Kila mmoja analalamika

 

Sifa mpya ya Watanzania sasa ni kulalamika. Malalamiko yameshamiri katika kaya, mitaa, ofisi, sehemu zote za kazi na kila mahali. Kinachosumbua zaidi ni kuona kuwa hakuna aliye tayari kuondoa malalamiko hayo hata kama mwenye dhima hiyo ni yeye mwenyewe.

 

Ninapowasikiliza viongozi wetu wakilalamika, sishangai kwa sababu haka ni kaugonjwa ketu sote. Mkuu wa Wilaya anapolalamika, nani atakayeondoa matatizo katika wilaya yake? Mkuu wa Mkoa anapolalamika kwamba mkoani kwake kuna njaa, mkoani kwake vijana hawajitumi kujiletea maendeleo, majambazi wanaongezeka, wahamiaji haramu ni wengi; tunapomsikia kiongozi mkubwa kama huyo akilalamika, matumaini yetu tuyaelekeze kwa nani?

 

 

Waziri mwenye dhamana ya uvuvi, kwa mfano, anapolalamika kuwa uvuvi haramu unashamiri; Waziri wa Maliasili na Utalii anapolalamika kwamba majangili wanamaliza wanyamapori; Waziri wa Kilimo anaposema Taifa letu lenye mito linakabiliwa na njaa, tumwelewe vipi?

 

Wakati fulani waandishi wa habari wa Ulaya walipata kumwuliza Rais wetu kwamba Tanzania, pamoja na rasilimali zake nyingi kupindukia, kwanini watu wake ni masikini wa kutupwa? Jibu la Mheshimiwa likawa kwamba, “Hata mimi sijui!”

 

Katika kaya zetu malalamiko ni ya ugumu wa maisha. Teknolojia ya mawasiliano ya simu imetusaidia kujua ukubwa wa tatizo la malalamiko. Ujumbe mfupi wa maandishi wa kuomba msaada wa fedha, ni ishara ya wazi kwamba kuna matatizo makubwa.

 

Ndugu zangu, kwa malalamiko haya katika Taifa letu, bila shaka kuna mahali ambako tunapaswa –  kwa umoja wetu – kuketi pamoja na kuona namna ya kuyaondoa.

 

Tatizo kubwa ninaloliona hapa ni kwa wananchi kuaminishwa kwamba Serikali ndiyo mwarobaini wa kila tatizo, au bila Serikali, hakuna kinachowezekana. Wananchi wa kawaida wanaamini hivyo. Wabunge wanaamini hivyo. Bungeni malalamiko ndiyo mengi.

 

Na kwa bahati mbaya hata viongozi wetu wengi wameendelea kujitwika mzigo wa kumaliza malalamiko ya wananchi! Kiongozi gani leo anahubiri kilimo jukwani? Zaidi ya kusikia vijembe vya CCM, Chadema na CUF, kuna kiongozi anayehimiza uchapaji kazi?

 

Malalamiko yetu mengi ni ya ugumu wa maisha. Wananchi wanalalamika kwamba watoto wao hawapati elimu nzuri kwa sababu shule hazina vitabu, walimu, vyumba vya madarasa, maabara na kadhalika. Tunalalamika kwamba katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu hakuna dawa za kutosha, na pale zinapopelekwa, wauguzi, waganga na wafanyakazi wengine huziiba. Zinauzwa katika maduka, zahanati na hospitali zao.

 

Suala la watoto kukosa huduma muhimu, tujiulize ni kwa namna gani tunazingatia uzazi wa mpango? Je, kwanini tunaendelea kuamini kuwa kila mtoto anakuja na riziki yake? Katika ulimwengu wa leo wa ubepari, nani anaweza kusomesha bure watoto wa mtu mwingine? Katika hili ni wazi kwamba bila kuzingatia uzazi wa mpango, bila kuwa na watu ndani ya familia wanaohimiza uzazi wa aina hiyo, kamwe hatuwezi kujikwamua.

 

Maana haiwezekani mtu awe bingwa wa kuzaa watoto, halafu atarajie kuwa Serikali au jamii itamfanyia kazi ya kuwatunza na kuwasomesha watoto hao. Mtu masikini anapoamua kuzaa watoto 15, ajue kwamba atakuwa amekula yamini na umasikini. Kwa bahati mbaya katika kaya ya watu 15 akitokea mmoja kasoma na kupata ajira au kajiajiri, basi wengine 14 watahamia kwake!

 

Pili, pamoja na ukweli kwamba suala la uzazi wa mpango ni utashi wa mzazi/wazazi, bado ni wajibu wa Serikali katika kuhimiza jambo hilo. Zamani hizo tulipata kusikia chombo kama UMATI ambacho pamoja na uchache wetu katika Taifa, kilihimiza sana uzazi salama na wa mpango. Leo hakipo.

 

Ndugu zangu, malalamiko mengine tunapaswa kuyamaliza sisi wenyewe. Kwa mfano, kwanini tukubali katika mitaa yetu tuwe na mitaro iliyoziba na hivyo kusababisha mafuriko wakati wa mvua? Kwanini tukubali kuwa na uchafu hadi milangoni ilhali sisi wenyewe tunaweza kufanya usafi? Kwanini tukose samaki ziwani kwa sababu ya wavuvi haramu?

 

Kwanini tuendelee kulia na kuomboleza vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani na majini? Kwanini tulalamike kila leo ilhali tunao viongozi wa kuwabana ili wasimamie sheria? Kama waliopo wameshindwa kutekeleza wajibu wao, na hivyo kutusababishia misiba isiyokoma, kwanini tusiwakatae?

 

Kwanini tuendelee kulia na kusaga meno kwa adha tunazopata kutoka kwa vibaka na majambazi? Mbona watu hawa tunaishi nao katika kaya na mitaa yetu? Kama polisi hawatekelezi  wajibu wao, au vyombo vya kutoa haki havitekelezi kile kinachopaswa kutekelezwa, kwanini tuishie kunung’unikia pembeni? Je, tukae kimya ili tumalizwe? Tanzania inayosifika kwa amani kwanini tutengewe muda wa kusafiri eti sababu ya kukwepa majambazi?

 

Kama watoto wetu wanaketi chini katika vyumba vya madarasa, ilhali tukiwa tumezungukwa na misitu minene yenye miti ya kila aina inayofaa kutengenezwa madawati, kwanini tuendelee kulialia? Kwanini tusiamke wenyewe tukamaliza tatizo la madawati?

 

Kwanini tuendelee kulia Tanzania inavamiwa na wageni wengi wanaoishi nchini kinyemela, wakati sisi wenyewe miongoni mwetu tunawakaribisha? Je, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, waziri au rais anaweza kufika katika kaya zetu kuwaumbua wageni hao? Je, hatuoni kwamba wajibu huu ni wetu sisi wananchi wenyewe? Katika hali kama hii tunapaswa kuwa na majibu kwa vilio hivi, vinginevyo hata sisi tunaochukizwa na kulialia huku, tunaweza kuwa sehemu ya matatizo. Je, tufanye nini sasa?

 

Yapo mambo kadhaa tunayopaswa kuyafanya. Jambo ninaloona kuwa ni la maana sana kwetu sote kuanza nalo ni la kujitambua. Tutambue tunataka kujenga Taifa la aina gani, Taifa la walalamishi au Taifa la watu wanaotumia bongo zao kukabiliana na kero zinazowasibu? Tukishaamua kuchagua aina ya Taifa na aina ya jamii tunayotaka kuijenga, basi tutakuwa tumemaliza nusu ya tatizo.

 

Pili, lazima tuwajibike. Mabadiliko ya kweli katika maisha yetu hayawezi kuletwa na subira na ndoto za, “one day yes”. Hiyo “one day yes” itakuwa na maana kama itaendana na vitendo. Kushinda vijiweni tukicheza pool au tukiwa mabingwa wa kufuatilia tamthiliya za Kinegeria hakuwezi kubadilisha maisha yetu kutoka ya shida kuwa ya neema.

 

Tatu, vijana wanaosoma wanapaswa kusoma kwa matarajio ya kuwa vyanzo vya kuibua ajira. Wasome kwa malengo ya kuanzisha ajira, na si kutafuta kuajiriwa. Ni vigumu kwa nchi kama Tanzania ambayo ina wasomi mamilioni kwa mamilioni kuwapa ajira rasmi wasomi wote. Haiwezekani.

 

Vijana waache kuchagua kazi. Tunawaona Wachina katika maeneo kama Kariakoo wakisukuma mikokoteni. Wale si mbumbumbu. Wamo wasomi wenye shahada moja au mbili, lakini kwa kutambua umuhimu wa kuyashinda maisha, wameweka kando usomi wa nadharia. Wanafanya kwa vitendo. Kwetu hapa kijana aliyehitimu kidato cha sita hataki kushika chepe.

 

Ni msomi! Kazi ya msomi ni ya kushika kalamu! Tumepuuza kazi za kutusaidia kujiajiri, sasa tunalalamika ooh! Wachina wengi; mara oooh! Wakenya wametuvamia. Acha waje maana sisi tumeamua kuwa walalamishi na wachaguzi wa kazi.

 

Nne, yote haya yawezekana yasifanikiwe isipokuwa kwa kutilia mkazo jambo moja tu – UZALENDO. Tukiwa wazalendo tutaipenda nchi yetu, hatutakubali kuona wageni wakiichezea. Hatutakubali kuona mali za umma zikihujumiwa (mfano alama za barabarani). Hatutakuwa radhi kuwasaidia wezi wanaoitwa wawekezaji kutughilibu kwa mikataba ya kihuni. Tukiwa wazalendo hatutakubali kuwatendea binadamu wenzetu mambo mabaya.

 

Tukiwa wazalendo tutazilinda rasilimali za nchi yetu ili ziweze kutunufaisha sisi tunaoishi sasa na kwa vizazi vijavyo. Tukiwa na uzalendo, hakika tutakuwa na tamaa ya kupata maendeleo makubwa mmoja mmoja na hatimaye tuwe nchi ya kupigiwa mfano. Tukiwa wazalendo hatutakubali kuwasubiri wafadhili watuchimbie visima, wala hatutakuwa radhi kuona shule zikifungwa na watoto wetu wakikosa masomo eti kwa sababu hakuna huduma ya choo!

 

Tukijenga uzalendo tutakuwa radhi kuwaunga mkono viongozi wetu wote walioamua kujitoa uhai wao kupambana na wezi wote wa mali za umma wanaokwamisha upatikanaji wa huduma za kijamii. Tuache kulialia. Tuyakabili maisha yetu kwa njia za kiungwana. Matatizo yetu yasitugawe kwa misingi ya kidini, kikabila, kikanda, rangi wala kwa njia yoyote iwayo. Tusemane wazi na kwa haki kwa lengo moja tu la kutuwezesha kusonga mbele kimaendeleo.

 

Kila mmoja wetu akitekeleza wajibu wake mahali alipo, malalamiko mengi tunayoyasikia sasa yatatoweka. Polisi watende haki. Hakimu na majaji watekeleze wajibu wao. Wanasiasa wahimize maendeleo na umoja wa kitaifa. Hospitalini na katika ofisi zote wananchi watendewe haki. Sote tutekeleze wajibu wa kuipenda nchi yetu na kuyafanya yale tunayopaswa kuyafanya, yakiwamo ya kuwakosoa viongozi wetu. Kwa pamoja tunaweza kabisa kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kila Mtanzania kuishi kwa furaha bila manung’uniko.