• CCM, Chadema, Profesa Shivji wasema muda hautoshi
  • Jaji Mtungi aonya, mnyukano waendelea, hofu yatanda

Kuna kila dalili kuwa Katiba mpya iliyotarajiwa kuzinduliwa Aprili 26, 2014 haiandikiki kwa maana kuwa muda huo hauwezi kutosha kukamilisha mchakato wa kupata Katiba hiyo, vyanzo vimelieleza gazeti la JAMHURI.

Vyanzo kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), vyama vingine na wanasheria kama Profesa Issa Shivji, vinaonesha wasiwasi kuwa muda uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Katiba mpya itapatikana ifikapo Aprili 26, 2014 hautoshi.

kama Profesa Issa Shivji, vinaonesha wasiwasi kuwa muda uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Katiba mpya itapatikana ifikapo Aprili 26, 2014 hautoshi.

Mnyika asema muda hutoshi

Mbunge wa Ubungo na Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, John Mnyika, aliiambia JAMHURI, kuwa muda uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Rais Jakaya Kikwete kuwa Aprili 26, 2014 Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani itatangazwa hautoshi.


Mnyika amesema katika mahojiano na JAMHURI kuwa Bunge la Katiba linapaswa kukaa kwa siku 70 kuanzia Januari, 2014, na sheria inataka kuwa wasipokubaliana waongezwe siku 20 na ikiwa wataendelea kutoelewana waongezwe siku 20 nyingine, hivyo akasema hizo siku 110 peke yake zinaifanya Katiba isiandikike ndani ya muda uliotajwa.


Alisema ukiacha hizo siku 110 kuna siku 90 za kuelimisha wananchi na kupiga kura ya maoni iwapo wanakubali Katiba mpya au la, hivyo ukichanganya hizo siku 90 na siku 110 zinakuwa siku 200 ambazo ni zaidi ya miezi sita.


“Katiba mpya haitapatikana tarehe 26 Aprili, 2014 kama ilivyotangazwa na Rais na Tume. Inabidi tu pande zote zijitokeze na kuwaeleza wananchi ukweli. Hii ni kwa kurejea muda unaohitajika kwa ajili ya Bunge la Katiba litakaloanza Januari, 2014 na hatimaye uchaguzi kwenye kura ya maamuzi/maoni,” Mnyika aliiambia JAMHURI.


Dhana ya Mnyika inatokana na ukweli kwamba kwa ratiba ya awali ilikuwa Bunge la Katiba lianze Novemba, mwaka huu, lakini kwa maelezo ya Rais Jakaya Kikwete kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya Alhamis (Novemba 6) kuwa ameiongezea Tume ya Jaji Warioba muda hadi Desemba 15, 2013, inathibitisha kuwa Bunge la Katiba haliwezi kukaa Novemba hii.


Chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM ambacho kwa hali yoyote hakiwezi kutajwa gazetini kutokana na hatari ya kujipalia mkaa, kilisema: “Kenya wakati NARC wanaingia madarakani waliahidi Katiba mpya ndani ya simu 100, lakini imewachukua miaka minane. Ukiongeza msuguano wa miaka minne chini ya Rais [Daniel arap], Moi basi imewachukua miaka 12 hadi 13.


“Busara inanituma kuwa tukubaliane na mawazo ya Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF anayesema wazi kuwa muda hautoshi, hivyo tufanye marekebisho ya Katiba katika maeneo machache kama Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, mapato ya vyama vya siasa na vingine vya aina hii, lakini kusema tutaandika Katiba mpya ndani ya muda huu ni kujidanganya.”

Profesa Shivji asema ni ngumu

Profesa Issa Shivji, Mhadhiri Mwandamizi (mstaafu) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameiambia JAMHURI kuwa muda hautoshi na kazi iliyoko mbele ni kubwa kuliko inavyodhaniwa. Profesa Shivji alisema kwanza inabidi kukubaliana iwapo inaundwa Serikali moja, mbili au tatu na baada ya hapo ndipo ujengwe mfumo na kuweka utaratibu wa mgawanyo wa mali za sasa.


Anasema nchi ikikurupuka itaingia kwenye matatizo yasiyo ya msingi, kwani; “Leo ukisema tunaunda Serikali tatu, Ikulu ya sasa itakuwa mali ya Tanzania au ya Tanganyika? Mali zinazomilikiwa na Serikali ya Muungano zinagawanywaje?


“Mimi sioni possibility (uwezekano), unless (vinginevyo) waharakishe kwa utaratibu ambao wananchi wasipewe muda wa kutosha na hii itakuwa ni hatari,” alisema Profesa Shivji.


Alisema kwa hali yoyote muda wa kuunda Serikali ya Tanganyika hauwezi kutosha, hivyo akapendekeza lazima yawepo maandalizi ya kutosha katika kufikia uamuzi iwapo Serikali ya ni ngapi na zitaendeshwaje.

Mgawanyiko mpya waibuka

Mkanganyiko mwingine uliojitokeza kutoka ndani ya vyama vya siasa, ni tuhuma kuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba ina msimamo unaokinzana na matakwa ya CCM, kwa sababu imeahidiwa kutetewa na Chadema iongezewe muda bungeni suala lililoshindikana.


Ingawa masuala haya yalikuwa yakisemwa kwa chini, Mnidhamu wa CCM Bungeni, William Lukuvi, alitoa kauli bungeni Jumamosi (Novemba 6) kuwa Chadema wana maslahi binafsi katika kushinikiza idadi ya wajumbe wa Bunge la Kutunga Katiba iongezwe kutoka 201 iliyopendekezwa na Serikali, kufikia 438.


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliliambia Bunge kuwa CCM wanakataa kuongeza muda wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kwa kuwa imependekeza uwepo wa Serikali tatu katika rasimu ya kwanza, hivyo wanataka iondolewe haraka.


Chanzo kutoka ndani ya CCM kiliwatuhumu Chadema kuwa wameingia makubaliano yasiyo rasmi na Tume ya Marekebisho ya Katiba kuwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba ipendekeze uwepo wa Serikali tatu; Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba Chadema wao wangeshinikiza Tume ya Jaji Joseph Warioba iongezewe muda.


“Hii iko wazi. Tume ya Marekebisho ya Katiba imekuwa Tume pekee katika historia ya nchi hii iliyotumia mabilioni ya fedha kuliko Tume yoyote. Wametumia Sh bilioni 30 kwa posho. Sasa wanatamani waongezwe muda waendelee kupata posho ya Sh 400,000 kila siku. Haikubaliki,” kilisema chanzo chetu kutoka CCM.


Chanzo kingine kiliiambia JAMHURI kuwa zimekuwapo Tume nyingi kama Tume ya Kawawa, Tume ya Amon Nsekela, Tume ya Nyalali, Tume ya Kisanga, Tume ya Msekwa, Tume ya Mboma na nyingine nyingi zilizovunjwa baada ya kukabidhi ripoti ya kazi ya msingi ziliyotumwa kupitia hadidu rejea, hivyo anashangazwa na vyama vya upinzani kung’ang’ania Tume ya Warioba iendelee kufanya kazi baada ya muda wake kuisha kisheria.


Chanzo hicho kilitoa shutuma nzito kuwa katika mapendekezo yaliyokataliwa na Serikali, Chadema ilipendekeza kila chuo kikuu kitoe wanafunzi watatu, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yatoe wajumbe 44 wa Baraza la Katiba, ila wakulima wawakilishwe na wajumbe 10 huku wafanyakazi ikipendekeza nafasi tano.


“Kwa mawazo yao, Chadema walidhani wanakubalika mno katika vyuo vikuu, hivyo wakawa wanajua kuwa wakipata wanafunzi watatu kutoka kila chuo kikuu ni wastani wa wanafunzi 100 ambao wangekuwa wafuasi wao. NGO nazo wakawa na imani kuwa zinawaunga mkono wao, ndiyo maana waking’ang’ania kuongeza idadi hadi wajumbe 438,” kilisema chanzo chetu.


Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema bungeni Jumamosi wakati akijenga hoja hiyo iliyokataliwa na Bunge, kuwa wanataka idadi ya wajumbe iongezwe hadi kuwa 438 kwa nia ya kuhakikisha uwakilishi wa makundi ya kijamii unakuwa na uwiano wa wabunge wanaotokana na vyama.


Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipowasiliana na JAMHURI alisema yeye hataki kulumbana na Chadema, isipokuwa jambo moja tu kwamba mwaka 2010 katika Uchaguzi Mkuu wananchi waliamua kuichagua CCM, hivyo Chadema hawapaswi kuwa na hofu yoyote juu ya wingi wa wabunge wa CCM.


“CCM haijawahi kufanya uamuzi wowote wenye nia mbaya kwa Taifa hili. Nawaomba wenzetu kama tulivyoaminiana tukafanya marekebisho ya sheria kuelekea kutungwa Katiba mpya, watuamini kuwa CCM kila uamuzi inaofanya unalenga kulinda maslahi mapana ya Taifa letu na si vinginevyo,” alisema Kinana.

Nape apigilia msumari

Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliiambia JAMHURI kuwa Chadema wanahangaika kwa sababu wamechukua fedha za wafadhili nje ya nchi kukwamisha mchakato wa Katiba mpya, lakini sasa zinawatokea puani.


“Chadema ni wanafiki na wana ubinafsi. Wanachoangalia hapa ni maslahi yao binafsi na maslahi binafsi ya chama chao. Nimesema mara kadhaa kuwa wamepewa pesa nyingi kutoja nje ya nchi na sasa wamevurunda, wameingia mchecheto watazilipaje.


“Haiingii akilini kuona hawa walioshiriki vikao na TCD (Tanzania Centre for Democracy), leo wanafika bungeni wanakana kila walichokikubali ndani ya TCD. Tatizo hapa, walipewa fedha wakazitumbua kwa kurusha helikopta bila ya kujua gharama yake, wafadhili wao bado wanadai chengi, na hawana mahala pa kupata fedha hizi.


“Mimi nasema kama wamezinunulia majumba, basi wauze hayo majumba wawarejeshee wafadhili fedha zao. Tanzania itaendelea kuwa salama, hizo chokochoko wanazoleta wala hazitatukuta,” alisema Nape na kuongeza kuwa ndiyo maana Chadema wameanzia vurugu za idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakidhani kuwa kwa kufanya hivyo wafadhili wao wanasikia sauti zao, na hivyo watawasamehe deni la fedha walizotumia vibaya. “Hasamehewi mtu, lazima walipe deni hili kwa wafadhili, ila si kwa gharma ya maisha ya Watanzania,” alisema.

Mnyika ajibu tuhuma

Mnyika, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, kwa upande wake alijibu tuhuma moja baada ya nyingine na kuviomba vyombo vya habari kuwa makini na taarifa kutoka ndani ya CCM, kwani zinaweza kuwa na lengo la kupotosha umma.


Hoja ya kuingia makubaliano maalum na Tume ya Marekebisho ya Katiba kuhakikisha inatoa rasimu ya pili ya Katiba yenye kuelekeza Serikali tatu nao waipigie debe bungeni iongezewe muda na kuendelea kufaidi posho, Mnyika alisema:


“Kama umefuatilia mjadala wa bungeni, niliwasilisha jedwali na kutoa hoja ya marekebisho kurejesha ukomo kama ulivyokuwa awali kwenye sheria kabla ya kuchakachuliwa na wabunge wa CCM na Mbunge mmoja wa TLP [Augustino Mrema]. Sijawahi kukutana na wajumbe wa Tume kunituma kufanya hivyo, bali nimefanya hivyo kwa kutokana na umuhimu wa hoja yenyewe kwenye kuboresha mchakato wa Katiba mpya,” alisema Mnyika.

Kuhusu hoja kwamba wamependekeza wanafunzi watatu kutoka kila chuo, na kutaka NGO zitoe wajumbe 44 wa Bunge la Kutunga Katiba, alisema: “Hakuna mahala popote ambapo tumepata kupendekeza kila chuo kipate wanafunzi watatu.


“Ni vizuri ukafanya rejea kutoka kwenye nyaraka zetu za bungeni, za kwenda kwa Rais [Jakaya Kikwete] na za kwenye Kamati za majadiliano utapata kwa undani mapendekezo yetu kuhusu mgawanyo wa kila kundi katika jamii na sababu husika.


“Ikumbukwe kwamba tulianza kupendekeza muundo wa Bunge la Katiba uanze kabla hata ya kutoka kwa rasimu iliyopendekeza shirikisho la serikali tatu. Hivyo, chukua tahadhari usipotoshwe na kuingizwa kwenye mtego wa kubeba propaganda potofu za kuhamisha mjadala kutoka kwenye hoja za msingi,” alisema Mnyika.


Wajumbe wa Tume karibu wote, akiwamo Mwenyekiti wao Jaji Joseph Warioba hawakupokea simu na hata baada ya kupelekewa ujumbe wa maandishi hawakujibu lolote, kuhusiana na tuhuma hizi.

Jaji Mutungi atoa wosia

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameiambia JAMHURI kuwa matatizo yote yanayojitokeza yanatokana na ubinafsi usio wa lazima. Alisema katika masuala yanayohusu Katiba mpya, wananchi wanapaswa kuungana na kuwa wamoja kujiepusha na kuwa na mitizamo ya kivyama.


“Mambo ya Katiba tufute element (mwelekeo) za vyama zinazoleta sintofahamu. Maana tukifika huko kama wananchi tutasema hata waendesha ndege sasa wanapaswa kuwa wa chama fulani. Katiba ya nchi ni sawa na kuendesha ndege, hakuna chama pale.


“Katiba hii mbele ya safari huenda ikapatikana wakati vyama vyote hivi havipo, sasa hili ni suala la kitaifa si la kiitikadi,” Jaji Mutungi aliiambia JAMHURI.


Kuhusu suala lililoleta mvutano mkubwa bungeni juu ya kuvunjwa kwa Tume ya Jaji Warioba, alisema dhana iliyopo ni mantiki ya kisheria kuwa Tume ikishavunjwa watakaoitwa kutoa maoni au ufafanuzi mbele ya Bunge watakuwa wanafanya hivyo kwa mamlaka yapi.


Hata hivyo, alisema hadidu rejea za Tume ya Marekebisho ya Katiba ziko wazi tu kuwa baada ya kukabidhi ripoti ya maoni waliyokusanya kutoka kwa wananchi inakuwa imemaliza kazi yake.

Wabunge watia ubani Katiba mpya

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, alisema anapata shida kuamini kuwa Chadema wanapendekeza idadi ya wabunge iongezwe kutoka 201 waliopendekezwa na Serikali kwenda 438.


Simbachawene alisema anakubaliana na ufafanuzi uliotolewa na Mnidhamu wa Chama tawala, William Lukuvi, kuwa hoja ya Zanzibar kuwa na wabunge sawa na Tanzania Bara ilikufa pale tu marekebisho ya Sheria yalipofuta utaratibu wa kupitisha vifungu vya Katiba kwa mfumo wa wengi wape (simple majority), hivyo hakuona sababu ya Chadema kuendelea kung’ang’ania hoja hiyo.


Lukuvi kwa upande wake, alilieleza Bunge kuwa Zanzibar walikuwa na wasiwasi kuwa kutokana na uchache wao, basi hoja zao zingeweza kumezwa bungeni chini ya mfumo wa wengi wape, lakini baada ya utaratibu kubadilishwa ikawa kuwa kila kifungu kitapitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura kwa theluthi mbili Zanzibar na theluthi mbili Tanzania Bara kuafiki kifungu husika, wakaona wingi wa idadi ya wawakilishi si hoja tena.


“Zanzibar sasa waliona kuwa kumbe hata mkiwa 10, alimradi ni theluthi mbili, hakuna linaloweza kupita kinyume na matakwa yao,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa hilo ndilo lililoua hoja ya Chadema kutaka idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba iongezwe hadi 438 kuleta uwiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.


Lukuvi ndipo alipoongeza kuwa Chadema wana imani kuwa vyama vya kijamii (NGOs) vinawaunga mkono, hivyo wana matumaini kuwa vikipata wawakilishi wengi bungeni, mbele ya safari hoja zao zitapita kwa urahisi.


Mnyika kwa upande wake, alipingana na kauli ya Lukuvi akisema yeye anatetea maslahi ya Taifa kwa ujumla wake. “Hata mwanafalsafa Socrests aliuawa kwa kueleza msimamo kuwa dunia ni duara. Hapa nasema hoja inayotolewa tuitambue hoja kama hoja si kwa kuangalia chama au anakotokea mtoa hoja.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alijenga hoja murua kuwa kundi kubwa la sekta binafsi limesahaulika katika mchakato wa kutunga Katiba, lakini kwa bahati mbaya hoja yake hiyo haikupata majibu mwafaka.


Mbunge wa kundi la Vijana (CCM), Ester Bulaya, kwa upande wake aliwaomba Chadema kukubali marekebisho yaliyofanywa ya kulifanya Bunge la Katiba kuwa na wajumbe 201 wasio wabunge kwa maelezo kuwa katika majadiliano kuna kupata na kukosa.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, kwa upande wake alisema Chadema wana hofu ya CCM kuwa kutokana na wingi wa wabunge wake, inaweza kupitisha kila itakacho katika Bunge la Katiba na hivyo akataka wabunge kuweka kando misimamo ya vyama na kufikiria nchi kwanza.


Mwanasheria Mkuu (mstaafu), Andrew Chenge, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, kuhusu suala la Tume ya Jaji Warioba kuongezwa muda alisema hilo si sahihi kwani Tume zote duniani zikishamaliza muda huwa zinavunjwa.


Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), alitetea Tume ya Mabadililiko ya Katiba kuongezwa muda kwa maelezo kuwa wajumbe wake wanao uzoefu wa kutosha na wakiwamo kwenye Bunge la Kutunga Katiba, basi itakuwa fursa kwao kufafanua masuala yenye utata kwa njia moja au nyingine.


Kwa upande wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliibua hoja mpya kuwa Bunge lisiogope wingi wa wajumbe katika Bunge la Kutunga Katiba kwa kisingizio cha gharama, kwani gharama za kulipa wajumbe wa Tume haziwezi kuwa kubwa sawa na madhara yanayoweza kujitokeza mbele ya safari.


Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jaffo, aliyetoa hoja ya kuvunja Tume ya Jaji Warioba kwenye mkutano uliopita, aliliambia Bunge kuwa wajumbe wa Bunge la Kutunga Sheria si mbumbumbu kwa kiwango cha kuhitaji washauri. “Hatuhitaji consultants (washauri) kutoka nje kwenye huu ukumbi. Tunataka Bunge la Katiba liwe na uhuru wa kutosha kujadili Katiba,” alisema Jaffo.


Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, aliwataka wabunge kujiepusha na kutumia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kama kinga au njia ya kufanikisha matakwa yao.  Abdallah alitoa kauli hiyo, baada ya Mnyika kutoa kauli kuwa Rais Kikwete katika hotuba ya Oktoba 4, alipendekeza suala la uhai wa Tume ya Marekebisho ya Katiba lizungumzwe. “Rais alisema jambo hili linazungumzika, ndiyo maana sasa tunazungumza,” alisema.


Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema dhana ya kutoongeza idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge la Kutunga Katiba imetokana na ukweli kwamba gharama ya Bunge hilo ni kubwa, na nafasi ya wabunge kuendesha mkutano wao inaweza kuwa tatizo ikiwa idadi itaendelea kuongezwa bila ukomo kutokana na kutokuwapo ukumbi wenye uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya wajumbe.


Baada ya mabishano ya muda kidogo, Mbunge wa Isimani, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, alisema: “Sasa naomba nitoe siri ambayo sikutaka kuitoa. Pendekezo la kuvunja Tume ya Katiba lilitolewa na Julius Mtatiro wa CUF. Walipendekeza mara mbili wakisema Tume hii ina gharama kubwa… ushahidi ninao… kwa kuwa Serikali hii ni sikivu ikalikubali,” alisema Lukuvi.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema kila mtu anaheshimu na kuenzi kazi mzuri iliyofanywa na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini akasema wakati wao wa kupumzika utakuwa umefika baada ya kukabidhi rasimu ya pili ya Katiba. Hata hivyo, alisema ikiwa watahitajika marekebisho ya sheria yaliyofanywa yanaruhusu wajumbe hawa kuitwa na kutoa ufafanuzi kama unahitajika.


Kimsingi, kuna wasiwasi iwapo muda uliosalia utaruhusu Katiba mpya kupatikana Aprili 26, 2014 kutokana na wingi wa shughuli zilizobaki, hali inayotoa tafsiri kuwa Katiba haiwezi kuandikika ndani ya muda mfupi uliosalia, hivyo ni vyema kuchukua ushauri wa Profesa Lipumba wa kufanyia marekebisho vifungu vichache ndani ya Katiba ya sasa kisha mchakato uendelee.


 

By Jamhuri