Mapema mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani alinukuliwa akisema haoni sababu ya kuweka kinga ya kisheria kwa wahamiaji kutoka nchi alizozifananisha na tundu la choo.

Alikuwa akizungumzia baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini na nchi za Afrika. Tafsiri fupi ya neno alilotumia, shithole (tundu la choo), ni: sehemu ambayo haifai kwa namna yoyote kukaliwa na binadamu. Tafsiri ndefu ina mengi zaidi: sehemu chafu, ambayo haina fursa zozote za kitamaduni, uchumi au ajira; yenye raia mbumbumbu; wajinga ambao hawana chembe ya ustaarabu. 

Makala yote hii inaweza kujaa maelezo ya ubaya wa eneo alilolitaja na hakuna jema ambalo linaweza kufananishwa na sehemu ambayo inafananishwa na choo.

Kama kuna sifa tunaweza kumpa Rais Trump, ni umahiri wa kukosa kabisa haya ya aina yoyote ya kudharau binadamu wenzake hadharani. Wengine wenye mawazo kama yake wako kimya; yeye kila kinachomjia kichwani anakitoa mdomoni. Hana kidhibiti mawazo.

Alisema kama Marekani inaona kuna haja ya kukaribisha wageni kutoka nje, basi wageni wa mfano aliowataja ni raia wa Norway.

Ndiyo maana leo inashangaza kuona kuwa mtu aliyesema maneno hayo anakabiliwa na tuhuma ambazo, kama tunakubali ukweli, tunaweza kuziona tu kutoka kwenye nchi zile alizozifananisha na shimo la choo.

Tunakataa mengi aliyoyasema Trump lakini tunaweza kukubaliana na baadhi ya maelezo juu ya nchi tunazoishi kama zisingefananishwa na tundu la choo. Ukweli ni kuwa kuna maeneo mengi ya nchi yake mwenyewe ambayo yana hali mbaya kuliko nchi anazozisema vibaya.

Tunakubali kuwa hatuna fursa za kutosha za kiuchumi, na hatuna ajira za kutosha. Baadhi ya viongozi wetu wanaingia madarakani maskini, na wanatoka madarakani matajiri wa mfano, si kwa umahiri wao wa kutafuta pesa kihalali, bali kwa umahiri wa kukwapua mali ya umma.

Hatuna mipango thabiti na ya kudumu ya kuondokana na umaskini wetu na tunaendeleza mipango inayohamisha utajiri wa Bara la Afrika na kuupeleka kwenye nchi hizo hizo zenye viongozi wanaotudharau kama Trump.

Tunapokabiliwa na majanga tunarudi tena kupigia magoti nchi zile zile ambazo tunazitajirisha kutokana na mipango yetu ya maendeleo ambayo haiachi utajiri wa rasilimali wa bara letu kubaki kwetu.

Tunaweza kuongeza pia kuwa baadhi ya nchi zetu ni nchi ambazo viongozi wake hawaheshimu kanuni, taratibu, sheria na katiba zao. Na kwa hili, na kwa yanaoyoendelea Marekani hivi sasa tunafanana na Trump kuliko yeye mwenyewe anavyotambua.

­­Katiba ya Marekani ndiyo katiba ya zamani kuliko katiba zote zinazotumika duniani. Ilipitishwa Juni 1, 1788. Ungedhani kuwa moja ya masuala ambayo hayapaswi kusikika kabisa kutoka Marekani ni tuhuma dhidi ya rais wake kukiuka katiba. Lakini hayo ndiyo tunayoyasikia.

Baraza la Wawakilishi limepiga kura ya kumuondoa Trump madarakani kwa madai ya kutumia madaraka vibaya, na kuzuia uchunguzi wa Baraza la Wawakilishi dhidi yake.

Trump hataondolewa madarakani mpaka hiyo kura ithibitishwe na Bunge la Seneti ambalo linaongozwa na chama chake, kwa hiyo hakuna uwezekano kuwa mchakato ulioanzishwa utafanikiwa.

Lakini haiondoi doa juu ya ofisi ya rais wa Marekani kwamba zimechukuliwa hatua za kikatiba dhidi yake za kumuondoa madarakani.

Kwamba inawezekana, kwa njia za kikatiba, kumuondoa madarakani rais anayekiuka katiba ni jambo la mfano ambalo linapaswa kupongezwa. Pamoja na kwamba Trump atakuwa rais wa tatu tu katika historia ya Marekani wa kupigiwa kura ya kuondolewa madarakani, bado inatushangaza wengi.

Kuna msemo kuwa kama unafuatwa na nzi sana, inawezekana kuwa umekalia kinyesi. Tuhuma za ukiukwaji wa sheria dhidi yake ni nyingi. Tungeweza kukubali hoja kuwa kinachomkabili Trump ni njama tu za kisiasa kutoka Chama pinzani cha Democrat cha kumchafulia hadhi yake na kuwa hakuna ukiukwaji wowote wa kikatiba, lakini zipo dalili kuwa anakosa uelewa mzuri wa tofauti ya kuongoza kampuni zake na kuongoza taifa la Marekani. Inawezekana huo uelewa mdogo umemfikisha pabaya.

Kwenye biashara unaweza kutenda kosa halafu ukatafuta wakili baadaye akutetee mahakamani halafu ukaendelea kupiga dili bila tatizo kubwa; kwenye siasa, hasa za Marekani, unahitaji kuongea na wakili wako kwanza kupata ushauri kuwa kila uamuzi unaochukua hautakutumbukiza kwenye mgogoro wa kisheria na kikatiba.

Tunachoshuhudia ni kiongozi ambaye haoni kabisa athari za kisheria, kikatiba na kisiasa za maamuzi yake, bali anaongozwa zaidi na haraka ya kuchukua maamuzi. Ni sifa nzuri sana kwenye biashara; ni sifa hatarishi kwenye siasa isipotumika kwa uangalifu.

Tunategemea nchi yenye katiba kongwe kabisa duniani iwe na rais ambaye kwa kila uamuzi mkubwa anaochukua atashirikisha jeshi la wataalamu na washauri wa kila aina ili kumlinda kutokana na athari mbaya za maamuzi yake.

Kwamba hilo halionekani kutokea ni dalili, si za tatizo la mfumo wenyewe, bali picha ya ukubwa wa majukumu kupiku uwezo wa aliyekabidhiwa.

Hatatendewa haki itakapoandikwa historia yake kama hatafananishwa na baadhi ya tabia za viongozi kutoka nchi alizozifananisha na tundu la choo.

Barua pepe: [email protected]

By Jamhuri