Waza au fikiri kwa kutumia picha kubwa. Ukiwaza kwa kutumia picha kubwa ni sawa na kuitabiri kesho. Kuiona kesho wakati bado unaishi leo. Watu waliofanikiwa wanajiona baada ya miaka mitano au kumi watakuwa wapi.

Je, wewe umewahi kujiuliza tarehe kama ya leo mwakani utakuwa umepiga hatua gani? Au kila siku kwako ni bora liende? Anza kufikiri kwa kutumia picha kubwa. Mahatma Gandhi aliwahi kusema: “Ulivyo sasa au leo ni matokeo ya kile ulichokiwazia siku za nyuma.”

Miongoni mwa watu wanaofikiri kwa kutumia picha kubwa ni wasanifu majengo. Hawa kabla ya ujenzi wowote kuanza hutengeneza nyumba inayotarajiwa kujengwa kwenye karatasi ngumu au maboksi. Hawa huliona jengo zima hata kabla ya ujenzi kuanza.

Unapojenga picha kichwani mwako na kuiweka katika uhalisia, unauweka ubongo wako katika hali ya kufanya kazi ili kufikia maono ya picha yako. “Kile unachokiwaza na kukiweka kwenye akili yako ndicho utakachoweza kukipata,” anasema Napoleon Hill.

Kumbe tukianza kutumia kanuni hii ya picha tutafika mbali. Kwa mfano, kama unataka kumiliki gari la aina

fulani, tafuta picha yake, bandika maeneo mbalimbali ambako utakuwa unaliona mara kwa mara, kwani maisha yetu yanafuata sana taswira ambazo ziko mbele yetu tunazoziangalia mara kwa mara.

Nakumbuka nikiwa kidato cha sita mwalimu wangu wa somo la elimu kumbakumba (GS) alizoea kutuambia, “Fumba macho.” Baadaye alituuliza, “Fulani unaona nini?” Hapa alitaka kutujengea utamaduni wa kujenga picha.

Wakati nasoma kidato cha nne nilibandika kikaratasi kwenye dawati langu kuhusu maksi nitakazopata kwenye mtihani wa taifa, Mungu si Athumani nilichokuwa nimekiandika ndicho nilichokipata. Kanuni hii ya kujenga picha inafanya maajabu makubwa.  “Anza na mwisho katika fikra zako,” anatukumbusha Stephen Covey.

Kanuni hii unapoanza kuifanyia kazi unaweza kuonekana wa tofauti sana kwa marafiki, ndugu au wazazi wanaweza kukucheka, lakini kuna msemo usemao: “Fanya mambo kama kichaa.”

Bandika picha kwenye sehemu maalumu kama vile kioo chako kwa wale wanawake wanaopenda vioo, bandika ukutani na sehemu utakapoweza kuona picha ya kitu unachotaka kukipata au kuwa.

Mojawapo ya faida ya kujenga picha au kutumia kanuni hii ni kwamba kila unapoiona picha inakukumbusha kwamba kuna kitu unadaiwa, hivyo hauna budi kuweka bidii ili ufanikishe ndoto zako. “Hauwezi kuzaa ndoto ambayo kwanza haujaiwazia. Lazima uiwazie ndani mwako kupitia macho ya imani kabla ya kuitoa nje. Badili kile unachokiona, utabadili kile unachokizalisha,” anasema Joel Osteen.

Kwenye utabiri wa hali ya hewa utaambiwa mambo yanayohusu kesho, mwezi ujao, mwaka ujao au hata miaka mitano ijayo. Hiki ni kitu cha kushangaza ambapo hayo yote hutokea.

Wewe pia unahitaji kuitabiri kesho yako. Ukitaka kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa unahitaji kutabiri kesho yako. Sifa mojawapo ya watu waliofanikiwa ni kuwa na maono makubwa, yaani kujiona wapo katika hali fulani ambayo wanaitarajia.

Wewe pia unahitaji kufikiri baada ya miaka mitano au kumi utakuwa mtu wa namna gani. Hii itakupa motisha ya kufanya jambo fulani kila siku ili usogee kule unakotaka kufika. Hellen Keller pia ni mwandishi gwiji wa karne ya ishirini, pamoja na kuwa kipofu akiwa na miaka miwili aliwahi kusema: “Ni bora kukosa kuona kuliko kukosa kuwa na maono.” Kama utabiri wa hali ya hewa unavyofanyika leo, wewe pia unahitaji kutabiri maisha yako ya kesho leo hii. Jione kama mtu ambaye tayari amekwisha kufanikiwa kufanya jambo fulani, hii itaifanya akili yako kupambana na kuhakikisha jambo hilo linafanyika. Hauwezi kufika kimwili kule unakokwenda kabla haujafika kiakili. Peleka mawazo yako kule unakofikiria kufika na lazima utafika.

“Nilimwambia baba yangu kwamba siku moja tutakuwa matajiri na tutakuwa na nyumba kubwa, naye alisema: ‘Mwanangu jambo hilo haliwezekani.’ Leo ninamiliki kile nilichomwambia baba yangu,” anasema Cristiano Ronaldo, mchezaji maarufu wa mpira wa miguu. Jifunze kuiona kesho yako, jifunze kuitabiri kesho yako.

Mwandishi wa safu hii anapatikana kwa simu: 0764145476

By Jamhuri