Kilichowaponza mawaziri

*Baadhi waliacha kazi wakawaza urais 2025, Kalemani bei ya mafuta yamponza

*Rais Samia aanza kufumua mtandao masilahi, apanga watumishi wa wananchi

 *Shibuda: Rais amepata gari la tani 100, magari ya tani tano yampishe

*ACT Wazalendo: ‘Rais Samia Suluhu amechelewa kufanya mabadiliko’

DAR ES SALAAM

Na Waandishi Wetu

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri, ambayo kwa kiasi kikubwa yanaakisi nia yake ya dhati ya kutumikia wananchi kwa vitendo.

Mawaziri watatu waliotenguliwa; Dk. Medard Kalemani aliyekuwa Nishati, Dk. Leonard Chamuriho aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Dk. Faustine Ndugulile aliyekuwa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kila mmoja anatajwa kuwa na jambo lililoikwaza mamlaka ya uteuzi.

Dk. Kalemani anatajwa kuwa ameliingiza taifa katika gharama kubwa ya kuongezeka kwa bei za mafuta nchini baada ya kuhamisha zabuni za uagizaji wa mafuta kwa pamoja kutoka kampuni za kimataifa na kuzipa kampuni za ‘wazawa’ kwa miezi ya Julai na Agosti, hali iliyopandisha bei ya mafuta nchini kwa kiwango cha kutisha.

Inatajwa kuwa Kalemani aliagiza hata kanuni zibadilishwe ila maofisa wa Wizara ya Nishari na Madini wakiongozwa na Injinia Leonard Masanja, wakakataa amri zake.

Bei za mafuta zimeongezeka kwa kasi katika miezi ya Julai na Agosti, kama lilivyoandika Gazeti hili la JAMHURI katika matoleo matatu yaliyopita zikionyesha kuwa ongezeko hili la bei limewagharimu wananchi zaidi ya Sh bilioni 13 kwa Agosti. Fedha zinazoaminika kuwa zimewanufaisha viongozi wa kisiasa kuelekea mwaka 2025.

Dk. Chamuriho kwa upande wake, inaelezwa kuwa kuna miradi ambayo bei zake zimekwenda nje ya kiwango kilichotarajiwa, ikiwamo ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria na ingawa hakutajwa moja kwa moja inaelezwa kuwa baadhi ya zabuni zilipita bila yeye kutia neno hali iliyoleta ‘sintofahamu’ katika miradi hiyo.

Kwa upande wa Dk. Ndugulile, miamala ya simu haikumwacha salama. Vyanzo vya uhakika vinasema mamlaka za uteuzi zinaamini kuwa Dk. Ndugulile kupitia kanuni zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali, tozo za serikali zilikwenda juu mno na Serikali imepata gharama kubwa ya kurejea viwango vya miamala ya simu suala alilopaswa kulidhibiti kabla halijatokea.

“Mhe. Rais amejipanga kuhudumia wananchi. Alikereka sana kuona bei za mafuta zinapanda, miamala ya simu wananchi wanatozwa fedha nyingi kuliko uhalisia na hata baadhi ya mikataba ya ujenzi wa meli imeacha maswali mengi.

“Kwa sasa ameanza na hawa watatu, ila bado kuna mawaziri ambao inatajwa wamo kwenye mtandao wa 2025, ambao wana Mweka Hazina wao Kanda ya Ziwa, nadhani zamu hii amewaacha, ila ataendelea kuwafyatua kidogo kidogo. Hapa suala ni kutumikia wananchi bila kuwaonea, ndilo analotaka Mhe. Rais,” alisema mtoa habari wetu. 

Hadi tunakwenda mitamboni mawaziri wateule walikuwa hawajaapishwa na Rais alitarajia kuwaapisha jana.

 Wadau wanasema hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan amesikia wito wa muda mrefu wa wadau wa siasa na uchumi nchini, waliokuwa wakimuomba kupangua na kupanga upya Baraza la Mawaziri.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Chamwino usiku wa Septemba 12 mwaka huu inasema Rais ametengua uteuzi wa mawaziri watatu na kuteua mawaziri wapya wanne.

Mmoja kati ya mawaziri wapya hao ni Dk. Stergomena Tax ambaye awali alimteua kuwa Mbunge na kuapishwa jijini Dodoma Ijumaa iliyopita.

Stergomena ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiziba nafasi iliyoachwa na Elias Kwandikwa, aliyefariki dunia. Anakuwa waziri wa kwanza mwanamke kushika wadhifa huu nyeti.

Rais Samia amewarejesha kwenye Baraza la Mawaziri aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba na kumteua kuwa Waziri wa Nishati kuchukua nafasi ya Dk. Kalemani na Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi akichukua nafasi ya Dk. Leonard Chamuriho.

Pia amemteua Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuchukua nafasi ya Dk. Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Katika uteuzi mwingine, Rais amemteua Eliezer Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Profesa Adelardaus Kilangi aliyeteuliwa kuwa Balozi.

Panga pangua hiyo ya mawaziri imekuja muda mfupi baada ya wachambuzi kadhaa wa masuala ya siasa nchini kubashiri uwezekano huo, hasa baada ya ya kuteuliwa kwa mwanadiplomasia na mchumi mahiri, Dk. Stergomena kuwa Mbunge.

Mwanamama huyo aliyemaliza muda wa nafasi yake ya Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwamo kwenye baraza jipya.

Akizungumza na JAMHURI kabla ya mabadiliko haya, mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, amesema ni kawaida kwa kila rais kuwa na ‘serikali yake’.

“Iwe nzuri au mbaya, lakini ni yake. Ameiunda yeye. Si ya kurithi. Dk. Mwinyi (Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi) amefanya hivyo Zanzibar na hata Mama Samia anapaswa kufanya hivyo sasa,” anasema.

Waziri huyo wa zamani katika serikali zote mbili; ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar, anasema Rais Samia ana nafasi ya kuondoa kasoro kubwa iliyopo katika Serikali ya Muungano tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

“Hakuna waziri wa Muungano anayetoka Zanzibar, ukimuondoa Rais wa Zanzibar anayeingia Baraza la Mawaziri la Muungano kwa nafasi yake.

“Ni wazi sasa Rais Samia ana nafasi ya kuangalia na kuwaingiza wabunge kutoka Zanzibar kuwa mawaziri kamili ndani ya Muungano katika wizara kama ya Ulinzi, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje na Wizara ya Fedha,” anasema.

Hamad anasema tayari Rais ameshawasoma na kuwafahamu mawaziri aliowarithi kutoka Awamu ya Tano ambao pia alifanya nao kazi akiwa Makamu wa Rais, hivyo anaweza kuendelea nao au hata kuwabadili pia.

Maoni ya Hamad Rashid yanashabihiana na kauli aliyoitoa Rais Samia Aprili Mosi, mwaka huu aliyioyatoa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, Rais alisema: “Nitakuwa na kipimo cha mabega, nikiona mtu mabega yanapanda juu, nitajua huyo si mtumishi bali ana – enjoy juu ya kiti chake.”

Swali la kujiuliza ni je, mawaziri waliotenguliwa wamepandisha juu mabega?

Hamad Rashid anasema Mbunge yeyote wa Zanzibar ana hakai ya kuwa waziri kamili (katika wizara yoyote ya Muungano) kwa kuwa serikali ya Tanzania Bara ni Serikali ya Muungano.

Akizungumza na gazeti hili kabla ya mabadiliko, kiongozi wa Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda, anakiri kwamba uteuzi wa Dk. Stergomena kuwa mbunge ni lazima utaleta mtikisiko wa aina yake.

Anamtaja mama huyo kama mjuzi wa masuala mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, ambaye atakuwa ‘rejereo’ (reference) kwa wabunge na hata mawaziri iwapo ataingia kwenye Baraza la Mawaziri.

“Siri ya mtungi aijuaye kata. Ni wazi Mama Samia amemteua Setrgomena kwa malengo muhimu kwa taifa,” anasema.

Shibuda anaamini Rais Samia anataka kuvuna uzoefu wa mama huyo anayemtaja kama mwaminifu, hivyo kupata nyongeza ya mng’aro kwa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Tayari mawaziri wameshatambulisha uwezo wao. Wapo wenye uwezo wa tani tano na wengine tani 10. Sasa Stergomena yeye ni sawa na gari lenye uwezo wa tani 100.

“Hili gari la tani 100 linapaswa kutumika na haya mengine yalipishe na baada ya muda wakipata uzoefu wanaweza kurejeshwa.

“Kama ni kiongozi wa benchi la ufundi, huwezi kumuacha nje mama huyu kwa kuwa akiwa ndani ya 18 ni lazima atafunga bao tu,” anasema Shibuda.

Shibuda aliyewahi kuwa mbunge miaka ya nyuma na mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anasema kazi inayofanywa na Rais Samia kwa sasa ni sawa na ya dobi na ndiyo maana Dk. Stergomena anahitajika zaidi.

“Ni kama kazi ya dobi. Mama Samia anang’arisha kanzu zilizofuliwa tangu Awamu ya Kwanza mpaka ya Tano. Sasa anazitakatisha zipate mng’aro zaidi,” anasema.

Stergomena ashukuru

Wakati joto la mabadiliko ya Baraza la Mawaziri likipanda, Dk. Stergomena, kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter amemshukuru Rais kwa kumteua kuwa mbunge na anaahidi kutekeleza majukumu yake mapya kwa manufaa ya Watanzania.

“Nimeupokea kwa heshima na unyenyekevu mkubwa (uteuzi). Nitajitahidi kadiri niwezavyo kutekeleza majukumu kwa manufaa ya Watanzania ili kazi iendelee,” anasema Dk. Stergomena.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, anasema Rais Samia amechelewa kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

“Sisi ACT-Wazalendo msimamo wetu uko wazi kwamba Rais Samia aje na baraza lake jipya la mawaziri, amechelewa kufanya hivyo. Tunadhani sasa hivi ana fursa nzuri ya kuanza upya na baraza lake,” anasema Ado na kuongeza:

“Aanze mwenyewe upya, hiyo fursa hakutaka kuitumia mwanzo ila sasa hivi anayo, kwa hiyo hapo sasa tunadhani Rais hatakiwi kufanya mabadiliko madogo, Rais angeanza moja kwa moja kuunda upya baraza lake la mawaziri, kwa sababu baadhi ya mawaziri aliowarudisha japo alilazimika kufanya uchambuzi wa mtu kwa mtu tunaona kana kwamba alikuwa anataka kuonyesha tu kwamba hajaja kupindua mambo.

“Rai yetu, afumue mfumo mzima wa usimamizi katika wizara na anatakiwa kubadilisha baraza zima kwa kuwa atakuwa na machaguo yake,” anasema.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba, anasema chama hicho kwa sasa hakiwezi kutoa maoni yoyote hadi baraza jipya litakapotangazwa. Kwa upande wa CCM hawakuwa tayari kuzungumza lolote.