Habari kubwa katika gazeti letu la leo inahusiana na mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani Njombe.

Serikali kupitia vyombo vya dola imeimarisha ulinzi na usalama Njombe. Bunge limeombwa kuunda kamati ya kuchunguza mauaji haya. Uchunguzi wa Gazeti hili la JAMHURI umebaini kuwa mauaji haya yanatokana na imani za kishirikina.

Mmoja wa watu wanaoshikiliwa na vyombo vya dola atakayefikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa, amekiri kwa Mlinzi wa Amani, kuwa ameua watoto watatu baada ya kuaminishwa na mganga wa kienyeji kuwa baba mdogo wake anamroga kupitia watoto hawa. Mwanzo alipanga kumuua baba mdogo wake, lakini alipomkosa akaona hasira zote azimalizie kwa watoto wa baba mdogo wake.

Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa mtuhumiwa anasumbuliwa na ugonjwa unaotokana na upungufu wa kinga mwilini. Ni masikitiko kuwa kwa muda mrefu sasa nchi yetu imeendekeza imani za kishirikina.

Tumeshuhudia mauaji ya aina hii katika mikoa kama ya Mbeya kwa watu kuchunwa ngozi, Kagera watu walikatwa makoromeo, Shinyanga vikongwe wanauawa kwa kuwa na macho mekundu na maeneo mengine ya aina hiyo.

Katika mikoa kama Simiyu na kwingine, bado nako mtoto akiugua wanaamini amerogwa badala ya kwenda hospitalini kupata maelezo ya kitabibu yenye uhakika. Katika mikoa mbalimbali, watoto au watu wazima wakiugua, kimbilio la kwanza ni kwenye makanisa ya kisasa badala ya kwenda hospitalini wakidai kuwa wametumiwa mapepo.

Imekuwa kawaida sasa kusikia katika familia mbalimbali kila wakisali sala iwe ni za asubuhi au jioni, mara zote wanakemea mapepo. Uombaji huu unadhihirisha kuwa nchi yetu bado ina tatizo katika mfumo wa tiba.

Wananchi kwa kutopata majibu sahihi hospitalini, ama kwa uzembe au madaktari kutindikiwa ujuzi, wanaishia kwenda kwa waganga wa kienyeji au wanaangukia katika mikono ya makanisa ya kisasa yasiyo na tofauti na waganga wa kienyeji.

Kila anayekwenda kuombewa anaambiwa ana mapepo, mashetani, ametumiwa majini na wengi hawana ‘sala ya upatanishi’ kwa sasa wanayo ‘sala ya kukemea mapepo’ kila kona. Waganga wa kienyeji wao wanaona uchonganishi unawasaidia kutunisha mifuko yao. Sisi tunadhani wakati umefika sasa serikali iongeze kasi katika kutoa elimu ya afya kwa wananchi.

Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kila ugonjwa una tiba. Badala ya kudhuliana na kushikana uchawi. Tunasema mauaji ya Njombe na sehemu yoyote hapa nchini hayakubaliki, hivyo serikali iwasake na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika kwa nia ya kukomesha vitendo hivi.

Please follow and like us:
Pin Share