Shahidi wa kwanza katika kesi ya kudaiwa kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema ameieleza mahakama kwamba  alimtolea bastola mbunge huyo kwa kuwa alikuwa akijaribu kutoroka.

Shahidi huyo, Damas Masawe (44) ambaye ni mkuu wa upelelezi wilaya ya Arusha (OC-CID)  ameileza Mahakama hiyo kwamba mnamo Juni 22 mwaka jana alilazimika kuchomoa bastola yake katika eneo la kambi ya Fisi ambapo kulikuwa na mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge huyo.

Akitoa utetezi wake mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Sekei, Devotha Msofe shahidi huyo amesema sio kweli kwamba ana ugomvi na Lema kwa kuwa hata watoto wa Mbunge huyo wanampenda sana.

Akijibu swali lililoulizwa na Wakili wa upande wa utetezi, Sheck Mfinanga kwamba gari lake liliwahi kuchomwa moto na wafuasi wa CHADEMA mkoani Iringa katika mkutano ambao Lema alikuwa akihutubia shahidi huyo alikiri ni kweli gari lake lilichomwa moto lakini hawakuwa wafuasi wa CHADEMA.

Shahidi huyo ameiambia Mahakama hiyo kwamba ingawa yeye sio mtaalamu wa masuala ya imani lakini anaamini kuota ndoto sio kosa lakini kosa ni kuhadithia ndoto.

Massawe ameiambia mahakama hiyo kwamba maneno aliyoyatamka Mbunge huyo laiti angeyatamka wakiwa  katika vikao vya nyumbani mkoani Kilimanjaro yasingekuwa na shida lakini aliyatolea kwenye mkutano wa hadhara.

“Kuota ndoto sio kosa, lakini kuhadithia ndoto yako ni kosa, hayo maneno laiti ningekutana naye uchagani kama kaka yake angeniambia wala nisingekuwa na shida lakini aliyatolea mkutanoni,” – Massawe

Hata hivyo, shahidi huyo amesema kwamba kwa mujibu wa kitabu cha biblia anachokijua yeye kinasema kwamba wazee pekee ndio wataota ndoto na wala sio vijana na hivyo Lema hakustahili kuota ndoto dhidi ya Rais Magufuli kwa kuwa bado ni kijana.

Shahidi huyo amesema kwamba Lema hajafikisha umri wa miaka 60 na hivyo hatakiwi kuota ndoto bali wazee ndio wanatakiwa wapumzike, watafakari na kuota ndoto.

Hata hivyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa serikali, Agnes Hyera ulimtaka shahidi huyo kuieleza Mahakama hiyo kwamba kulikuwa na idadi ya watu wangapi katika mkutano ambao Lema alitamka maneno hayo na kusema ni takribani watu 200.

Kesi hiyo nambari 440 ya mwaka 2016 inatarajiwa kuendelea tena mnamo Januari 22,23 na 24 ambapo upande wa mashtaka unatarajia kuwaleta mashahidi wengine mbele ya mahakama hiyo.

1582 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!