Wiki iliyopita, tulichapisha sehemu ya kwanza ya makala haya yenye kufafanua tatizo linaloendelea hapa nchini juu ya haki ya kuchinja. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hizi. Wapo walioahidi kuandika makala za kuhalalisha msimamo wa sasa wa kuchinja baada ya kusoma makala haya, tunatarajia yakitufikia tu, nayo tutayachapisha kwa nia ya kuongeza uelewa. Endelea…

Kihistoria dini ya Kiislamu imeanza mwaka 610 B.K. Swali ambalo mtu yeyote anaweza kujiuliza ni hili kabla Uislamu haujaanza Wakristo na Wayahudi walikuwepo? Ninaamini mtu yeyote angejibu kuwa  ndiyo walikuwepo. Swali la pili lingekuwa Je, walikuwa wanakula nyama? Jibu lake ni ndiyo na walikuwa wanakula nyama.


Swali la tatu lingekuwa walikuwa wanachinjiwa na nani? Jibu ni kwamba walikuwa wakichinja wao wenyewe. Swali jingine lingekuwa Kwa nini leo hao waliokuwa wakijichinjia wenyewe kabla ya Uislamu kuja hawachinji? Majibu ya swali hili unaweza kumsikia mtu akikujibu kuwa akichinja Mkristo au Myahudi Mwislamu hali chakula hicho, lakini akichinja Mwislamu, Mkristo au Myahudi anakula chakula hicho bila tatizo lolote.


Hoja kuu hapa ni ni nani aliyebadilisha utaratibu wa uchinjaji nyama kama ulivyokuwa siku zote za Wayahudi na Wakristo kujichinjia na kurasimisha taratibu hizo kwa dini moja tena iliyokuja nyuma kuhodhi masuala ya uchinjaji?


Je, Wakristo walipokuwa wanachinja wanyama kabla ya Uislamu kuja walikuwa wanachinja kwa jina la nani? Je, jina hilo sasa hivi halipo? Huenda ukanijibu lipo. Kama lipo ina maana kwa sasa inapofikia Wakristo na Wayahudi kutaka kuchinja jina hilo la kuchinjia hupotea kwa muda ule tu wa kuchinja, lakini kwenye ibada  linajitokeza tena? Nini kimetokea kuhusu uchinjaji wa wanyama hata kuwa chanzo cha migogoro na misuguano katika jamii yetu?


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la 2005, Ibara ya 3 (1) inasomeka hivi: “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”


Kuhusu usawa kwa watu wote katika Katiba hiyo hiyo Ibara ya 13(1) inasomeka hivi: “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo  haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”


13 (2) “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”


Vifungu hivyo vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vinaeleza usawa wa watu wote mbele ya sheria katika nchi isiyo ya kidini kama Tanzania, na kupiga marufuku ubaguzi wa aina yoyote unaoweza kufanywa na mamlaka yoyote.

Kupitia suala la uchinjaji wanyama, Watanzania wengine wasio Waislamu wanabaguliwa kwa kutoshiriki katika uchinjaji wa wanyama kwenye machinjio ya Serikali ambayo wao wenyewe wameshiriki kuzijenga kwa kodi zao wanazozitoa, na zaidi sana wanatozwa kodi kwa wanyama wao. Kodi hiyo haiendi serikalini bali inakwenda kutunisha mfuko wa Uislamu. Huu ni ubaguzi wa dhahiri na uvunjaji wa Katiba tena kwa makusudi.


Ibara ya 19(1-2) inasomeka: “Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani, na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake. Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuia za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”


Katiba ya nchi inaeleza wazi kuwa mambo ya dini yatakuwa ya hiari ya mtu binafsi.  Lakini inavyoonesha kuna kundi moja la dini ambalo lingependa watu wa dini zingine washurutishwe kufuata taratibu zao kama waraka wa Bakwata – Misungwi unavyojieleza. Huku ni kutokuitii Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama ya nchi yetu.


Madai ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya watu wakidai kwamba Serikali ndiyo iliyowaruhusu Waislamu peke yao kuchinja wanyama si sahihi. Serikali ya Tanzania kwa sababu haina dini, kwa vyovyote vile isingeweza kuruhusu dini moja kuhodhi utawala katika maeneo ambayo yanamilikiwa na Serikali yenyewe kupitia kodi za wananchi, vinginevyo jambo hilo lingetoa tafsiri moja tu kuwa Tanzania kuna Serikali mbili. Moja ya kisekula isiyo na dini na nyingine ya pembeni (a parallel government) jambo ambalo halipo.


Kwa muda mrefu Waislamu wamekuwa wakijaribu kuishawishi Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itunge sheria moja itakayoitambua dini moja tu ya Kiislamu kwamba ndiyo ihusike na uchinjaji wa wanyama kwa ajili ya matumizi ya kibiashara na nyumbani kwa Watanzania wote.


Hoja ya namna hiyo iliwahi kupelekwa katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani (CCM) Zanzibar katika Mkutano wa Tano, Kikao cha Tano cha Bunge, cha Novemba 6, 2009 kama alivyonukuliwa na taarifa rasmi ya Bunge (HANSARD) uk.55 na 56 inasomeka hivi:


“Sasa Mheshimiwa Waziri, ningemwomba basi akaangalia  na sehemu zote hizi mbili. Sitaki aende ndani sana lakini ninachosema ni kwamba bodi ifike mahali iweke sheria, kuwe na  kanuni ya uchinjaji wa nyama ambao tunataka tuwatumie.


Tusichinje tu. Ndiyo nikasema kwamba Tanzania haina dini lakini Watanzania wana dini, tunakula kula nyama hii. Sasa kuwe na utaratibu maalumu. Sasa Mheshimiwa Waziri, hili atakuja kutuambia vipi angalau basi tuweke utaratibu unaofahamika. (Makofi).


Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano ukienda nchi za wenzetu hasa nchi za Kiarabu, si kwamba wote watakuwa Waislamu kwa sababu ni nchi za Kiarabu hapana. Ndani ya nchi za Kiarabu kuna watu wana dini nyingine na wala usije ukasikia mtu anaitwa Hafidh Al-Saad kwa mfano, ukafikiria ni Mwislamu, hapana ni jina tu hilo. Lakini dini yake ikawa nyingine.


Abdulaziz utasema kwa jina hili huyu Mwislamu hapana si Mwislamu jina kitu kingine, dini kitu kingine. Sasa wenzetu kwa sababu ya kuweka tofauti pale ambapo kunachinjwa nyama halali, basi unapokwenda katika ranchi yao ya kuchinjia  kile kisu kimeandikwa Bismillah na kule alikoelekea yule ng’ombe ndiko kunakokubalika.


Mheshimiwa Mwenyekiti, nyama zinauzwa Dar es Salaam, Dodoma na mahali pengine,wallah hawaulizwi kwenye bucha wamechinja wapi nyama hiyo, hawaulizi wala hawaulizwi kwamba ngombe huyo alivyochinjwa kaelekea Kibla, sote tunakwenda kununua nyama, tunaondoka.


Lakini nasema lazima kama ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunataka kupitisha jambo hili lazima tuwe na tahadhari. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri awe na tahadhari na hili mbaya hajitokezi sasa anajitokeza baadaye.” Mwisho wa kunukuu.


Hilo ndio ombi lililopelekwa bungeni ili Bunge litunge sheria ya namna ya uchinjaji wa nyama. Hii maana yake ni kwamba sheria hiyo mpaka sasa haipo.  Mh. Hafidh Ali Tahir alipendekeza sheria itakayotungwa lazima izingatie zaidi utaratibu wa Ibada ya Kiislamu wakati wa kuchinja, akimaanisha wanyama wanapochinjwa wachinjwe kwa kuelekezwa Kibla, uelekeo ambao Waislamu wote huelekeza nyuso zao wakati wa kufanya ibada zao, yaani Makka.

Je, unajua Waziri alijibu nini? Usikose sehemu ya tatu ya makala haya kupitia gazeti la Jamhuri, Jumanne ijayo na kila Jumanne.

Daniel amesema ni msomaji mzuri wa Jamhuri na ameamua kuchangia katika kuielimisha jamii kupitia makala haya. Daniel anapatikana kwa namba 0687931313.


By Jamhuri