Jogoo wanaowika yalikuwa mayai

Mwanzo wa mkeka chane mbili. Hatupaswi kudharau mwanzo wa jambo lolote lile. Usidharau kidogo ulicho nacho. Mambo yote makubwa huanzia madogo. Yesu alianza maisha yake duniani zizini, pangoni na horini. Kwa sasa Yesu Kristo ni kitovu cha historia ya dunia. Historia inaelezwa kwa kutumia vifupisho B.K (Baada ya Kristo) na K.K (Kabla ya Kristo).

Kuanzia kwake tunatazama mbele, tunatazama nyuma. “Mistari yote ya historia inakutana kwake,” alisema Mchungaji Mashuhuri, Charles H. Spurgeon. Maisha ya zizini ni mapito. Maisha ya pangoni ni mapito. Maisha ya horini ni mapito. Maisha ya kibandani ni mapito. Maisha ya kuwa mfanyakazi wa nyumbani (house girl) ni mapito.

Joseph Fels alizaliwa kwenye kibanda huko Virginia. Wazazi wake walikuwa maskini. Hakupata elimu nzuri. Alianza kazi kama muuza sabuni. Kwa kujitoa sadaka na kubana matumizi aliweka akiba dola 4,000 za Marekani, pesa ambazo alizitumia kununua kiwanda kidogo cha sabuni. Kiwanda kilipanuka na kuwa kiwanda kikubwa cha sabuni na kumfanya awe bilionea. Jogoo wanaowika yalikuwa mayai. Joseph Fels aliwika katika biashara ya sabuni.

Bila shaka msomaji ulikwisha kuona wembe unaoitwa Gillette. Unaitwa hivyo kwa sababu ya King Camp Gillette. Alizaliwa Wisconsin. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na saba baba yake alipoteza kila kitu katika janga la moto. Kijana Gillette ilibidi kuchakarika. Kilichobaki ni historia. Baadaye alikuwa na kiwanda cha kutengeneza nyembe aina ya Gillette.

Alikuwapo kijana mwenye ulemavu akiitwa Elias Howe. Familia yake ilikuwa ni familia ya watu maskini. Wakati mwingi hawakula milo miwili kwa siku. Walishinda njaa na wakati mwingine walilala njaa. Aligundua mashine ya kushona, lakini haikununuliwa. Karakana yake iliungua moto. Mke wake aliaga dunia. Aliendelea kujaribu. Mwishowe mashine yake ya kushona ilinunuliwa. Mauzo yalishika kasi. Baadaye Elias Howe alikuwa milionea. Siri ya mafanikio yake ni kuendelea kujaribu bila kukata tamaa.

Mwaka 1879 mtoto alizaliwa katika familia maskini ya Kiyahudi. Mwanzoni alijikataa kutokana na unyanyapaa aliokutana nao kwa sababu ya chuki dhidi ya Wayahudi. Kila mara alikuwa anashika mkia darasani. Wazazi wake walimpeleka kwa mtaalamu wa akili kuona kama alikuwa na akili timamu.

Mwaka 1895 alishindwa mtihani wa kuingia Chuo kilichoitwa Polytechnicum huko Zurich, Uswisi. Mwaka uliofuata alijaribu na kufanikiwa.  Baadaye alipata shahada ya uzamivu kutoka Chuko Kikuu cha Zurich. Alipata kazi ambayo haikuendana na kisomo chake katika ofisi ya hatimiliki.

Ni nani huyo? Ni Albert Einstein, mtu ambaye baadaye ameitwa mtu mwenye akili nyingi katika Fizikia. Aliwika sana katika uwanja wa Fizikia. Kushindwa kwake mwanzoni hakukuwa na kauli ya mwisho.

Kitabu cha kwanza cha Beatrix Potter, The Tail of Peter Rabbit, kilikataliwa na wachapishaji wa vitabu sita kabla ya kuwa kitabu pendwa cha watoto. Beatrix Potter baadaye aliwika katika uwanja wa uandishi. Kitabu cha Robert M. Pirsig Zen and the Art of Motorcycle Maintenance kilikataliwa na wachapishaji vitabu zaidi ya 100 kabla ya kuchapishwa mwaka 1974 na ziliuzwa nakala milioni nne. 

Robert M. Pirsig aliwika katika uwanja wa uandishi wa vitabu. Usikate tamaa mwanzo wako ukiwa unasuasua. Kumbuka mwanzo wa ngoma ni lele. Watoto huanza kutambaa. Shughuli kubwa duniani zinaanza kwa mwendo wa kutambaa. Mwanzo mgumu, lakini lisilowezekana linawezekana.

827 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!