Watu wengi wana maeneo lakini wameyatelekeza. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, kutelekeza eneo ni kosa ambalo mtendaji wake ambaye ni mwenye eneo anatakiwa kuadhibiwa. Nitoe tahadhari kuwa si vema watu kujisahau baada ya kuwa wamemiliki maeneo.
Wakati mwingine si rahisi kujua kama suala la kufutiwa umiliki lipo kama halijakufika. Lakini, amini lipo, na wapo watu wamefutiwa umiliki na maeneo yao kuingia mikononi mwa Serikali au kugawiwa kwa watu wengine.
Wakati mwingine baadhi ya watumishi wa ardhi wanalitaka eneo lako na wanakusubiri kwa hamu ukiuke masharti, ili eneo lako wachukue wao au wampatie mshirika wao ambaye yuko nyuma ya mchezo huo. Haya yapo, sisi tunaoshughulika na masuala ya ardhi tumeyashuhudia.
Binafsi nina kesi ambazo watu wamefutiwa umiliki na maeneo yao wamepewa watu wengine. Hivyo, hili si jambo la mzaha hasa kipindi hiki ambacho Wizara ya Ardhi imeamua kufanya kazi kwa kufuata taratibu na kufuatilia kila jambo. Nimezungumzia kutoendeleza maeneo lakini sababu si hiyo tu bali zipo nyingi kama tutakavyoona.
 
Utaratibu wa kufutiwa umiliki
Sheria ya Ardhi kifungu cha 48(1)(g) (i-iii) imetoa maelezo ya taratibu (procedures) za  kufuata kabla mtu hajafutiwa umiliki wa ardhi.
Kifungu hicho kinaelekeza kuwa kwanza mmiliki aliyevunja masharti ya umiliki ambayo tutayaona baadaye, atatakiwa kupewa taarifa rasmi ya maandishi iliyo katika mfumo rasmi, ikieleza masharti aliyokiuka mmiliki na nini mamlaka za ardhi zinatarajia kufanya kutokana na ukiukaji huo.
Mhusika atapewa taarifa na hatafutiwa umiliki mpaka zitakapoisha siku 90 tangu kupewa ile taarifa. Zitakapoisha siku 90 na mmiliki hajafanya kile kinachotakiwa basi taratibu za kumfutia umiliki zitaanza mara moja.
Pili, sheria inasema taarifa ya kufutiwa umiliki itatakiwa kusambazwa kwa wahusika wote ambao wana maslahi katika ardhi ile. Wenye maslahi katika ardhi ni kwa mfano kuna taasisi  ya fedha iliyomkopesha mmiliki na ardhi hiyo ndiyo iliyotumika kama dhamana, au ardhi ile ni ya familia na hivyo taarifa hatapewa baba tu au mama tu isipokuwa watapewa wote wawili, au ardhi kama ni ya urithi basi taarifa atapewa msimamizi wa mirathi pamoja na warithi wote.
 
Nani mwenye mamlaka ya kufuta umiliki
Kifungu cha 48(3) cha Sheria ya Ardhi kinasema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye mwenye mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi.
Aidha, taratibu zote za awali zitafanywa na Kamishna wa Ardhi ikiwamo ile ya kumpatia mmiliki taarifa na baada ya hapo atatoa taarifa kwa Rais pamoja na mapendekezo yake ya kutaka mmiliki kufutiwa umiliki. Kwa hiyo, Rais husikiliza mapendekezo ya Kamishna wa Ardhi kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya sekta  hiyo.
 
Mambo yanayoweza kusababisha umiliki wa ardhi kufutwa
Kifungu cha 45 (2)(i-vi) cha Sheria ya Ardhi kinaeleza sababu za msingi zinazoweza kusababisha mhusika kufutiwa umiliki ardhi.
(a) Ni iwapo eneo limetelekezwa kwa muda usiopungua miaka miwili. Muda usiopungua miaka miwili maana yake ni kuanzia miaka miwili na kwenda mbele. Kutelekeza eneo kwa mujibu wa maana hii hapa ni pamoja na kutoonekana ukishughulika na eneo lako kwa namna yoyote tangu upatiwe umiliki.
(b) Jaribio lolote la kutaka kuuza au kugawa ardhi kwa mtu asiyekuwa Mtanzania. Ni kosa mtu asiyekuwa raia wa Tanzania kumiliki ardhi, hivyo jaribio lolote la kumpatia ardhi linatosha kuwa kosa la kufutiwa umiliki.
(c) Kama eneo unalomiliki si chini ya ekari mia tano na umekuwa hutumii eneo hilo kwa namna ulivyoainishiwa matumizi yake kwa kipindi kisichopungua miaka mitano.
(d) Jaribio lolote la kutoa ardhi kwa mamlaka nyingine kinyume na namna ulivyoagizwa na mamlaka wakati unapewa eneo husika.
(e) Kutumia eneo kinyume na masharti yaliyo kwenye hati ikiwa ni pamoja na matumizi yoyote yaliyo kinyume na sheria ya ardhi, sera, miongozo na kanuni zake.
(f) Pia, Rais kwa mamlaka aliyonayo, anaweza kufuta umiliki wa ardhi ya mtu yeyote kwa sababu zozote zinazohusu maslahi ya umma.

 

By Jamhuri