Akiba haiozi, wekeza ukiwa kijana

Wanasema akiba haiozi na ikioza hainuki. Nitafanya makosa makubwa kama nikiandika mambo mengi kuhusu vijana na nikakosa kuongelea kuhusu kijana na uchumi.

Ni wazi kwamba pesa katika maisha yetu haikwepeki. Tangu unapoamka mpaka pale unaporudi kulala kuna mahali pesa itakuwa imetumika. Unaweza usitoe pesa mfukoni siku hiyo lakini kuna vitu utavitumia ambavyo vilikugharimu pesa kuvinunua, hivi vinaweza kuwa bidhaa au huduma.

Ni muhimu sana kujifunza matumizi mazuri ya pesa hasa wakati unapokuwa kijana. Umri wa ujana ni umri unaoweza kufanya mambo mengi yatakayokuingizia pesa kuliko umri wa uzee. Lakini ni katika umri huu ambapo unatakiwa kuwa na nidhamu juu ya pesa unayoingiza na matumizi yake.

Njia mojawapo ya kujifunza kuwa na matumizi mazuri ya fedha ni kuweka akiba. Hii ni tabia unayohitaji kuwa nayo kama kijana. Haba na haba hujaza kibaba. Pesa chache unazoziweka leo baada ya miaka si pesa chache tena.

Wazee unaowaona wamefanikiwa kiuchumi leo hii walianza kuweka akiba enzi za ujana wao, walijua kuweka akiba ni jambo zuri litakalokuja kuwasaidia siku za mbeleni.

Ujana ni muda wa kufanya mambo makubwa, ujana ndiyo umebeba asilimia kubwa ya maisha. Maisha ni muda, utumie vizuri.

“Katika ujana wako hukukusanya utapata wapi upatapo kuwa mzee?” (Yoshua Bin Sira 25:3).

Tunapotafakari kuhusu kuweka akiba, tuchukue mfano bora wa Mfalme Sulemani. Yeye alitutaka tujifunze kuweka akiba kwa kutazama wadudu wadogo kama sisimizi wanavyojua umuhimu wa kuweka akiba. Anasema: “Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima kwa maana yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa njaa, hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” (Mithali 6:6-8).

Kama sisimizi mdudu mdogo sana anaweza kukumbuka kuweka akiba, sisi binadamu wenye akili na utashi tunashindwaje? Tuamke sasa kutoka usingizini.

Suala la kuweka akiba linaanzia katika kuwa na matumizi bora ya fedha. Usipojua matumizi bora ya elfu moja hauwezi kujua matumizi bora ya elfu kumi. Usipojua matumizi bora ya elfu kumi hauwezi kuwa na matumizi bora ya milioni kumi. Hauhitaji kurudi darasani kujua kama nilichokiandika hapa ni kweli au la, ipo hivyo.

Jilipe kwanza. Unapopata kiasi fulani cha fedha, chukua asilimia fulani ya fedha hiyo na uiweke kama akiba.

Tunapopata pesa mfano mshahara au faida inayotokana na biashara tunakimbilia kulipia bili zetu badala ya kukimbilia kuweka akiba. “Kuweka akiba lazima kiwe kipaumbele si wazo tu. Jilipe kwanza,” anatukumbusha Dave Ramsey mwandishi wa vitabu na mshauri wa masuala ya kifedha.

Jenga tabia ya kuweka akiba ya pesa unayoipata kwanza ndipo matumizi yafuate. Matumizi yafuate baada ya akiba na si vinginevyo. Naunga mkono hoja ya John Poole aliyesema: “Jifunze kuweka akiba kwanza na kutumia baadaye.”

Mara nyingi ukianza kutumia pesa kabla ya kuweka akiba unakuja kushtuka imekwisha hata kile kiasi kidogo ambacho ungeweka akiba hakionekani kimepotelea wapi.

Ishi kadiri ya uwezo wako, ishi kadiri ya kipato chako. Usiishi kadiri ya unavyotaka kuonekana. Acha mambo ya kujifanya eti unakwenda na fasheni. Fasheni huwa haziishi rafiki yangu, sasa utakuwa mtu wa kufuata fasheni hadi lini?

Nakubaliana na Edward Norton aliyewahi kusema: “Tunanunua vitu tusivyohitaji kwa kutumia pesa tusiyokuwa nayo ili kuwafurahisha watu tusiowapenda.”

Achana na mambo ya kila simu toleo jipya likitoka wewe uwe unayo watu waone kwamba unakwenda na fasheni. Achana na habari za “Sitaki kuchuja.”

Acha mambo ya kukopa ukanunue nguo ulizoziona Instagram msanii fulani amevaa ili uwaonyeshe watu kuwa na wewe umo.

Achana na akili za kwenda kwenye vikoba na kukopa pesa ili uende kushona kitenge kinachobamba muda huu huko mtaani kwenu. Ishi kadiri ya uwezo wako. “Chura alipotaka kufanana na tembo alipasuka,” inatukumbusha methali ya Kiafrika.

Tengeneza bajeti. Serikali inajua umuhimu wa bajeti ndiyo maana kabla ya mwaka wa fedha inajua itahitaji kutumia fedha kiasi gani. Bajeti itakuwa ni ramani ya kukuonyesha ni wapi pesa yako inatakiwa kutumika.

“Bajeti inaiambia pesa yako wapi iende badala ya kushangaa imekwenda wapi.” (John C. Maxwell).

By Jamhuri