Mwl. Julius Nyerere na Rais Keneth Kaunda wa Zambia wakati wa uzinduzi wa Reli ya TAZARA mwaka 1976.

Habari iliyopewa uzito wa juu kwenye gazeti hili toleo la leo inahusu ‘kuuzwa’ kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Mengi yamebainishwa kwenye habari hiyo, lakini lililo kubwa ni mpango wa ‘ubinafsishaji’ wake kwa kampuni ya Afrika Kusini.

Tunatambua kuwa Reli ya TAZARA au kwa jina jingine Reli ya Uhuru, imekuwa ikipitia vipindi vigumu vya uendeshwaji wake. Mara kadhaa imelazimika kupokea msaada wa kifedha kutoka kwa wafadhili wakuu walioijenga, yaani China; na mataifa mengine rafiki.

Reli ya TAZARA ni mfano katika ujenzi wa Afrika mpya kiuchumi. Ndiyo mradi mkubwa wa kwanza uliofanywa na China nje ya taifa hilo. Ilijengwa kwa kuzingatia misingi imara ya urafiki na udugu kati ya mataifa matatu ya Tanzania, Zambia na China.

Umuhimu wake kiuchumi ulikuwapo, upo na utaendelea kuwapo licha ya Zambia sasa kutumia Bandari ya Beira baada ya hali ya usalama kuimarika nchini Msumbiji.

Pamoja na kudorora kwa shehena inayosafirishwa kutoka na kwenda Zambia, bado TAZARA ni muhimu kwa upande wa Tanzania, hasa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Matatizo yake yanaonekana kuchangiwa zaidi na mfumo wa menejimenti. Tunadhani mfumo wa menejimenti uliowekwa tangu miaka ya 1976 unapaswa kutazamwa upya ili pengine kuwapa fursa Watanzania kuwa na sauti kuliko ilivyo sasa.

Matatizo ya TAZARA hayana budi yashughulikiwe haraka na kwa umakini na pande zote mbili, na kwa kweli kwa kufanya hivyo kutakuwa ni kuwaenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwenyekiti Mao Tse Tung na Baba wa Taifa la Zambia, Kenneth Kaunda.

Reli ya TAZARA inapaswa kubaki kuwa alama ya urafiki wa kweli wa China na Bara la Afrika, hususan kwa nchi za Tanzania na Zambia zilizoshiriki kwa hali na mali kwenye mapambano ya ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Tunatoa mwito kwa serikali zote mbili kuketi pamoja na kuja na majibu ya kuikwamua TAZARA badala ya utaratibu huu wa ‘ujanja ujanja’ unaofanywa na upande mmoja.

Ulimwengu utatucheka endapo tutazembea na kuacha reli hii ya kipekee katika Afrika ife. Tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda hatuna budi kuhakikisha njia kuu za usafiri, hasa reli zinapewa umuhimu wa kipekee. Gharama ya kuendesha TAZARA haiwezi kulingana na mzigo wa kujenga au kukarabati barabara kila uchao.

Hatujachelewa. Viongozi na wataalamu wa pande zote mbili waketi pamoja kwa lengo la kupata suluhu ya uhai wa TAZARA ambayo ni alama ya uhuru. Linalowezekana leo lisingoje kesho.

Please follow and like us:
Pin Share