Na Mwamvua Mwinyi, JamhiriMedia, Kibaha

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa rai kwa maofisa maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuacha tabasamu kwa wananchi badala ya kujivunia ujenzi wa majengo pekee.

Ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Maendeleo ya Jamii kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha Julai 29,2026 kilichowakutanisha maofisa maendeleo ya Jamii, wakuu wa divisheni na vitengo, wakuu wa idara pamoja na viongozi wa taasisi za Serikali na binafsi.

Kunenge alisema matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona viongozi wanaacha alama ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi, akisisitiza kuwa mafanikio ya Serikali hayapaswi kupimwa kwa idadi ya majengo yaliyojengwa bali kwa tabasamu la wananchi kutokana na huduma bora wanazopata.

Kunenge alieleza Maofisa Maendeleo ya Jamii ni kiungo wanaozifahamu changamoto za wananchi katika maeneo yao, hivyo wanapaswa kuonyesha ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aliongeza kuwa shughuli zote za maendeleo zinapaswa kuendana na dira hiyo, akieleza kuwa kufanya kazi nje ya mwelekeo wake ni kupoteza muda na rasilimali za Serikali.

Hata hivyo Kunenge aliwataka ,makatibu wakuu wa wizara mbalimbali kujadili changamoto zinazotokana na mwingiliano wa majukumu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuongeza ufanisi wa utendaji wao.

Alisema Serikali imeelekeza wizara kupitia upya sera na sheria zake ili ziendane na mahitaji ya sasa na kuwezesha utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alifafanua kikao hicho kinalenga kukumbushana wajibu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Jeremiah Mwambange, aliwaasa maofisa maendeleo ya Jamii kuhakikisha kila mmoja anakuwa na kijiji cha mfano kitakachoonyesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwambange alieleza, TAMISEMI itaanzisha utaratibu wa kukutana kila mwezi Septemba ili kupokea mrejesho wa utekelezaji wa majukumu kutoka kwa maafisa hao.

Aliagiza halmashauri zote kuhakikisha zinatekeleza utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi stahiki na kuandaa dokumentari fupi za vikundi vilivyofanya vizuri ili kuhamasisha wananchi kupitia vyombo vya habari.

Vilevile, aliwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kutumia takwimu sahihi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Pwani, Grace Tete, alisema kikao hicho cha siku mbili ni sehemu ya kuwakumbusha maafisa wajibu wao, kuwajengea uwezo na kuwapa miongozo ya utekelezaji wa majukumu.