Bunge la Tanzania
Bunge la Tanzania
NA MANYERERE JACKTON

 

Tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na ufisadi zimeanza kufichuliwa ndani ya uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwenye mlolongo huo, kumeibuka madai ya kuwajiriwa kwa watoto wa vigogo.

Waziri mwanamke anatajwa kuwa miongoni mwa wanufaika wa hali hii, akiwa na mtoto mmoja; na wengine wawili wa ndugu yake.

Kwa kigezo cha muundo mpya, Kamati ya Ajira ya Tume ya Utumishi ya Bunge (iliyopita), inadaiwa kuajiri watumishi wengi, wakiwamo wasiokuwa na kibali cha ikama kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kuanzia Julai 2015  hadi Februari, mwaka huu wameajiriwa watumishi zaidi ya 100; ikiwa watumishi wapya ni 30, watumishi wa mkataba 38 na watumishi waliohamia kutoka wizara na idara nyingine za Serikali ni 34.

Ajira za upendeleo katika Bunge sasa zinakaribiana na zile zilizokwishaibuliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambako watoto wa wakubwa, ama waliajiriwa au wanaendelea na ajira zao kutokana na malipo manono katika chombo hicho.

Bunge, mhimili wa dola ambao ni nadra kufuatuliwa mambo yake kama ilivyo kwa Serikali na Mahakama, limekuwa halitajwitajwi kwenye masuala ya upendeleo na ufisadi, lakini sasa mambo hayo yameanza kuibuliwa. 

“Wapo ambao hawakufanya hata interview (usaili) kabisa na wengine walifanya interview, lakini walishindwa vibaya, lakini leo hii wameajiriwa nafasi nyeti kwa vigezo vya undugu, ukabila, kuwa watoto wa mawaziri na watoto wa watu wakubwa serikalini,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limeambiwa kuwa kuna idara ambazo watumishi wamefurika hata wengine hawajulikani wanafanya shughuli gani. Baadhi ya idara hizo ni za Utawala, Uhasibu, Ugavi na Kamati za Bunge.

“Kwenye Kamati za Bunge, Kamati moja inapaswa kuwa na maafisa wawili na msaidizi mmoja, badala yake kuna makatibu watatu au wanne na msaidizi mmoja.

“Wakati huo huo kuna idara ambazo zina uhaba wa Watumishi kwa muda mrefu ikilinganishwa na mahitaji kwa mfano Idara ya Utawala, Maktaba na Utafiti. Kati ya hao waajiriwa wapya wapo ambao walifanya interview Idara ya Hansard na wakashindwa vibaya, lakini leo hii wengine wamechomekwa katika Idara ya Kamati za Bunge kwa kuwa wazazi wao wana nafasi kubwa serikalini,” kimesema chanzo chetu.

Inaelezwa kuwa kwa mara ya kwanza katika muundo wa uongozi wa Bunge, kumeanzishwa nafasi ya Msaidizi wa Katibu wa Bunge; nafasi ambayo msaidizi wake huyo naye ni Mkurugenzi!

“Hili limeleta shida kutokana na ukweli kuwa muundo wa ofisi baada ya Katibu wa Bunge anafanya kazi kwa kusaidiwa na Naibu Makatibu wa Bunge wawili, Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu (DAP), na Menejeimenti nzima.

“Lakini kwa muundo huu uliopo, Msaidizi wa Katibu wa Bunge ana mamlaka ya kumuagiza DAP na Mkurugenzi yeyote na ikawa ni agizo bila kuhoji. Lakini pia muundo huo unaongeza ukiritimba. Jambo lolote ni lazima lipitie kwa Msaidizi wa Katibu wa Bunge kabla halijamfikia Katibu wa Bunge mwenyewe.

“Kuna haja gani kuwa na Msaidizi wa Katibu wa Bunge, ambaye naye ni Mkurugenzi wakati chini ya Katibu wa Bunge kuna Naibu Makatibu wa Bunge wawili, DAP na Menejimenti?

“Pamoja na hiyo pia kuna Mkurugenzi wa Tume ambaye naye anatoa maagizo moja kwa moja kutoka Tume, kwa bahati mbaya sana aliyeteuliwa kwa nafasi hiyo sasa ni afisa mdogo aliyekuwa na cheo cha Afisa Tawala Daraja Kwanza na kupandishwa cheo kuwa Mkurugenzi kamili,” JAMHURI limeabiwa.

Pia kuna malalamiko ya kuwapo kwa utitiri wa idara ambazo nyingine majukumu yanajirudia.

“Kuwepo kwa wingi wa Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kunaongeza matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi bila sababu za msingi. Iwapo tunahitaji kubana matumizi inabidi kupunguza utitiri wa Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi na Wakuu wa Vitengo,” kimesema chanzo chetu.

 

Ukodishaji magari

Uchunguzi umebaini kuwa kuna magari kadhaa ya Bunge yalipaswa kufanyiwa matengenezo, lakini yameachwa na badala yake mhimili huo umekuwa ukikodisha magari kutoka kampuni binafsi.

Ofisi ya Bunge imekiri kukodisha magari kutoka kampuni ya WALPHA, lakini imekana kutumia fedha nyingi kwa shughuli hiyo.

Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, majibu yake ya maandishi kwa JAMHURI amekana Katibu wa Bunge kuwa miongoni mwa wanufaika wa ukodoshaji wa magari hayo.

Katika majibu yake kwa niaba ya Katibu wa Bunge, Mwandumbya amesema: “Hakuna mkataba wowote wa kutumia gari hilo nyumbani kwa Katibu wa Bunge ila Kampuni ya Walpha imekuwa ikishinda zabuni kadhaa za kutoa huduma za usafiri katika shughuli za Kamati. Hakuna posho ya dereva wa kukodi ililipwa na Ofisi ya Bunge hata wakati mmoja.”

Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI unaonesha kuwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililla, mbali na gari lake la ofisi analotumia, analo jingine alikodisha aina ya Land Cruiser V8 lenye namba T317 CKA kutoka WALPHA kwa takriban miaka miwili sasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake.

Mbali na malipo ya kukodisha gari hilo kwa siku, bado huduma nyingine kwa gari hilo zililipwa na Ofisi ya Bunge.

Baadhi ya nyaraka zinaonyesha kuwa gari hilo unaonesha kuwa Februari 6, 2013 lililipiwa Sh milioni 14.16 kupitia hati ya malipo Na. 330. Februari 12, 2014 Sh milioni 37.518 zililipwa; na Mei 5, mwaka huo malipo yalikuwa Sh 472,000.

 

Utata ununuzi magari ya Ofisi

Kabla ya kuagiza magari mapya kwa ajili ya Spika na Naibu Spika wa Bunge jipya, mmoja wa viongozi waandamizi wa Bunge na timu ya watumishi wengine zaidi ya 10 walienda Ubelgiji na Ujerumani kwa muda wa siku 10 ambako pamoja na mambo mengine, walienda kukagua aina ya gari ambalo lingetumiwa na Spika mpya.

Mwandumbya, anajibu hoja hiyo kwa kusema ukaguzi wa magari ni jambo la kawaida kwa magari ya viongozi, lakini anakanusha idadi ya maofisa waliokwenda kufanya ukaguzi huo bila kutaja idadi ya walioshiriki.

“Si kweli kuwa timu iliyohusika na swala hilo ilikuwa na maafisa 12,” anasema.

Kumekuwepo na sintofahamu ya matumizi ya fedha kwenye ununuzi wa magari, huku bei za ununuzi zikitajwa kuwa kubwa mno.

Magari 10 aina ya Land Cruiser Prado yaliyonunuliwa hivi karibuni yameacha maswali mengi.

Awali, JAMHURI iliambiwa kuwa Ofisi ya Bunge iliagiza magari hayo aina ya Land Cruiser GX na malipo yalifanywa kwa thamani ya aina hiyo ya magari.

“Lakini magari yaliyokuja ni Land Cruiser Prado kwa gharama ya Land Cruiser GX,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Baada ya watumishi kuanza kuzungumzia ununuzi huo tata ikafanywa mipango ya kuchakachua hoja hiyo. Kitengo cha Ununuzi  kikawatafuta wajumbe wa Bodi ya Ununuzi kusaini muhtasari ambao waliuandaa kuonesha kuwa Bodi iliridhia ununuzi wa magari aina ya Land Cruiser Prado, na si Land Cruiser GX.

“Muhtasari huo ulisainiwa Mei 13, mwaka huu; ukiwa umerudishwa nyumba (backdated) Novemba 18, 2015.

“Magari yaliyonunuliwa mwaka jana na yapo ofisini yakitumika, muhtasari ulisainiwa Mei 13, mwaka huu kwa tarehe za mwaka jana.”

Kwa upande wake, Mwandumbya anasema: “Ununuzi wa  aina ya magari yanayotumiwa na Bunge uliamuliwa na menejimenti ikiwa ni mkakati wa kupunguza gharama ili kwenda na circular (waraka) ya Serikali kuhusu aina ya magari yenye gharama nafuu.”

Anaongeza: “Gari binafsi la Katibu wa Bunge siyo sehemu ya magari haya, amekopa mkopo benki kujinunulia gari kama wanavyofanya watumishi wengine pia. Kuhusu muhtasari si kweli kwamba ulikuwa backdated.”

 

Tiketi za ndege

 Eneo jingine linalolalamikiwa ni la tiketi za ndege za kusafiria nje na ndani ya nchi. Kwa sababu za kitaaluma, wakala wa tiketi hizo tunaendelea kumhifadhi kwa sasa.

“Gharama zao za tiketi hujumuisha gharama ya tiketi pamoja na hoteli kwa baadhi ya wasafiri kama Makamishna wa Tume ya Huduma za Bunge, Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge na Wasidizi wao.

“Lakini tiketi zinapoletwa Ofisi ya Bunge msafiri hulazimika kujilipia huko aendako gharama za malazi (hoteli) na huwa hawaelezwi kuwa tiketi yake imelipiwa pia hoteli. Hapo hapo kama ni mbunge au mtumishi hulipwa posho ya kujikimu (per diem) kumwezesha kumudu maisha yake safarini. Hapa Ofisi hufanya malipo mara mbili.

“Watumishi hasa wa Ofisi Binafsi za viongozi hulipiwa tiketi za aina hiyo na hupewa fedha za masurufu juu, ambazo katika historia ya Bunge hakuna ambaye huwa anafanya retirement na kurudisha chenji! Kama msafiri analipwa per diem hakuna sababu ya kulipa tiketi iliyojumuisha gharama za hoteli.

“Kwa muda mrefu Ofisi imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwa utaratibu huo wa kulipia tiketi kwa bei ya juu bila kuitumia huduma hiyo ya malipo ya hoteli yaliyojumuishwa kwenye tiketi.

“Fedha hizo za ziada nani alikuwa akichukua? Kwanini kampuni hiyo ya wakala wa tiketi za ndege iendelee kutoa huduma hiyo kwa Bunge kwa miaka nenda rudi?” kimehoji chanzo chetu.

Nyaraka zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Bunge ilitumia Sh bilioni 7 kwa ununuzi wa tiketi za ndege na masufuru mengine.

Ofisi ya Bunge, kupitia kwa Mwandumbya inasema: “Mkataba wa (anataja kampuni ya uwakala wa tiketi) na Bunge si kweli kama una maelezo kama hayo kwa watumishi wa Bunge, na si kweli kwamba tiketi zao hukatwa pamoja na hoteli kama inavyodaiwa. Hii (ya tiketi na per diem kulipwa pamoja) hutokea pale tu endapo kuna stopover mahali ambayo itazidi saa nane ambapo watumishi hupatiwa hoteli.”

 

Aongezewa mkataba mara tatu

Mmoja wa maofisa usafiri, Kabunju S. Kabunju, ambaye alistaafu kazi kwa mujibu wa sheria miaka saba iliyopita, bado ameongezwa muda mwingine wa miaka mitatu wa kuendelea kuhudumu licha ya kuwa na umri wa miaka 67.

Mwandumbya anajibu suala hili la Kabunju kwa kusema: “Ni kweli alistaafu, lakini kama nilivyokueleza awali, Tume ya Utumishi wa Bunge ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuajiri na hata kutoa mkataba kwa mtumishi yeyote kulingana na Sheria ya Utumishi wa Bunge.

“Kwa msingi huo, Kabunju alipewa mkataba na Tume iliyopita baada ya kuwepo haja ya kuendelea kumtumia.”

By Jamhuri