Na Benny Mwaipaja, Washington D.C

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuweka mipango ya kuhakikisha kuwa maji salama yanapatikana kwa ajili ya matumizi ya binadamu na shughuli za kiuchumi lakini pia kulinda vyanzo vya maji.

Mhe. Balozi Omar alisema hayo wakati akichangia mada katika mkutano ulioangazia umuhimu wa sekta ya maji katika maendeleo ya watu na uchumi wa dunia, chini ya kauli mbiu “usalama wa maji kwa mustakabali wa bara la Afrika: mtazamo wa mbele” ulioandaliwa na Benki ya Dunia, pembezoni mwa mikutano ya majira ya Kipupwe ya Benki hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, uliofanyika jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Akijibu swali la namna rasilimali za maji zinavyoweza kulindwa na kutumika kama rasilimali za kiuchumi, Mhe. Balozi Omar alisema ni muhimu ieleweke kwamba maji ni rasilimali muhimu hivyo ni lazima kufanya utafiti wa kutambua vyanzo vya maji vilivyopo ikiwemo mito na maziwa na kuweka utekelezaji wake kwenye mipango ya kitaifa ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu.

“Pia ni muhimu kuvifuatilia na kuvilinda vyanzo hivyo na kuzitumia rasilimali hizo kwa uangalifu mkubwa ili tuendelee kuwa na maji safi, kuvilinda vyanzo hivyo dhidi ya uvamizi na uchafuzi wa maji, pamoja na kuondoa upotevu wa maji.” Alisema Mhe. Balozi Omar

Alitahadharisha kuwa idadi ya watu inaendelea kuongeza kwa kasi barani Afrika hatua iliyosababisha kuwa na uhitaji mkubwa wa maji na kushauri kuwepo kwa ushirikiano madhubuti kati ya sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kama Benki ya Dunia ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili kutekeleza mira ya maji.

Mkutano huo wa maji uliwashirikisha Mawaziri wa Fedha na wadau wengine kutoka nchi wanachama wa Benki ya Dunia kutoka baadhi ya nchi za Bara la Afrika ambapo walijadili namna sera, uwekezaji, mabadiliko ya kimfumo wa kitaasisi unavyoweza kuboresha na kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama barani Afrika.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (katikati), akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop (kulia), wakati wa mkutano ulioangazia umuhimu wa sekta ya maji katika maendeleo ya watu na uchumi wa dunia, chini ya kauli mbiu “usalama wa maji kwa mustakabali wa bara la Afrika: mtazamo wa mbele” ulioandaliwa na Benki ya Dunia, pembezoni mwa mikutano ya majira ya Kipupwe ya Benki hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, uliofanyika jijini Washington D.C, nchini Marekani. Kushoto ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Kanda, Bi. Anna Wellenstein.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington D.C, Marekani)
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akichangia mada katika mkutano ulioangazia umuhimu wa sekta ya maji katika maendeleo ya watu na uchumi wa dunia, chini ya kauli mbiu “usalama wa maji kwa mustakabali wa bara la Afrika: mtazamo wa mbele” ulioandaliwa na Benki ya Dunia, pembezoni mwa mikutano ya majira ya Kipupwe ya Benki hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, uliofanyika jijini Washington D.C, nchini Marekani.