale wanaoathiriwa na uamuzi au matendo ya wafujaji wa mali za umma. Haiwezekani iwe haki kwa mtumishi wa umma mwizi kuishi, lakini isiwepo haki kwa yule anayokoseshwa huduma muhimu za kumwezesha kuishi. Haki za binadamu ziwe kwa wote – watenda na watendewa.

 

Kwa mfano, wezi wa dawa za umma katika hospitali na maghala ya umma wanapotiwa hatiani, adhabu zao zilingane na madhara yaliyowapata wale waliokosa dawa na huduma za afya. Hicho ndicho kinachofanywa na kina Balozi Lu nchini mwao.

 

Walipombaini mwenye kiwanda katengeneza maziwa yanayosababisha vifo vya watoto, mhusika naye alipewa adhabu inayolingana na kosa hilo. Tukifanya hivyo, bila shaka Tanzania, siku si nyingi, itasonga mbele kimaendeleo. Lakini mwa mtindo huu wa kuchekeana-chekeana, tusitarajie muujiza wa kutufikisha kwenye pepo waliyonayo China na wenzake.

 

1358 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!