Bunge limeambiwa kwamba kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohsin Abdallah Shein, ni mmoja wa majangili wa kimataifa wanaomaliza tembo hapa nchini.

Shein ametajwa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Peter Msigwa.

Msigwa anayesifika kwa kutomung’unya maneno, alisema Sheni anaendesha ujangili kupitia kampuni zake zinazoendesha uwindaji wa kitalii katika mapori mbalimbali nchini.

 

Alisema taasisi ya kiintelejensia ya kimataifa ya Environmental Investigations Agency imemtuhumu Shein kama jangili wa kimataifa ambaye anajihusisha na biashara na mtandao wa pembe za ndovu (tembo).

 

“Ni jambo linalojulikana kuwa jangili huyo yupo karibu na baadhi ya viongozi wakuu na waandamizi wa Serikali ya CCM. Kamati ya Uchunguzi imeonesha anamiliki vitalu 16 kwa majina tofauti.

“Anatumia kampuni zake kuhodhi vitalu wakati hana uwezo wa kuviendeleza na badala yake watu makini wanakosa vitalu. Pia kuna makada wengine wa CCM ambao kutokana na tabia zao, Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa alikwishawaweka ndani na hivi sasa ndiyo wanaoua tembo bila kificho na vyombo vyote vya dola vinaelewa.

 

“Je, kwa ushahidi huu wa wazi wa uhusiano uliopo kati ya makada wa CCM na ujangili ni kweli Serikali na vyombo vyake havina taarifa?” Amehoji Msigwa.

 

Msigwa alizitaja kampuni ambazo Shein pamoja na ndugu wanazimiliki, na ambazo Msigwa anasema zinatumika kuendesha ujangili wa tembo.

 

Alinukuu Taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge iliyotolewa bungeni mwaka jana iliyosema, “Kampuni zenye majina yanayoelekea kufanana na zina ofisi katika jengo moja. Royal Frontiers of Tanzania Limited, Game Frontiers of Tanzania Limited, Western Frontiers of Tanzania Limited, na Northern Hunting and Enterprises Limited

 

“Katika uchunguzi, Kamati ilibaini kuwa kampuni hizo nne zina jumla ya vitalu 16. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa wanahisa wa kampuni hizo wana nasaba za kifamilia hivyo kuleta hisia kuwa lengo la Sheria na Kanuni kuzuia mtu mmoja kumiliki vitalu zaidi ya vitano linapuuzwa kwa ujanja kwa kusajili kampuni mpya kwa malengo fulani.

 

“[Royal Frontiers of Tanzania Limited, Game Frontiers of Tanzania Limited, Western Frontiers of Tanzania Limited, na Northern Hunting and Enterprises Limited] Kamati ilipata ushahidi wa maelezo ya kampuni zinazofanya biashara ya uwindaji wa kitalii kuwa mmiliki ni mmoja, na hata maelezo ya baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kumshauri Waziri Kuhusu Ugawaji wa Vitalu yanaashiria kuwa kampuni zote hizo zinamilikiwa na mtu mmoja, hali inayoweza kusababisha mtu huyo kupata vitalu vingi kinyume cha Sheria.”

 

Ukiukwaji wa Mkataba wa Matumizi ya Vitalu

Msigwa aliendelea kuhoji ukiukwaji wa Mkataba wa Matumizi ya Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii uliofanywa na Shein kupitia kampuni yake ya Game Frontiers.

 

“Mheshimiwa Spika mkataba husika, ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa SIRI unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika kwa jina la Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Bwana Mohsin M. Abdallah  na ndugu Nargis M. Abdallah.  Kampuni hii ya uwindaji, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni, za kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya uranium katika kijiji cha Mbarang’andu kwa malipo yafuatayo:-

a) Malipo ya dola 6,000,000 za Marekani, ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya dola 3,000,000. Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa urani utakapoanza.

b) Malipo ya dola 250,000 za Marekani baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini.

c) Malipo ya dola 55,000 za Marekani kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu! Malipo hayo yatafanyika kila tarehe 31 Machi.

d) Malipo ya dola 10,000 za Marekani kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani. Malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni za madini!

“Mheshimiwa spika, nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu,” amesema.

 

Shein kwenye Ripoti ya Jaji Warioba

Mohsin Abdallah ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mmoja wa wafadhili wakubwa wa chama hicho. Pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama wa Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA). Mtu huyu ameshatuhumiwa ukwepaji kodi na ‘kuwanunua viongozi’ wa kisiasa na wa vyombo vya dola.

 

Mwaka 1996, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliunda Tume ya Kuchunguza Kero ya Rushwa nchini. Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe kenda, iliongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba.

 

Katika ripoti hiyo, Mohsin, pamoja na washirika wake, walituhumiwa kwa mambo mbalimbali. Ifuatayo ni sehemu ya ripoti hiyo ililiyomhusu Mohsin na wenzake-neno kwa neno:

 

Hill Top Hotel and Tours Ltd inayomilikiwa na Mohsin Abdallah na Hitesh P. Arjun ilipewa Certificate of Approval Enterprise na Kituo cha Uwekezaji Rasilimali tarehe 3/1/1991. Baadaye watu hao walianzisha kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel iliyosajiliwa tarehe 2/4/1992 na ambayo ilirithi ‘Certificate of Approval Enterprise iliyokuwa imetolewa kwa kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel and Tours kuendeleza ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya Kigoma. Kampuni hii mpya inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Hitesh Arjun na Deusidedit Kisisiwe. Wamiliki hawa pia wanamiliki makampuni mengine ama kwa pamoja au mmoja kama ifuatavyo:

(i) SHENIS COMMERCIAL LTD inayoshughulika na mauzo ya nguo, vitambaa na vipuri vya magari na mashine inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Mrs Nargis Mohsin Abdallah na Deusdedit Kisisiwe. Kampuni hii ilisajiliwa tarehe 27/7/1988.

(ii) TILE ANDA TUBE LTD iliyosajiliwa tarehe 7/12/1992 inashughulikia na biashara ya vifaa vya ujenzi, umeme, pombe na dawa na inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Deusdedit Kisisiwe na Tariq Mirza.

(iii) FIVE WAYS CLEARING AND FORWARDING AGENCY iliyosajiliwa tarehe 23/10/1992 kwa ajili ya kuondoa mizigo bandarini na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia mbalimbali biashara ya vipuri na vifaa vya ujenzi, uchimbaji na uuzaji wa madini nchi za nje inamilikiwa na Triphon Maji na Deusdedit Kisisiwe.

(iv) ROYAL FRONTIER (T) LTD iliyosajiliwa tarehe 7/3/1994 kwa ajili ya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa watalii inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Deusdedit Kisisiwe na Rashid Omar.

(v) GAME FRONTIER (T) LTD nee MNM Hunting Safaris Ltd, inafanya shughuli zinazofanana na zile za Royal Frontier na inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Mr. Abdikadir Mohamed na Mr. Ahmad Muhidin.

 

Shenis Commercial Ltd ndiyo Kampuni ya kwanza kisha ikafuatiwa na Kigoma Hill Top. Baadaye makampuni mengine yaliibuka haraka haraka, jambo linaloashiria kwamba yalitokana na Kigoma Hill Top na yanafanya shughuli zake kwa kushirikiana. Vifaa vilivyoagizwa na Kigoma Hill Top na kusamehewa kodi ni vingi kuliko mahitaji ya hoteli. Kwa mfano, kampuni iliagiza vigae vya sakafu 27,248, containers 3 za marumaru zenye ujazo wa mita za mraba 3264.8, magodoro 120 na taulo 4,00 wakati hoteli ina vitanda 60 tu.

 

Aidha, iliruhusiwa kuagiza boti tatu na injini nne (outboard engines) na kufanya Hoteli hiyo kuwa na boti 7. Idadi hii ya boti ambazo imeelezwa kwamba zitatumika kwa uvuvi wa kitalii ni nyingi sana ikilinganishwa na idadi ya vyumba vya Hoteli hiyo na inawezekana zitatumiwa kwa shughuli nyingine. Vifaa vya ziada inaaminiwa viliuzwa na makampuni mengine yanayomilikiwa na wakurugenzi wa Kigoma Hill Top Hotel.

 

Taarifa ya IPC inaonyesha kwamba ingawa kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel ilipatiwa misamaha ya kodi, IPC haikuona na haikupendekeza aina ya vifaa vya ujenzi wa Kigoma Hill Top Hotel vinavyotakiwa kusamehewa kodi. Wakurugenzi wa kampuni walikuwa wanawasiliana na Hazina moja kwa moja kuanzia mwaka 1991 hadi Julai 1995 walipoanza kupitisha maombi ya misamaha hiyo IPC. Hata hivyo, baadhi ya vifaa ambavyo vilisamehewa kodi na Hazina havikustahili kusamehewa kodi.

 

Kwa mfano, kampuni ilisamehewa kodi magari Na. TZF 5059 Toyota S/Wagon, TZF 8455 Toyota L/Cruiser, TZF 8612 Land Cruiser S/Wagon na TZF 6001 ambalo ni gari ya kifahari aina ya magari ya Mercedes Benz Sportscar, na ndege moja. Ijapokuwa magari na ndege hiyo vyote vilisamehewa kodi chini ya mradi wa Kigoma Hill Top yamekuwa yanatumika na kampuni zao nyingine hapa Dar es Salaam na Kigoma. Kwa mfano, gari TZF 8454 lililoandikishwa tarehe 16/6/1994 kama mali ya Kigoma Hill Top, chini ya Import Declaration, mwagizaji alikuwa Royal Frontiers na Import Entries zilionyesha Kigoma Hill Top.

 

Kampuni hii ilikuwa iagize ndege mwaka 1995 na ikasamehewa kodi kwa barua Kumb. Na TYC/1/150/9/176/7. Uchunguzi umeonyesha kwamba hakuna ndege iliyosajiliwa hapa nchini kwa jina la kampuni hiyo, lakini kampuni ya Game Frontiers ina ndege yenye namba za usajili 5H-GFT (Cesna 206) iliyosajiliwa mwaka 1995. Uchunguzi pia unaonyesha kwamba kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel inatumia sana ndege hiyo kwa kuwapeleka watalii na wageni huko Kigoma Hill Top Hotel ingawa haina leseni ya biashara ya usafiri wa anga.

 

Ifuatayo ni taarifa ya Idara ya Forodha kuhusu misamaha ya kodi iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya magari, marumaru, sanitary ware na vifaa vya umeme.

 

Tume imezungumza na mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Kigoma Hill Top, Bw. Deusdedit Kisisiwe, lakini maelezo aliyoyatoa kuhusu tuhuma hizo hayakuridhisha.

 

Tume inaamini kwamba:

(i) Bwana Mohsin Abdallah na wenzake, hasa Deusdedit Kisisiwe wamefungua kampuni nyingi za biashara na kuomba misamaha ya kodi kwa kampuni moja ya Kigoma Hill Top Hotel. Kampuni imeagiza vitu vingi vilivyosamehewa kodi na kuvitumia au kuviuza kupitia makampuni yao mengine ambayo hayakupata misamaha ya kodi.

 

(ii) Wafanyabiashaa hawa wamekuwa wanawatumia viongozi wa Serikali katika kuficha maovu yake. Kwa mfano, Kampuni ya Fiveways Clearing and Forwarding Agency ilimpa hisa Bw. Tryphon Maji aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo alikuwa habughudhiwi na Polisi anapofanya vitendo kinyume cha kanuni na taratibu.

Katika makampuni ya Royal Frontier (T) Ltd hisa zimetolewa kwa ndugu wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Utalii na Mazingira Bw. Juma Hamad Omar na katika kampuni ya Game Frontiers (T) Ltd hisa zimetolewa kwa Ahmed Muhidin ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mkurigenzi wa Wanyamapori Bw. Muhidin Ndolanga. Hisa hizi zimetolewa kwa wakubwa hawa kama kivuli (cover) ili waweze kuyapatia makampuni haya vitalu vya uwindaji pamoja na kurahisisha shughuli za uwindaji.

(iii) Bw. Mohsin Abdallah na Kisisiwe wanapenda kuwatumia viongozi kama chambo katika biashara zao ili waweze kuvuka kikwazo chochote kile kitakachokwamisha biashara zao.

 

By Jamhuri