Kashfa nzito

Serikali ya Rais John Pombe Magufuli imo hatarini kupoteza zaidi ya Sh bilioni 120 kutokana na mradi wa kukopesha matreka kwa wakulima ambao mkataba uliingiwa siku 8 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kugeuka ‘kichomi’, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Mkataba huo unaotajwa kuwa na mazonge mengi, uliingiwa Oktoba 22, 2015 ikiwa ni wiki moja na siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 30, 2015 kati ya Kampuni ya URSUS ya Poland na SUMA JKT ya Tanzania.

Vyanzo vya uhakika vinaupigia kelele mkataba huu kuwa una matundu mengi, na utekelezaji wake ulikwama katika hatua za awali, ukahamishwa kutoka SUMA JKT kwenda Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Mkataba huo umehamishiwa NDC kwa mkataba mpya Agosti 9, 2016 na baada ya hapo wakaanza kulipwa mabilioni.

Uchunguzi unaonyesha mradi huo wenye thamani ya dola milioni 55, sawa na Sh bilioni 126.5 ulitiwa saini harakaharaka na mzabuni aliyeingia mkataba na serikali kwa nia ya kutengeneza matrekta ya awali nchini Poland, kuyaleta nchini na kujenga kiwanda cha matrekta hapa nchini, anaelekea kufilisika kwani amewekwa chini ya usimamizi wa mahakama (mufilisi) nchini humo.

Kinachosikitisha zaidi, hata pale NDC waliposafiri kwenda Poland kumuulizia mzabuni huyo inakuwaje anashindwa kutimiza matakwa ya kimkataba, mbali na kuanza kukana majukumu yake ya kimkataba kama kulipa walinzi wa kiwanda na matrekta, amekuwa wazi kuwa “kwa sasa hana uwezo wa kutekeleza mkataba huo hadi mahakama ya Poland itakapoamua hatima yake ya kufilisiwa.”

Hadi sasa mzabuni, Kampuni ya URSUS S.A., ya Uholanzi amelipwa dola milioni 33 sawa na Sh bilioni 75.9, ameleta matrekta 826 kati ya 2,400 yanayotakiwa kuletwa, na hadi tunaandika habari hii wakulima tayari wamekopeshwa matrekta karibu 500, lakini kwa bahati mbaya matrekta hayo yana viwango vya chini na ukaguzi wa ubora haukufanyika kabla ya kuletwa nchini.

Wakulima wengi waliokopa matrekta hayo wanasema yanakatika rimu za matairi ya mbele, tairi zinapata pancha kwa kiwango cha kutobolewa na ‘mbigiri’, mfumo wa umeme ni dhaifu, honi hazipigi kwa matrekta mengi, majembe hayalimi inavyotakiwa na matatizo mengine mengi yaliyoainishwa.

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), chenye makao yake makuu jijini Arusha, ambacho kina wataalamu waliobobea katika zana za kilimo na kilipewa jukumu la kuchunguza ubora wa matrekta ya URSUS kabla ya kuyauza kwa wakulima, nacho kimekiri kuwa matrekta hayo yana upungufu mkubwa.

JAMHURI limeshuhudia mawasiliano ya Juni 13, 2017 kutoka CAMARTEC kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kupitia barua yenye Kumb. Na. MRT/C/02/17/VOL. II/003 kuhusu Majaribio ya Matrekta ya URSUS na Utekelezaji wa Majukumu Mengine ya Uunganishaji Matrekta.

CAMARTEC wanasema wameamua kumwandikia rasmi Mkurugenzi wa NDC barua ya kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa matrekta hayo na barua nyingine wameziwasilisha kwa njia ya barua pepe kwa ajili ya uharaka wake hapo nyuma.

Taasisi iliingia mkataba wa kufanya majaribio ya matrekta ya Kampuni ya URSUS S. A ya Poland Oktoba 4, 2016 na kuanza majaribio ya matrekta hayo kuanzia Desemba, 2016 baada ya matrekta hayo kuingizwa nchini.

Matokeo ya jumla ya matrekta hayo kutoka Poland yameonyesha matokeo mazuri ya kulima (ekari 0.97 hadi 1.75 kwa saa) na matumizi ya mafua (lita 5.7 hadi 5.9 kwa saa). Matrekta mengi huwa yanakuwa na viwango kama hivi. “Tulifanya pia vipimo vya uhimili (durability test). Kwa upande huo tumegundua mapungufu kadha wa kadha ikiwemo:-

“i. Mfumo dhaifu wa umeme unaosababisha vifaa mbalimbali kama vile taa kuharibika mara kwa mara. ii. Udhaifu wa matairi ya mbele uliopelekea rimu za matairi hayo kuvunjika mapema na pancha za mara kwa mara.

iii. Mifumo dhaifu ya uinuaji jembe (three point linkage) uliosababisha baadhi ya vifaa vyake kuvunjika mara kwa mara.

iv. Mfumo dhaifu wa kuvuta mafuta (throttle), kutoa moshi (exhaust) na kuchuja hewa (air cleaner) iliyokuwa ikiharibika mara kwa mara.

v. Baadhi ya sehemu zilizoharibika kama vile “front axle support” na “rim” zinaonyesha udhaifu wa baadhi ya vipuri vilivyotengenezwa kwa kumiminwa (casting). Hivyo, upo uwezekano wa sehemu mbalimbali zilizotengenezwa kwa kumiminwa kuwa dhaifu.

vi. Udhaifu mwingine umeelezwa zaidi kwenye ripoti zetu tulizoambatanisha,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo iliyoandikwa na Prof. Siza Tumbo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC na kunakiriwa kwa Katibu Mkuu (Viwanda), Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, inasema majibu hayo ni utekelezaji wa barua ya Mkurugenzi Mkuu wa NDC yenye Kumb. Na. CAN. 143/547/01/101 ya Januari 6, 2017.

CAMARTEC pia ilipeleka wafanyakazi wake wawili (secondment) Kibaha kujiunga na watumishi wengine wanaounganisha matrekta eneo la TAMKO kuanzia Mei 5, 2017. Pia, wanaye mtaalamu mmoja anayehudhuria katika Kamati ya Ufundi inayoshughulikia mradi huo.

“CAMARTEC inashauri madhaifu yaliyoanishwa kwenye ripoti zetu yafanyiwe kazi kabla ya matrekta hayo kuanza kuuzwa. Matrekta hayo yakisambazwa kama yalivyo sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kuharibika kabla ya kumaliza msimu mmoja wa kilimo. Suala la msingi ni kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa na serikali kupitia mradi huu yanafikiwa kikamilifu,” inasema CAMARTEC.

Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Pythias Ntella, aliyechukua nafasi ya Prof. Tumbo, ameliambia JAMHURI kuwa yuko vikaoni, hivyo hakuweza kuizungumzia barua hii.

Malipo yatolewa licha ya onyo

Kampuni ya URSUS pamoja na kukiri kuwa kwa sasa haina uwezo wa kuendelea na mradi huo hadi hali yake ya ufilisi itambulike hatima yake, bado imeendelea kudai malipo na sasa imekwisha kulipwa asilimia 60 ya malipo yote.

Mradi huu una thamani ya dola milioni 55, sawa na Sh bilioni 126.5, hivyo kwa kulipwa asilimia 60 kama alivyokiri Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ni wazi serikali imekwisha kulipa dola milioni 33, sawa na Sh bilioni 75.9.

Barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Doto M. James, ya Desemba 20, 2016 yenye Kumb. Na. CAN. 143/547/01/97 ikirejea mkataba wa Oktoba 22, 2015 kati ya URSUS na SUMA JKT kama ulivyohamishiwa NDC Agosti 9, 2016, aliruhusu kufanyika malipo yenye thamani ya dola milioni 22 kama sehemu ya mkataba kati ya Serikali ya Poland na Tanzania kupitia mkopo wa masharti nafuu.

Doto alilipa dhidi ya barua ya URSUS yenye Kumbu. Na. DUA-DZ. 5532.1.2016.TZ.BK ya Novemba 8, 2016. Fedha hizi zilikuwa zinakwenda katika Benki ya GOSPODARSTWA KRAJOWEGO, kulipia ankara ya URSUS Na. FZT/LX/2016/00001 ya Novemba 7, 2016 yenye thamani ya dola milioni 22.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Doto, alitoa malipo hayo baada ya kuthibitishiwa na NDC kupitia barua Na. NDC/URSUS/25112016 ya Novemba 25, 2016, ikithibitisha kuwa Kampuni ya URSUS yenye anwani ya Freezerow 7 Street, PC: 20-209 Lubdili Poland, imewasilisha ankara iliyotajwa baada ya kuleta matrekta yenye ubora kwa mujibu wa mkataba.

URSUS yawekwa chini ya Mufilisi

Novemba 7, 2018 Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Urekebishaji na Ufilisi ya jijini Lublin yenye makao makuu yake Swidnik, 9th Department, kupitia Jaji Katarzyna Sacharuk baada ya kusikiliza madai ya wadeni wa Kampuni ya URSUS S. A jijini Lublin, alianzisha mchakato wa ufilisi. Ilimteua Mshauri wa Urekebishaji, Dariusz Warda mwenye leseni Na. 248 kusimamia kazi hii.

NDC, URSUS wafanya kikao kigumu

Machi 25 na 26, 2019 NDC na URSUS walifanya kikao jijini Warsaw na Lublin katika ofisi za URSUS, kilichobainisha wazi kuwa URSUS hawana tena uwezo wa kuzalisha matrekta au kujenga kiwanda nchini Tanzania, bali wanasubiri majaliwa ya Mungu kupata uwezo huo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa URSUS S. A, Michal Nidzgorski, Mhandisi wa URSUS S. A, Roman Kusiak, Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mikidadi Alli, Mhandisi kutoka CAMARTEC, Fred Magamba, Mhandisi kutoka NCD, Pascal Malesa na Katibu wa Shirika la NDC, Henry Bakaru, rangi na uwezo wa URSUS ulionekana wazi.

Katika kikao hicho, Mhandisi Malesa alieleza bayana kuwa safari ya ujumbe huo kutoka Tanzania ilihusiana na mkataba kati ya URSUS S. A na NDC. Pia aliomba radhi kwa kutofika kwa Mkurugenzi wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ambaye kibali chake cha kusafiri nje ya nchi kilichelewa kupatikana hivyo akashindwa kusafiri.

Mwenyekiti wa kikao, Nidzgorski, alieleza historia ya URSUS S. A iliyoanzishwa mwaka 1893, hivyo ilikuwa na umri za zaidi ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwake. Pia aligusia mabadiliko ya kiuchumi yaliyotokea nchini Poland. Alieleza kuwa kampuni hiyo inazalisha pia mabasi ya umeme na vifaa vingine vya kilimo.

Ujumbe wa Tanzania uliulizia juu ya taarifa za Kampuni ya URSUS S. A kuwekwa chini ya Mufilisi kuanzia Novemba 7, 2018, na kwamba ina matatizo makubwa ya kifedha. Katika kikao hicho, ilibainika kuwa soko kubwa la matrekta ya ARSUS lilikuwa nchini Poland na nchi nyingine za Jumuiya ya Ulaya. Ilielezwa kuwa kwa mwaka URSUS ilikuwa na uwezo wa kuuza matrekta 22,000 nchini Poland pekee.

Hata hivyo, baada ya Jumuiya ya Ulaya kuiondolea ruzuku Kampuni hii ya URSUS S. A, uwezo wa kuuza matrekta yake ulishuka hadi matrekta 6,000 kwa mwaka na yakawa yanauzwa nchini Poland pekee, hali iliyowaumiza kimapato. Hii ilitokana na uamuzi wa Serikali ya Poland wa mwaka 2016 ambapo ilisitisha utoaji wa ruzuku za matrekta chini ya mpango wa ruzuku wa Jumuiya ya Ulaya.

“Kutokana na hali hii, matrekta yote yaliyokuwa yamezalishwa kuuzwa katika Jumuiya ya Ulaya ikawa hayauziki tena. Hali hii imeathiri mapato ya kampuni na ikashindwa kutimiza matakwa ya wateja, ikiwamo uzalishaji wa matrekta ya kuuzwa Tanzania,” anasema mtoa taarifa kutoka URSUS.

Kutokana na kuondolewa ruzuku, Kampuni ya ARSUS S. A inasema imeanza kufanya marekebisho kuepusha isifilisike, na iliwasilisha mpango wake wa marekebisho mahakamani Machi, mwaka huu, ambao uamuzi wa hali ya kampuni iwapo ifilisiwe au la, ulipaswa kutolewa ndani ya siku 60, hivyo walitarajia kufikia Juni, mahakama ingekwisha kutoa uamuzi kufahamu hatima yake. Hata hivyo, hadi leo hakuna kinachoendelea.

Kwa matumaini hayo, URSUS ikauaminisha ujumbe wa Tanzania kuwa kufikia Oktoba, mwaka huu ingeweza kuzalisha matreka yote 2,000 yaliyosalia kwa ajili ya soko la Tanzania na kuyaleta nchini. Matumaini yao yalilegezwa na uamuzi wa awali wa mahakama iliyoizuia URSUS kuzalisha baadhi ya bidhaa zilizokuwa zinauzwa kwa mkopo.

“Wawakilishi wa NDC walipata shida kusikia kuwa URSUS imewekwa chini ya Mufilisi. Ujumbe uliomba kupewa nakala ya amri ya mahakama kabla ya kurejea nchini. URSUS iliahidi kutoa nakala ya Amri ya Mahakama kabla ya kuondoka Poland, ila hilo halikuwezekana,” kinasema chanzo chetu.

Kwa minajili hiyo, URSUS kwa upande wake ikataka mkataba kati yake na NDC ufanyiwe marekebisho kwa maelezo kuwa mchakato wa kuwa chini ya mufilisi umewapotezea muda, hivyo wasingeweza kuzalisha matrekta kwa wakati. NDC iliahidi kuwasilisha ombi hilo serikalini.

Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha matrekta pale TAMCO Kibaha, URSUS walisema NDC ilikuwa na jukumu la kumaliza matatizo ya mgogoro wa mpaka wa ardhi kati ya TAMCO na TANROADS. NDC imeishamaliza mgogoro huu, ila URSUS hadi leo wakipigiwa simu au kuandikiwa barua hawajibu.

NDC imekwenda hatua mbele ikamteua Mhandisi Rebecca Masalu kuwa Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Matrekta. Mhandisi Rebecca amezungumza na JAMHURI na kuliambia kuwa ujenzi umechelewa kutokana na taratibu za kupata msamaha wa vifaa vya kujengea kiwanda hicho na bidhaa za hapa ndani.

“Hivi tunavyozungumza, suala hili na kila kitu kwa upande wetu kinakwenda vizuri. Kuna masuala ya msamaha kwa local content (bidhaa za ndani) kama saruji na nondo wakati wa ujenzi. Exemption (msamaha) ya vifaa vya viwanda wamepata (URSUS), ila local content ndiyo tunayofuatilia, hata leo kuna watu wamekwenda Dodoma, ila yote haya taratibu zinakwenda vizuri… sasa suala la ubovu wa matrekta niombe umuulize anayesimamia matrekta ndiye anayepokea malalamiko, mimi nipo upande wa kiwanda,” amesema Mhandisi Rebecca.

Kwa upande wake, NDC imeamua kuachana na mpango wa kuwaombea msamaha wa vibali vya kufanya kazi wataalamu kutoka URSUS wakati wanajenga kiwanda na kuamua kulipa gharama hizo, ila bado mambo magumu.

Malipo ya walinzi

Katika kikao hicho, URSUS walipoambiwa suala la kulipa walinzi wanaolinda matreka na eneo la kiwanda, ambao kwa zaidi ya miezi 12 sasa hawajalipwa mishahara, na kwamba NDC iliingilia na kulipa mishahara ya miezi miwili kwa matumaini kuwa itarejeshewa na URSUS, URSUS imegeuza kibao na kusema jukumu la ulinzi kimkataba lilikuwa la SUMA JKT, hivyo wao hawawajibiki.

Walikwenda mbali zaidi na kutangaza kuwa tayari wametoa taarifa ya nia ya kujiondoa kwenye suala la ulinzi wa matrekta, hivyo jukumu hilo lihamie NDC. Walijichanganya na kuongeza kuwa kwa wao kuwa chini ya Mufilisi, hakuna uwezekano wa kulipa gharama za ulinzi.

Hata hivyo, ingawa URSUS wanasema ulinzi si jukumu lao, wanasema: “Ikiwezekana tuingie makubaliano (MoU) na NDC walipe walinzi kwa niaba yetu na hali yetu (URSUS) ya fedha ikiwa nzuri au kupitia malipo ya kimkataba [kwa URSUS kutoka Serikali ya Tanzania] tutalipa gharama hizo za walinzi.”

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya PRC Associate Security Tanzania Limite, Pantaleo Butunga, amesema waliingia mkataba wa ulinzi na URSUS miezi 18 iliyopita na siku chache zilizopita waliwaandikia wakidai kuwa wanataka kuvunja mkataba walete walinzi wengine, ila hadi sasa hawajaleta walinzi wengine.

“Mpaka sasa huu ni mwezi wa 18 walinzi wangu wanaishi kwa shida, mpaka sasa naendelea kuwasaidia. Kuanzia Januari [mwaka huu] NDC walichukua jukumu la kuwa wanawalipa walinzi. Hii ni baada ya wao kwenda Poland,” Butunga ameliambia JAMHURI na kuongeza:

“Nikawaambia kwa nini wasitulipe? URSUS hawajibu barua zetu zaidi ya miezi 8 hatuna mawasiliano nao. Niliwaomba NDC kwamba kwa nini wao wasichukue jukumu la kuvunja mkataba, tukaingia nao mkataba.” Baada ya hoja hiyo, anasema NDC walimweleza kuwa walikwenda Poland na URSUS wakasema “hawatasema lolote hadi mwezi wa 10 mwaka huu.”

Ameliambia JAMHURI kuwa sasa hivi NDC wanawalipa walinzi kila mwezi, ingawa si kwa mkataba walioingia na URSUS. Anasema, kipindi kilipokuwa kigumu walinzi wengine wamekwenda kufungua kesi kwenye Kamati ya Kazi, TUICO Mkoa.

“Wamefungua kesi kutushitaki kuwa sisi hatulipi mshahara, walidiriki kumfungia Mzungu aliyekuwa pale mara kwa mara. Alipoona wanamfungia mlango wakati walikuwa na silaha, nasi tukawasimamisha kazi wawili. Tutawalipa haki zao tusubiri hadi Oktoba, maana na sisi tunaendelea kudai,” amesema.

Kampuni hii ya ulinzi imepeleka suala lao Wizara ya Fedha, kupitia NDC ambao wameanza kutoa mishahara ya walinzi sita sawa na Sh 180,000 kila mwezi, ila gharama nyingine za kimkataba hazilipwi.

“Miezi 18 sisi tunawadai URSUS, tuliwaomba watulipe watawakata URSUS, wakasema wao hawana mkataba na URSUS [kuwaruhusu walipe walinzi], wanaweza kuja wakakataa kwamba hatuna huo mktaba. Basi tukasema sisi ni Watanzania, mali ni ya Watanzania, ukiacha kuwalipa walinzi chochote kitokee, tukasema kiutu, wakasema angalau tutafute fund. Walipopata hizo fund wenyewe wanajua, sasa angalau walinzi wanalipwa na NDC ila bado tunawadai URSUS,” amesema.

Kuhusu URSUS kuvunja mkatba, PRC Associate Security Tanzania Limited, imesisitiza kuwa iliingia mkataba na URSUS. “Tuliwaomba kazi hao hao URSUS. Walituandikia barua ya ku-terminate (kuvunja) mkataba wakasema wataleta walinzi wengine. Wakasisitiza Agosti, 2018 tunavunja mkataba tunakuja kuleta walinzi wengine na kuwalipa haki zenu, lakini hadi leo hatujawaona. Tunashindwa kukimbia lindo… Mzungu (Roman) aliyekuwa mwakilishi wao hapa kiwandani aliondoka kama anakwenda Krismasi, Desemba mwaka jana, pengine baada ya kuona kila siku anafungiwa geti na watu wenye silaha ambao hawajalipwa akaogopa, akasema anaweza kupigwa risasi… akaondoka. Mimi niliwaambia walinzi msifanye tatizo la kumpiga tukaonekana sisi tunafukuza wawekezaji,” amesema.

Deni la dola 272,586.5

NDC ililazimika kuilipa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) dola 272,586.5 sawa na Sh milioni 626.94 kutokana na URSUS kuchelewesha nyaraka za kutolea matrekta 826 yaliyowasili mwanzo. NDC ilitaka kulipwa deni hilo ifikapo Oktoba 2018. URSUS waliahidi kulipa deni hilo mara tu mchakato wa ufilisi uliopo mahakamani utakapokamilika, lakini hadi leo ni Agosti, 2019 haijalipa deni hili.

Ubovu wa matrekta

Matrekta yaliyoingizwa nchini kwa ujumla wake katika ripoti mbalimbali yamebainika kuwa na ubovu wa aina 20. Kati ya aina hizo za ubovu, aina 5 zinaonekana kuwa kila trekta lina ubovu huo, ambao ni betri mbovu, tairi za mbele kupata pancha, rimu za mbele kuvunjika, mfumo wa umeme na mkao wa jembe la kulimia.

NDC wamewaeleza URSUS kuwa kwa mujibu wa CAMARTEC, matrekta waliyoleta nchini ni mabovu, yanahitaji marekebisho. URSUS walichosema ni kuwa waandaliwe orodha ya ubovu uliopo na inapowezekana NDC ifanye marekebisho na matengenezo yanayowezekana kisha wao watairejeshea NDC fedha zake kutokana na fedha za kimkataba zilizoko Tanzania.

NDC imeeleza bayana kuwa gharama za kurekebisha trekta ya 75HP iliyouzwa Tanzania ni Sh 2,185,00 kwa kila trekta na kwa trekta ya 50HP ni Sh 2,153,500. Ripoti ya CAMARTEC iliongeza kuwa ubovu huo umebainika wakati matrekta yakiwa yamekwisha kufika Tanzania kutokana na ukweli kwamba haukufanyika ukaguzi kabla ya kuyaingiza nchini. URSUS waliomba kupewa muda kuipitia taarifa ya CAMARTEC.

Mradi huu ni mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Poland, ambapo kwa Tanzania Shirika la Suma JKT ndilo lililoingia mkataba wa kuzalisha na kusambaza matrekta hayo kwa kushirikiana na URSUS, lakini baadaye mkataba huu ulihamishiwa NDC.

Kuanzisha vituo vya ukarabati

NDC imewajulisha URSUS masikitiko yake kuwa pamoja na kwamba matrekta 826 yamekwisha kufikishwa hapa nchini, bado hawajajenga vituo vya matengenezo ya matrekta hayo na vifaa ya kutumia kuyakarabati kama ilivyo kwenye mkataba.

Hadi NDC wanawasiliana na URSUS, Machi mwaka huu, waliwaambia kuwa tayari wamekopesha matrekta zaidi ya 450 kwa wakulima, lakini kwa kutokuwapo vituo vya kukarabati matrekta hayo kusaidia wakulima walioyanunua ni tatizo kubwa.

URSUS kama walivyojibu katika hoja zote, wamesema wataleta vifaa ya kukarabati matrekta hayo na kujenga vituo vya kukarabati matrekta hayo, mara tu wakiishajua hatima ya kesi yao ya ufilisi iliyoko mahakamani.

Wakulima waeleza matatizo

Wakulima kutoka Iringa, Babati, Morogoro na maeneo mbalimbali ya nchi waliozungumza na JAMHURI, wamesema kuwa matrekta hayo ya URSUS yanawasumbua kwa kiasi kikubwa na wanapata shaka iwapo yataweza kufanya kazi kwa miaka miwili na zaidi.

Martine Qamary Ori wa Babati, Manyara, ameliambia JAMHURI kuwa betri mbovu, rimu zimevunjika, breki, wiring, taa zinazimika, cable ya accelerator (chapuzi) imekatika, gearbox inavujisha mafuta.

Athumani Hemed Kazikubwa – Kilindi, amesema pini ya kati ya kwenye kifua cha trekta inachomoka, wakati trekta linalima wanarudishia.

Ibrahim George Voniatis wa Ndanda, Mtwara, anasema kuhusu tairi za mbele: “Inakuwa kama vile unatembelea ‘tyubu’, yaani miba kidogo tu, tunakuta umepata pancha, hilo ndilo tatizo kubwa ambalo naliona.” Amenunua tairi za mbele mpya kwa Sh 400,000 na akaongeza: “Wiring ilikuwa inasumbua ile ya mwanzo ya 4wheel, honi switch inakataa, switch ya taa, switch… tairi hizi ni za Ulaya, hazifai hapa kwetu.”

Peter William Hhayuma, Mwenyekiti wa URSUS Tractors Family, katika maeneo ya Hanang, Karatu, Babati, Mbulu na Itigi, umoja ambao una wanachama 50, anasema: “Hili tatizo la rimu linachangiwa na adjustment ya jembe wakati unalima.

“NDC kwa sababu ni wageni na hiki chombo hawakuwa na wataalamu wa kuendesha haya matrekta, lakini mafundi wa vijijini kwa sababu ni wazoefu wamebaini, kuwa kisu cha nyuma kimenyooka, wamekipindisha kwa kukata shafti, unaipindisha ili iweze kuvuta, usipofanya hivyo unailazimisha kwenda kwenye system (mfumo) ambayo siyo.

“Oil kuvuja, kuna matatizo ya uvujaji na hilo linachangiwa katika hali ya ufungaji, zinakuja kuungwa hapo Dar es Salaam, kuna uzembe katika hatua za ufungaji ninavyoona mimi… ni kwamba chombo chako unapochukua, hata kama ungechukua gari mpya ukaamua kuanza nayo kwa kudhani kuwa ni mpya unakwenda mbele lazima itakuletea shida.

“Kununua nati, bolti… la kwangu, uvujaji ulikuwa kwenye tela nyuma, ilikuwa kumbe kuna seal kule nyuma imekufa, lakini kwa sababu ilikuwa kwenye ‘guarantee’ waliruhusu tuitengeneze.”

Wakulima wanalipa asilimia 10 ya bei ya kununulia trekta hiyo iliyopata msamaha wa kodi na kukabidhiwa trekta, hivyo 75HP inauzwa wastani wa Sh milioni 56 na ya 50HP inauzwa Sh milioni 45. “Mrejesho wake ni miaka 4, unarejesha bila riba, na mwaka wa 5 ndipo unalipa 10%. Kwa kweli huu ni ukombozi kwa mkulima, maana benki nyingine mpaka upeleke hati.

“Katika mpango huu unapeleka barua ya kijiji, kata au mkurugenzi wako anayekufahamu unakopeshwa trekta… kwa hiyo inarahisishia wakulima, baada ya kuona kwamba hili jambo ni zuri, watu tumeamua kuanzisha umoja na kama kuna tatizo mawasiliano yetu mtu anapiga simu unawajulisha huko NDC.

“Yalikuwa na tatizo la matumizi ya mafuta, kwenye system ya mafuta suala la injector kwenye chombo kilichopo kwenye guarantee huwezi kugusa, akatushauri fundi wetu kwamba tufanye adjustment, huyu kijana sasa hivi NDC wamempeleka Mwanza, Mafinga kurekebisha matatizo ya matrekta haya.”

Benki ya Kilimo yalalamika

Benki ya Kilimo (TADB), imeandika barua NDC ikilalamika kuwa wakulima 32 iliowakopesha fedha kununua matrekta hayo hawalipi mikopo yao kwa maelezo kuwa matrekta ni mabovu na ikaiambia NDC kuwa kuanzia sasa haitakopesha mkulima mwingine hadi matatizo ya matrekta ya URSUS yawe yamepatiwa ufumbuzi.

JAMHURI limewasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kilimo, Japhet Justine na kumuuliza amejibiwa nini kwani orodha ya waliokopa gazeti limeiona. Mkurugenzi huyo amejibu kupitia kwa Meneja wa Mawasiliano wa TADB, Chaba Rhuwanya, kuwa benki imewakopesha wakulima hao kama wakopaji wengine na si jukumu la benki kufahamu mkulima ananunua trekta kutoka kampuni ipi, ila kwao wakulima wanapofika kukopa ni fursa kwao kufanya biashara.

Hata hivyo amesema mawasiliano kati ya TADB na NDC yana mwelekeo mzuri kwani NDC imewajulisha kuwa imeomba ushauri wa kitaalamu kutoka BICO pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivyo wanaamini kama matrekta ya URSUS yana matatizo yatarekebishwa na mkulima ataendelea kufaidika.

Prof. Gabagambi NDC alonga

Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ameliambia JAMHURI katika uchunguzi wa habari hizi na hasa suala la rimu kuvunjika akakiri kuwapo kwa tatizo hili na akaongeza kuwa wamepata ufumbuzi: “Yale matatizo yote yale yanarekebishika. Kwa sasa tunatumia KMCC Moshi, Kilimanjaro Machine Tools, tunabadilisha rims kabla hatujauza katika ku-arrest situation (kunusuru hali). Tunajitahidi kuyahudumia. Kuhusiana na yale ambayo hayajaja 1,575, hayo hatutakubali yaje bila kurebishwa kabla hayajaja.

“Defects hizi ni za kawaida, hata ukienda katika hizo akina Massey Ferguson ukiangalia kuna tatizo fulani wakati wanaanza,” amesema Prof. Gabagambi. Alipoulizwa tairi kupata pancha mara kwa mara, akasema: “Ni kweli matairi yale yametengenezwa kwa ajili ya Ulaya, yamekuja Afrika, tutayarekebisha na yatatulia. Wananchi wanaomba kukopeshwa. Hadi sasa tumeleta matrekta 825, demand (mahitaji) ni kubwa sana. Na bado watu wanataka kuchukua matrekta hayo.

“Napata shaka hizi kelele za mabovu, mabovu, zisije zikawa zinatoka kwa washindani wetu ambao nina uhakika hawawezi kuuza trekta hata moja kwa sasa. Trekta kuharibika ni jambo la kawaida, maana hata barabarani tunakuta magari yameharibika.”

Alipoulizwa kama hayana shida kwa nini wameingia mkataba na KMCC ya Moshi na BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwamba gharama za matengenezo wanayofanya nani atazilipa kwani URSUS  walipaswa kuleta matrekta yasiyo na matatizo, amesema: “Tumekubaliana na URSUS kwamba watazilipa, tuendelee na marekebisho.”

JAMHURI limehoji hii ya URSUS kampuni iliyoko chini ya Mufilisi ikifirisiwa hizo fedha atalipa nani, Prof. Gabagambi akaongeza: “Huu ni mkataba kati ya nchi mbili, si mkataba kati ya URSUS na NDC. Ni jukumu la kila nchi kuhakikisha kila mtu ana-deliver (anautekeleza). Kwetu mkataba huu ulikuwa chini ya SUMA JKT, wakashindwa kuutekeleza, Serikali ya Tanzania ikauhamisha haraka sana kuja NDC ili mradi uendelee.

“Itakapodhihirika wameshindwa, ni jukumu la Serikali ya Poland kumbail-out (kumwezesha) ARSUS afufuke amalizie mradi kulinga na mkataba…,” alipoulizwa kama Serikali ya Tanzania ameijulisha matatizo ya URSUS, akajibu: “Si kwamba tumekaa kimya, kuna taratibu zake za kiserikali ambazo zimeishafanywa. Zote zimeishafanywa.”

Amesema serikali imekwishalipa asilimia 60 ya malipo ambayo ni dola milioni 33, sawa na Sh bilioni 75.9, na kwamba URSUS wamekwishaleta matrekta 825, ingawa takwimu halisi ambazo JAMHURI linazo zinaonyesha yameingia nchini matrekta 826, na kwamba hayo 1,574 yaliyosalia kampuni hii iliyowekwa chini ya Mufilisi inayosema haina fedha inadai kuwa itayaleta kwa wakati ifikapo Oktoba hii bila wasiwasi. Mradi wote gharama yake ni dola milioni 55 sawa na Sh bilioni 126.5.

Pamoja na kupokea asilimia 60 ya malipo, matrekta iliyoleta URSUS ni sawa na asilimia 34 ya mradi wote wa matrekta 2,400. Kwa wastani Tanzania ilikuwa inaingiza matrekta 200 kwa mwaka. Matrekta huwa yanafanya kazi hadi miaka 50 bila kuharibika. Idadi hii ya matrekta 2,400 ingechukua wastani wa miaka 12 kuingizwa nchini chini ya utaratibu wa kawaida, ila bahati mbaya matrekta haya yanayoingizwa mengine yanaharibika kabla ya kufikishwa shambani.

Wakala wa URSUS anena

Mtanzania anayetajwa kuileta Kampuni ya URSUS nchini, Julius Zellah, alipohojiwa na JAMHURI kwa nini kampuni hii imeshindwa kutekeleza wajibu wake kimkataba na kwamba imeleta matrekta mabovu nchini, amesema: “Ule ni mradi wa Serikali ya Tanzania. Hivyo hizo habari ungewasiliana na NDC kabla hujazitoa. Mimi sikubaliani nazo kwani wakulima kadhaa wanatumia instructions (maelekezo) tofauti na manual (kitabu cha maelezo).”

Hata hivyo, Zellah amesema ni lazima URSUS walete “service van”, yaani gari la kufanya matengenezo kwa matrekta hayo liwasaidie wakulima maeneo ya vijijini.

JAMHURI limemweleza Zellah kuwa tangu URSUS waingie kwenye msukosuko wa kufilisiwa, hawajibu barua za NDC, hawapokei simu wala kuijibu Kampuni ya Ulinzi inayolinda eneo la TEMCO pale Kibaha, naye akasema: “Ni kweli, juzi tulikaa na URSUS. Wataanza kujibu kila e-mail.”

Naibu Waziri Bashe ajibu

Kwa kuwa suala la matrekta linagusa kilimo, JAMHURI limemtafuta Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliyesema: “Suala la matrekta ni suala ambalo lipo Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya NDC, kwa hiyo sisi hatuna cha kusema kwa sasa, lakini tutafuatilia kujua kama wakulima wameathirika.”

Waziri Bashungwa amrushia KM

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alipoulizwa na JAMHURI na kupewa vielelezo jinsi Kampuni ya URSUS isivyokuwa tayari kuendelea na mkataba kwa sasa hadi ifahamu hatima yake katika kesi inayoikabili kufilisiwa, amesema: “Nipo mkutano wa SADC, naomba uwasiliane na Katibu Mkuu.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Buchweishajia, yeye amejibu kwa ufupi. “Tuwasiliane baadaye.”

JAMHURI linafahamu kuwa suala hili limegeuka kaa la moto na ndani ya wiki hii NDC itawasilisha taarifa nzito serikalini kuonyesha ubovu wa matrekta yanayoingizwa nchini na URSUS, ambapo kwa nia ya kuokoa fedha za walipa kodi inayo mapendekezo kadhaa ikiwamo kuangalia uwezekano wa kuvunja mkataba, ingawa baadhi ya watendaji wa NDC wanakataa hoja ya kuvunja mkataba huo bila kueleza unawanufaisha au nchi kwa kiwango gani.