Utata umegubika kuhusu umiliki wa gari la mfanyakazi wa Benki ya CRDB Tawi la Moshi, Haika Mawala, lenye namba za usajili T 991 DMS aina ya Toyota Vangurd, baada ya taarifa mpya kuibuka zikidai gari hilo ni la wizi na liliingizwa nchini kwa njia za panya.

Gari hilo ni miongoni mwa magari matatu yaliyokamatwa na polisi mkoani Kilimanjaro Septemba 14, mwaka jana yakiwa yamefichwa maeneo tofauti Marangu Mtoni, Wilaya ya Moshi Vijijini ambako watuhumiwa watatu walikamatwa wakihusishwa na magari hayo.

Magari mengine yaliyokamatwa pamoja na gari hilo ni yenye namba za usajili T 140 DAE aina ya Honda na T 803 CBY aina ya Isuzu pick up, ikidaiwa kuwa yalikutwa yamehifadhiwa nyumbani kwa Steven Makuri.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, gari la mfanyakazi huyo wa CRDB lilikutwa na polisi likiwa limefichwa eneo la Marangu Mshiri nyumbani kwa Deogratius Mtui (30), ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Kirareni.

Kutokana na kukamatwa kwa magari hayo yakiwa mafichoni, polisi waliwakamata watu watatu kwa ajili ya mahojiano na kusaidia uchunguzi wakituhumiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari, miongoni mwao akiwamo mzee wa miaka 60, James Kyara.

Mtuhumiwa huyo ni mlinzi kwa watawa wa Ushirika wa Neema Kituo cha  Marangu, Christopher Kipuyo (29), ambaye ni fundi ving’amuzi vya televisheni, maarufu kwa jina la ‘madishi’ na mkazi wa mji wa Himo, Moshi Vijijini, pamoja na Mwalimu Deograitus Mtui.

Kipuyo licha ya kuwa fundi wa madishi, taarifa ya polisi inasema kuwa ndiye dereva aliyekuwa akifanya kazi ya kuyaendesha magari hayo kuyatoa huko yalikokuwa na kwenda kufichwa.

“Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na kuwepo kwa taarifa kuwa wamekuwa wakijihusisha na mtandao wa wizi wa magari. Jeshi la Polisi pia tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa mmoja ambaye ni Steven Makuri ili akamatwe,” inaeleza taarifa ya polisi.

Haika Mawala alikiri kukamtwa kwa gari hilo alipozungumza na JAMHURI na kueleza kuwa ni mali yake halali na hivi karibuni lilikamatwa na polisi wilayani Hai lakini waliliachia baada ya kujiridhisha kuwa analimiliki kihalali.

“Hilo gari ni mali yangu halali, na lilikwisha kukamatwa na polisi Wilaya ya Hai na kuachiliwa baada ya kujiridhisha kwamba ni mali yangu halali. Asante,” alisema kwa ufupi katika ujumbe mfupi wa simu alioutuma kupitia simu yake ya kiganjani.

Pamoja na Haika kudai kuwa gari hilo ni mali yake halali, taarifa mpya ambazo JAMHURI limezipata zinadai kuwa gari hilo ni miongoni mwa magari mawili ambayo yaliibwa katika Bandari ya Mombasa nchini Kenya na kuingizwa nchini kupitia njia za ‘panya’, likiwamo Toyota Harrier.

Mtoa taarifa aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake anasema gari hilo liliingizwa nchini likiwa na rangi nyeupe lakini lilipelekwa katika moja ya gereji za Arusha kubadilishwa rangi na kuwa nyeusi.

Kuhusu gari aina ya Honda lenye namba za usajili T 140 DAE ambalo ni miongoni mwa magari yaliyokamatwa na polisi Septemba 14, mwaka jana, mtoa taarifa wetu anadai gari hilo nalo ni la wizi.

JAMHURI limezungumza na Bosco Kyara ambaye ni mume wa Haika Mawala kuhusu madai ya wao kumiliki magari yanayodaiwa ya wizi, naye amekana madai hayo na kudai tuhuma hizo zinalenga kuchafuliana majina.

Amesema baada ya magari hayo kukamatwa na kuwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa miezi sita, walirejeshewa pamoja na nyaraka zao zote baada ya vyombo hivyo vya uchunguzi kujiridhisha kuhusu uhalali wa umiliki wao.

“Muulize huyo aliyekuletea hizo taarifa ni kwa nini Bosco amerudishiwa magari? Maana yake ni kwamba wamefanya uchunguzi wao wakajiridhisha kwamba tunayamiliki kihalali,” amesema.

Magari hayo yalikamatwa wakati Bosco akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi na  mwenzake Gabriel Mombuli wakituhumiwa kuwa vinara wa  mtandao wa wizi wa magari katika nchi za Kenya na Tanzania.

Bosco, mkazi wa Makuyuni, Himo na mwenzake mkazi wa Majengo mjini Moshi, walikamatwa Agosti 19, mwaka jana katika kizuizi cha polisi  Bomang’ombe Wilaya ya Hai eneo la Kwa Msomali wakiwa na gari linaloaminika kuwa la wizi aina ya Nissan Patrol V8 mali ya Kampuni ya Nisk Capital Limited ya Kenya.

Gari hilo ambalo namba zake halisi ni KCP 184 R lilikamtwa katika kizuizi hicho likielekea mkoani Arusha likiwa tayari limebandikwa namba bandia za Tanzania ambazo ni T 184 DEQ na liliingizwa nchini kupitia eneo la Holili, Wilaya ya Rombo, eneo linalopakana na nchi ya Kenya.

“Baada ya upekuzi uliofanywa ndani ya gari hilo kulipatikana stika ya Kampuni ya Bima ya Kenya ikiwa na namba halisi za usajili wa gari hilo ambazo ni KCP 184 R,” alisema Kamanda Issah katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Bosco na mwenzake walifikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro wakikabiliwa na mashitaka mawili, likiwamo la unyang’anyi wa kutumia silaha, shitaka ambalo kisheria halikuwa na dhamana.

Walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Devota Msofe na kusomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mkaguzi wa Polisi, Hawa Hamis, ambapo walikana mashitaka yao.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, wote kwa pamoja walidaiwa kuwa mnamo saa na siku isiyojulikana mwaka 2018 huko Jijini Nairobi, nchini Kenya kwa pamoja waliiba gari aina ya Nissan Patrol V8  lenye namba za usajili KCP 184 R mali ya Kampuni ya Nisk Capital Ltd.

Washitakiwa hao walidaiwa kabla na baada ya kuiba gari hilo walimtishia kumuua kwa bastola mtu mmoja aitwaye Luke Indechi Abboo, shitaka ambalo pia walilikana.

Katika shitaka la pili, washitakiwa hao walidaiwa kuwa mnamo Agosti 19, mwaka jana saa 1:30 usiku katika eneo la Kwa Msomali walikamatwa wakimilika mali inayoaminika kuwa ni ya wizi ambayo ni gari aina ya Nissan Patrol lenya namba za usajili KCP 184 R, lenye thamani ya shilingi milioni 200 mali ya Nisk Capital Ltd.

Walinyimwa dhamana baada ya mahakama kuelezwa na upande wa mashitaka kuwepo kwa taratibu za kisheria za kuwasafirisha washitakiwa hao kwenda nchini Kenya kujibu mashitaka ya wizi wa gari.

Hata hivyo taarifa ambazo JAMHURI linazo ni kwamba baada ya kusafirishwa hadi eneo la Tarakea, Wilaya ya Rombo na kukabidhiwa kwa maofisa wa Jeshi la Polisi upande wa Kenya, kwa sasa wapo huru baada ya kutotambuliwa kwenye gwaride la utambuzi nchini Kenya.

1202 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!