Serikali imesema itachukua uamuzi mgumu dhidi ya Chama cha Ushirika wa Mazao cha Lyamungo AMCOS kutokana na chama hicho kukaidi maagizo yake kuhusu kuondoa zuio mahakamani linalohusiana na shamba la kahawa la Lyamungo.

Shamba hilo limekuwa kwenye mgogoro usiokwisha kwa miaka 14 sasa kutokana na msuguano uliopo kati ya Lyamungo AMCOS na Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU), ambapo kila upande unadai shamba hilo ni mali yake.

Hata hivyo nyaraka ambazo JAMHURI linazo, ikiwamo barua ya aliyekuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kwa wakati huo, Sr. George Kahama, ya Oktoba 21, mwaka 2005, yenye namba ya kumbukumbu namba CFA. 64/207/01/18, shamba hilo ni mali ya KNCU.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa 35 wa KNCU uliofanyika hivi karibuni mjini Moshi, Afisa Ushirika Mkuu, Benjamin Mwangwala, kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, amesema serikali itafanya uamuzi mgumu juu ya ukaidi wa chama hicho wa kuondoa zuio hilo mahakamani.

“Naomba niseme wazi kwamba kwa suala la Lyamungo sasa imetosha. Waziri alishafanya uamuzi, nani anazuia, nani ameweka zuio mahakamani? Hatutakubali suala hili liendelee kutuumiza vichwa, serikali tutafanya uamuzi mgumu kuondoa hilo zuio mahakamani,” ameonya.

Mwangwala ambaye alimwakilisha Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini katika mkutano huo alisema serikali haitavumilia ukaidi unaofanywa na chama hicho ambacho pia ni mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa KNCU.

Waziri Kahama katika barua yake yenye kumb. Na. CFA.64/207/01/18 ya Oktoba 21, mwaka 2005 ambayo ilitumwa kwa mwenyekiti na wajumbe wa Bodi ya Chama cha Msingi cha Ushirika Lyamungo kwa wakati huo ilihitimisha mgogoro huo baada ya kuweka wazi kuwa shamba hilo ni mali ya KNCU.

Barua hiyo ya Kahama ambayo JAMHURI inayo nakala yake ilikuwa ikijibu rufaa ya chama hicho iliyokatwa dhidi ya uamuzi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini wa Machi 26, mwaka 2005 ulioipa haki KNCU kuwa mmiliki halali wa shamba hilo.

Msingi wa shamba hilo kuwa mali ya KNCU ni kutokana na chama hicho wakati huo kikijulikana kwa jina la New Machame Lyamungo Co-operative Society kupewa mkopo Sh 210,000 kutoka KNCU kwa ajili ya ununuzi wa shamba hilo .

“Kwamba baada ya mawasiliano ya muda mrefu kuhusu jinsi ya kurejesha mkopo huo, chama chenu kiliwasilisha kwa KNCU Ltd utaratibu wa kulipa deni la shamba ambapo mlipendekeza kulipa deni hilo kidogo kidogo kwa miaka mitano kuanzia 31/12/1967 hadi 31/12/1971.

“Kwamba mapendekezo yenu yalijadiliwa na kukubaliwa kwenye kikao cha Halmashauri ya KNCU Ltd cha tarehe 25 -27/10/1967 na hatimaye kuwekwa saini tarehe 16/12/1967,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Barua ya Waziri Kahama inaainisha kuwa hadi kufikia mwaka 1972 baada ya muda wa kulipa deni kumalizika, chama hicho kilikuwa kimeweza kulipa Sh 34,000 tu kama marejesho ya mkopo wa shamba.

Inafafanua kuwa, kutokana na makubaliano ya Desemba 16, 1967 kukiukwa, KNCU iliitisha mkutano mkuu uliofanyika Julai 14 na 15, 1972 na kupitisha azimio kuwa shamba la Lyamungo lichukuliwe na KNCU na kwamba Chama cha Msingi Lyamungo kirejeshewe Sh 34,000 ambazo kilikuwa kimelipa KNCU.

Waziri Kahama alieleza katika uamuzi wake kuwa baada ya mkutano huo wa KNCU, chama hicho cha Lyamungo kupitia kwa aliyekuwa mwenyekiti wake, Shemikaeli Nikodemo, kilisaini hati ya kuhamisha umiliki wa shamba hilo kwenda KNCU Agosti 20, 1973 na kuanzia hapo shamba hilo likaorodheshwa kwenye mizania ya KNCU.

Barua hiyo ikasisitiza kuwa, ni dhahiri kuwa mabadiliko ya umiliki wa shamba la Lyamungo kutoka kwenye chama hicho kwenda KNCU Ltd yalizingatia taratibu na sheria ya vyama vya ushirika ambapo uamuzi hufanywa na wanachama kwenye mikutano mikuu.

“Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 52(6) ya kanuni za vyama vya ushirika 2004, nakubaliana na uamuzi wa mrajis wa tarehe 29/3/2005 kuwa shamba la Lyamungo ni mali ya KNCU Ltd. Kwa hiyo, kwa barua hii mnaelekezwa kuondoa vikwazo vyovyote vile mlivyokuwa mmeweka ili KNCU waendelee na umiliki wa shamba hilo na kulitumia kadiri watakavyoona inafaa,” inahitimisha barua hiyo.

Hata hivyo chama hicho kupitia kwa Mwenyekiti wake wa sasa, Gabriel Ulomi, kinasisitiza kuwa samba hilo ni mali yake na kwamba KNCU walighushi nyaraka na kujimilikisha shamba hilo.

Mwenyekiti huyo wa Lyamungo AMCOS, anasema katika taarifa yake kuwa shamba hilo lilinunuliwa kutoka kwa raia mmoja wa Ugiriki, Philip Filios, mwaka 1965 na kilichokuwa Chama cha Ushirika cha New Machame Lyamungo Co-operative Society.

Amesema chama hicho ambacho kwa sasa ndicho kinaitwa Lyamungo AMCOS, kilipewa stakabadhi ya malipo namba 1150 kutoka kwenye kampuni moja ya udalali ya mtu anayetajwa kwa jina la ‘Mrs Z. Ramzan’ baada ya shamba hilo kununuliwa kwa njia ya mnada.

“Mwaka 2003 wanachama na wananchi wa Lyamungo walipigwa butwaa walipoona gazetini kuwa shamba lao litauzwa kwa njia ya mnada chini ya kampuni ya udalali kutokana na deni la Sh milioni 500 lililokopwa na KNCU kutoka KCBL,” amesema Ulomi.

Mwaka 2007 aliyekuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. A. K. Kashuliza, alikiandikia barua chama hicho cha Lyamungo na kukipa siku 21 kuondoa zuio lake mahakamani lakini hadi sasa chama hicho hakijafanya hivyo.

Katika barua yake ya Agosti 23, mwaka 2007 yenye namba ya kumbukumbu FA.64/207/04/79 kwenda kwa mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya chama hicho, mrajis huyo alionyesha kusikitishwa na hatua ya chama hicho kukataa kutekeleza maagizo hayo ya serikali.

“Hii ina maana kwamba kati yenu kuna kundi la watu ambao wanapinga amri halali ya serikali na wangependa kuendeleza migogoro inayokwamisha juhudi za maendeleo ya wananchi wa Kilimanjaro,” inasema barua hiyo.

Hata hivyo ni miaka 12 sasa Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini haijachukua hatua.

By Jamhuri