Mwamvua Mwinyi, Pwani
Julai 30,2026

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia msichana mwenye umri wa miaka 16, Rahma Musa Tito, mkazi wa Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Chalinze, kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Hadija Hemedi Shaha (51), kwa kumchoma kichwani kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Salim Morcase alieleza, tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 28, 2026, baada ya marehemu kumzuia binti yake kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake iliyokuwa ikifanyika jirani na Hospitali ya Msoga.

Morcase alieleza, baada ya kuzuiwa kwenda kwenye sherehe hiyo, mtuhumiwa alianza kumshambulia mama yake kabla ya kumchoma kichwani na kusababisha kifo chake.

Alifafanua kwamba, asubuhi ya Julai 29, fundi ujenzi aliyefika nyumbani kwa marehemu kufuata mfuko wa saruji na malipo yake aligonga mlango na kufunguliwa na binti huyo. Baada ya kuingia ndani, alikuta mwili wa marehemu ukiwa umelala sakafuni ukiwa na majeraha kichwani na damu ikitiririka.

Mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Msoga kwa uchunguzi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi, huku Jeshi la Polisi likisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Kamanda huyo aliwataka wazazi, walezi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuimarisha malezi ya watoto na kufuatilia changamoto wanazokumbana nazo ili kuchukua hatua mapema na kuzuia matukio ya aina hiyo.