Wiki iliyopita nilihitimisha mada yangu kwa kuhoji iwapo msomaji unafahamu viwango vinavyotozwa kwenye Kodi ya Zuio. Nirudie kukiri kuwa hadi sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inacho kituo kimoja tu cha Elimu kwa Mlipakodi kilichopo Dar es Salaam. Baada ya kuandika makala hii nashawishika kusema TRA wanapaswa kufungua vituo vya aina hii kila wilaya nchini haraka inavyowezekana.

Wafanyabiashara wanaonipgia simu kuomba ushauri juu ya aina ya kodi zinazolipwa na utaratibu wa kulipa kodi ni wengi kwa kiwango kinachonieleza kuwa kuna shida kwenye biashara. Watu wanahitaji kuelimishwa. Tumeona viongozi wa kisiasa wakituhumiwa kulazimisha malipo ya kodi bila kufahamu hata aina ya kodi zinazopaswa kulipwa.

Sitanii, leo nataka kujikita katika eneo la Kodi ya Zuio na viwango vinavyopaswa kutozwa. Kwanza inapaswa kufahamika kuwa kuna aina mbili ya Kodi za Zuio. Kuna Kodi ya Zuio ya Kifedha na Kodi ya Zuio isiyo ya Kifedha.

Kodi za Zuio za Kifedha, mlipaji hawezi kuzitumia kulipa deni la kodi nyingine. Kwa mfano, mlipakodi hawezi akatumia PAYE kuziba pengo la kodi anayodaiwa au kurejeshewa kodi aliyolipa aliponunua bidhaa na huduma.

Kodi ya Zuio isiyotokana na Fedha, ni kiwango cha kodi ambacho mlipaji anahesabiwa kupitia huduma anayotoa ndani ya mwaka husika wa fedha kuwa huduma aliyotoa ndani yake inabeba kodi ya kiasi fulani. Ikihesabika na kutambulika, mlipaji anaweza kutumia hesabu hizo kulipa kuziba pengo la kodi aliyostahili kulipa kwa fedha.

Viwango vya Kodi ya Zuio

Kwa mujibu wa sheria ya Fedha, yapo maeneo yaliyoainishwa na viwango vya Kodi ya Zuio inayopaswa kutozwa. Viwango ni kama ifuatavyo na asilimia kwenye mabano:- Gawio kutoka Soko la Mitaji la Dar es Salaam kwa kampuni zilizoorodheshwa (5%) kwa wageni na wenyeji, gawio kwa kampuni iliyosajiliwa hapa nchini iwapo inamiliki hisa zipatazo asilimia 25 au zaidi katika kampuni inayotoa gawio (5%) kwa wenyeji na wageni (0%).

Gawio kutoka mashirika mengine ambayo shirika halina hisa (10%) kwa wageni na wazawa, riba (10%), mrabaha (10%), malipo yatokanayo na uwekezaji (15%) kwa wote na kodi ya pango (10%) wenye nyumba wazawa na asilimia 15 kwa wageni.

Huduma ya ujuzi (uchimbaji madini) ni (5%) kwa wazawa na (15%) kwa wageni, usafirishaji kwa ndege isiyomilikiwa na wazawa wageni wanalipa asilimia 5. Malipo ya bima kwa wazawa hawalipi kodi ila kwa wageni ni asilimia 5. Malipo yatokanayo na maliasili ni asilimia 15 kwa wote. Kodi ya huduma (5%) wazawa na (15%) wageni. Ada za wakurugenzi (wasio waajiriwa) ni asilimia 15 ya kiasi kilicholipwa kwa wote.

Mawakala wa fedha za mtandaoni kwa simu za mkononi wanapolipwa kamisheni zao wanapaswa kutozwa asilimia 10.

Malipo kwa ajili ya bidhaa zilizouzwa kwa serikali na taasisi zake, yanapaswa kukatwa asilimia 2 ya malipo yote kwa wazabuni wazawa, ila wageni hawakatwi kiasi hiki.

Sitanii, kama nilivyoeleza katika makala zilizotangulia, mlipaji anapaswa kujaza fomu maalumu ambazo zina nakala tatu. Nakala moja anapewa mlipwaji, nakala nyingine anabaki nayo na nyingine anaipeleka TRA na malipo ya Kodi ya Zuio yanalipwa ndani ya siku 7 tangu mwezi alipokata kodi hiyo unapokwisha.

Mpendwa msomaji, je, unafahamu kodi inayoitwa Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gains Tax) na inatozwa kwenye bidhaa zipi? Ni bidhaa mbili ambazo kwa njia moja au nyingine watu wengi hata wasiokuwa wafanyabiashara kwa nyakati tofauti wameshiriki kufanya biashara hiyo, lakini aghalabu ni wachache wanaoilipa kodi hii, ila ikumbukwe kuwa kutolipa kodi ni jinai.

Ni bidhaa zipi hizo na viwango vya kodi hii? Usikose nakala yako ya Gazeti la JAMHURI Jumanne ijayo kupata sehemu ya 25 ya mwendelezo wa somo hili muhimu katika mada ya Jinsi ya Kufanya Biashara Tanzania.

492 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!