Tunamuenzi vipi?

 

Kwanza, naomba niwapongeze sana vijana hawa; Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI Ndugu Deodatus Balile na Naibu Mhariri Mtendaji, Ndugu Manyerere Jackton, kwa tuzo za uandishi bora walizopata mwaka huu kwa kazi zao nzuri sana. Walistahili kabisa tuzo hizo. Naipongeza timu yote ya gazeti hili kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Kwenye makala zangu ninazoandika kwenye gazeti hili maarufu la JAMHURI wakati wa kumbukizi ya kuzaliwa na ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nimekuwa nikijaribu kuwakumbusha Watanzania wenzangu kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kazi kubwa sana na nzuri sana aliyoifanya nchini mwetu.

Alijitoa ‘mhanga’ akishirikiana na wenziwe kuikomboa nchi yetu kutoka kwa wakoloni na akaendelea kujitoa ‘mhanga’ kuwatumikia wananchi wanyonge wa taifa lake na kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuyakomboa mataifa mengine barani Afrika.

Kuhusu kifo chake, Mwalimu aliugua kwa muda mfupi na akatutoka bila Watanzania kutarajia siku ile ya Alhamisi tarehe 14, Oktoba 1999 kwenye kitanda cha Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza.

Miaka miwili kabla, yaani mwaka 1997 alipotimiza umri wa miaka 75, Taasisi ya Mwalimu Nyerere ilimfanyia Mwalimu sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake (Birthday Party), ingawa mwenyewe hakupenda kufanyiwa sherehe kubwa za aina hiyo. Siku ile Mwalimu alipanda ngazi kwenda jukwaani kwa kukimbia. Ni wazi kwamba alikuwa na nguvu na angeweza kuendelea kuishi. Lakini Mungu hakupenda!

Kwa wale waliokuwa na umri wa ufahamu watakumbuka jinsi hali ilivyokuwa siku ile baada ya Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kupitia vyombo vya habari, kututangazia umma wa Tanzania na dunia kwamba Mwalimu Nyerere ameaga dunia saa 4:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na saa 2:30 kwa saa za London, Uingereza!

Baada ya tangazo hili, Tanzania ilizizima. Wananchi waliokuwa majumbani, maofisini na mitaani waliangua vilio kumlilia Baba wa Taifa! Watanzania walikuwa wamefiwa na baba yao, wakashikamana kuomboleza. Salamu za rambirambi zilimiminika kutoka pande zote za dunia. Viongozi kutoka nchi mbalimbali waliwasili nchini kuhudhuria mazishi yake.

Jumatatu ya Oktoba 18, 1999 tulioishuhudia tunaiona kama jana. Saa 3:02 asubuhi ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam ikileta mwili wa Baba wa Taifa.

Wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo walilipuka kwa vilio vya uchungu baada ya kumuona Mama Maria Nyerere akiteremka kwenye ndege akibubujikwa machozi. Kwa siku tatu nzima wananchi walimiminika Uwanja wa Taifa (Uhuru) kutoa heshima za mwisho.

Alhamisi Oktoba 21 yalifanyika mazishi ya kitaifa jijini Dar es Salaam ambako viongozi; marais, mawaziri wakuu na wageni mbalimbali kutoka nchi za nje na wananchi kwa ujumla walihudhuria. Jumamosi ya Oktoba 23, Mwalimu akaziwa kijijini kwake Butiama.

Rais Mkapa aliongoza maziko yake yaliyoendeshwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakiwapo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais wa zamani wa Zambia Kenneth Kaunda, Mama Graca Machel aliyekuwa pembeni mwa Mama Maria akimfariji tangu kifo cha Mwalimu kitokee, watoto, wajukuu na wanafamilia wa Mwalimu, viongozi wengine mbalimbali na wananchi wengi kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Kifo cha Mwalimu kilitufadhaisha sana. Watanzania wema hawakuwahi kupata hata wazo kwamba iko siku Mwalimu Nyerere atafariki dunia! Wengi walijiuliza sasa Tanzania itakuwaje bila Mwalimu kuwapo? Wapo waliodhani kutatokea machafuko na kadhalika. Lakini haikuwa hivyo. Zimepita awamu zilizopita na sasa tuko Awamu ya Tano – tuko shwari.

Tuko shwari kutokana na misingi bora aliyoiweka Mwalimu katika ujenzi wa taifa letu. Tuko shwari kwa sababu marais wa awamu zote hadi sasa, kwa kadiri ya uwezo wao, wamejitahidi kutuongoza Watanzania kuilinda amani yetu. Watanzania tusiichezee amani yetu. Tuendelee kuidumisha na kuilinda kumuenzi Baba wa Taifa letu, kwa manufaa yetu na ya vizazi vijavyo kwa kutenda yale aliyotuelekeza Mwalimu.

Rais wetu mpendwa, Dk. John Magufuli wakati wote anatukumbusha kwamba Watanzania tuvumiliane ili tudumishe amani yetu.

Pamoja na hayo, Mwalimu Nyerere katika kipindi chake chote cha uongozi kabla na baada ya nchi yetu kupata Uhuru alikuwa kila wakati akizungumza na wananchi kwa njia ya hotuba na kuandika machapisho mbalimbali vikiwemo vitabu vikubwa na vidogo.

Kwa hotuba hizo na maandishi yake, Mwalimu alikuwa akitufundisha Watanzania kuishi kindugu kwa upendo, amani, utulivu, mshikamano, kwa kujitegemea na kujiletea maendeleo yetu wenyewe.

Kila alipokuwa akitoa hotuba tulikuwa kama tuko darasani tukisikiliza alichokuwa akitufundisha. Wakati wote tulikuwa tukipokea mafunzo yake kwa makofi, vigelegele na vicheko alipotuchekesha, kuonyesha kukubaliana na kufurahia alichokuwa akisema. Hadi leo hii, miaka 20 bila yeye kuwapo, hotuba zake haziishi hamu masikioni mwetu, hazijachakaa hata kidogo na zinaendelea kuwa ni za wakati ule, wakati huu na wakati ujao pia.

Awamu hii ya tano chini ya Rais Magufuli, mwana halisi wa kisiasa wa Mwalimu Nyerere, ameweka utaratibu mzuri. Kila siku chombo cha habari cha Serikali, TBC, kinachoongozwa na kijana wa wakati huo Ndugu Dk. Ayoub Ryoba, hutoa hotuba za Mwalimu alizozungumzia juu ya mambo mbalimbali. Tunamshukuru sana Rais wetu na TBC kwa hilo. Watanzania hasa vijana wajizoeze kusikiliza vipindi vya ‘Wosia wa Baba’ vinavyorushwa TBC, ITV na kadhalika, ili wapate hii hazina ya maneno aliyowahi kuyasema Baba wa Taifa.

Ni mengi aliyowahi kusema Mwalimu Nyerere kwenye hotuba zake nyingi alizotoa kwa lugha ya Kiswahili. Zipo zaidi ya hotuba 3,000 zilizowahi kurekodiwa ukiacha zile ambazo hazikurekodiwa alizokuwa akizungumza na wananchi hapa na pale wakati akizunguka nchi nzima kuhamasisha maendeleo. Pia alitoa hotuba nyingine nyingi kwa lugha ya Kiingereza kwenye mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Kwa kuwa mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani Udiwani, Ubunge, Uwakilishi na Urais, nitaandika machache juu ya aliyosema Mwalimu kuhusiana na uchaguzi wetu ili tutafakari miaka 20 bila yeye kuwapo tumemuenzi vipi na tutamuenzi vipi Mwalimu katika hilo na mengine?

Akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Nyerere alitoa hotuba ndefu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa uliofanyika jijini Dar es Salaam, Agosti 16, 1990. Hotuba ile iliyopewa jina la “WASIA WA MWALIMU NYERERE KWA CCM” ilizungumzia mambo mengi yaliyohusu mwenendo wa shughuli za Chama Cha Mapinduzi wakati ule, ikiwemo chaguzi. Maneno hayo kwa sasa yanahusu pia mwenendo wa vyama vyote vya siasa.

Katika hotuba hiyo Mwalimu alisema hivi: “…Lazima niseme pia kwamba siku hizi kuna watu wengi mno ambao huingia katika chama na kugombea nafasi za uongozi kwa matumaini ya kupata fedha na vyeo kwa faida zao wenyewe. Siku hizi watu wanatazamia kulipwa posho na ujira kwa karibu kila shughuli ya chama au ya uongozi. Ni shughuli chache sana zinazofanyika kwa misingi ya kujitolea kutokana na imani katika shabaha za chama. Moyo wa kujitolea umefifia mno. Katika hali kama hiyo ni vigumu sana kuwapata viongozi wenye moyo wa kuwatumikia wenzao…Uongozi na kazi katika chama unahitaji ushahidi kidogo wa kutaka kutumikia chama na wananchi wenzetu… ”

Shabaha za chama chochote cha siasa ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo. Je, ni wagombea wangapi wanaogombea uongozi kwa shabaha hiyo aliyoitaja Baba wa Taifa ya kujitolea kuwatumikia wananchi kwa dhati kabisa bila kujali watakachopata wao?

Kwenye kipindi kuelekea uchaguzi wa wabunge na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu mwaka 1995, Mwalimu aliombwa na Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa wakati huo, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, kwenda kuhudhuria Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kusaidia kutoa mawazo yake juu ya uchaguzi wa Rais uliokuwa ufanyike.

Mwalimu Nyerere alisema: “Teueni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya wananchi, acha matarajio yako wewe. Tupeni kiongozi atakayekidhi matarajio ya Watanzania. Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Wanataka uongozi uyafanye mengi tu. Nitataja manne.

Watanzania wamechoka na rushwa. Wajumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu ya CCM watakumbuka nimepigia kelele rushwa nikiwa ningali Mwenyekiti wao hapa hapa Dodoma. Nilipiga kelele kiasi cha Waziri Mkuu wa wakati huo (Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba) alikwenda kwa Rais; alikuja kwako Ndugu Rais kuja kutoa hati yake ya kujiuzulu. (Makofi). Sasa hivi hali ya rushwa ni mbaya zaidi nchini. Wasaidieni wananchi ku-deal (kushughulika) nayo.

Mgombea mtakayemteua lazima tumtetee, wote tumtetee. Lakini inatakiwa ukiulizwa swali, huyu atatusaidia kupiga vita rushwa? Jibu litoke ndani ya roho yako si mdomoni tu kwamba; ndiyo anaweza.” (mwisho wa kunukuu).

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM walipiga makofi sana Mwalimu aliposema Waziri Mkuu wa wakati huo alikwenda kwa rais kutoa hati yake ya kujiuzulu. Waziri Mkuu huyo alitaka kujiuzulu kwa sababu aliichukia sana rushwa kama alivyoichukia Mwalimu. Bila shaka alipoona hapati ushirikiano wa kutosha katika kukomesha vitendo vya rushwa, aliamua bora ajiuzulu.

Je, wajumbe wale waliopiga makofi ya nguvu Mwalimu alipozungumzia jambo hilo, ni wangapi baada ya kutoka kwenye mkutano ule waliyachukua maneno aliyoyasema Mwalimu na kwenda kuyafanyia kazi kuwaelimisha na kuwashawishi wananchi wa maeneo waliyotoka waache kutoa na kupokea rushwa, waelewe madhara ya rushwa? Wajumbe wale walichukua hatua gani kutokomeza rushwa nchini?

Tangu wakati ule imepita zaidi ya miaka 20. Rushwa iliendelea kushamiri na kuota mizizi. Rais wa Awamu hii ya Tano sasa ndiye anafanya kazi kubwa kujaribu kuitokomeza. Rais huyu anahitaji msaada wa viongozi wa juu – waziri mkuu, mawaziri, wabunge, wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za CCM na vyama vya siasa, wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wananchi wa kawaida, kwa sababu Tanzania ni yetu sote na rushwa ni adui wa haki za Watanzania wote.

La pili, alilolisema Mwalimu lilihusu umaskini wa watu wetu, alisema:

“Nchi yetu hii ni ya maskini, wakulima wetu, wafanyakazi wetu maskini. Nchi hii bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao wote ni watu maskini. Nchi hii haijawa nchi ya matajiri. Chama hiki (CCM) hakijawa chama cha matajiri. (Makofi). Tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wa watu wetu. Tushughulike kwa dhati na matatizo ya wananchi; ya hali yao ya uchumi, hali yao ya viwandani, hali yao ya mashambani, hali yao ya shuleni, hali yao ya hospitalini.

Tunataka tuwe na uhakika kwamba mtatuteulia mtu ambaye ukiulizwa swali, mtu huyu anajua kwamba nchi hii bado ni nchi ya maskini, nchi hii bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi? Uweze kumjibu yule anayekuuliza hivyo, umjibu kwa moyo wa dhati kwamba: Naam! Huyu anatambua hivyo. (Makofi). (mwisho wa kunukuu).

Hili la pili alilolisema Mwalimu nalo bado linamuumiza kichwa Rais wa Awamu hii ya Tano. Inavyoelekea yeye alikuwa ni miongoni mwa Watanzania waliomuelewa Mwalimu vizuri sana. Je, ni viongozi wangapi, wabunge wangapi, wajumbe wangapi wa mikutano ya ngazi za juu na chini waliomuelewa Mwalimu na wanaomuelewa rais wetu waliokuwa tayari na leo wako tayari kwa dhati kabisa kuyafanyia kazi hayo yaliyosemwa?

Pamoja na makofi yaliyokuwa yakipigwa kwenye mikutano kila Mwalimu alipozungumza, wajumbe wengi walitoka na kwenda makwao kila mtu kuhangaikia ‘ka muhogo kake’ kama alivyowahi kusema nguli wa uandishi Jenerali Ulimwengu. Walikuwapo waliotumia nafasi zao kujipatia mali na kujilimbikizia kwa njia halali na haramu bila kujali umaskini wa Watanzania wenzao waliowazunguka.

La tatu alilosema Mwalimu lilihusu udini, na la nne lilihusu ukabila. Mwalimu Nyerere alieleza jinsi ambavyo watu wa Uganda na Kenya walivyokuwa wakijuana kwa makabila yao – huyu Mkikuyu, huyu Mjaluo, huyu Mluiya, na kadhalika. Watu wa Tanzania popote walipokuwa wakiwa na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo, walikuwa kabisa hawajulikani makabila yao.

Lakini hali hiyo ya kutokuwapo udini na ukabila taratibu ilianza kubadilika, Watanzania walianza kuwa na udini na ukabila na kutishia umoja na mshikamano uliokuwa umejengeka. Mwalimu aliwaeleza wajumbe wa mkutano ule kwamba Wazungu (Waingereza) waliotutawala walikuwa wanatafuta kuungana na kushirikiana na mataifa mengine ya Ulaya. Wajerumani na jeuri yao yote waliungana kuwa taifa moja, waliona vitaifa vyao vile ni vidogo mno, wakaungana. Akawashangaa Waswahili wenye vi-nchi vidogo vidogo wanazungumzia makabila!

Mwalimu akasisitiza kwamba anataka wajumbe watuchagulie mtu ambaye anajua huko kwenye udini na ukabila ni hatari na upumbavu.

Akakumbusha kwamba wenzetu majirani sisi ndio ulikuwa mfano wao. Walikuwa wakisema mbona wenzetu Watanzania hawazungumzii ukabila, sisi kwa nini tunazungumzia ukabila?

Hivi sasa nchini mwetu, haya mawili ya udini na ukabila yanafifia. Jambo la udini nadhani linaanza kupotea kutokana na kizazi kipya kuwa na uelewa mzuri zaidi wa madhara ya kukumbatia udini. Lakini yawezekana pia kwamba kizazi hiki kipya si waumini wazuri sana wa dini zao!

Wengi hawaendi makanisani wala misikitini kusali ipasavyo. Pia, vijana wa Kitanzania siku hizi wanakimbizana na kuhangaikia maisha yao, hawana muda wa kufikiria kubaguana kutokana na kabila. Wale wenye kuingia mitandaoni na huko mitaani wanataniana kuhusu makabila na si kubaguana.

Lugha ya Kiswahili nayo imesaidia sana kuondoa ukabila nchini. Hakuna Mtanzania asiyejua Kiswahili japo kwa kiasi tu na Watanzania tumefaulu kuambukiza majirani zetu sasa nao wanaongea Kiswahili. Afrika na dunia nao wanataka kujua Kiswahili!

Mwalimu alimalizia hotuba yake ile kwa kusema: “Ndugu Mwenyekiti, ndugu wananchi, mimi mliniomba nije kusaidia, nilikubali kuja kusaidia. Kwa nini? Kwa sababu hiyo hiyo, tunataka nchi yetu ipate kiongozi safi. Kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM! (Makofi na vigelegele). Ninyi wapiga kura mnaweza kutupatia kiongozi safi kwa kura zenu. Basi tupatieni kiongozi safi kwa kura zenu!

Asanteni. (Makofi na vigelegele).” (mwisho wa kunukuu).

Bila shaka wengi tunakumbuka jinsi ambavyo maneno aliyoyatamka Mwalimu mwanzo wa hotuba yake kwamba: “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM watatafuta nje ya CCM,” na haya ya mwisho: “Kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM”, yalivyotumika kishabiki kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Maneno haya ya Mwalimu yalikuwa na ujumbe mzito zaidi ya ushabiki. Wakati mwingine, baadhi ya mambo aliyoyasema Mwalimu yamekuwa yakipindishwa na kutolewa tafsiri isiyo sahihi na watu wenye ajenda zao.

Kwa maoni yangu, Mwalimu aliyasema hayo kwa sababu Chama Cha Mapinduzi kilikuwa kimepoteza mwelekeo na ndiyo sababu ya wananchi kuanza kutaka mabadiliko ya hali iliyokuwapo. Mwalimu alitahadharisha kwamba Watanzania watayatafuta nje ya CCM endapo chama hicho hakitabadilisha mwenendo wake.

Kwamba kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM, Mwalimu alikuwa anaamini kabisa kwamba Chama Cha Mapinduzi ni chama madhubuti chenye misingi bora na imara ukilinganisha na vyama vingine vilivyokuwa vichanga wakati huo. Kwa maana hiyo, kiongozi safi asingeweza kutoka nje ya chama madhubuti na kikongwe kilichoenea nchi nzima – CCM.

Maneno hayo aliyoyatoa Mwalimu mwaka 1990, 1995 na miaka mingine yote, yalikuwa ya kutufundisha tunatakiwa tuweje na tuchague viongozi wa namna gani kwa manufaa yetu sote na ya nchi yetu. Mgombea anatakiwa ajichunguze kama kweli ana ‘udhu’ na ana kidhi vigezo vya kuwa kiongozi bora.

Mpiga kura naye anawajibika kumchunguza mgombea na kujua kama anastahili kuwa kiongozi safi – kiongozi asiye na doa la rushwa; anayejali na anayetaka kutumia nafasi anayogombea kuboresha maisha ya wanaomchagua, si maisha yake pekee; asiyebagua wananchi wenziwe kwa misingi ya dini, ukabila ama ubaguzi wa aina yoyote ile; na kiongozi ambaye yuko tayari kujitolea kwa hali na mali kuwasaidia wananchi anaowaongoza.

Mwisho, katika hotuba yake aliyoitoa Kilimanjaro Hotel kwa lugha ya Kiingereza wakati akiitafutia Taasisi ya Mwalimu Nyerere michango ya fedha za kuiendesha, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo: “There are many good and honest people who believe that those ideas which in my country are associated with my name are now, dead and should be properly buried. You will not be surprised to hear that I disagree! Great ideas do not die so easily, they continue nagging and every human society in history ignores them in its own peril…”

Tafsiri yangu isiyo rasmi: “Wapo watu wazuri na waaminifu wanaoamini kwamba hizo fikra katika nchi yangu ambazo zinahusiana na jina langu hivi sasa zimekufa na inabidi zizikwe rasmi. Hamtashangaa kusikia nikisema kwamba sikubaliani na hiloFikra nzito hazifi kirahisi, zinabakia zikikera, na kila jamii ya binadamu katika historia inajipalia makaa kwa kuzipuuza…

Naam, hadi leo miaka 20 bila yeye kuwapo, kila tukisikiliza hotuba zake zilizotokana na fikra zake nzito bado Mwalimu yupo, bado maneno yake yanatugusa, yanagusa mambo yaliyopita, yaliyopo sasa, na kuendelea kugusa mambo yajayo hadi mwisho wa dunia! Tunajipalia makaa tukizipuuza.

Maneno ya Mwalimu niliyoyazungumzia yanagusa juu ya viongozi bora na namna ya kuwapata. Tujiulize, tangu Mwalimu atuusie hayo na katika miaka hii 20 bila yeye kuwapo, tumemuenzi vipi kwa kuzingatia maneno yote aliyowahi kuyasema kwa manufaa ya taifa letu?

Tumemuenzi vipi? Tunamuenzi vipi na tutamuenzi vipi Baba wa Taifa katika uchaguzi wetu ili tupate viongozi bora watakaoleta maendeleo ya haraka kwa wanyonge na maendeleo endelevu kwa taifa letu?

Majibu yako kwetu sote Watanzania.

ZIDUMU FIKRA NZITO ZA BABA WA TAIFA LETU, MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE!

 

Mwandishi wa makala hii, Anna Julia Chiduo-Mwansasu

(Bibi Mstaafu) ni Katibu Muhtasi mstaafu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Anaishi Kivule Yangeyange, Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0655774967

1341 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!