Kituko tovuti ya BoT

Mpita Njia (MN) anakumbuka miaka ile ya enzi zao watu waliofanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) walionekana kama vile ni wateule wa Mungu.

Walionekana wateule kwa sababu mazingira, aina ya kazi na mishahara yao viliwafanya wengi waamini kuwa hakuna zaidi ya BoT!

Waliamini BoT ni sehemu teule kwa sababu ndiyo iliyoshika usukani wa uchumi, na ndipo mahali kuliko na chungu cha utajiri wa nchi yetu. Ni kwa sababu hizo na nyingine nyingi, Mpita Njia ameendelea kuamini kuwa kwenye masuala yote ya uchumi wa nchi yetu sehemu pekee anayoweza kupata taarifa za uhakika ni BoT.

Wataalamu wa teknolojia wamesaidia mengi. Zama zile za miaka ya 1980 kina MN walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda BoT kupata taarifa mbalimbali za kibenki na kiuchumi. Lakini siku hizi mambo yote ni kwenye mtandao.

Pamoja na sifa zote nzuri za BoT, Mpita Njia amebaini kuwa kuna udhaifu unaoitia aibu taasisi yenyewe na nchi pia.  Aibu hii ni ya nchi, kwa sababu BoT ndiyo benki kuu ya nchi. Mtu unaweza kujiuliza, kama wazazi ndani ya nyumba hawapigi mswaki, haki itakuwaje kwa familia ya hao wazazi!

Juzi Mpita Njia aliingia kwenye tovuti ya BoT akilenga kupata taarifa za idadi ya benki pamoja na taarifa mbalimbali za kiuchumi. Alipoingia kwenye upande wa orodha ya benki, akapigwa butwaa! Akakuta idadi ya benki ambazo nyingine zilikwisha kufa miaka mitano iliyopita, yaani benki ambazo zilikwisha kuacha kufanya kazi bado zinatambulishwa kwenye orodha ya benki ambazo ziko – regulated na BoT.

Mpita Njia akajiuliza, hiki kinachofanywa na BoT ni cha bahati mbaya au ni kujaribu kuonyesha kuwa ule umakini unaoimbwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni wa midomoni tu, na si mioyoni na akilini? 

Akajiuliza, iweje chombo kikubwa, nyeti na muhimu cha kiwango hiki kikose watu weledi wa ku-update taarifa za mabenki ili wao kina MN wajue benki zipi ziko hai na zipi zilizokwisha kufa? Je, huu ni uzembe au ni hujuma?

Basi, kwa kuwa Mpita Njia si mtu wa majungu, akaona alifikishe hili kwa wahusika, maana kuona kuna taarifa chakavu kiasi hicho hiyo inamaanisha hata gavana mwenyewe huwa haingii kwenye tovuti ya taasisi anayoiongoza. BoT waondoe aibu hii.