KIJANA WA MAARIFA (11)

Mitandao ya kijamii ni fursa wanayoitumia wachache. Jumamosi ya Januari 11, mwaka huu ilikuwa siku ya furaha kubwa maishani mwangu. Ni siku ambayo nilikuwa nikizindua kitabu changu cha tatu kiitwacho ‘yusufu nina ndoto’, ambacho sasa kipo sokoni.

Kabla ya kufanya uzinduzi wa kitabu hicho niliunda kamati ya watu 30 ili kunisaidia kwa namna moja ama nyingine kufanikisha tukio hilo la kihistoria. Kutokana na uzinduzi wa aina yake uliofanyika, kuna kitu kikubwa nilijifunza. Kitu hicho ni kwamba mitandao ya kijamii ni fursa kubwa ambayo watu wengi wameifumbia macho.

Siku takriban 20 kabla ya tukio tulitengeneza tangazo lililohusu uzinduzi, ambalo tulianza kuliweka katika mitandao ya kijamii. Tulifanya jambo hilo kwa ushirikiano wote kama kamati ya uzinduzi. Kadiri siku zilivyopungua, tangazo letu lilionyesha siku zilizobaki, nasi hatukuchoka kutangaza.

Baada ya muda kidogo tangu kuanza kutangaza kupitia mitandao ya kijamii lilitokea jambo la kushangaza kidogo. Kila nilikopita kuna mtu alinisimamisha akiniuliza bado siku ngapi. Hapo nikaona kumbe mbinu yetu inafanya kazi. Kupitia mitandao ya kijamii tuliweza kuziteka hisia za watu kuhusu uzinduzi wa kitabu.

Kutokana na ratiba kuwa ngumu kwa wanakamati kukutana uso kwa uso mara nyingi, hiyo haikuwa shida kwetu, tuliunda kundi la WhatsApp ambako huko tulifanyia vikao vyetu muhimu. Kumbe mitandao ya kijamii inaweza kuwa sehemu nzuri ya kukutana mkazungumza mambo yenye tija na yakaenda kama mlivyotarajia.

Nilishangaa pia baada ya kuweka tangazo letu kwenye mitandao ya kijamii tukiwa na baadhi ya wadhamini, watu wengine walijitokeza ili wawe wadhamini wa tukio hilo.

Hapo ndipo nikakumbuka msemo wa mwandishi Austin Kleon aliyesema: “Onyesha kazi yako.” Ukionyesha kazi unayoifanya watu wanaopenda kile unachokifanya watajitokeza, ukificha kile unachokifanya tegemea hakuna atakayejali kuhusu hicho unachokifanya.

Jambo hilo halikuishia hapo. Siku kadhaa kabla ya tukio nilianza kupokea simu za redio mbalimbali wakidai kuwa wameona tangazo langu kupitia mitandao ya kijamii na walihitaji walau muda kadhaa nizungumze hewani kuhusu kitabu cha ‘yusufu nina ndoto’ (kazi niliyoifanya baada ya uzinduzi).

Mitandao ya kijamii inaweza kukukutanisha na watu muhimu kwenye maisha yako kama unafanya mambo ya muhimu sana. Miezi kama miwili iliyopita niliona katika mtandao wa YouTube dada mmoja aliyetumia makundi ya WhatsApp kuunganisha wafanyabiashara kutangaza biashara zao.

Dada huyu si mwingine bali ni Nazarena Myenzi, mtu ambaye amekuja kuwa rafiki yangu wa karibu. Wakati ninatafakari kuhusu uzinduzi wa kitabu changu nilitamani dada huyo awe mmoja wa wazungumzaji katika sherehe hizo za uzinduzi. Hivyo nilimtumia rafiki yangu mmoja ili kupata mawasiliano yake.

Baada ya kupata mawasiliano yake nilimpigia na kumweleza jukumu lililokuwa mbele yangu na kumuomba awe mmoja wa wazungumzaji wa tukio hilo, kwa bahati nzuri alinikubalia. Moja kwa moja nikampanga katika ratiba za uzinduzi na kumpa aongelee faida za mitandao ya kijamii.

Katika mafundisho yake moja ya kitu muhimu ambacho alisema na ninataka nikushirikishe leo ni kwamba mitandao ya kijamii ni fursa kubwa sana lakini ni watu wachache wameikumbatia fursa hiyo.

Kupitia mtandao wa WhatsApp pekee, Nazarena, ambaye wengi wanamwita Naza, ameweza kuwaunganisha wajasiriamali 3,000 ambao anasema anawasaidia kukuza biashara zao nao wanamsaidia kukuza biashara zake. Hapo ndipo ninakuja kukubaliana na maneno ya Zig Ziglar aliyewahi kusema: “Utapata chochote unachohitaji kwa kuwasaidia wengine kupata wanachohitaji.”

Naza ni mkurugenzi wa kampuni mbili, moja inaitwa Naza Group Ltd, na nyingine inaitwa Naza Wig. 

Makundi aliyoyaunda ya WhatsApp huwa kila siku wanachukua na kutangaza biashara ya mtu mmoja aliyeko kwenye kundi. Ina maana kama leo wanatangaza biashara ya Edius kila mtu kwenye ‘status’ yake ataweka tangazo la biashara ya Edius. Fikiria watu 3,000 wanatangaza biashara yako, unaweza kuwafikia watu wangapi kwa siku moja?

Watu kama Naza wameona fursa katika mitandao ya kijamii na wanaitumia vema. Tuache kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu tu ya kuona picha za marafiki zetu au kutazama vichekesho tu. Kuna vitu vikubwa tunaweza kuvifanya kupitia mitandao ya kijamii.