Wiki iliyopita Taasisi ya utafiti ya Spurk Media Consulting Ltd ya Uswisi kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT), imetangaza matokeo ya utafiti wake uliohusu ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari nchini kwa mwaka 2018.

Matokeo ya utafiti huo kwa vigezo vya watafiti, vikalifanya Gazeti la JAMHURI kuongoza. Tunawashukuru wasomaji wetu pamoja na timu nzima ya wafanyakazi wa JAMHURI katika kuhakikisha tunazidi kubaki katika ubora.

Ukisoma kwa makini taarifa hiyo ya utafiti, utagundua kwamba bado vyombo vya habari vina upungufu kadhaa, ikiwemo kutowapatia watuhumiwa katika habari zinazoandikwa nafasi ya kujieleza, changamoto ya kutumia takwimu katika habari, vyombo vya habari kujikita katika matukio pamoja na habari za vijijini kutopewa kipaumbele.

Ni wakati sasa wa vyombo vya habari kuyatumia matokeo ya utafiti huu na kubadili changamoto ambazo zimeonyeshwa. Kinacholeta faraja angalau sasa vyombo vya habari vimepunguza kuandika habari zinazohusu siasa, badala yake vimejikita katika habari za maendeleo.

Endapo wahariri wataitumia ripoti hiyo, tunatarajia maboresho makubwa katika maudhui, huku vyombo hivyo vya habari vikitoa nafasi maalumu kwa habari za vijijini pamoja na kuzingatia misingi ya taaluma ya habari.

Sambamba na hilo, utafiti huo umebaini kwamba ni vyombo vya habari vichache ndivyo vinaandika habari zinazokosoa utendaji wa serikali, hiyo ikimaanisha kwamba jukumu lake la kuelimisha, kuonya na kuhabarisha linaingia shakani.

Utafiti huo ulijumuisha sampuli 1,886, idadi hiyo inajumuisha habari, makala na maoni kwa upande wa magazeti, habari na vipindi vya redio  na televisheni, pamoja na posti za blogu na mtandao kutoka vyombo vya habari 25 Tanzania Bara na Zanzibar.

Matokeo ya utafiti huu ni kioo kwa vyombo vya habari na nyenzo maalumu ya kutathmini maeneo yenye  kuhitaji mafunzo. Utafiti huu pia unaweka ulinganifu wa matokeo kwa magazeti, redio na televisheni.

Ni wakati sahihi kwa taasisi za kihabari kama Baraza la Habari Tanzania, Jukwaa la Wahariri pamoja na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari kuisoma ripoti hiyo na kuiwekea mkakati wa pamoja ili kuboresha maudhui.

Please follow and like us:
Pin Share