pg1

Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM linaundwa na wajumbe sita ambao ni wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu Taifa wa chama hicho. Nao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Makamu Mwenyekiti mstaafu (Tanzania Bara), Pius Msekwa (Katibu); Benjamin Mkapa (Mjumbe); Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour; na Waziri Mkuu mstaafu na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), John Malecela.
Habari kutoka vyanzo vya kuaminika zinasema Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa, tayari ameshaandika barua kwenda kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Rajab Luhwavi, akimtaka aitishe kikao cha Baraza hilo.
Kwa maelekezo hayo, Baraza la Ushauri la Wazee linatarajiwa kuketi wiki hii, Juni 25.


Kwa maelekezo ya Msekwa, waalikwa kwenye kikao hicho, ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Dk. Edward Hoseah, na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman.
Haijajulikana sababu za kualikwa kwa wakurugenzi hao wanaoongoza taasisi nyeti, lakini kuna tetesi kwamba watatakiwa kutoa maelezo, na hata kuthibitisha, tuhuma za kuwapo vitendo vya rushwa miongoni mwa wagombea; huku mlengwa mkuu akibaki kuwa Lowassa.
Kufanyika kwa kikao hicho cha keshokutwa kumekuja baada ya kikao cha awali cha Baraza hilo kugubikwa na utata; hasa baada ya baadhi ya wajumbe kuona mtu aliyekamiwa ni Lowassa. Kikao cha awali kikiwa na wajumbe watatu pekee, kiliandaa “Tamko la Wazee”; lakini baadaye likawekwa kapuni baada ya mjumbe mmoja kuwasili na kutoa hoja za kutokubaliana na uamuzi huo. Hoja kubwa ilikuwa kwamba tamko kama hilo lingekuwa na maana zaidi endapo lingekuwa limetolewa na wajumbe wote wanaounda Baraza hilo.
Msukumo wa Mwenyekiti Rais Kikwete


Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa Mwenyekiti Rais Kikwete, kwa makusudi, amenuia kuwatumia wazee hao kutoa tamko ambalo atalitumia kama ngao kumng’oa Lowassa na wagombea wengine wanaotajwa kuwa ni hatari kwa umoja na mshikamano wa chama.
Inaelezwa kwamba Rais Kikwete anaona itakuwa kazi ngumu na ya lawama kwake, kuongoza mpango wa kulikata jina la Lowassa; hasa kutokana na urafiki wao wa siku nyingi, na hofu ya kisasi endapo mbunge huyo wa Monduli atakuwa rais.
“Anachofanya mwenyekiti ni kuhakikisha anatumia ‘ushauri’ wa wazee kama ngao atakayoitumia kwenye vikao vya CC na NEC kumkata Lowassa,” kimesema chanzo chetu.
Chanzo hicho kimeongeza kwamba kwa bahati nzuri wazee wameshang’amua mpango huo, na ndiyo maana kikao cha awali hakikutoka na tamko la moja kwa moja ambalo Msekwa na Malecela walikamia litolewe kwa umma.
Inaelezwa kuwa mbinu nyingine inayokwenda sambamba na mpango huo ni hii ya kuwapo utitiri wa wagombea urais.


“Hawa wagombea urais hujiulizi kwa nini mwaka huu wamekuwa wengi? Iweje wanachama 40 au zaidi wajitokeze kuwania nafasi hii?
“Hili limewezekana kwa sababu kumewekwa mapandikizi. Ndiyo maana unaona wapo wanaotangaza nia hawazunguki mikoani kusaka wadhamini, lakini baada ya siku chache utasikia wanarejesha fomu. Hao wanatafutiwa wadhamini na vyombo maalum,” kimesema chanzo chetu.
Kwenye mpango huo, imekusudiwa kuwa majina mengi ya wagombea “wa kweli” yatakatwa pamoja na yale ya mapandikizi, na mwishowe watakaolalamika ni wagombea “wa kweli”, akiwamo Lowassa.
“Watafanya hivyo ili Lowassa akilalamika, aulizwe ‘mbona wengine waliokatwa hawalalamiki, iweje wewe tu ndiye ulalamike’. Ataulizwa, hivyo na mwisho itaonekana yeye ndiye mwenye nongwa,” kimesema chanzo chetu.
Wakuu wa vyombo vya usalama walioitwa kazi yao kubwa wanayotarajiwa kuifanya ni kuanika “madudu” ya wagombea wote, lakini jicho la pekee likielekezwa kwa Lowassa.
Mnyukano ndani ya Baraza la Wazee


Mnyukano ndani ya Baraza la Wazee ni jambo lililo wazi. Dk. Salmin amekuwa hahudhurii vikao hivyo kutokana na kudhoofu kwa afya yake.
Malecela anatajwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Lowassa, ukweli ambao unathibitishwa na kauli zake za mwaka jana pale alipoita waandishi wa habari na kumpongeza Paul Makonda, kwa kitendo chake cha kumtukana Lowassa.
Hata hivyo, baadhi ya mambo yenye kuzua utata ni kumuona Malecela akishiriki vikao vya Baraza la Ushauri la Wazee kujadili wagombea, akiwamo mtoto wake, Dk. Mwele Malecela, ambaye ni miongoni mwa waliochukua fomu kuwania urais.


Dk. Mwele ni miongoni mwa wanaodhaniwa kuwa hawana nia ya dhati ya kuwania urais, lakini yupo ili jina lake likiondolewa, basi Malecela aweze kusema: “Lowassa analalamika nini, mbona hata mimi mtoto wangu jina lake limekatwa”.
“Mzee Malecela hawezi kutenda haki kwa wagombea wengine. Huwezi kutarajia asifu wagombea wengine zaidi ya mtoto wake. Lakini ni huyu huyu ambaye ameshaonesha msimamo mkali dhidi ya wagombea wengine, hasa Lowassa. Kiungwana ilitakiwa asihudhurie kikao hiki kinachokuja,” kimesema chanzo chetu.
Kwa upande wake, Mzee Mwinyi anaonekana kutokuwa na uamuzi wa moja kwa moja. Mara zote amekuwa akiwasikiliza wajumbe kabla ya kufikia uamuzi.


Wanatoa mfano wa kikao kilichopita ambako wazee wawili hawakudhuria, na wa nne alipoingia ukumbini akakuta tayari limeshaandaliwa tamko la kulaani “matumizi ya fedha na rushwa” ambalo kimsingi lilimlenga Lowassa.
Hata hivyo, mmoja wa wazee alipinga mpango huo akisema ilikuwa vyema wajumbe wote, hasa wanaoonekana kuutaka urais kwa dhati, wakajadiliwa taarifa zao. Hofu ya mzee huyo ilikuwa kwamba kutamka tu fulani ni mtoa rushwa bila kuwa na maelezo ya kujitosheleza, ni sawa na kufanya kazi kama ya magazeti ambayo yamekuwa yakiimba wimbo huo huo bila ushahidi wa moja kwa moja.


“Sisi hatuwezi kufanya kazi kama magazeti yanavyofanya. Tutoe tamko linalofanana na yanayoandikwa kwenye magazeti? Nadhani si vizuri,” amekaririwa mmoja wa wazee hao akiwaeleza wenzake.
Wakati Lowassa akiandamwa, habari zilizo wazi zinaonesha kuwa karibu watia nia wote wamekuwa wakigawa fedha kwa wanachama wanaowadhamini huko mikoani na hata kuwalipa waendesha bodaboda.
Rais mstaafu Karume hakuhudhuria kikao kilichopita. Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na wasaidizi wake zimesema atafanya kila analoweza ili ahudhurie kikao cha Juni 25.
Wazee wanaotajwa kuwa wako mbele kubeba ajenda ya Rais Kikwete ya kumng’oa Lowassa ni Malecela na Msekwa.


Wakati Rais Kikwete akipambana kuhakikisha wazee wanakuwa kivuli cha kumwezesha kuchukua “uamuzi mgumu”, taarifa za awali zinasema baadhi ya wazee hao wanapendekeza wagombea urais waachwe wapambane ili hatimaye kura ziamue mshindi.
Wanaitilia mkazo hoja hiyo kwa kigezo kuwa Sekretarieti na Kamati ya Maadili ya CCM zilichelewa kuwachukulia hatua baadhi ya wanachama tangu mwaka 2010.
Wanaamini kuwa idadi kubwa ya waomba urais wana dosari ambazo kama chama kitasimama kwenye misingi iliyozoeleka ya kuwapata wagombea wake, wengi watakosa sifa.
Watu walio karibu na Rais Kikwete wanasema hata yeye alidhani njia hiyo ingekuwa sahihi, lakini hofu yake ni kwamba kufanya hivyo maana yake ni kumwambia Lowassa ajiandae kuapishwa.
“Mwenyekiti hataki lawama. Aliona kukwepa lawama njia ya kuwaacha washindane kwa kura ingekuwa nzuri.


“Lakini baadaye akaja na wazo la kulitumia Baraza la Ushauri akiamini watatoa tamko ambalo maudhui yake yatakuwa yamemlenga moja kwa moja Lowassa, na wahakikishe linasambazwa kwenye vyombo vya habari.
“Anaamini kwa kufanya hivyo kazi yake itakuwa nyepesi. Atatumia hoja ya ‘wazee wameshauri’ ili kumdhibiti Lowassa. Hapo atakuwa amefanikiwa mambo makuu mawili, kwanza ni kumpata rais anayemtaka, na pili ni kukwepa lawama. Hii ndiyo sayansi itakayotumika.
“Mambo yakienda kama ilivyokusudiwa, keshokutwa (baada ya kikao cha Baraza la Wazee) utasikia ‘kauli ya wazee’ ambayo mlengwa ni Lowassa,” kimesema chanzo chetu.
Chanzo hicho kinasema kwamba wazee wameshautambua mpango wa Rais Kikwete wa wao kutumika kubeba lawama, na kwa maana hiyo inawezekana kukawapo ugumu wa kutolewa kwa tamko lililoridhiwa na wazee wote.

 
8723 Total Views 1 Views Today
||||| 15 I Like It! |||||
Sambaza!