✅Al Mansour Group Yaonesha Nia Kuwekeza kwenye Uongezaji Thamani wa Dhahabu, Nikeli, Kobalti na Chuma

✅Teknolojia, Mitambo, Mafunzo na Uzalishaji wa Mbolea Vyatajwa Maeneo Muhimu ya Ushirikiano

✅Wachimbaji Wadogo Waguswa

📍 Doha, Qatar

Tanzania imeendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa katika Sekta ya Madini baada ya Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Madini ikiongozwa na Kamishina Msaidizi wa Madini anayesimamia Uongezaji Thamani wa Madini, Mhandisi Modest Apolinary, kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Mansour Group, Mhe. Sheikh Mansour Bin Jabour Bin Jassim Al Thani, ambaye pia ni Mwanafamilia wa Kifalme wa Qatar.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Juni 1, 2026 yalilenga kujadili fursa za uwekezaji na maeneo ya ushirikiano katika Sekta ya Madini nchini Tanzania, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji wa kimkakati kufuatia ziara ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, aliyoifanya nchini Qatar mwezi Februari 2026.

Katika kikao hicho, pande zote mbili zilijadili fursa mbalimbali za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa madini, hususan madini muhimu na ya kimkakati. Kampuni ya Al Mansour Group ilionesha nia ya kuwekeza katika shughuli za uongezaji thamani wa madini ya dhahabu, nikeli, kobalti na chuma, hatua inayokwenda sambamba na mkakati wa Tanzania wa kuongeza thamani ya rasilimali zake kabla ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Majadiliano hayo pia yalihusisha uwezekano wa ushirikiano katika utengenezaji na usambazaji wa mitambo pamoja na vifaa vinavyotumika katika shughuli za utafiti, uchorongaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Kutokana na dhamira hiyo, ilikubaliwa kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lifanye tathmini ya mahitaji ya wachimbaji wadogo ili kubaini aina ya vifaa vinavyohitajika kwa lengo la kuimarisha shughuli za utafiti na uchimbaji nchini.

Aidha, pande hizo mbili zilijadili fursa za ushirikiano katika mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa wataalamu wa sekta ya madini, hususan katika maeneo ya utafiti wa madini, teknolojia za uchorongaji, usimamizi wa miradi na elimu ya fedha. Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kitaalamu na kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya madini nchini.

Katika hatua nyingine, majadiliano yaligusia uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana Tanzania. Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa mbolea, kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Modest Apolinary alisema Wizara ya Madini ipo tayari kushirikiana na Al Mansour Group katika maeneo mbalimbali ya utafiti, uchimbaji, uongezaji thamani wa madini na maendeleo ya rasilimali watu ili kuhakikisha pande zote zinanufaika na ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, alisema Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji kutokana na mazingira yake tulivu, sera rafiki za uwekezaji na mifumo ya kisheria inayolinda mitaji ya wawekezaji.

‘’Tunaikaribisha Al Mansour Group kuwekeza nchini Tanzania na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini, Viwanda na Kilimo,” alisema Balozi Habibu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, alisema shirika hilo liko tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika maeneo yote ambayo imeonesha nia ya kuwekeza, akibainisha kuwa ushirikiano huo utaongeza uwekezaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuimarisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mazungumzo hayo ya wataalam kutoka Wizara ya Madini, STAMICO na kampuni hiyo yanaashiria hatua mpya katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Qatar, huku yakifungua fursa za uwekezaji, teknolojia na uongezaji thamani wa rasilimali madini kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

Aidha, timu hiyo inatarajia kukutana na Kampuni mbalimbali za uwekezaji.

InvestInTanzania

MiningSector

MineralForGrowth

StrategicMinerals

ValueAddition

TanzaniaQatarPartnership