Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambayo inasifika kwa kuwa na mifumo mingi ya ulinzi dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto. 

Hilo si suala la bahati mbaya, kwani mifumo hiyo imewekwa makusudi na serikali na sekta binafsi kama njia ya kukabiliana na ukatili huo. 

Hili lilifanyika ili kuonyesha jinsi ambavyo jamii haikubaliani ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya baadhi ya makundi katika jamii.

Mathalani, kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/2018-2021/2022, serikali imepanga ifikapo mwaka 2022 vitendo vya ukatili viwe vimepungua kwa asilimia 50. Mpango huu pia unalenga kuiwezesha nchi kutekeleza na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 katika eneo hili.

Pia, mpango huu unachochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, pamoja na Ajenda ya Maendeleo ya Tume ya Umoja wa Afrika (2063), kwamba, ukatili wa aina zote nchini unatakiwa kufikia ukomo haraka ili kuiweka jamii hiyo katika jukwaa salama na sawa.

Wakati serikali ikiwa kwenye utekelezaji wa mpango huo wa taifa, ukatili wa kijinsia bado unaendelea kuchipua mbele ya mamlaka zinazosimamia sheria za nchi.

Mathalani, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara, wasichana wawili, Bhoke Charles (23) na mdogo wake, Nyankuru Charles (19) walizuiwa kutoa heshima zao za mwisho wakati wa ibada ya kumuaga baba yao mzazi aliyefariki dunia Agosti 13, 2019, kwa sababu tu hawajakeketwa.

Zuio kama hilo lilimkumba pia mama mzazi wa wasichana hao, Kegocha Charles, aliyezuiwa hata kukaribia kaburi la mume wake huyo waliyekuwa wametengana naye, kutokana na kuishi na watoto ambao hawajakeketwa.

Tukio hilo linalotafsiriwa kukanyaga sheria na haki ambazo zinatolewa kikatiba, limeripotiwa kutokea Agosti 16, 2019, katika Kijiji cha Kegonga – Nyanungu, wilayani Tarime ambako kuna Kanda Maalumu ya Polisi.

Taarifa zinasema kuwa, siku ya maziko wasichana hao walizuiliwa hata kusogelea jeneza wala kaburi la baba yao huyo, kitendo wanachosema si tu kimewanyima haki yao ya msingi, bali kimewaathiri pia kisaikolojia.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii kwa niaba ya mdogo wake, Bhoke Charles, anasema wana wasiwasi huenda baba yao hajafariki dunia, kwani hawajaelezwa chanzo cha kifo cha mzazi wao wala hawajapewa taarifa yoyote ya daktari, inayothibitisha mauti hayo.

Bhoke amemtaja mtu aliyedai kuwa ni baba yake mdogo (jina tunalihifadhi kwa sasa) kuwa yeye na baadhi ya wana ukoo ndio waliohusika kuwazuia kutoa heshima zao za mwisho siku ya maziko ya baba yao mzazi.

Anasema taarifa walizonazo zinadai baba yao amefariki dunia kwa kunyweshwa sumu na mmoja wa wanafamilia hiyo.

“Najisikia vibaya sana mimi na mdogo wangu Nyankuru, kwa kitendo hiki cha kutuzuia kumuona na kumuaga baba yetu mzazi siku ya maziko yake. Tunajiuliza, kwa nini wametupa hukumu kubwa hivi? Siku ya msiba mdogo wangu alikuwa anaumwa jino. Nilikwenda mimi na bibi yangu… jeneza limekuja naliona hivi,” anaeleza kwa masikitiko na kuendelea:

“Niliishia kuona tu jeneza la baba yangu, nikazuiliwa kumsogelea wala kuona alipozikwa baba yangu, eti sijakeketwa. Hivi Tanzania kuna sheria inasema lazima mtoto wa kike akeketwe?”

WHO

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu ulimwenguni amekutana na ukatili wa kimwili (vipigo) au kingono katika maisha yake.

Kupitia taarifa zilizopo katika mtandao wa Shirika la TGNP Mtandao, WHO inasema takriban wanawake wanne kati ya 10 nchini wamepitia ukatili wa kimwili, huku asilimia 17 wakikumbana na mikasa ya kingono.

Kulingana na watoto hao wa marehemu, wameishi na baba yao hadi wakiwa na umri wa miaka minane kabla ya kwenda kuishi na mama yao, baada ya wawili hao kutengana miaka kadhaa iliyopita.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mikoa ya Mara na Shinyanga ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa mikasa ya ukatili dhidi ya wanawake nchini, kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya kiraia.

Kulingana na taarifa hizo, matukio ya ukeketaji katika Wilaya ya Tarime yanatajwa kuwa kikwazo cha maendeleo dhidi ya mtoto wa kike. Changamoto hii inaanza kuibua maswali kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu iwapo Tanzania kweli itaweza kufikia lengo la kutokomeza matukio haya ifikapo mwaka 2030 kama ilivyopangwa.

Katika maelezo yake, Bhoke anasema tangu utotoni mwake hakuwahi kuambiwa wala kuamriwa na baba yake kukeketwa, hivyo kwa sasa inampa shida kisaikolojia baada ya kuzuiwa kumuona mzazi wake siku ya maziko.

Watoto hao wawili wanaiomba serikali na jumuiya za kiraia waingilie kati ili wapate fursa ya kuzuru kaburi la baba yao, kwani zuio walilopewa limeondoa amani ya mioyo yao, na wanafikiri wametengwa na ulimwengu.

“Ukweli walitudhalilisha sana. Hata siku ya pili tulikwenda kuona baba yetu alipozikwa wakatuzuia. Mama na yeye alizuiliwa kuona wala kusogelea kaburi la baba, eti anaishi na sisi hatujakeketwa. Walimpiga pia mama na kumdhalilisha kwa matusi ya nguoni pale msibani,” anasimulia.

Bhoke anawataja watu watatu, akiwamo baba yao mdogo (majina yao tunayo) anaodai kuhusika kumdhalilisha kijinsia na kumpiga mama yao wakati wa msiba hapo Kegonga, Tarime.

Mashirika ya utetezi wa haki za binadamu yametaka kuchunguzwa kwa tukio hilo na hatua za haraka kuchukuliwa kuhusu waliohusika na mikasa hiyo, kwa sababu kuna kila dalili kuwa ni kinyume cha sheria mama.

Ibara ya 30(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema: “Haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii, havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingilia kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine, au masilahi ya umma.”

Aidha, tukio hilo la mabinti hao kuzuiwa kutoa heshima za mwisho wakati wa maziko ya mpendwa wao, linavunja kanuni ya kwanza ya tamko la haki za binadamu la Desemba 10, 1948.

Yassin Ally, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini linalohusika na utetezi wa wanawake na wasichana, anasema Jeshi la Polisi lazima lichukue hatua kuhusiana na tukio hilo.

“Kwanza hilo ni kosa la jinai. Wanachopaswa hawa ndugu zetu (Bhoke, Nyankuru na mama yao Kegocha) waende kuripoti polisi kwenye dawati la jinsia. Lazima hatua zichukuliwe,” anasema.

Kufukuliwa?

Katika hatua nyingine, watoto hao wameomba vyombo vya dola visaidie ili mwili wa baba yao ufukuliwe ili ufanyiwe vipimo vya daktari kubaini hasa nini chanzo cha kifo chake. Wanasema wana kiu ya kujua chanzo cha kifo cha mzazi wao, kwani hadi sasa hawajaelezwa na ndugu zao aliugua nini wala hawajapewa taarifa sahihi za kitabibu.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mama yao mzazi, Kegocha Charles.

“Ukweli ile siku walinidhalilisha kupita kiasi. Kwanza, nilipigwa mbele ya waombolezaji na kutolewa matusi mabaya. Nililia sana….lakini yote nimemuachia Mungu,” anasema.

Anasema baada ya kufanyiwa dhihaka hiyo, aliripoti Kituo cha Polisi cha Kegonga, wakakataa kupokea baadhi ya malalamiko.

Anasema: “Mkuu wa Kituo cha Kegonga alipokea taarifa ya mimi kupigwa na kutukanwa matusi ya nguoni tu. Hilo la kuzuiwa kumuaga marehemu aliniambia wao hawawezi kuingilia mambo ya kimila.”

Watengwa 

Taarifa zinaeleza kuwa, watoto hao wa marehemu pamoja na mama yao wameachwa kando katika ushirikishwaji wa masuala ya mirathi. Kegocha anadai wanazo taarifa kuwa tayari kuna mtu ameshapewa jukumu la kusimamia mirathi pasipo yeye na watoto wake kushirikishwa. Wamepaza sauti kuomba mamlaka ziingilie kati suala hilo ili kuwasaidia kupata haki zao za msingi.

Agosti 17, 2019, mmoja wa wana ukoo wa familia ya marehemu aliyetajwa kwa jina la Gibuswa Charles Marwa, alimkana Kegocha kuwa si mke wa ndugu yake. Lakini Agosti 21, Marwa alimuomba msamaha mke huyo wa marehemu kwa njia ya maandishi. Guragura Obogo, Kimunye Chacha na Marwa Gikaso, wamesaini kwenye nyaraka za kijiji hicho kuwa mashuhuda wa suala hilo.

Baadhi ya wanakijiji waliodai kushuhudia tukio hilo msibani hapo, wamelaani wakiomba wahusika wote wakabiliwe na shinikizo la sheria.

“Sijawahi kuona vitu vya namna hii. Yaani unawazuia watu kumuaga marehemu ndugu yao. Tupo dunia ya ngapi?” anahoji mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Marwa.

Mtendaji wa Kijiji hicho cha Kegonga, Mwita Nyaluli, kupitia barua yake ya Oktoba 22, 2019, amekiri Kegocha na wanaye Bhoke Charles na Nyankuru Charles kukumbwa na mkasa huo.

“Na baada ya kufa, wana familia waliamua kumtenga na watoto wake bila sababu za kimsingi. Wakidai kuwa huyu mama amekataa kukeketa watoto wake, kinyume cha sheria. Hivyo, wana familia hao wanalazimisha watoto wakeketwe. Kama hawataki nao hawawataki, hawako tayari kuwa nao pamoja au kushirikiana kama familia moja, waondoke,” mtendaji ameandika katika barua.

RPC aonya 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Mkoa wa Mara, Henry Mwaibambe, alipoulizwa, anasema atachukua hatua kwa wahusika wote.

“Kumzuia mtu kumuaga marehemu kwa sababu hajakeketwa ni uvunjifu wa sheria, maana serikali inazuia ukeketaji. Na kama walimpiga huyu mama wakamdhalilisha kwa matusi ya nguoni mbele ya watu, hili ni kosa la jinai, lazima hatua zichukuliwe,” RPC Mwaibambe anasema wakati wa mahojiano na JAMHURI.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Msafiri Mtemi, ameahidi kufuatilia tukio hilo, kwani halikubaliki kisheria.

64 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!