Mpendwa msomaji wa makala ya Katiba Mpya, Tanzania Mpya, wiki iliyopita nilianza kuzungumzia historia ya Muungano wetu, jinsi ulivyoanza kama fikra na utashi wa viongozi waasisi wa taifa letu la Tanzania.

 

Wakati haya yanatokea sikuwapo, lakini nafurahi kwa sababu nimeisoma vizuri historia ya nchi yangu. Historia inatueleza mambo mengi, na ni vyema hata kuujua mfumo wa Muungano tulionao ulitoka wapi na matatizo yalianzia wapi? 

Leo niendelee tulipoishia wiki iliyopita ili baadaye tupate kujibu swali la je, tunayo ya kujadili kuhusu Muungano? Kama tunayo, tuyajadili katika mtindo gani?

 

 

 

Baada ya kupitishwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Katiba ya Tanganyika kufanyiwa marekebisho kukidhi haja ya sura mpya ya dola, mwaka 1965 Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of Tanzania) ilipitishwa.

 

Kupitishwa kwa Katiba hiyo ya mpito kulileta sura mpya ya mambo katika siasa za Tanzania.  Kwanza, Katiba hiyo iliyopitishwa na Bunge la Katiba ilileta mabadiliko ya kipekee katika nyanja ya siasa za nchi na uendeshwaji wa shughuli zote za kisiasa Tanzania, nchi ambayo ndiyo kwanza tu ilikuwa ikilea mfumo mchanga wa demokrasia ya vyama vingi.

 

Pili, mabadiliko haya ya kipekee yalilenga kuweka mfumo tofauti kabisa wa kisiasa na kiuchumi Tanzania, kinyume na matarajio ya awali kipindi cha mwanzoni cha Uhuru wa Tanganyika. 

 

Kwa mujibu wa Katiba hiyo ya mpito ya mwaka 1965, na kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Tanzania huru, vyama vyote vya siasa vilisitishwa, isipokuwa tu vile vilivyokuwa madarakani Tanzania Bara, yaani Tanganyika African National Union (TANU), na Tanzania Visiwani, Afro-Shirazi Party (ASP). Baada ya Muungano hatukuendelea kuwa na Tanganyika wala Zanzibar pekee, bali Tanzania Visiwani na Tanzania Bara.

 

Lengo hasa la kusitisha vyama vingi lilikuwa kuleta mfumo wa chama kimoja katika Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania, azma ambayo waasisi wa Taifa la Tanganyika na chama cha TANU walikuwa nayo tangu mwaka 1962. Kwa mtindo huo, bila kujadili mabadiliko mengineyo kama yale ya kuanzishwa kwa Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea mwaka 1967, mwaka 1975 vyama vya TANU na ASP vilijikita ndani ya Katiba kwa mstari wa mbele na mamlaka yote. Dhana ya Bunge kushika hatamu ya juu (supremacy of parliament) iligeuzwa na kumezwa na dhana mpya ya chama kushika hatamu (party supremacy). Kwa hali hiyo, vyombo vingine viliwajibika kwa chama tawala na matakwa yake.

 

Katiba hiyo ya mpito ilitokana na mchakato wa Tume ya Rais ya Katiba iliyokusanya maoni kwa baadhi ya wananchi. Katiba hii ilitamka bayana chama kushika hatamu ya uongozi na nchi ambako Halmshauri Kuu ya TANU ikawa na nguvu kuliko Bunge na hata Katiba yenyewe.

 

Lakini pia mambo ya Muungano yakaanza kuongezeka na uhuru (autonomy) ya Serikali ya Zanzibar ukagubikwa na utata na kuwa moja ya kero za Muungano hata leo. Sasa kuunganika kwa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 5, 1977 lilikuwa tukio jingine la kipekee lililokamilisha ustadi wa wakongwe wa siasa za Tanzania na lililoweka mazingira mapya ya kisiasa na kiuchumi yaliyohitaji Katiba mpya.

 

Miaka 12 baada ya kupitishwa kwa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1965, ilipitishwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na ndiyo iliyopo hadi sasa. Imeshafanyiwa marekebisho 14 ya msingi hadi sasa. Ndani ya Katiba hii, mtazamo na sura ya kisiasa iliyokuwa imejengwa kwa miaka 12 na Katiba ile ya muda ya mwaka 1965 uliendelezwa. CCM ikawa chama pekee na kilichoshika hatamu za uongozi Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. 

 

Katiba ya mwaka 1977 ilipatikana kutokana na Tume ya Rais iliyokuwa na wajumbe 20, kwa idadi sawa kutoka pande zote za Muungano ikiongozwa na Sheikh Thabit Kombo akisaidiwa na Pius Msekwa kama Katibu wa Tume. Hata hivyo, tume hii ni ileile iliyotunga katiba ya CCM. Katiba hiyo ilipitishwa ndani ya muda wa saa tatu na Bunge Maalumu lililoteuliwa na Rais kutokana na Bunge la kawaida.

 

Pamoja na kupatikana kwa Katiba yenye chama kimoja tu Bara na Visiwani, tabia ile iliyorithiwa tangu mwanzo wa mabadiliko ya Katiba miaka ya nyuma haikufichwa, badala yake iliwekewa mazingira mazuri zaidi na yaliyowaondoa wengi katika ushiriki. Kwa mfano, Kamati ya Chama iliyokuwa imehusika katika jukumu la kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya kuwapo kwa chama kimoja cha siasa kwa pande zote za Muungano, ndiyo iliyogeuzwa kwa maagizo ya Kamati Kuu ya chama kufanyika kuwa Tume ya Katiba (Constitutional Commission) na kutakiwa kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Ripoti ya mapendekezo hayo iliwasilishwa kwa Halmashauri Kuu ya chama (NEC) na si bungeni kwa vile chama ndicho kilichokuwa na uamuzi wa mwisho.  Yote haya nayasema kwa sababu historia haina tabia ya kuficha kitu, na ni vyema kuijua historia ya nchi yako kwani ni uzalendo na kuudhihirisha utaifa wako.

 

Baadaye, NEC ikaliagiza Baraza la Mawaziri kuandaa rasimu ya muswada ambao ungewasilishwa kwa Bunge la Katiba kuhusu kutungwa kwa Katiba mpya. Muswada huo ukapitishwa moja kwa moja bungeni na Katiba mpya ikapatikana mwaka 1977.

 

Mfumo wa chama kimoja ukazidi kujikita na dhana yake ya chama kushika hatamu ikaneemeka zaidi. Kwa hali hii ni dhahiri kuwa hata Katiba tuliyo nayo hivi leo haikuwashirikisha wananchi wote kwani si wote waliokuwa wanachama wa chama tawala. Hivyo, utaratibu wa kutunga Katiba mpya kwa kuitisha kongamano la Katiba (constitutional conference) haujawahi kufanyika wala kuwa sehemu ya desturi nchini Tanzania.

 

Kutokana na historia ndefu ya nchi yetu, inaonekana wazi kwamba Muungano wetu hauna fikra za Watanzania wengi na ndiyo maana wanadai haki ya kuujadili Muungano. Hivyo hakuna sababu ya msingi ya kupinga umma wa Watanzania kujadili mambo ya Muungano. Nini hasa cha kujadili kuhusu Muungano? Tukutane wiki ijayo katika makala ya Katiba Mpya Tanzania Mpya.

2480 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!