Kamwe tusijisahau, tuwe macho dhidi ya magaidi

Kwa mara nyingine genge la magaidi limeshambulia na kuua majirani zetu kadhaa wa jijini Nairobi, Kenya. Imeripotiwa watu 21 wamepoteza maisha kwenye shambulizi hilo.

Tunawapa pole ndugu wa marehemu, majeruhi na wote walioathiriwa kwa namna moja au nyingine na tukio hilo.

Kwa namna nyingine magaidi wamedhihirisha kuwa wapo na pia dunia si salama kama baadhi yetu wanavyodhani.

Hizi ni salamu zinazopaswa kutuamsha ili tuchukue hadhari kwa ajili ya kukabiliana na majahili hawa kwa muda, majira na siku yoyote.

Pamoja na kutong’amua mapema shambulizi hili la karibuni jijini Nairobi, bado tuna kila sababu ya kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua madhubuti za kufuatilia na kuwatia nguvuni washukiwa wengi.

Tumeona namna teknolojia ya kisasa ilivyosaidia kuwanasa washukiwa hao kutoka pande mbalimbali za taifa hilo.

Tanzania si kisiwa. Mara kadhaa tumejaribiwa na majahili hawa, lakini tunashukuru vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote waliosimama imara kuhakikisha wabaya wa Watanzania na Tanzania wanasakwa na kutiwa nguvuni.

Bado tunayo kumbukumbu ya matukio kadhaa yaliyotokea mikoa ya mwambao mwa Bahari ya Hindi na Kanda ya Ziwa. Tusibweteke wala kupuuza tishio la magaidi hawa.

Vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi wote wenye mapenzi mema na usalama wa taifa letu hatuna budi kuungana kuhakikisha tunawafichua washukiwa wote popote walipo ili kuendelea kuiweka nchi yetu katika hali ya usalama.

Ugaidi hauna dini, rangi, jinsia, taifa wala hali ya mtu. Magaidi wanaua bila kuchagua. Hiyo ina maana hakuna aliye salama kwa maisha yake na usalama wa mali zake pia.

Wala tusichukulie vitendo vya kigaidi kuwa ni imani ya madhehebu fulani. Ugaidi ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine – unafanywa na yeyote anayekuwa na nia hiyo mbaya. Tuendelee kuishi kwa upendo bila kunyosheana vidole kwamba dini fulani ni magaidi.

Tunachukua fursa hii kuhimiza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vya umma na vya binafsi kuendelea kuwa macho muda wote na sehemu zote ili kuwakabili wabaya hawa.

Ulinzi uimarishwe sehemu zote zenye mikusanyiko na tuache mazoea ya kuamini kuwa mahali fulani ni salama.

Tumeona namna Kenya walivyojitahidi kuweka CCTV katika miji yao. Hali kama hiyo imefanywa pia Zanzibar. Huu ni wakati kwa serikali yetu kuanza kufunga mashine hizo kila kunakohitajika ili kujiwekea mazingira mazuri ya kuukabili ugaidi na magaidi. Tusisubiri tupigwe ndipo tuanze kuhaha kununua na kufunga CCTV. Tuanze sasa.

Tunawapa pole Wakenya huku tukiwaomba Watanzania wote kuendelea kuwa macho dhidi ya magaidi. Usalama ni dhima ya kila mwananchi.

7662 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons