Mapema mwaka huu nilikuwa miongoni mwa maelfu ya wakazi wa mji wa Iringa, waliokwenda kushuhudia sakata la misukule katika Frelimo, iliyodaiwa kuwa kwenye nyumba ya mama mmoja mfanyabiashara maarufu mjini hapa. Licha ya kufika mapema sana eneo hilo lakini sikubahatika kuona misukule!

Watu wengi, pamoja na  kurusha mawe na kumpiga sana mama yule, hakuna aliyeiona misukule kwa macho zaidi ya kusikia tu! Sakata lenyewe lilivyoanza hadi kufika hapo ni habari ndefu, na sitaiandika hapa kwa sababu wengi wenu mlisoma katika magazeti na mitandao mbalimbali.


Niharakishe tu kuwashauri wafanyabiashara kuwa makini na namna wanavyoishi na jamii zinazowazunguka. Wakati mwingine fedha inapoongezeka ni bora ukajenge nyumba mitaa ya kitajiri. Kuishi ama kujenga nyumba uswahilini – ikiwa wewe ni milionea – ni kujitafutia matatizo na kashfa zisizo za lazima. Kutokana na tukio lile nimeona ipo sababu tujadili hili jambo la ushirikina katika biashara.


Kwa miaka mingi hapa Tanzania na duniani kwa jumla kumekuwapo na imani, hisia, visa na matukio yanayohusisha ushirikina na mafanikio ya mtu kibiashara. Katika uzoefu wangu wa kusoma na kusikiliza, sijakutana na utafiti ama maandishi yoyote rasmi yanayodhihirisha nafasi ya ushirikina katika mafanikio ya mtu kibiashara.

 

Katika makala hii sitachambua kabisa habari za ‘Freemason’, bali nitajikita kwenye ushirikina wa kijadi unaoaminika kuwapo Tanzania tangu zamani. Hata hivyo, kuhusiana na habari za ‘Freemason’ na ‘janja’ yao ya kutoa utajiri na mafanikio; nilishalichambua hili katika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Inakuwaje mnampa Shetani umaarufu?” Waliokosa bahati ya kuisoma wanaweza kutembelea tovuti yetu  www. (jamhurimedia.co.tz) ambapo watapata makala zote nilizoandika huko nyuma.


Wataalamu wa masuala ya biashara, taasisi za maendeleo, dini na watu wa kada ya kawaida mara zote wasimamapo katika hadhara, husisitiza watu kutoamini mchango wa ushirikina katika mafanikio ya mtu katika biashara. Pamoja na hayo; je, ni kweli ushirikina haupo? Je, mioyo ya watu inaamini nini kuhusu hili?


Ukweli ni kwamba watu wengi wanaamini kuwapo kwa imani hizi za kishirikina katika biashara mbalimbali. Ni wachache wanaokiri iwapo wanatumia ushirikina, lakini siku kwa siku idadi ya wanaofika kwa waganga wa kienyeji kutaka ndumba za kuwatajirisha inaongezeka. Tena upo uhalisia fulani (ambao haujathibitishwa) kwamba ndumba hizi huwapatia watu mafanikio.


Tunasikia mara nyingi matangazo na habari za wataalamu wa jadi ambao wanajinadi kuwa wana uwezo wa kuwapatia watu mafanikio ya kibiashara. Vipo visa vya watu kutoa kafara za damu za binadamu kwa kuua watu (hasa ndugu zao) na kupewa dawa.


Huku Nyanda za Juu Kusini, kabila la Wakinga ni maarufu sana kibiashara. Ni kawaida kusikia habari za wafanyabiashara hawa zinahusishwa na ushirikina (bahati nzuri na mimi ni Mkinga pia). Ukweli na uhalisia wa Wakinga na watu wengine kutumia ushirikina ni jambo ambalo huwezi kulithibitisha wala kulikanusha kirahisi.


Pia hivi karibuni kumevuma habari za kuwapo kwa waganga wa jadi nchi za jirani (Zambia, Malawi na DRC) ambao wanatoa ‘utajiri’ kwa mtindo wa aina yake. Inasemekana kuwa, huko kuna kuku wa uganga ambapo ‘mteja’ huchota punje za mahindi na kuzirusha chini; kisha kuku wa uganga huanza kuyadonoa. Idadi ya punje atakazodonoa ndio miaka ya uhai ukiwa na utajiri wa kupindukia.


Cha ajabu ni kuwa kuku huyo hawezi kuzidisha punje kumi. Kwa hiyo anaweza kudonoa punje moja, mbili ama kumi zote kutegemea na bahati ya mhusika. Mamia ya Watanzania wanamiminika huko kila kukicha.


Katikati ya mwaka 2005 nilikuwa katika ibada ya kawaida kanisani kwetu, siku hiyo kulikuwa na mtu aliyeamua kumgeukia Mungu na kuachana na utumwa wa dunia hii. Kwa bahati nzuri ninamfahamu mtu yule, alikuwa ni mmoja ya matajiri wakubwa na maarufu katika eneo letu.


Kuokoka kwake kuliambatana na uchomaji wa ndumba. Katika ushuhuda wake, alieleza kuwa kwa miaka karibu 16 amekuwa akifanya biashara kwa kutumia ushirikina. Alidai kuwa mganga alimpa masharti ya kutoa kafara ya binadamu kila baada ya miaka miwili na kulala makaburini kila siku ya Ijumaa na Jumapili. Hadi kufikia wakati huo alikuwa ameshawaua ndugu zake wanane kwa ushirikina wakiwamo baba, mama na mwanaye wa kwanza!


Mtu huyu alitueleza kuwa alikuwa na chumba maalumu ambako alikuwa akitunza misukule ya wanaokufa kiuchawi, na kila asubuhi alikuwa akifungua chumba kile na kukuta kimejaa mamilioni ya noti! Fedha hizo zilikuwa zinatoka wapi? Hata yeye hakuwa akijua, lakini mtindo huu wa mtu kuletewa fedha kishirikina ni maarufu sana, ukiitwa ‘chuma ulete.’


Haitakuwa busara kwa wataalamu na wadau wa biashara kukaa kimya, ama kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu. Lazima tutafiti na kujiridhisha kuhusu suala hili. Je, kwa ukweli kiasi gani kuwa ushirikina unaweza kumnufaisha mtu kibiashara? Kama ushirikina hauna nafasi katika biashara, mbona kuna watu wanaoutumia na wanakiri kuwa wanafanikiwa?


Wakati fulani nilikutana na mganga wa kienyeji eneo la Makambako, Njombe, na nikabahatika kuzungumza naye mambo kadha wa kadha kuhusu ndumba katika biashara. Mganga huyu alikiri kuwa zipo dawa na utundu wa kijadi ambao humuwezesha mtu kufanikiwa kibiashara. Ingawa mganga huyu alisema kuwa wanatumia zaidi kanuni za kisaikolojia kuliko ‘dawa’.


Kwa mfano, mtu apewapo dawa hizi hupewa masharti mbalimbali yakiwamo ya kutokula nyama, ambapo ulaji wa nyama huongeza bajeti na kupunguza faida. Kutotembea nje ya ndoa, kwa sababu kutembea nje ya ndoa hutapanya fedha kwa kuhonga! Kutovaa nguo nzuri wala kulala mahali pazuri nako hupunguza bajeti ya matumizi na kujikuta mtu anaongeza mzunguko wa fedha katika mtaji na kufanikiwa.

 

Kinachosababisha watu wengi wahangaike na kufuatilia ndumba katika biashara, kunatokana na ukosefu wa elimu sahihi ya mambo ya kibiashara. Kanuni nyingi zinazotumiwa na waganga wa kienyeji zikitolewa kama masharti kwa wateja wao zipo katika sayansi ya biashara pia.


Kuna wakati waganga huwaambia wateja wao kuwa ili kuwapata wateja wengi katika biashara; waweke dawa katika milango ya kuingilia na kisha wahakikishe wanazungumza vizuri na kila mteja anayeingia. Suala la kumjali mteja na kumchangamkia aingiapo katika biashara ndilo linalozalisha wateja wazuri na wa kudumu. Hii ni kanuni katika sayansi ya biashara na kamwe dawa iliyotundikwa haina cha maana inachokifanya pale!


Kutokana na kuendekeza imani za kishirikina, biashara nyingi zilizopo katika nchi yetu zinakuwa sio za kudumu ama endelevu. Kwanza ni namna zinavyoendeshwa na pili ni kukosa maono endelevu.


Wengi wa wafanyabiashara wanaotumia ndumba katika biashara zao hawana mfumo wa uendeshaji. Biashara ndiyo wao na wao ndiyo biashara. Kwa kuwa mganga alimwambia ‘dawa hii uweke katika droo ya mauzo na asishike mtu mwingine yeyote’, basi mfanyabiashara analazimika kuwapo eneo la biashara saa zote ili kutokiuka masharti!


Wengi hawaajiri wafanyakazi na kuwaelekeza ‘A-Z ya biashara zao kwa sababu ya masharti ya kipuuzi wanayopewa na waganga wa jadi. Wapo wafanyabiashara ambao hata wake zao hawajui namna biashara zao zinavyoendeshwa kwa sababu tu wameambiwa kuwa “mke wako akishika fedha za mauzo akiwa kwenye siku zake za hedhi atakuwa amekiuka masharti na hivyo kufilisika!”


Tena mara nyingi mmiliki wa biashara anapofariki biashara zake humfuata nyuma yake (hufilisika). Utawasikia watu wakisema, fulani alikuwa tajiri sana alipofariki, mke wake ama watoto wake walishindwa ‘kufuata masharti’ ya mganga ndiyo maana wamefilisika.

Sehemu kubwa ya ukweli si kukiuka masharti ya mganga wa kienyeji, bali ni kushindwa kwa walioachiwa kuendesha biashara kwa sababu hawakushirikishwa katika uendeshaji wake pindi mmiliki alipokuwa hai.

 

Kukosa maono endelevu kuhusu biashara nalo ni tatizo kubwa. Kikawaida bidhaa ama huduma yoyote duniani, ina muda fulani wa kuwa hai na baadaye hufa ama kutoweka (product life cycle). Mtu anapoanzisha biashara ya bidhaa ama huduma fulani ni lazima kuzingatia jambo hili kuwa ipo siku zitakufa (products decline). Hata kama biashara ikiwa na mtaji mkubwa namna gani, kuna wakati ambao hufika bidhaa na huduma zake ‘kufa’ na hivyo biashara yenyewe ‘kufa’.


Ili kupambana na ukomo wa bidhaa ama huduma, mfanyabiashara anatakiwa kufanya mambo mawili. Mosi ni kuboresha huduma na bidhaa zake (kama ni mzalishaji) kulingana na mahitaji na wakati husika. Pili ni kuwa na mpango wa kuachana na biashara hiyo inapokoma na kugeukia biashara nyingine.

 

Kuamini ushirikina imekuwa ni sumu mbaya sana kwa sababu watu wanabweteka wakiamini kuwa ndumba ni kila kitu. Kuna visa vingi tunashuhudia vya kufilisika kwa wafanyabiashara mbalimbali ambako huambatana na maneno kuwa huenda wamekosea masharti ya waganga wao.

 

Kumbe uhalisia ni kuwa huwa hawatambui kabisa biashara zina ukomo na bila kuzihuisha, kuziboresha na kubuni mpya; muda utafika  nguvu ya soko itakulazimisha uondoke na kujikuta umefilisika.


Ni kawaida katika nchi yetu kushuhudia mfanyabiashara anayemiliki mtaji wa milioni 500 akiwa hana muhasibu, meneja, afisa mwajiri na wala biashara zake hazijasajiliwa. Yeye ndiye kila kitu. Shida kubwa inayojitokeza hapa ni moja; kukosekana kwa usimamizi yakinifu na upangaji wa mipango endelevu.

 

Wengi hawana ushauri wa kitaalamu kuwajulisha, je, biashara zao zinazalisha faida kiasi gani kwa mwaka? Je, hali ya masoko na ushindani ikoje na ina athari gani? Je, biashara zake zitakuwa na hali gani miaka mitano, 10 ama 20 ijayo? Je, mikakati na mipango gani ifanyike kuhakikisha biashara zinadumu hadi kizazi cha wajukuu zake?


Wajasiriamali wanatakiwa kufundishwa elimu ya biashara ikiwamo namna ya kutafuta masoko ya bidhaa na huduma, namna ya kuendesha biashara katika mifumo rasmi, jinsi ya kushindana katika ulimwengu wa kistaarabu pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kimahesabu. Kubwa kuliko yote ni namna wanavyoweza kufundishwa na kujizoeza kuwa wabunifu (creative and innovative) katika biashara zao.


Haiwezekani mtu awe na mgahawa wenye mazingira ya uchafu, vyakula visivyo na ubora na wahudumu wachafu halafu aseme kuwa jirani yake anatumia, ‘chuma ulete’ eti kwa sababu ana wateja wengi; wakati mwenziye ana mazingira mazuri, kauli nzuri na vyakula vyenye ubora.


Badala ya kukaa na kufikiria kuwa haiwezekani mtu kuwa bilionea kwa njia za halali, ni vema wajasiriamali waanze kutafuta elimu na maarifa ya ujasiriamali ili wafanye biashara zao pasipo mbinyo wa imani za kishirikina.

Wajasiriamali tunastahili ushindi.

stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901

 


 

 

 

 

 

10179 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!