Gerezani na vitu feki Uingereza

MIAKA ya 1990 baada ya kubahatika kununua kagari kangu mgongo wa chura, nilipitia machungu baada ya kuibiwa saiti mira. Nilijaribu kujiganga bila mafanikio, kwa sababu nilikuwa nimejikung’uta kila senti mfukoni nami niwe na gari na kuliweka barabarani kwa kujidai.

Nakumbuka ilikuwa katikati ya mwezi, kwa hiyo usawa kipesa ulikuwa mgumu ile mbaya, na jamaa wakaniambia trafiki wakinikatama nikiendesha gari hivyo, ningetokwa na pesa nyingi au kwenda mahakamani.

 

 

Ilikuwa miezi michache tu baada ya kuanza kujidai na kwenda kazini na gari yangu, jioni tunapita kwenye viti virefu, naipaki na kila mtu anaiangalia, sasa nikafikiria kuiegesha nyumbani nikaona aibu.

Rafiki yangu aliyekuwa na magari mawili wakati huo – pick up na gari dogo – aliniokoa kwa kuniwezesha kupata kioo kipya eneo la Gerezani,  Ilala, Dar es Salaam, tulikokuta vioo vingi na hati kibao vipo ‘genuini’, wakaniangalia na wakwetu mmoja akaniambia; “tikyawe wenka,” yaani haupo peke yako.

Hapo pameshindikana kwa vitu vya wizi, kughushi na kwa miaka mingi wahusika wa kisiasa na kiutendaji hawakuthubutu kupasogelea. Labda Nchimbi wa Mambo ya Ndani atatupia jicho maana amepewa rungu sasa.

Wakati nchi masikini zinasemwa kwa ukosefu wa utawala bora, kukua kwa uhalifu na rushwa, Uingereza nayo inapitia kwenye hali ngumu. Watu wamepigika kiasi kwamba wanaojidai werevu wachache wamejitumbukiza kwenye biashara feki kama ya Gerezani.

Hawa ‘wameendelea’ zaidi, kwa sababu wanafanya biashara yao kimtandao kabisa, tena inakatiza hata mipaka ya kisiwa hiki kikubwa. Udanganyifu huu umekwenda mbali kiasi cha kutengeneza vitambulisho feki, hati za mishahara (salary slips) na hata kumbukumbu za uongo za historia ya kibenki na hali ya fedha ya ‘mteja’.

Unaambiwa watu wanaofanya biashara hii wamefanikiwa kuziliza benki maelfu ya paundi kila siku kwa sababu wateja wakishapitia ‘Gerezani’ hii ya Uingereza, wakienda benki kuomba mikopo, wanatoa hati zote zinazotakiwa ambazo ni za uongo na kumiminiwa mipesa!

Hapa wanachonga hadi anwani za mitaa na miji ambazo hazipo, lakini wanaunganisha kwenye mtandao hivyo kwamba kule benki au taasisi nyingine za kukopesha wakifuatilia wanaona ni ‘genuine’ kabisa mwana na kutoa mikopo.

Ukiona kwenye nchi iliyoendelea kama hii nayo mambo haya yanapamba moto, ujue kweli uchumi wa dunia umeyumba na tusipokuwa makini twafa! Polisi wanakuambia uhalifu huu ukichanganywa katika sehemu zote Uingereza unagharimu pauni bilioni 73 kila mwaka!

Sasa kuna jamaa zangu wapo roho juu kwa sababu polisi wamesema wameanza kufuatilia ‘wateja’ waliokuwa wakipita ‘Gerezani’ na kujipatia hatia, kisha kwenda kuziliza benki na vyama vya kuweka na kukopa.

Kuna jumla ya watu 11,000 kwenye mtandao huo waliofaidi, sasa wengine wanajaribu kukimbia, wengine kubadilisha anwani au hata jina moja au yote kukwepa kitanzi hiki.

Ijumaa iliyopita jamaa sita wenye ofisi kama hizo, waliburuzwa mahakamani baada ya kukutwa na rundo la nyaraka zilizoonekana kama zilikuwa za kweli kumbe ni za kughushi.

Haya wana-Jamhuri, hebu kila mmoja ajitahidi kuchapa kazi ili mkono uende kinywani, maana Mtume Paulo anasema asiyefanya kazi na asile. Lakini kazi yenyewe iwe halali, kwa sababu mkono mrefu wa dola usipokupata leo utakupata kesho, na hili ni moja ya mambo ninayowasifu nayo wakoloni wetu hawa wa zamani.

[email protected]