Tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, utoaji wa mimba zisizopangwa na uzazi usiofuata kanuni za uzazi wa mpango umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Matumizi hayo ya njia za uzazi wa mpango yameleta tija katika familia nyingi, japo mimi kama daktari nakiri kuwa bado elimu zaidi inahitajika ili wazazi wapate uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya njia za uzazi huo.

Hata hivyo, suala la matumizi ya njia za uzazi wa mpango linaweza kuibua maswali kadhaa na kusababisha mdahalo kwenye jamii yetu, maswali hayo wakati mwingine huwa yanaelekezwa kwa wahudumu wa afya. Baadhi ya maswali hayo ni kama vile:

Je, matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango zinazingatia usawa wa kijinsia?

Njia hizi za uzazi wa mpango ni rafiki kwa afya ya mtumiaji? (hasa mwanamke kama ilivyozoeleka).

Maswali mengi yanayohusiana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango huwa yanalenga maeneo hayo mawili, lakini leo nitajikita kueleza kuhusu usawa wa kijinsia.

Tendo la ndoa, na hasa linalofanywa bila kutumia kinga, mara nyingi linakuwa na matokeo mawili. Matokeo haya  ni magonjwa mbalimbali ya zinaa na mimba. Lakini hii haina maana kwamba kila washiriki wanapofanya tendo la ndoa bila kutumia kinga wanapata matokeo hayo.

Wanaweza wakapata moja tu ya mambo hayo, au wasipate kabisa. Itategemea tu wapo hatarini kiasi gani kupata moja ya matokeo haya au yote kwa pamoja.

Suala la kujikinga au kuzuia magonjwa ya zinaa imezoeleka kuwa ni jukumu la wote wawili, yaani mwanaume na mwanamke, lakini suala la kuzuia mimba na kupanga uzazi wengi wanadhani kuwa ni jukumu la mwanamke.

Ndiyo maana inapofikia kwenye suala la kupanga uzazi, mzigo wote wa kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi unabaki kwa mwanamke. Nina imani kuwa wengi wanadhani wanaume hawana njia zao za uzazi wa mpango, la hasha!

Wanaume wanazo njia za kupanga uzazi, wakizitumia kwa ufasaha zinaweza kuleta matokeo chanya hata kama wake zao wasipotumia njia hizo.

Hivyo nina imani wanaume kuanzia sasa wataanza kuzingatia njia za uazazi wa mpango kwa lengo la kuwasaidia majukumu wanawake wenu kama nitakavyoeleza.

Kuchunga kalenda, ni njia rahisi na ya asili ambayo mwanamke anaweza kuitumia katika kupanga uzazi, lakini njia hii haionekani kutumiwa na wanawake wengi kutokana na wengi kusema ni vigumu kuichunga.

 Wanawake wengi hutumia njia mbadala kama vile vidonge, vitanzi, sindano na vinginevyo. Kisayansi, pamoja na utendaji kazi wa njia hizi, bado zimeonekana kuleta madhara mengine ya kiafya na madhara haya yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu. 

Kuvurugika kwa mfumo wa homoni na mzunguko wa hedhi, hedhi iliyopitiliza au kukosa kabisa hedhi, maumivu ya tumbo, kiuno na mgongo wakati wa hedhi na kupata uzito wa mwili uliopitiliza ni baadhi tu ya matatizo ya kiafya ambayo wanawake wengi huyapata kutokana na matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango, hasa kwa muda mrefu.

Nadhani watu wanapaswa kujua kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango si jukumu la mwanamke pekee, hapana, ni jambo linalobeba usawa wa kijinsia.

 Baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo mwanaume anaweza kuzitumia ambazo ni rafiki kwa jinsia ya kiume ni pamoja na; matumizi ya kondomu, njia ya kutoa mbegu za kiume nje wakati mwanamke akiwa kwenye siku za kushika mimba, au ile inayohusisha upasuaji mdogo kwa lengo la kufunga mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ili zisisafiri kwenda ukeni wakati wa tendo la ndoa. Njia hii kitaalamu inaitwa ‘vasectomy’.

By Jamhuri