DODOMA

Na Javius Byarushengo

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, alipofanya ziara nchini Ghana mwaka 2009 akiwa madarakani, alisema kuwa ili Bara la Afrika lipate maendeleo, halihitaji kuwa na watu imara bali taasisi imara.

Kimsingi Obama, Mmarekani wa kwanza mweusi kuwa kiongozi mkuu wa taifa hilo kubwa, kuhitaji taasisi imara Afrika ni kutokana na mifumo ya kiuongozi aliyoiona.

Kwa nyakati tofauti mataifa mengi ya Afrika yamekuwa yakiongozwa na watu fulani ambao kuna wakati walionekana kufanya vizuri lakini baada ya kustaafu au kutangulia mbele ya haki, mambo mengi yamekuwa yakisimama yalipo au kurudi nyuma kabisa.

Mambo mengi kurudi nyuma ni matokeo ya mataifa hayo kuwekeza nguvu nyingi kwa watu imara kuliko kuimarisha taasisi zao, hivyo kusahau kuwa binadamu hata kama angetawazwa milele mwishowe angefariki dunia.

Katika miaka ya karibuni hapa nchini kutokana  na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii pamekuwapo na uhitaji mkubwa wa Katiba mpya kiasi kwamba baadhi ya wananchi wanaona kuwa katiba iliyopo haikidhi matakwa ya wakati tulio nao.

Ni wazi mabadiliko ya katiba huwa ni muhimu ili kwenda sambamba na mabadiliko yaliyopo katika wakati husika lakini kabla ya mabadiliko hayo kuna haja ya kujiuliza maswali kadhaa kama ifuatavyo:

Je, ni kweli Katiba iliyopo ya mwaka 1977 haikidhi matarajio ya taifa letu kwa sasa?

Je, kuna uhakika kwamba katiba ikibadilishwa taifa letu na viumbe waliomo watakidhi matarajio yao au kuna suala jingine la kufikiria kufanya zaidi ya katiba?

Je, mambo yanakwama kutokana na katiba iliyopo au ni udhaifu wa kitaasisi katika kutekeleza na kusimamia katiba iliyopo?

Swali la tatu hapo juu linaweza kutupeleka kutafakari zaidi ya nini cha kufanya kabla ya kuhitaji katiba mpya, kwamba yamkini kwenye taasisi zetu kuna upungufu wa hapa na pale.

Mfano taasisi ya kifamilia ambayo ni ngazi ya mwanzo katika jamii imefanya nini kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya kitaifa yanakwenda kama yalivyopangwa?

Je, ni kwa namna gani wazazi wanakuwa mfano bora kwa malezi ya watoto wao katika kuwafundisha maadili mema ili watakapopata nafasi za uongozi wasikengeuke na kufanya maovu mfano ubadhirifu, rushwa, ufisadi au kuongoza kwa matabaka huku wakitumia mkono wa chuma?

Je, taasisi za kidini katika mahubiri yao ya kila siku makanisani na misikitini yana tafsiri gani katika kuwajenga waumini wao ili wakipata uongozi waongoze kwa unyeyekevu na moyo wenye huruma usio na ubaguzi?

Je, taasisi za kielimu zinawachonga wasomi wawe watu wa namna gani hasa wakija kuwa watu fulani katika jamii?

Je, elimu inayofundishwa inatuandalia wasomi ambao baada ya kupata maarifa watajiona wao ni tofauti kabisa, hivyo kuwatenga na kuwanyanyapaa binadamu wenzao ambao hawakupata fursa za kusoma?

Je, taasisi za elimu zinatuandalia wasomi ambao wakipata nafasi za madaraka watageuka watawala badala ya viongozi?

Je, taasisi za elimu zinatuandalia viongozi majizi na yenye kujilimbikizia mali?

Je, vipi kuhusu taasisi za kibunge na kimahakama katika kusimamia majukumu yao waliyopewa?

Je, tunao wabunge wa kusifia na kujipendekeza kwa viongozi walioko serikalini badala ya kushauri/kuelekeza au kukosoa panapostahili kwa lengo la kuleta ufanisi kwa wananchi ambao kimsingi ndio waajiri wao kutokana na kuwa ni wapiga kura?

Je, mahakama zilizopo zinafanya kazi kwa ajili ya umma au zinafanya kazi kwa ajili ya nyapara mkuu wa serikali?

Vipi kuhusu taasisi za vyama vya siasa hapa nchini ndani ya mfumo wa vyama vingi?

Je, viongozi wa vyama vya siasa ambao kwa muda mwingi wamekuwa wakidai demokrasia ya kweli kutoka serikalini, wao wenyewe wanayo demokrasia ya kweli ndani ya vyama vyao au ni kutaka kutoa kibanzi ndani ya jicho la mwenzio ilhali ndani ya jicho lako kuna boriti?

Je, viongozi wa vyama vya siasa ambao wanadai Katiba mpya ya taifa, vipi za vyama vyao zinatekelezwa au ni kutimiza methali isemayo mkuki  kwa nguruwe kwa binadamu mchungu?

Je, kama viongozi wakuu ndani ya vyama vya siasa wanaipiga teke demokrasia kiasi kwamba wengine wamegeuka wafalme, ni vipi wataweza kutetea demokrasia ya nchi kipindi wakipewa kushika uongozi wa nchi?

Je, kama viongozi wakuu wa vyama vya siasa wanaweza kupiga teke katiba zao kwa ajili ya masilahi binafsi, ni kwa namna gani wataweza kuilinda na kuitetea katiba ya nchi pindi wakipewa nafasi ya kuongoza nchi?

Maswali yote haya yakijibiwa kwa kutumia uhalisia uliopo ndipo uhitaji wa Katiba mpya unaweza kuangaliwa kwa mapana yake.

Inawezekana changamoto zilizopo ndani ya nchi  hazitokani na katiba iliyopo bali ni taasisi zilizopo kutotimiza wajibu wake.

Inawezekana tukawa na katiba nzuri sana ambayo haijawahi kutokea hapa duniani lakini kutokana na taasisi zetu kulala usingizi na mambo yenyewe yakalala usingizi.

Katiba iliyopo ya Marekani ni ya mwaka 1789 lakini bado inaendelea kufanya kazi vizuri na kila kukicha taifa hilo linasonga mbele kimaendeleo, wala hatujawahi kusikia taifa limepinduliwa na kutawaliwa kijeshi.

Je, ni mara ngapi baadhi ya marais wa Afrika wamekuwa wakizibadilisha katiba zao nzuri ili waweze kuendelea kubaki madarakani?

Ni mara ngapi tumekuwa tukishuhudia mataifa mengi yenye katiba nzuri yakiendelea kuuumizwa na wimbi la ufisadi na rushwa kutokana na ukosefu wa uadilifu ambao chimbuko lake ni ngazi ya taasisi ya kifamilia?

Ni mara ngapi baadhi ya mataifa barani Afrika na kwingineko duniani yenye katiba nzuri kwa nyakati fulani yamejikuta viongozi wake waliochaguliwa kidemokrasia wakipinduliwa na majeshi bila hatia?

Ni dhahiri katiba bora ni muhimu kwa taifa letu ili kwenda sambamba na mabadiliko yaliyopo, lakini bila taasisi imara itakuwa ni kama mchezo wa paka na panya.

[email protected], 0756521119

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta

By Jamhuri