ChanjooChanjo iliyotolewa na mwekezaji wa Kampuni ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi kwenye miamba iliyopo chini ya maji katika eneo la kusini mwa Ziwa Tanganyika, imeelezwa itateketeza taratibu watu zaidi ya 190 kati yao Watanzania wakiwa asilimia 90, imefahamika.
Chanjo hiyo ya magonjwa ya tumbo ‘typhoid’ ilitolewa na Kampuni ya Beach Petroleum inayomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Australia, Novemba na Desemba 2014, kwa wafanyakazi wake waliopo mikoa ya Rukwa na Kigoma.
Kabla ya kutolewa kwa chanjo hiyo na uongozi wa Beach Petroleum, wafanyakazi walipewa vitisho vya kufukuzwa kazi iwapo wangekataa kufanyiwa chanjo hiyo, jambo lililowalazimu kukubali kupatiwa chanjo.
Vyanzo hivyo vya habari kutoka ndani ya kampuni hiyo vinaeleza kuwa chanjo hiyo ilianza kutolewa Novemba 18, 2014 mchana na James na mkewe, Katherine Ann (raia wa kigeni), wakitokea Kipiri Mkoa wa Rukwa na kufika Katavi, Wilaya ya Mpanda, Tarafa ya Kalema, Kijiji cha Kalema, na kuanza kutoa chanjo kwa wafanyakazi walio chini ya Kampuni ya BGP ya Wachina. Wafanyakazi 39 walipatiwa chanjo hiyo.


Chanjo hiyo ilitolewa kwa kipindi cha miezi miwili kwa wafanyakazi wapatao 190 huku baadhi yao wakiwa wameanza kupata madhara kutokana na chanjo hiyo.
Pamoja na mwekezaji huyo kutoa chanjo hiyo, baadhi ya watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini wameshtushwa na chanjo hiyo iliyotolewa bila kuhusishwa wizara hiyo.
Katika mahojiano na JAMHURI, Msajili wa Madaktari, Palloty Luena, anasema kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kutoa chanjo bila idhini ya Wizara ya Afya nchini.
Luena anaeleza kuwa iwapo kuna chanjo iliyotolewa bila Wizara hiyo kufahamishwa, ni kosa kisheria na daktari iliyetoa chanjo hiyo anapaswa kutoa ufafanuzi wa kina.


“Wacha tufanye utaratibu wa kufuatilia suala hilo kwa kina kama kweli limetokea, ila nitawasiliana na Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya kujua nini kimetokea,” anasema Luena.
Katika nyaraka ambazo JAMHURI imeziona, Beach Petroleum Tanzania Ltd walinunua dawa aina ya Typhoid Vaccine Ad Single Dose (TYPHIM) 200 ambazo zilikuwa na thamani ya Sh. 8,010,000 kutoka duka la dawa la JD lililopo jijini Dar es Salaam.
Nyaraka ya upokeaji (delivery note) ya Novemba 5, 2014 kumbukumbu namba 90187 inabainisha kupokewa kwa chanjo hizo na Kampuni ya Beach Petroleum (T) Ltd, Novemba 6, 2014.
Aidha, nyaraka ya malipo ya chanjo hizo yenye namba 90187 ya Novemba 6, 2014 inabainisha malipo hayo kulipwa na Beach Petroleum Tanzania Ltd TT 061114 inayobainisha kufanyika kwa malipo ya chanjo hizo.
Mkurugenzi wa JD Pharmacy, Kiran Pattni, akizungumzia mauzo ya dawa hiyo anaeleza kuwa “Ni kweli dawa hiyo itakuwa ilinunuliwa katika duka letu la dawa lililopo Kariakoo Barabara ya Uhuru.”


Pattni anasema kuwa wao siyo waagizaji wa chanjo hiyo kutoka nje ya nchi bali hununua katika kampuni ya Vaccines and Specialties ya Jijini Dar es Saalam, hivyo hao ndiyo wanaoweza kuongelea zaidi usajili na uingizwaji wa dawa hiyo nchini.
“Dawa za aina hii sisi huwa tunauza kwa oda maalum, unaweza kukaa nazo mwaka mzima bila kuuza popote, ndiyo maana tunauza kutokana na mahitaji yake maalum. Kuhusu usajili wake kukoma miaka saba iliyopita, wenye product (bidhaa) ndiyo wanaotakiwa kufuatilia hilo TFDA, siyo sisi wanunuzi,” anasema Pattni.
JAMHURI iliwasiliana na  Mkurugenzi wa Kampuni ya Vaccine and Specialties, Gilbert Mushi, ambapo anaeleza kuwa kampuni hiyo ilishafungwa ila wao siyo wahusika wa dawa hiyo bali ni kampuni ya Ufaransa.
Hata hivyo, baada ya muda aliwasiliana tena na gazeti hili na kusema kuwa tayari amewasiliana na wahusika waliopo Ufaransa kuweza kufuatilia usajili wa dawa hiyo, ambao wameeleza kuwa tayari wamewasilisha nyaraka TFDA.
“Nimewasiliana nao wameniambia kuwa wamesharenew usajili wa dawa hiyo mwaka 2015, nenda kawaone TFDA watakwambia, labda kama nyaraka hazijafika,” anasema Mushi.


Akizungumzia utoaji wa chanjo hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk. Joseph Msemwa, anasema kuwa amepata taarifa za kutolewa chanjo hiyo mwezi mmoja na nusu uliopita.
Dk. Msemwa anasema kuwa ofisi yake haikuwa na taarifa zozote kuhusu utoaji wa chanjo hiyo, na amepata taarifa kwa baadhi ya watu waliopatiwa chanjo hiyo kwamba wamepata madhara na hivyo ilimlazimu kufuatilia suala hilo.
“Niliweza kufika eneo la tukio, niliwakuta baadhi ya wafanyakazi waliokubali kupatiwa chanjo hiyo, lakini hawakunieleza kuhusu madhara, ila wafanyakazi karibu wote walikuwa wamerudi makwao. Lengo langu la kufika pale ni kufuatilia kwa ukaribu maana ni maagizo niliyopewa na mkuu wangu wa kazi (RMO), ambaye alipelekewa taarifa hizo,” anasema Dk. Msemwa.


Alipoulizwa kuhusu utaratibu wa kutolewa chanjo, anasema kuwa swali hilo ni gumu kwake kulijibu, kwani anakuwa na mazingira magumu kuzungumzia. Ila kutokana na mazingira hayo mwekezaji huyo hakuona umuhimu wa kuitaarifu ofisi yake, jambo ambalo si sahihi maana ni lazima ofisi hiyo ifahamishwe.
Gazeti hili liliwasiliana na msimamizi wa Beach Petroleum kutoka Shirika la Petroli Tanzania (TPDC), Josephat Shigela, kuweza kupatiwa ufafanuzi kuhusu chanjo hiyo ambako anaeleza, “Ni kweli nina taarifa hizo,” lakini hawezi kuliongelea suala hilo maana yuko likizo nje ya ofisi hivyo atafutwe Mkurugenzi wa Utafutaji, Kelvin Komba.


JAMHURI ililazimika kufika katika ofisi za TPDC kuweza kukutana na Mkurugenzi wa Utafutaji kama ilivyoagizwa, ambapo  ilielezwa kuwa Komba kwa sasa anakaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu na alitoa maelekezo ya kukutana na ofisa habari wa shirika hilo.
Afisa Habari wa TPDC, Venosa Irenei Ngowi, alionesha kushtushwa na taarifa hizo na kuitaka JAMHURI kumpatia muda ili aweze kufuatilia taarifa hizo, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na uongozi wa shirika.
Hata hivyo baada ya muda, aliweza kuwasiliana na gazeti hili na kusema, “Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania hajapata taarifa yoyote aidha ya mpango au utekelezaji wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa typhoid (Typhoid Vaccine Ad. Single Dose -TYPHIM) kwa wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi katika Meli ya Utafiti Mwongozo, kambi ya Kapiri, Kalema na huko Ikola.”


Mmoja wa watendaji wa TPDC (jina linahifadhiwa) anasema kuwa mwekezaji huyo amekiuka taratibu zilizowekwa na shirika hilo maana zipo taratibu za kitabibu zilizowekwa kwa wawekezaji hao lakini mwekezaji huyo alijiamulia, jambo ambalo si sahihi.
“Kawaida huwa tunakutana na wawekezaji nao wanatupatia mpango kazi wao wa mwaka mzima, kama watatoa chanjo lazima ifahamike na kuwasiliana na Wizara ya Afya, wao walijiamulia tu, hili jambo si sahihi. Uzuri ni kwamba limefika hapa kwetu litaweza kufuatiliwa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua stahiki,” anasema.
Vyanzo vya habari vimelidokeza gazeti hili kuwa uongozi wa Beach Petroleum umeanza kutafuta mbinu za kujinasua na suala hilo baada ya kuona likifuatiliwa kwa ukaribu na gazeti hili, ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola kwa kutafuta msaada kutoka kwa kigogo mmoja wa Serikali kuu, jambo ambalo halijazaa matunda.
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) inabainisha kuwa chanjo hiyo ilikoma usajili wake miaka saba iliyopita, hivyo kutokuwapo katika orodha ya dawa zinazotumika hivi sasa.


Afisa Habari wa TFDA, Gaudensia Simwanza, anasema kuwa dawa hiyo ya chanjo iliwahi kusajiliwa hapo awali na usajili wake ulikoma miaka saba iliyopita, hivyo tangu mwaka 2008 TFDA haijawahi kutoa usajili wa dawa hiyo nchini.
Anasema kuwa uhalali wa mtoa chanjo hiyo kwa binadamu iwapo mtoaji wa chanjo hiyo ni daktari halali na amesajiliwa na Wizara ya Afya si tatizo, ila kama mtoaji huyo hana vigezo vinavyohitajika ni tatizo maana anaweza kusababisha mauaji.
Hata hivyo, anaeleza kuwa utoaji wowote wa chanjo una taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe, ni lazima kuwasiliana na TFDA kabla ya kutoa chanjo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watu wanaotakiwa kupatiwa chanjo hiyo, kuhakikisha kuwa wana afya njema.


Mmoja wa madaktari katika Kitengo cha Chanjo cha Taifa (jina linahifadhiwa) anaeleza kuwa nchi ya Tanzania ilishaacha kutoa chanjo hiyo tangu miaka ya 1980 na kuwa chanjo hiyo haitolewi kabisa hapa nchini na alishangazwa na utoaji wa chanjo hiyo kwa kampuni hiyo ya kigeni.
Pia alilidokeza gazeti hili kuwa utunzaji wa chanjo unahitaji uangalizi wa kitaalamu na iwapo hazitotunzwa ipasavyo chanjo husika hugeuka na kuwa sumu, hivyo ni lazima kufuata sheria za chanjo kabla na wakati wa kutoa chanjo husika.
Baadhi ya wafanyakazi waliopatiwa chanjo hiyo wamelidokeza gazeti hili kuwa utoaji wa chanjo hiyo ulikuwa tofauti na chanjo nyingine ambazo wamewahi kuona zikitolewa, kutokana na utoaji wenyewe na sindano ya chanjo ambao haukuzingatia sheria za afya.
Anasema, “Kwa kawaida kabla hujachomwa sindano yoyote lazima eneo litakalochomwa sindano hiyo liandaliwe kwa kusafishwa lakini kwetu hatukufanyiwa kitu hicho, tulikuwa tunachomwa na kuondoka bila hata tahadhari yoyote kuchukuliwa.”
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza, Dk. Janeth Mgamba, alipigwa na butwaa baada ya kuulizwa kuhusiana na uwepo wa chanjo hiyo nchini.


Dk. Mgamba anasema kuwa chanjo hiyo haipo kwenye mpango wa Taifa wa chanjo nchini, hivyo utoaji wa chanjo hiyo si sahihi na Wizara haina taarifa zozote kuhusiana na utoaji wa chanjo uliofanywa na kampuni hiyo ya kigeni.
Anasema kuwa katika sheria za kutoa chanjo hakuna mtu anayelazimishwa kutoa chanjo kama ambavyo kampuni hiyo imefanya kwa wafanyakazi wake, pia utoaji wa chanjo hiyo haukufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Afya nchini.
Akizungumzia utolewaji wa chanjo hiyo, Meneja  Mwakilishi wa Beach Petroleum, Marcus Jacob Mng’ong’o, anasema kuwa kampuni hiyo ilianza kazi nchini mwaka 2010 katika Ziwa Tanganyika  wakati wakifanya kazi katika meli ya Mwongozo  wakiwa na wanajeshi wa JWTZ Wanamaji (Navy), kulitokea matatizo ya mmoja wa askari hao kuugua ugonjwa wa typhoid na kuhara ambao uliwasumbua mno na kulazimu kusimamisha kazi kwa zaidi ya saa tano ili kutafuta njia ya kuokoa maisha ya askari huyo.


“Tulisimamisha kazi na kujikuta tukitafuta njia ya kuokoa maisha yake, kisha tuliweza kufanya utaratibu wa kumpeleka Sumbawanga kwa matibabu. Ugonjwa huo alitoka nao kambini kwake. Kutokana na usumbufu huo tulioupata tuliona lazima kuweka tahadhari kwa wafanyakazi wetu,” anasema Mng’ong’o.
Mng’ong’o anasema kuwa  kampuni hiyo ilifanya utafiti wao wenyewe na kugundua Ikola, Kalema na Kipiri maji yake kuwa na matatizo pamoja na typhoid hivyo walipanga kuwapatia wafanyakazi kinga ya ugonjwa wa typhoid.
Anaeleza kuwa walitoa chanjo kwa makundi matuta ambayo ni wafanyakazi wa meli ya Mwongozo iliyotolewa mkoani Kigoma ambao walikuwa wanakadiriwa kuwa 60, Kipiri wafanyakazi 40 na Kalema wafanyakazi kati ya 120 na 140 walipatiwa chanjo hiyo.
 “Sisi tunaamini ya kuwa hii ni kinga kwa ajili ya wafanyakzai wetu, dawa hizi zinauzwa katika duka la dawa. Hatukuona haja ya kutoa taarifa zozote kwa Wizara ya Afya na hatukupewa wala kuomba kibali cha kutoa chanjo hiyo. Tumekuwa tukinunua dawa JD siku zote hatukuelekezwa kama kuna kibali cha Serikali kinahitajika,” anasema Mng’ong’o.
Anaendelea kusema, “Hii chanjo imefanyika tangu mwaka jana mwezi wa 11 mpaka wa 12, lakini hili suala limeibuka sasa nashangaa.”


Hata hivyo, meneja huyo anaeleza kuwa waliwaambia wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa watawapatia chanjo hiyo ili kuepuka kuugua mara kwa mara, na mfanyakazi yeyote ambaye hatokuwa tayari kupatiwa chanjo hiyo kampuni hiyo haitoweza kufanya naye kazi.
“Dawa zilizonunuliwa zilikuwa paketi 200 na zilipotumika zilibaki 10 tu ambazo zipo kempu huko Kalema. Tulipozinunua tulizisafirisha kwa ndege ya shirika la ndege la Auric Air mpaka Sumbawanga, wafanyakazi wa Beach walikuja kuzichukua na kuzisafirisha mpaka Kipiri kwa boti kisha zilisafirishwa kwa njia ya maji mpaka Kalema,” anasema.
Anaeleza kuwa yeye binafsi haoni kama kampuni hiyo ilifanya kosa lolote katika utoaji wa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wake zaidi ya kuwasaidia ili wasikumbwe na maradhi.
“Kama hizi dawa zina tatizo kwanini Serikali iruhusu ziuzwe? Sidhani kama wauzaji wanakurupuka tu na kuanza kuziuza,” anasema Mg’ong’o.


Mwanasheria wa Beach Petroleum, Victoria Lyimo wa Kampuni ya Sheria Velma Law, alipoulizwa kuhusiana na wateja wake kutoa chanjo hiyo, anasema kuwa yeye binafsi hajui lolote kuhusiana na kampuni hiyo kutoa chanjo kwa wafanyakazi wake.
Lyimo anaeleza kuwa pia hawezi katu kuzungumzia suala hilo maana mkataba wake na kampuni hiyo haumruhusu kuzungumzia masuala ya mteja wake bila makubadiliano yoyote.
JAMHURI ilimdokeza kuwa kauli yake hiyo mbona inapingana na taarifa zilizopo kuwa ameshiriki kuzungumzia utoaji wa chanjo hiyo ambapo aliwaeleza kuwa hakuna kosa lolote la kisheria walilolifanya zaidi ya kutoa msaada? Lyimo anasema yeye si mzungumzaji wa kampuni, hivyo mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni Beach Petroleum wenyewe.


Majina ya baadhi ya wafanyakazi waliopatiwa chanjo hiyo:
1.  Evanns Lomala Emeto
2.  Raymond Kusiima     
3.  Coliins Kiumuro
4.  Moses Ayebale
5.  Geoffrey Byamukama
6.  Geofrey Ochai
7.  Ronald Okello
8.  Eliufoo Nkungu Kitoto
9.  Yusuf Musa Nampembe
10. Daudi Mashenene
11. Magreth Kapata Muheza
12. Debora Ackim
13. Happyness C.Khamsihi
14. Mariselo Padrick Kikoti
15. Vehas Mabute
16. Antoni Alforisi Kakokele
17. Kililiamu Aloizikabue
18. Adriano Kumbi
19.  John Athanas Kilubi
20. Josephat Katambwa
21. Hagai George Ndazi
22. Philibeth Mwingha Kapela
23. Florence A. Kaisari
24. Alex Abel Makanyaga
25. Mick Abdullha Mwidadi
26. Twalibu Ahmed Kabaju
27. Ibensha N. Kahawa
28. Peter Kobongo Mons
29. Peter Michael Rupia
30.Maganga S.Heshinge
31. Mthew  M. Ngola
32. Justine Benezeth Mgobela
33. Juma R.Almas
34. Havard Alfred Kaoga
35. Joakimu Peter Selemani
36. Cosmas Sixto Chipinds
37. Robat Jonas Makonobwe
38. Logatus Simon Munwe
39. Amosi Emanuel Mbuye
40. Martini K. Chapanlinge
41. John Komedi Chapanlinge
42. Abdul Bashir Mohamed
43. Abuu Mohamedi Muka
44. Emmanuel Paschal Mahushi
45. Gelazi Paulo Kiluba
46. Rajabu Ahamadi Amiri
47. Yusufu Shabani Shambi
48. Jamesi Peter
49. Emmanuel Mwambali
50. Tazi  Haruna
51. Yohana Willian Nyangasa
52. Abihudi Samwele msele
53. Emanuel L. Mlagala
54.  Faustine Nicholaus Nwaisak
55. Joseph Euzebius Damiano
56. Ally Twaha
57. Hizdori  Katili
58. Simon Maicwaya
59. Bittu Puran Singh
60. Suleiman H. Abedan
61. Inocent Mwaipopo
62. Jumanne Jula
63. Juma Hamisi Ramadani
64. Mbaraka Abdallah Mfaume
65. Jumanne Ally Mketo
66. Paulo Joseph Molely
67. Nadhaliyu Issa Balemba
68. Pepino William Kanoni
69. Salehe Juma Manimba
70.  Hamisi Ramadhani Masumpa
71.  Kombo Maulid Issa
72. Hassan Hamisi Omar
73.  Daniel Francis Nchimbi
74. Rashidi Jumanne Chambuso
75. Charles Shilimeael Munuo
76. Mbaraka Hussein Mwaisaka
77. Abdallah Shabani Kasanga
78. Hussein Ramadhan Othuman
79. Pascal Kizito Zunda
80. Emanuel Kimali James
81. Sebastian S.Sinu
82. Nsajigwa Wiliam Mwaisaka
83. Mahamudu Mohamed Mwalin
84. Deodatus Cloud Matapila
85. Benjamini Jonah Kasera
86. Josephene Shibiby
87. Scola  Kabenze
88. Thomas Ngozi Rufina
89. Zubeda Haruna
90. Geoge Lugemalila Masasi
91. Happiness Kabenze
92. Diana Mwangamba
93. Francisco Pembe
94. Joseph F. Kabenze
95. Clares M. Matipa
96. Saphia Said
97. Abdalah Yusufu Malambo
98.Said Yufuph Mgunda
99. Said Asinawi Makutka
100. William Aloiz Kabwe
101. John Comedi Chapaulinge

 

By Jamhuri