Miongoni mwa wajibu wa kiongozi ni kuelimisha anaowaongoza. Anapata fursa nyingi zaidi za kujielimisha na anao wajibu wa kutawanya elimu hiyo kwa wengine. Hiyo elimu inahitajika sana kwenye uanaharakati.

Naamini hivi kwa sababu lipo kundi kubwa la watu linaingizwa kwenye harakati mbalimbali bila kufahamu vyema malengo, faida, hasara, ya wanachounga mkono.

Uanaharakati una maana pana zaidi ya ule tunaouhusisha na viongozi wa vyama vya siasa. Kwa fasili rahisi kabisa mwanaharakati ni mtu anayeanzisha au kushiriki katika kampeni za kuleta mabadiliko ya kisiasa au ya kijamii.

Mwanaharakati anayefanikiwa ni mtu mbunifu ambaye yuko tayari kutumia mbinu zozote kufikia malengo. Wapo wanaharakati ambao, kwa imani ya umuhimu mkubwa wa kile wanachokusudia kufanikisha, hawaweki umuhimu mkubwa juu ya uhai wao. Wapo wengine ambao hawasumbuliwi na uwezekano wa kupoteza maisha ya wengine, hata wenzao.

Wapo wanaoendesha harakati zao kwa siri; wapo wenye kuweka mapambano yao wazi ili kushawishi watu wengine kujiunga na harakati hizo.

Mwaka 1952 Nelson Mandela alichoma moto kitambulisho kilichotolewa na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini chini ya sheria zake za kibaguzi zilizowagawa raia kwa misingi ya rangi yao ya ngozi kwa madhumuni ya kudhibiti kuhama kwao kutoka vijijini kwenda mijini. Ni sheria iliyolazimu weusi kuwa na vitambulisho wakati wote na ambayo chimbuko lake lilikuwa kuwarahisishia wakulima wazungu kupata vibarua kwenye mashamba yao.

Mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1960 yalisababishwa na wanaharakati, wakiongozwa na vyama vya siasa, kuamua kwenda kwenye kituo cha polisi bila vitambulisho na kuwataka polisi kuwafungulia mashtaka. Walivunja sheria kwa makusudi ambayo hawakukubaliana nayo na wakawa tayari kukabiliana na adhabu ya kuvunja sheria hiyo.

Ninachoshuhudia kukosekana kwenye baadhi ya harakati zetu ni ukweli; ukweli kwamba katika kuendesha harakati hujitokeza pia suala la kuvunja sheria. Kiongozi mwanaharakati hapaswi kusumbuliwa sana na suala la kuvunja sheria na athari zitakazompata, lakini anao wajibu mkubwa kuelimisha umma kwanini anaona ni muhimu kuvunja sheria, hata kama sheria yenyewe haifai.

Tofauti na hali hiyo, mara kadhaa utaona kuwa aliyevunja sheria hutetea kitendo chake cha kuvunja sheria badala ya kunyoshea mkono ubovu wa sheria aliyoivunja.

Sheria zinatungwa na binadamu na si zote zina manufaa kwa jamii au kuzingatia haki. Tume ya Nyalali, iliyoundwa mwaka 1991, chini ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ilipendekeza kufutwa au kurekebishwa kwa sheria 40.

Mwaka 2010 Tume ya Kurekebisha Sheria ilitoa taarifa kusema kuwa marekebisho makubwa yalifanywa kwenye sheria 28 kati ya hizo 40. Migongano ambayo inasikika mara kwa mara kati ya wanaharakati wa kisiasa na serikali inaashiria kuwa bado zipo sheria ambazo hazikubaliki kwa wote.

La msingi kuzingatia hapa ni kuwa waandishi wa taarifa ya Tume ya Nyalali hawakusema kuwa zile sheria 40 zinapaswa kupuuzwa au kukiukwa; walisema zinapaswa kufutwa au kurekebishwa ili kuendana na mfumo wa siasa wa vyama vingi. Na tusingetarajia washauri uvunjifu wa sheria ikinzigatiwa kuwa tume iliongozwa na Jaji Mkuu mstaafu na iliundwa na serikali.

Lakini hatutarajii pia kuwa uanaharakati na uamuzi wa mbinu gani vitumike kufikia malengo ya harakati usubiri au kupata idhini ya mamlaka yoyote. Mtu au kundi la watu ambalo linaweza kuamua kuwa miaka 28 ni muda wa kutosha kabisa kusubiri serikali kukamilisha mapendekezo ya kurekebisha au kufuta zile sheria 40, au sheria nyingine zozote zinazosemwa kuwa na hitilafu, na kuamua kuanzisha harakati zenye mbinu zinazokinzana na sheria.

Lakini wanaharakati wakubali pia kuwa uanaharakati wa kukiuka sheria ni sawa na kujiingiza kwenye tanuli. Kwa kawaida moto unaunguza.

Tunaamini kuwa mbunge aliyependekeza hivi karibuni kuwa sheria zirekebishwe kuruhusu biashara ya kuuza bangi anaendelea kushawishi jamii na wabunge wenzake mpaka tukubaliane naye na kushuhudia mabadiliko ya sheria na bangi kuuzwa kama peremende.

Lakini mbunge huyo huyo angekusudia kuwa mwanaharakati wa mfano angeanzisha mara moja shamba na mnada wa bangi. Ila tutamshangaa sana kuwa baada ya kufanya hivyo kulalamika kukamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka kwa kuvunja sheria ambayo haijabadilishwa.

Uanaharakati wa kukiuka sheria unahitaji programu ya elimu kushawishi umma kuwa sheria fulani haifai, lakini kusema pia kuwa sheria inavunjwa kwa makusudi kwa madhumuni ya kuleta mabadiliko. Uanaharakati wa aina hii unampa heshima zaidi mwanaharakati, lakini unaweka bayana kuwa tatizo ni mfumo, siyo utekelezaji wake.

Zipo taratibu za kisheria za kubadilisha sheria; taratibu ambazo zinahitaji wingi wa watoa hoja bungeni. Kwamba miaka 28 baada ya kutolewa mapendekezo ya Tume ya Nyalali bado kuna baadhi ya mapendekezo hayajakamilika ni kielelezo cha kukosekana kwa wingi huo wa wale wanaotaka hayo mabadiliko.

Wanaotafuta suluhisho kwenye katiba mpya wanalazimika kupitia kwenye mlango huo huo ambao unafungua ukumbi wa kundi la watu wenye mawazo yanayogongana na ambao wataamua muundo, vipengele, na mchakato wa kupata katiba mpya.

Sifa za kiongozi ni pamoja na kuwa mvumilivu kuwa mabadiliko, hata mabadiliko mazuri, yanahitaji maafikiano na wale ambao wapo na yanaweza kuchukua muda mrefu kufikiwa.

Maoni: barua.muhunda@gmail.com

713 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!