Kwa muda sasa tunapata taarifa kutoka sehemu mbalimbali za nchi juu ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa watoto walioshinda mtihani wa darasa la saba kwenda kidato cha kwanza mwaka 2018. Malalamiko ya ukosefu wa vyumba vya madarasa yameanza kujitokeza si tu katika ngazi ya sekondari, bali hata ngazi ya shule za msingi.

Kwa mfano Shule ya Msingi Kyakailabwa, katika Manispaa ya Bukoba darasa moja lenye nafasi ya kuchukua wanafunzi 45, sasa linalazimika kuchukua wanafunzi hadi 100 na zaidi. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutokana na wahamiaji kwenye Kata hii ya Nyanga. Lakini bila hata wahamiaji, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ilitoa angalizo la wazi nchini.

Sensa ilionyesha kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni asilimia 34.7. Idadi ya watoto wenye umri wa miaka 0 – 15, ni asilimia 50.1. Jumla ya kundi hili la watoto na vijana ni asilimia 84.8. Kwa hakika takwimu hazidanganyi. Waliokuwa na miaka 7, mwaka 2012 kwa sasa wana umri wa miaka 14. Ni wazi kundi hili ni kubwa.

Kwa maana kama walikuwa ndiyo wanaingia darasa la kwanza sasa wamemaliza darasa la saba. Hawa ni sehemu ya asilimia 50.1, hivyo wanahitaji vyumba vya madarasa katika shule za sekondari. Shule ya Msingi kama Kyakailabwa tuliyoitaja, tayari imelemewa. Uongozi wa Kata ya Nyanga unaangalia uwezekano wa kujenga shule mpya eneo la Nyamyalilo. Kwa sasa wanaomba msaada kujenga chumba kimoja katika shule hii.

Hali iko hivyo sehemu nyingi nchini. Watoto wengi wamefaulu mtihani, hawana mahala pa kwenda. Serikali tayari imezuia wananchi kulazimishwa michango ya kujenga shule. Hata hivyo, kwa hali ilivyo, kuna hatari ya wanafunzi wengi kushindwa kupata nafasi ikiwa kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa inaendelea kuwa kama ilivyo sasa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Charles Msonde, anasema watahiniwa 733,103 kati ya 943,318 wamefaulu mtihani wa mwaka 2018. Idadi ya wahitimu 733,103 kushinda mtihani ni jaribu kubwa kwa idadi ya vyumba vya shule za sekondari zilizopo na walimu wa kufundisha elimu ya sekondari.

Walimu wengi wamo mitaani hawajaajiriwa. Sisi tunadhani wakati umefika serikali ipitie upya uamuzi wa kuzuia michango ya ujenzi au itenge fungu la dharura kuokoa hali hii. Pia tunaisihi serikali iajiri walimu, kwani waliomo kazini nao wamelemewa na mzigo. Tusipowekeza katika elimu kama nchi, muda si mrefu tutajuta.

By Jamhuri