SONGEA

NA MUNIR SHEMWETA

 

Uwekezaji ni jambo muhimu hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ambayo msisitizo wake mkubwa ni Serikali ya Viwanda na kuelekea katika uchumi wa kati.

 

Hali hiyo inatokana na uwekezaji kuwa kitu kinachoweza kusaidia upatikanaji huduma muhimu sambamba na kutoa fursa ya ajira kwa wananchi na kubiresha maisha yao.

 

Katika suala la uwekezaji eneo linalopigiwa upatu zaidi ni eneo la ardhi ambalo kila mwekezaji analihitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli.

 

Ni kwa mantiki hiyo Serikali imekuja na dhana ya uhawilishaji mashamba lengo likiwa ni kuyatumia maeneo ambayo hayatumiki ipasavyo katika shughuli zitakazowezesha uboreshaji huduma na wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

 

Hata hivyo, uhawilishaji ni sharti upate ridhaa ya wananchi wanaozunguka eneo linalowekezwa pale watakapokuwa wameridhika na kuingia makubaliano na mwekezaji anayehitaji kuhawilishiwa eneo hilo.

 

Dhana ya kushirikisha wananchi ni kuwawezesha wao kuwa wanufaika wa kwanza hasa ikizingatiwa wao ndiyo walioridhia eneo lao kutumika na mwekezaji ingawa mamlaka ya ardhi yako chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alizuru mikoa ya Lindi na Ruvuma ambako mbali na mambo mengine alihakiki uhawilishaji mashamba kwenye maeneo ya Kichonda, Wilaya ya Liwale mkoa wa Lindi, Muhukulu Lilahi na Nakawale  katika Jimbo la Peramiho, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

 

Mabula pia alifika katika maeneo yenye migogoro ya ardhi katika vijiji vya Ngadinda na Lutukila katika Halmashauri ya Madaba, Songea.  Kubwa kwa Naibu Waziri wa Ardhi ni kujiridhisha na uhawilishaji mashamba kwenye maeneo husika sambamba na kuhimiza mpango wa matumizi bora ya ardhi.

 

Mwanzo wa ziara yake ulikuwa katika Kijiji cha Kichonda, Liwale mkoani Lindi ambako changamoto kubwa aliyokutana nayo ni wananchi kuonekana kutokubaliana na mwekezaji M/S KSM & AGL EXPORT FARM Co. LTD ambaye awali walikubali awekeze katika eneo la ekari 1,000.

 

Tatizo kubwa ni kutotekeleza baadhi ya ahadi alizowapa. Baadhi ya makubaliano yalikuwa ni kuwajengea kisima cha maji, msikiti, na kusaidia vifaa katika zahanati ya kijiji hicho. Vyote hivyo hakuvitekeleza.

 

Hata hivyo, baadhi ya wanakijiji walimtetea mwekezaji kwa kusema alishindwa kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na uhakika wa kulipata eneo husika; jambo lililopingwa na baadhi yao kwa maelezo kuwa makubaliano yalikuwa yatekelezwe hata kabla ya kupatiwa eneo.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Omar Saidi akasema mwekezaji huyo anawashangaza kwani ameahidi kufanya mambo mengi, lakini hadi wakati Naibu Waziri anafika alikuwa kimya, hivyo kwao wanaona kama anawababaisha.

 

Akizungumza na wanakijiji wa Kichonda, Naibu Waziri Mabula akasema uamuzi wa kuridhia uhawilishaji shamba hakumpi fursa ya moja kwa moja mwombaji kuwa mmiliki, bali kuna hatua za kupitia kisheria kabla ya kumilikishwa.

Mabula aliyekuwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini, Gasper Luanda, na  Kaimu Kamishna wa Ardhi Vijijini, Kokwika Ishenkumba, aliwaambia wakazi wa kijiji hicho kuwa uhawilishaji ni mchakato mrefu na kwamba hata rais akikubali, lazima mchakato upitie taratibu zote za kisheria ikiwamo kutolewa siku 90 kwa mwekezaji kukaa na wana kijiji ili kukubaliana.

 

Kutokana na maelezo hayo, wananchi wa Kijiji cha Kichonda walibadili uamuzi wa awali wa kukataa eneo hilo kuhawilishwa kwa mwekezaji huyo na kukubali apatiwe kwa ajili ya uwekezaji. Ombi la ekari 1,000 kwa mwekezaji M/S KSM & AGL EXPORT ni kwa ajili ya kuzalisha alizeti, kufuga nyuki, kuku, ng’ombe, mbuzi na samaki. Liliwasilishwa mwaka 2010 na uwekezaji huo umeelezwa kuwa utaisadia Serikali kupata kodi sambamba na kupatikana huduma nyingine za kijamii pamoja na fursa ya ajira kwa wananchi wa eneo la kijiji.

 

Aidha, changamoto ya uhawilishaji ardhi ilijitokeza pia kwenye eneo la Lutukila katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma ambako wanakijiji wanamlaumu mwekezaji kampuni ya Montara Land inayojishughulisha na kilimo mchanganyiko kwa kushindwa kutekeleza makubaliano waliyofikia.

 

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Agelaus Luambano, amemlaumu mwekezaji kwa kuingia makubaliano na wanakijiji aliyoyaita ya kidanganyifu kwa kuwa kati ya mambo aliyoahidi hakuna hata moja alilotekeleza.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mabula ameitaka Serikali ya Kijiji na wananchi kuwa makini na makubaliano wanayoingia na wawekezaji.

Anasema iwapo mwekezaji hatatekeleza makubaliano waliyoingia kama vile kutoendeleza eneo la uwekezaji kinachotakiwa kufanywa na Serikali ya Kijiji ni kumpelekea ilani na asipotekeleza ndipo hatua za kumnyang’anya zifanyike.

Kinachoonekana katika maeneo hayo ni uelewa mdogo juu ya makubaliano ya uhawilishaji ardhi pamoja na kutosimama imara kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji katika kushughulikia makubaliano baina yao na mwekezaji.

 

Katika Kijiji cha Lutukila, Mabula alikumbana na mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Namtumbo na Halmashauri ya Madaba iliyopo wilayani Songea.

Wanakijiji walimweleza Naibu Waziri kuwa pamoja na wao kupimiwa eneo na kupatiwa hati za kimila, bado wamekuwa na mgogoro kuhusiana na mpaka kati yao na Wilaya ya Namtumbo hasa baada ya baadhi yao kuelezwa eneo lao liko Wilaya ya Namtumbo.

 

Akitoa ufafanuzi, Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kusini, Gasper Luanda alisema tatizo la mipaka hutafsiriwa na Tangazo la Serikali (GN), na siyo watu wengine na kusisitiza kuwa kabla ya kutangazwa lazima kazi ya kitaalamu ifanyike kuhusiana na mgawanyo wa mipaka kwa kushirikisha pande husika ikiwamo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

 

Kamishna akasema ni lazima wananchi watambue kuna ardhi ya jumla ambako Kamishna wa Ardhi ana mamlaka nayo, Ardhi ya Kijiji iliyo chini ya Serikali ya Kijiji, na Ardhi ya Hifadhi inayosimamiwa na mamlaka husika.

 

Katika ziara yake hiyo Mabula aliingilia kati mgogoro mwingine katika Kijiji cha Ngadinda, Halmashauri ya Madaba wilayani Songea ambako wananchi wanadai kukosa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikimiliki eneo kubwa la ekari 6,000.

Kwa mujibu wa wanakijiji hao, awali ilikubalika wapatiwe ekari 2,000 na wizara ibakiwe na ekari 4,000 lakini utekelezaji umekuwa mgumu na hivyo kuwaacha wakiwa njia panda.

 

Wakazi wa kijiji hicho, walisema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakitafuta maeneo ya kulima na wakati mwingine kuenda katika wilaya nyingine ya Namtumbo ambako hufukuzwa.

 

Katika kushughulikia suala hilo, Mabula aliiagiza Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kusini ishirikiane Halmashauri ya Madaba kupima eneo lote la kijiji hicho kwa lengo la kufahamu matumizi sahihi ya eneo hilo na kupanga matumizi bora.

 

“Kuanzia mwaka ujao wa fedha unaoanzia Julai 2018 lazima mje Madaba, Kamishna upange watu wako lazima suala hili lifikie mwisho na baada ya kupima ndipo itajulikana eneo hilo litagawiwa vipi kulingana na matumizi,’’ alisema Mabula.

 

Aliwataka wanakijiji wa Ngadinda kutoa ushirikiano wakati wa timu itakayokuja kufanya shughuli hiyo na kusisistiza wale wanaojua mipaka wakiwamo wazee maarufu washirikishwe ili kurahisisha kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Mabula, mara baada ya eneo hilo kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi wananchi watapata fursa ya kupata hati za kimila ambazo zitawasaidia kuondoa migogoro na kujiletea maendeleo.

 

Mabula aliwatahadharisha wanakijiji wa Nakawale, Peramiho kutofanya udanganyifu wowote wakati wa mchakato wa uhawilishaji ardhi kwenda kwa mwekezaji.

Alitoa kauli hiyo baada ya kubaini baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kusainiwa katika orodha ya wanakijiji walioshiriki mkutano wa kupitisha uamuzi wa uhawilishaji ardhi ekari 35,000 kwenda kwa mwekezaji Nkusu Theo Sugar Ltd.

Alisema udanganyifu wowote utakaofanyika katika orodha ya mahudhurio ya kupitisha uamuzi wa uhawilishaji ardhi unaweza kusababisha mchakato mzima kuchelewa.

Katika muda mfupi aliopitia orodha ya majina ya wananchi wa kijiji hicho waliohudhuria kupitisha uamuzi wa uhawishaji ardhi ya kijiji, Mabula alibaini baadhi ya wanakijiji wakiwa wamesainiwa na watu wengine.

Akasema hata kama baadhi yao hawajui kusoma ni vyema wakatumia dole gumba badala ya kusainiwa na watu wengine.

 

Alivipongeza vijiji hivyo kwa kupima maeneo yao na kuweka matumizi bora ya ardhi na kubainisha maeneo ya uwekezaji, kilimo na mifugo.

1168 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!