Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia wanafamilia wa ukurasa wa TUZUNGUMZE na wasomaji wote wa  Gazeti la JAMHURI heri ya Noeli na Mwaka Mpya wa 2020.  

Napenda kuwatakia miezi 12 ya furaha, wiki 52 za baraka, siku 366 za mafanikio, saa 8,784 za afya, dakika 527,040 za amani na  sekunde  31,622,400 za upendo. Heri ya Mwaka Mpya 2020.

Kusamehe ni siri ya mafanikio katika maisha. Kila mmoja wetu ameitwa kuwa mponyaji wa majeraha ya wengine licha ya kwamba  yeye mwenyewe  anayo majeraha yake.  Binadamu wote tunayo majeraha ya kihisia, kiakili, kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia.

Inawezekana una  majeraha ya kusalitiwa na  mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha  ya  kufiwa  na mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kuishiwa mtaji wa biashara. Inawezekana una majeraha ya kiuchumi. Majeraha ni mengi. Nafasi hainiruhusu kuyataja majeraha yote. Itoshe kusema kwamba, makala hii ina nia ya kuyaponya majeraha yako ya kihisia, kiuchumi, kifamilia, kiafya na kiroho.

Nilipotoa makala yangu iliyokuwa inasema: ‘Nguvu ya msamaha’ katika Gazeti la JAMHURI linalotolewa nchini Tanzania na kuchapishwa na JAMHURI Media, Toleo No. 249, ISSN1821-8156, Julai 5-11, 2016, msomaji mmoja ambaye kwa sababu maalumu sitataja jina lake, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi:

Nimeumizwa sana katika maisha yangu. Tena  nimeumizwa mno. Sina furaha kabisa katika maisha yangu. Nina mtoto wa kiume mwenye umri  wa miaka kumi na mitatu (13). Nilipata ujauzito  nikiwa chuoni mwaka wa tatu. Kwa sasa nipo  naishi na mwanagu. Kila mwisho wa mwezi  ninamtumia mama yangu mzazi pesa za matumizi.  Baba yangu simtumii kwa sababu hatupatani  kabisa. Baba alinibaka na kunipa ujauzito wa  huyu mtoto wangu.

Baba alipogundua kwamba nina ujauzito wake  alinilazimisha kuitoa mimba. Nilikataa kwa sababu nilihofia kufa. Niliamua kuhama nyumbani na kwenda kuanza maisha ya peke yangu.  Namshukuru sana Mungu nilijifungua salama.  Mtoto amekua, lakini baba yangu hataki hata  kuniona. Hataki hata niende nyumbani.  Ndugu  na majirani wanashindwa kufahamu chanzo cha  ugomvi wangu na baba yangu. Mama yangu  humlilia baba yangu anisamehe kama nilimkosea  lakini baba hataki.

Siri kubwa niliyoiweka moyoni ni kwamba,  baba  yangu ndiye  aliyenibaka mpaka nikashika  mimba  ya  huyu mtoto. Mpaka leo mimi na baba ndio  tunajua  jambo hili.  Kiukweli ninamchukia sana  baba yangu.  Aliniumiza sana.  Mama, ndugu na jamaa hawamfahamu baba wa mtoto wangu. Baba hataki kumwona mjukuu wake. Mtoto wangu  anataka kumfahamu baba yake. Je, niiambie jamii  baba alinibaka au nimwambie baba yako ni baba  yangu?  William nimechanganyikiwa kabisa.

Jibu  la msamaha ni msamaha. Kusamehe ni  kupita njia aliyoipita Yesu Kristo.  Mwana michezo Jonathan Lockwood aliwahi kusema: “Wasamehe wengine si kwa sababu  wanastahili, bali kwa sababu wewe unastahili amani.”

Msamaha ni amani. Msamaha ni uponyaji. Msamaha ni manukato kwa walioumizwa kihisia, kiupendo, kiafya na kiimani. Jifunze  kusamehe. Jifunze kuwa na amani ndani ya  moyo wako. Kusamehe ni kumuachilia mtu uliyemshikilia katika moyo wako. 

Kumbuka: Kutokusamehe ni kuendelea  kuyakumbatia maumivu ndani ya moyo  wako. Achilia uchungu ulionao. Usiuweke moyoni. Mchungaji Joel Osteen anasema: “Tusiposamehe, hatumuumizi mtu mwingine, hatuiumizi kampuni iliyotukosea, hatumuumizi Mungu. Tunajiumiza sisi wenyewe.”

Papa Fransisko anasema: “Asiyesamehe anaugua kimwili, kihisia na kiroho.” Katika makala hii nitauzungumzia msamaha. Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni za kuwania urais alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu mpinzani wake aliitwa Edwin  McMasters Stanton. Edwin McMasters  Stanton alikuwa tayari kufanya lolote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa Baraza la Mawaziri, alimteua Stanton kuwa Waziri wa Ulinzi. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ili Stanton asiteuliwe kuwa waziri. Hata hivyo, rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za wasaidizi wake.

Rais akasema: “Huyu ananichukia mimi ila si Marekani. Huyu ana sifa za kuiongoza Marekani na watu wake.” Akamteua kuwa waziri wa ulinzi. Stanton aliposikia uteuzi wake alishangaa mshangao mkubwa. Akaukubali ule wadhifa na akaifanya hiyo kazi kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema: “Hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa huku akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.” 

By Jamhuri