Uamuzi wa Busara (6)

Uamuzi wa Busara

Uamuzi wa Busara ni jina la kitabu kilichochapishwa na Ofisi ya Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU, kimebeba mambo muhimu yaliyoamuliwa kuhusu taifa kabla ya kupata uhuru.

Yapo mambo ambayo kama yasingefanyika ingekuwa vigumu kujua historia ya nchi hii ingekuwaje leo. Mathalani, kama TANU ingekataa kushiriki katika Uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958, sijui tungekuwa wapi.

Hali kadhalika kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere asingeamua kuacha kazi ya ualimu, historia ya nchi yetu huenda ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.

Kupitishwa kwa Azimio la Arusha, kuukubali Mwongozo wa Chama na mengine mengi. Hivyo kitabu hiki ni cha maana sana kwa historia ya nchi yetu kwani bila uamuzi uliomo humu kitabuni, historia yetu isingekuwa kamili. Endelea…

TANU ilikuwa imedai siku zote kwamba liwepo  Baraza la Kutunga Sheria la watu waliopigiwa kura na watu wote wazima nchini. Ni dhahiri katiba iliyotarajiwa kuwepo kwa Baraza la Kutunga Sheria la wajumbe wa mseto waliochaguliwa na watu wenye mali, wakuu wa ukoo na wenye kujua kusoma na kuandika peke yake ilikuwa kinyume cha matakwa ya TANU.

Hatua ya maendeleo iliyopatikana ni kwamba ungekuwepo uchaguzi. Lakini ulikuwa uchaguzi usioridhisha. Kwa jinsi hali hiyo ilivyokuwa, wajumbe wengi walioanza kushiriki katika mjadala huu walishauri kuwa TANU ikatae kushiriki katika uchaguzi huo.

Wengine walisema kwamba huo ulikuwa mtindo wa Mwingereza kutoa katiba zisizoridhisha na ulikuwa mtindo kwa vyama vya wananchi kukataa kushirikiana nao.

Wengine waliona kuwa kukubali kushiriki uchaguzi kwa katiba hiyo ingelikuwa ni sawa na kutangaza kuwa TANU ilikubali Serikali ya Mseto, hivyo TANU na U.T.P. visingelikuwa na tofauti na ingelivunja nguvu za moyo wa uananchi wa Kiafrika.

Wengine waliona kuwa TANU ikishiriki katika katiba hiyo itakuwa imejiuzulu katika kuwatetea Waafrika na watu hawatakuwa na imani nayo tena na ingebidi waelekee kwenye African National Congress ili wapate haki yao.

Wengine walishauri kwamba TANU isijiingize katika haramu ya uchaguzi huo na iwagomeshe Waafrika wote kupiga kura, ila kura hiyo ipigwe na Wahindi, Wazungu na wageni na vibaraka wao wachache wala si na wazalendo. Maneno haya yalikuwa ya kusisimua sana, hivyo yalivuta wajumbe wengi kwamba ni ya kimapinduzi na yasiyoleta suluhu na mkoloni.

Upande uliokuwa ukiongozwa kimawazo na Rais wa TANU, Mwalimu Julius K. Nyerere, pia uliziona hatari hizi. Lakini uliingia zaidi katika kufikiria na kupima hasara na faida ambazo zingeliweza kutokea katika kuacha kushiriki kupiga kura chini ya katiba hiyo.

Kupiga kura kungeliweza kuleta hasara kwa TANU kama walivyoogopa wapingaji, lakini kama wanachama wa TANU na wananchi wangelielezwa vizuri ulikuwepo uwezekano wananchi waweze kuelezwa vizuri kulikuwapo na uwezekano wananchi waweze kuelewa kuwa kushiriki katika kupiga kura hakukuwa na maana kwamba imekubaliana na serikali au U.T.P. kuhusu siasa yake.

Ilionekana wazi kuwa serikali ya kikoloni ingeliendesha uchaguzi huu ikiwa TANU ingelikubali kushiriki au kutoshiriki. Na kama uchaguzi ungelifanywa bila TANU kushiriki,  ingemfurahisha sana mkoloni kwani wajumbe wa U.T.P. na vibaraka wengine wangesimamishwa na kupita bila kupingwa.

Kama kungelikuwa na kupingana, kungelikuwa kupingana baina ya U.T.P. na vibaraka wao au vibaraka kwa serikali.

Baada ya uchaguzi wa namna hii, sheria na maazimio yangepitishwa katika Baraza la Kutunga Sheria kinyume cha matakwa ya wazalendo na kutangazwa kuwa ni sheria na maazimio ya waheshimiwa waliochaguliwa na watu na kwamba ni kauli ya watu.

Itakumbukwa kwamba serikali ya kikoloni iliwahi kupeleka wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria katika Baraza la Udhamini na kusema kwamba hao wajumbe walikuwa ni kauli ya watu. Madai ya TANU yangelizidi kuitwa kuwa ni maneno ya wahuni waliokuwa wamepoteza hata heshima zao kwa makabila yao ili wavuruge nchi kwa uhuni wao.

Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere alishauri. Aliwaeleza wajumbe kuwa kama TANU ingeshiriki katika uchaguzi huo, ingeliweza kuwa na wajumbe wake hasa Waafrika katika Baraza la Kutunga Sheria na kuweza kuipinga serikali si nje tu ya baraza hilo, bali hata ndani, hivyo, nguvu za TANU katika madai yake zingeongezeka.

Vilevile Mwalimu Nyerere na waliokubaliana naye walisema kwamba iliwezekana TANU, kama ingejiandaa vizuri, iweke hata Wazungu na Waasia wanaokubaliana na siasa yake.

Kwa kufanya hivyo, TANU ingeweza kuvichukua viti vingi au vyote vya Baraza la Kutunga Sheria vya wajumbe

wa kuchaguliwa na watu. Wajumbe wa mkutano walikuwa wanafahamu kwamba kupatikana viti katika baraza hilo kwa wajumbe waliochaguliwa na watu, ingawa kwa katiba ya hila na ujanja, kulitokana na madai ya TANU.

Swali lilikuwa; Je, ni nini busara kwa TANU kuvichukua au kuvikataa viti hivyo ambavyo kupatikana kwake kulikuwa hakukamilishi madai ya TANU? Hapo ndipo wajumbe wa mkutano huo wa Tabora walipoiona na kuikubali rai ya Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere, ya kusema kuwa ni busara ikiwa mtu amedai kiasi fulani kwa mdeni wake, akimlipa sehemu fulani ya kiasi anachodaiwa inafaa kipokewe kiasi hicho na palepale iendelee kudaiwa sehemu iliyobaki, kwani hata hicho kidogo ni haki yake. Hivyo hivyo unaweza kuendelea kulipwa mpaka haki yako yote uipate.

Kikao hiki kilipitisha maazimio mengi kuhusu elimu, uchaguzi katika Baraza la Kutunga Sheria, uhusiano baina ya TANU na machifu, uchumi wa Tanganyika, wajumbe wa mkutano wa kila mwaka, Halmashauri Kuu, ushuru wa pamba, kahawa, kupunguza ng’ombe na mengine.

Kuhusu uchaguzi katika Baraza la Kutunga Sheria, mkutano huu uliazimia kwamba:-

(a) Kuhusu yote ya uchaguzi, yaani mali, elimu, vyeo na kura ya watu watatu yalikuwa mabaya.

(b) TANU ishiriki katika uchaguzi ambao ulifanyika mwezi Septemba, 1958.

Matokeo ya uamuzi huu wa busara, uchaguzi uliofanyika Septemba, 1958 TANU ilipata viti vyote 15, katika hivyo 3 bila kupingwa, katika majimbo ya kwanza matano. Uchaguzi uliendelea Februari, 1959 ulifanyika katika majimbo matano yaliyobaki. TANU ilizidi kujipatia ushindi mkubwa na majimbo mengine wajumbe waliosimamishwa na TANU walipita bila kupingwa.

Kama TANU isingeamua kushiriki katika kura tatu 1958, majira yetu haya yangekuwaje sasa?

Kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere katika uwaziri mkuu

Kujiuzulu kwa waziri mkuu, wakati huo akiwa Mwalimu Julius K. Nyerere, majuma machache tu baada ya kupata

uhuru kulileta mshangao mkubwa ndani na nje ya Tanganyika na kueleweka vibaya katika nchi za nje.

Mwalimu Nyerere alikwisha kufanya mipango ya uamuzi huo siku nyingi kabla na sababu yake ikiwa ni kuwa chama kama kiungo kati ya watu na serikali mpya kwa kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa chama na kuwasaidia watu kujitambua katika taifa huru.

Tokeo kubwa la kujiuzulu huku nchini Tanganyika ilikuwa ni kuwapa watu moyo kujiamini na mabadiliko ambayo yalikuwa yakitokea. Kutokueleweka katika nchi za nje kuliondolewa baada ya kuona nchi ikiwa katika hali ya usalama chini ya Waziri Mkuu, R. M. Kawawa na ushirikiano kati ya viongozi hao wawili.