Je, mpangaji anaruhusiwa kumpangisha mwingine?

Upangaji una mambo mengi sana. Hii ndiyo sababu suala hili nalo limeguswa na sheria na kuwekewa taratibu aake mahususi. Kila mtu anajua kuwa upangaji si lazima uwe wa nyumba ya kuishi tu. Hata maeneo ya biashara na shughuli nyingine pia hupangishwa.

Kutokana na suala hili la upangaji kuhusisha mikataba na fedha, mara nyingi inatokea misuguano katika miamala ya upangaji na upangishaji. Ipo misuguano inayotokana na ukorofi, lakini ipo misuguano inayotokana na kutojua baadhi ya mambo ya msingi ya kisheria kuhusu dhana nzima ya upangaji na upangishaji. Leo nitaeleza kuhusu uwezekano wa mpangaji naye kumpangisha mtu mwingine katika aneo ambalo yeye amepanga.

Sheria haimkatazi mtu kupanga sehemu halafu naye akaamua kuitumia sehemu hiyo kumpangisha mtu mwingine. Hili lipo ndani ya sheria, hivyo kufanya hivyo si kinyume cha sheria. Na zaidi, hata huyu aliyepangishwa naye anaweza kumpangisha mtu mwingine wa tatu, na huyo wa tatu akampangisha wa n ne na kadhalika. Yaani ikiwa ‘A’ amempangisha ‘B’, ‘B’ naye ana uhuru wa kupangisha eneo hilohilo kwa ‘C’ na ‘C’ naye pia anaweza kulipangisha eneo hilo kwa ‘D’ na kuendelea.

Hii yote inaruhusiwa na upangaji wa kila mmoja katika hawa unalindwa na sheria na kila mmoja anapata haki zake kwa nafasi yake. Kwa mfano, kila mpangishaji ataitwa mwenye nyumba, yaani ‘A’ ataitwa mwenye nyumba na ‘B’, na ‘ B’ naye ataitwa mwenye nyumba na ‘C’, na ‘C’ naye ataitwa mwenye nyumba na ‘D’. Halikadhalika kila aliyepangishwa ataitwa mpangaji.

Suala la msingi sana katika upangaji wa namna hii ni kuwa ule mkataba wa mwenye nyumba halisi ambaye ni mmiliki kabisa, yaani yule ‘A’, ni lazima uwe unatoa ruhusa kwa mpangaji aliyempangisha naye kuruhusiwa kumpangisha mtu mwingine, na yule mwingine naye mkataba wake pia unapaswa umruhusu kumpangisha mwingine na kadhalika. Ni muhimu suala hilo likawepo kwenye mkataba kwa sababu ndicho kipengele kitakachompa nguvu mpangaji kuweza kupangisha eneo ambalo naye amepanga.

Ikiwa mkataba wa mmoja haumruhusu kupangisha zaidi, basi huyo asiyeruhusiwa hawezi kumpangisha mtu mwingine na akifanya hivyo atakuwa anakiuka sheria na mkataba wake. Kisichowezekana ni kuwa huwezi kuwa mpangaji halafu ukampangisha mwingine bila kuwa umeruhusiwa kufanya hivyo na mwenye nyumba katika mkataba wenu.

Lakini pia katika upangaji wa namna hii unaohusisha ‘A’, ‘B’, ‘C’ na ‘D’ kama tulivyoona ni lazima kila anayempangisha mtu wake ampangishe muda mfupi zaidi kuliko ule aliopanga yeye.

Mathalani, ikiwa ‘B’ amepanga jengo kwa muda wa miezi kumi, basi yeye atakapotaka kumpangisha mtu mwingine ni lazima muda wa upangaji uwe chini ya miezi kumi. Hili linalenga kuhakikisha kuwa ule mkataba wa pili wa upangishaji hautavuka muda wa mkataba wa kwanza ambao unampa mpangaji wa kwanza mamlaka juu ya jengo alilopanga.

Ikiwa mpangaji ‘B’ amepanga miezi kumi, basi atakapompangisha ‘C’ inabidi ampangishe miezi tisa au chini yake.

Kama ‘B’ akipangisha zaidi ya muda ambao yeye amepanga kwa ‘A’, ina maana kuwa mkataba wake wa upangaji utakapomalizika, hatakuwa na mamlaka juu ya eneo hilo, hivyo ule mkataba aliompangisha ‘C’ utaingia kwenye matatizo kwa sababu ‘B’ hatakuwa na mamlaka na eneo hilo.

Pia masharti ya upangaji ambayo amepewa ‘B’ ndiyo hayohayo anayopaswa kumpa ‘C’ kama mpangaji wake. Haiwezekani mpangishaji anayepangisha baada ya kupanga akaweka masharti yanayozidi yale ambayo yeye ameyatumia kupanga.

Mathalani, yeye aliambiwa asitumie chumba au uwanja fulani ikiwa kama sehemu ya mkataba wake halafu yeye katika kumpangisha mwingine akamruhusu kutumia uwanja au chumba kile. Masharti lazima yawe yaleyale, isipokuwa yanaweza kupungua lakini yasiongezeke. Kwa mfano ‘B’ anaweza kuwa amepanga vyumba viwili na akapangisha kimoja, lakini hawezi kuwa amepanga viwili halafu akampangisha mwingine vitatu. Hivi ndivyo ilivyo kwa maeneo yote ya biashara au makazi.

Kwa ufupi hivi ndivyo jambo hili linavyowezekana.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.