Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema utekwaji madereva wa Kitanzania uliofanywa na kikundi cha waasi cha MaiMai nchini Congo  hauna uhusiano wowote na uwepo wa askari wa jeshi hilo nchini humo.

Akizungumza na JAMHURI, msemaji wa Jeshi la Ukinzi la  Wananchi wa Tanzania, Kanali Ngemela Lubinga, anasema tukio hilo kamwe lisihusishwe na uwepo wa makamanda na wapiganaji hao kwani hawajaenda kulinda nchi nzima ya Congo DRC.

“Unajua, sisi hatujaenda kupambana na waasi kama wengi wanavyodhani ila tumeenda kule kwa makubaliano ya kusimamia urejeshwaji wa amani ndani ya nchi hiyo kwa lengo la kudumisha ustawi wa wananchi.

“Tukio la kutekwa madereva wa Tanzania limetokea maeneo ya mbali ukilinganisha na maeneo waliko makamanda na wapiganaji wetu,” anasema Lubinga.

Anasema JWTZ inaongozwa na misingi ya kijeshi na haiwezi kufanya kazi kinyume na matakwa ya Umoja wa Mataifa ambao ndiyo waangalizi wakubwa wa masualayaamaninchinihumo.

“Jeshi letu lipo nchini Congo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, hatujaenda kule kama sisi na hata hivyo Watanzania wala wasihofu juu ya tukio hilo vijana wapo imara na wataendelea na majukumu yao kama kawaida,” anasema Lubinga.

Juu ya utekaji wa  magari ya Kitanzania, anasema kwa sasa ni mapema mno kwao kuweza kusema chochote juu ya suala hilo kwani lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.

“Haya ni masuala ambayo yanaweza kumalizwa kwa kuitumia wizara husika sisi  kama Jeshi wala halituhusu tukiingilia itakuwa tunaingilia majukumu ya watu wengine,” anasema Lubinga.

Anasema majukumu ya Jeshi la wananchi si kwenda kushugulika na masuala yanayotokea nchi nyingine bila ya kufuata utaratibu unaotakiwa na sheria zinazoliongoza jeshi hilo.

Wiki iliyopita kuliripotiwa utekwaji wa madereva kutoka Tanzania huko Congo wanaodaiwa kutenda kitendo hicho ni kikundi cha waasi wa Maimai baada ya utekaji huo waliwashusha madereva kwenye magari yao na kutoa saa 24 wakitaka kulipwa kiasi cha dola za Kimarekani 4,000 kwa  kila mmoja huku watekaji wakitishia kuwa na endapo madai hayo yasipotekelezwa.

Jumla ya magari yaliyotekwa ni 12 kati ya hayo magari 8 ni ya Tanzania na manne ya Kenya. Magari manne ya Tanzania yalichomwa moto na madereva wote walichukuliwa na waasi lakini bahati nzuri madereva wawili wa Tanzania walifanikiwa kuwatoroka. Tukio hilo lilitokea sehemu inayoitwa Kasebebenana Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka mji wa Namoya.

Taarifa za awali zimedai kuwa madereva wawili kutoka Tanzania walifanikiwa kutoroka na ndiyo waliotoa taarifa za kuhusu tukio hilo.

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa AfrikaMashariki imeishirikisha serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhakikisha kuwa madereva hao wa malori wanaachiwa huru bila masharti yoyote.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Mindi Kasiga, anasema Serikali itahakikisha mateka hao wanaokolewa.

“Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Kongo inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha madereva hao wanaachiwa huru haraka iwezekanavyo na kurudishwa nchini wakiwa salama.

“Waasi hao wa Maimai wametoa masaa 24 hadi kufikia leo wawe wamelipwa kiasi cha dola 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia huru na kutishia kuwadhuru endapo hawatapata fedha hizo, hivyo basi Serikali imeendelea kuwa na mazungumzo na Serikali ya Kongo ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” anasema Kasiga.

Malori yaliyotekwa nyara ni 12 kati ya hayo manane ni mali ya mfanyabiashara Azim Dewji na mengine ni mali za wafanyabiashara kutoka nchini Kenya.

Serikali imewataka Watanzania kufahamu hali ya usalama wa nchi wanazokwenda ili kujikinga na matatizo mbalimbali yanayoweza kuwapata wakiwa  huko.

Madereva wa malori kutoka nchini Tanzania waliokuwa wametekwa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameokolewa na vikosi vya jeshi la nchi hiyo.

Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ambaye ameiambia BBC kuwa wote wapo salama.

Baadhi ya askari wa JWTZ wako nchini Congo DR, katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo.

By Jamhuri