Madeni KipandeMamlaka ya Bandari Tanzania imegeuzwa sehemu ya ulaji wa hali ya juu. Hata hivyo, kutokana na mtandao mpana wa kuchota fedha unaoanzia wizarani hadi bandarini, yeyote anayetaka kuonesha paka yuko wapi, basi anaishia ama kufukuzwa kazi kwa njia ya vitisho, au kufanyiwa ‘kitu mbaya’.

Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, anamkingia kifua Mkurugenzi wa ICT, Phares Magesa, ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kuzamisha jahazi la bandari Tanzania.

Baada ya kuchapisha sehemu ya kwanza ya matukio yanayoendelea bandarini, wiki hii JAMHURI inakumegea sehemu tu kati ya madudu mengi yanayoendelea bandarini, ambayo kwa kila hali yanadhihirisha kuwa Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, ama hajui kitu kinachoitwa utawala wa sheria, au amedanganywa na watu wanaombeba pale Ikulu, hivyo amepoteza mwelekeo.

Ifuatayo ni sehemu ya barua ya ushauri wa kitaalamu, ambayo ilitolewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi, Mei mwaka jana, akieleza hatari inayoinyemelea bandari kutokana na mfumo wa mawasiliano (Information and Communication Technology – ICT) kuchezewa katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kupoteza mapato, imani ya wateja na kuhatarisha mizigo inayopitia bandarini.

Kwa mshango wa wengi, Dk. Jabir Bakari aliyeandika barua hii na kutoa ushauri, kwa mizengwe tu kama alivyosema Kipande kwenye kikao kati ya Wakurugenzi wa Bodi na Dk. Mwakyembe, Agosti mwaka jana huko Dodoma, kuwa “yeye ni mteule wa Rais na hivyo wakurugenzi hawambabaishi”, Kipande alifanya mbinu Dk. Jabir akafukuzwa katika Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari kwa kutoa ushauri huu. Ifuatayo ni tafsiri isiyo rasmi ya barua hiyo. Endelea…

Mwenyekiti wa Bodi,

Dar es Salaam,

Mpendwa Prof. Msambichaka,

Yah: Hali ya Sasa ya ICT na Uongozi wa TPA

Kwa barua hii napenda kukufahamisha Kamati ya ICT na Usalama ya Bodi [ya Mamlaka ya Bandari] ilichobaini juu ya utendaji wa uongozi wa TPA kwa kipindi cha miezi sita iliyopita katika eneo la kunusuru ICT na kutekeleza maagizo ya Bodi kuhusiana na ICT na Usalama [wa Bandari].

TPA inatambua umuhimu wa kuboresha huduma zinazotolewa kwa kutumia fursa ya matumizi sahihi ya ICT. Hata hivyo, mwelekeo wa miezi sita iliyopita unaonesha kuwa TPA hakujakuwapo na mabadiliko yoyote tangu uongozi mpya uchukue madaraka. Wameendeleza utamaduni ule ule kwa misingi ya fikra, mlengo na mtazamo dhidi ya Bodi.

Ripoti iliyoambatanishwa kuanzia ukurasa wa pili inatoa muhtasari wa yaliyobainishwa na Kamati ya ICT na Usalama. Hii inahitaji hatua za haraka kama ilivyopendekezwa katika sehemu ya sita (6). Kwa kila siku tunayochelewa kutatua tatizo hili, kuna upotevu mkubwa wa mapato kwa TPA ambayo sisi kama Bodi ama sasa au baadaye tutapaswa kuyatolea maelezo.

Ni matumaini yangu kuwa nimefahamisha kwa ufasaha Bodi ya Wakurugenzi juu ya suala hili na njia bora ya kulitatua.

Wako,

Jabir Kuwe Bakari, PhD.

HALI YA SASA YA ICT NA UONGOZI WA TPA

1.       Utangulizi

TPA inatambua umuhimu wa kuboresha huduma zake kwa kutumia fursa inayotolewa na matumizi ya ICT. Lengo la msingi la kutumia ICT ilikuwa ni kupunguza muda wa meli kushusha na kupakia mzigo, kurahisisha na kuharakisha uondoshaji wa mizigo, kuongeza ulinzi na usalama, hali inayopunguza gharama za uendeshaji na kuhakikisha udhibiti wa mapato.

Ripoti hii inalenga kutoa muhtasari wa yaliyobainishwa na Kamati ya ICT na Usalama ya Bodi juu ya utendaji wa Menejimenti ya TPA kwa kipindi cha miezi sita katika eneo la matumizi ya ICT na utekelezaji wa maagizo ya Bodi yanayohusiana na ICT na Usalama.

2.       Hali halisi [ya ICT bandarini]

TPA ina miradi mingi inayojitegemea kuhusiana na ICT, yenye mkatiko wa mawasiliano kati ya watumiaji na timu ya wataalamu ambayo mwisho wa siku haitoi ufumbuzi wa kuendeleza biashara ya TPA na hivyo kugeuka rasilimali zisizoongeza tija. Hali hii inatokana na kuwapo mipango shirikishi wakati wa utekelezaji wa miradi ya ICT bandarini, hivyo kushindwa kuunganisha mifumo kwa maendeleo ya biashara. Kuendelea kuingiza mifumo mipya ya ICT bila kuwapo mpango wa kuunganisha mifumo hii, ni sawa na kujenga ghorofa ndefu bila ramani, hali itakayozaa matatizo makubwa kuliko yaliyopo sasa.

Itakumbukwa kuwa eneo la TEKNOHAMA (ICT) lilikuwa moja ya maeneo yaliyotiliwa mkazo na Kamati ya Uchunguzi ya Mbakileki iliyotoa mapendekezo ya kina baada ya kushtushwa na hali halisi. Ripoti ya Mbakileki ilibainisha udhaifu wa mfumo wa ICT ndani ya TPA juu ya usimamizi na matuMIzi yake, hali iliyoilazimu Serikali kuunda Kamati ya Kuendeleza bandari ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kusaidia ufanisi kwa kutumia ICT kwa TPA.  Dondoo za ripoti ya Mbakileki zimeambatanishwa kama kielelezo 1 na 2 cha ripoti hii.

3.       Bodi kunusuru hali

Mara tu Bodi ya Wakurugenzi ilipoteuliwa, ilitambua kuwa mfumo wa ICT una uwezekano wa kubadili utendaji wa TPA haraka iwapo yangekuwapo matumizi sahihi ya teknolojia hii. Baada ya kupitia ripoti ya Kamati ya Uchunguzi iliyoteuliwa na Waziri na kupewa maelezo na uongozi wa Bandari, tuliazimia kufanya yafuatayo:-

(1)    Tuliunda Kamati ya ICT na Usalama ya Bodi ya Wakurugenzi kusaidia kushauri Bodi katika uongozi, uangalizi na usimamizi wa masuala yote ya ICT. Hii ilitokana na kwamba ICT inategemewa kwa kiwango kikubwa katika biashara ya msingi ya TPA, hivyo tatizo lolote linalohusiana na ICT huwa ni hatari. Hii ilitulazimu kuhakikisha yanakuwapo matumizi/usimamizi sahihi wa ICT.

(2)    Tuliandaa na kupitisha mkataba wa Kamati ya ICT na Usalama ya Bodi katika mkutano wa kwanza – uliofanyika Desemba 30, 2012.

(3)    Katika mkutano huo wa Desemba 30, 2012 kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Kamati iliuagiza uongozi wa Bandari kuajiri mshauri aweze kufanya uchambuzi wa haraka juu ya miundombinu ya ICT, mfumo na programu (software), ikiwamo kuangalia mfumo wa uongozi na uwezo wa watendaji katika Kurugenzi ya ICT. Ilikuwa ni matumaini ya Kamati na Bodi kwa ujumla kuwa ungetolewa ushauri wa kitaalamu juu ya hali halisi ilivyo na nini kifanyika baada ya hapo kuhusiana na matumizi ya ICT bandarini.

Tuliamini kuwa ushauri wa kitaalamu ungetuwezesha kuwa na ramani ya mwelekeo juu ya suluhisho la matatizo yanayotokana na ICT, kwa kujua mfumo upi unahitajika, aina ya Kurugenzi ya ICT kwa TPA na utaalamu unahoitajika. Matokeo ya uchambuzi yangesaidia kuunganisha mifumo kuendana na biashara ya TPA. Tungeweza pia kuunganisha juhudi zinazofanyika sasa kupata suluhisho la haraka na mifumo iliyojitenga. Kamati ya Uongozi iliahidi ingemaliza kazi hii ndani ya siku 60, lakini Bodi ikaamua kuwapa siku 90 kuanzia Januari 1, 2013. Hata hivyo, tulibaini kuwa uongozi ulihitaji msaada katika kuandaa hadidu za rejea, na tuliwasaidia kufanya hivyo.

(4)    Wakati wa kikao cha Kamati ya Mipango na Uwekezaji (Januari 16, 2013) tulifahamishwa uwepo wa miradi 21 ya ICT inayopendekezwa. Baada ya mjadala ilibainika kuwa miradi hii kama iliyobainishwa na Kamati ya Mbakileki inafanana. Kwa mfano, wakati mradi wa Epicar (ERP) uliogharimu Sh milioni 694 unakaribia kukamilika, kuna mradi mpya unaopendekezwa wa ERP. Mpango huu haukukubalika na pengine hautakaa ukubalike wakati wa uongozi wetu. Kamati iliamua kusitisha miradi yote mipya, isipokuwa mitatu ambayo ni Electronic Single Window, Integrated Security System na MIS (kwa sharti la kufuata taratibu za ununuzi), hadi uchambuzi wa haraka wa mfumo wa ICT bandarini utakapofanyika na kila kitu kufahamika. Umuhimu wa uchambuzi wa mfumo wa ICT haraka ulisisitizwa katika mkutano.

(5)    Bodi ya Wakurugenzi ilichagua uchambuzi wa mfumo wa ICT bandarini kama kipaumbele namba moja kwa miezi sita ya kwanza

(6)    Kwa nyongeza, Bodi iliagiza Menejimenti kutumia mifumo ya ICT iliyopo kutatua matatizo yanayoendelea bandarini. Hasa hasa kufufua kamera za CCTV ambazo miundombinu ipo na imeunganishwa na kutumia mifumo iliyopo kuondoa matatizo ya watumiaji.

(7)    Kwa asili yake, Bodi iliagiza Menejimenti kufanya uchambuzi wa haraka wa ndani juu ya usalama, zimamoto na ulinzi kwa nia ya kupata sura ya hali halisi na ramani ya kutoka hapo. Menejimenti ilipangiwa kukamilisha kazi hii ifikapo Juni s2013.

4.       Nini kinaendelea

(i)                  Kushindwa kwa Idara ya ICT kutumia mifumo ya msingi ya ICT kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayokabili TPA. Hali ya Idara ni kwamba hakuna kazi ya kitaalamu inayoweza kufanyika kwa weledi. Utendaji umeelekea kama hali ilivyokuwa miaka 6 iliyopita. Rejea Ripoti ya Mbakileki kiambatanisho III.

(ii)                Kukataa kufanya uchambuzi wa haraka: Agizo hili halikupewa umuhimu pamoja na kukumbushwa mara kwa mara. Idara ya ICT ilitoa ushauri mbovu kwa ICT na kutafuta mshauri wa kufanya kazi hii asiye na uwezo. Kulikuwapo na ucheleweshwaji wa makusudi kuanza kwa mradi huu na mara ya mwisho tuliambiwa kuwa zabuni za kumpata mshauri zingefunguliwa Aprili 18 [2013], zikafanyiwa uchambuzi kwa siku nne na baada ya hapo menejimenti ingekuwa imekwishaamua mradi huo uanze. Kwa mshangao, katika mkutano wa pili wa ICT na Usalama, tulijulishwa kuwa mchakato wa zabuni unapaswa kuanza upya kwani wazabuni waliomba kwa bei kubwa kuliko kiasi kilichotengwa kwa kazi hiyo. Sasa wanataka kutangaza zabuni ya kimataifa ambayo itachukuwa walau nusu mwaka mchakato kukamilika. Huu ni uthibitisho mwingine kuwa ushauri wa Bodi haukupewa umuhimu.

(iii)               Kuidanganya Bodi kwa nyakati tofauti:

a)      Menejimenti iliidanganya Bodi kuwa mfumo wa malipo unaotumiwa na TPA ni IFMS na si ERP, hivyo Mamlaka inapaswa kununua ERP.

b)      Kwamba IFMS ilikuwa imekamilika kwa asilimia 95 na hivyo mfumo huu ungekabidhiwa kwa Bandari Januari 15, 2013, lakini sehemu nyingine ikionesha kuwa mfumo haukuwa umekamilika bali ungekamilika Machi 15, 2013. Tulipotafuta [Bodi] mshauri alibainisha kuwa mfumo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 99.9 na baada ya hapo Idara ya ICT na Menejimenti ikabadili kauli na kudai kuwa mfumo umekamilika kwa asilimia 60.5, huku idara inayotumia mfumo huo kwa malipo ikidai umekamilika kwa asilimia 40 tu. Wakati mshauri akiwasilisha alichobaini, iligundulika kuwa mfumo wa malipo ulikuwa umekamilika bali tatizo lilikuwa ni network na watumiaji kutoufahamu. Siku hiyo, Idara ya ICT ilitoa tarehe mpya ya kukabidhiwa kwa mfumo huo, ikidai kuwa ungekabidhiwa Mei 7, 2013 lakini hadi leo haifahamiki nini kinaendelea.

c)       Mshauri alionesha kuwa mifumo mitatu ya Harbor View Plus, BillSys, na Cargo System haina tatizo lolote. Lakini ukizungumza na watumiaji katika idara wana malalamiko lukuki juu ya mifumo hii. Mshauri, Stan De Smet, alisema wakati wa uwasilishaji kuwa mbali na mifumo hiyo mitatu ambayo yote ni mipya, TPA ilikuwa imenunua mfumo wa nne ujulikanao kama Yard View, na akaongeza:-

i)                    Kwamba Yard View haijawahi kutumika tangu kununuliwa kwake

ii)                   Baadhi ya mifumo inayodaiwa kufanya kazi vyema, haifanyi vyema na ilifungwa siku hiyo hiyo ya uwasilishaji. Ilionekana baadhi ya mifumo ilikuwa mipya kabisa iliyofungwa siku hiyo.

iii)                 Kwa mujibu wa Mshauri, mifumo hiyo yote minne iliyonunuliwa imetumiwa kwa asilimia 50 tu.

iv)                 Sura tuliyopata kutoka kwa watumiaji ni kuwa mfumo ulikuwa unatumiwa kwa asilimia 40 tu na baadhi ya taarifa zikihitajika hazipatikani.

v)                  Mfumo hauna kazi na watumiaji wamelalamika kwa muda mrefu

vi)                 Kulikuwapo dalili za ufungaji mbaya wa mfumo

vii)               Mifumo mitatu ya awali inapaswa kufanya kazi pamoja na kuunganishwa na mfumo wa fedha (kama sehemu ya IFMS), kwa ajili ya TPA kujihakikishia mapato yote yanapitia kwenye mfumo. Kwa sasa mizigo yote ya wateja wakubwa inafanyiwa malipo bila kupitishwa kwenye mfumo na kupunguza ufanisi, hali inayoleta wasiwasi wa uvujaji wa mapato. Kushindwa kwa menejimenti kuunganisha mifumo hii kumeendeleza uvujaji wa mapato na kutoa fursa kwa watu binafsi kuhujumu Bandari.

(iv)              Kushindwa kutekeleza maagizo ya Bodi kama inavyoelezwa:

a)      Bodi iliiagiza menejimenti mara tatu kutumia mfumo wa ICT uliopo kutanzua matatizo yanayoikabili TPA. Hasa hasa kufufua kamera za CCTV ambapo miundombinu ipo. Hakuna taarifa yoyote juu ya hili hadi leo.

b)      Kutoa taarifa kwa njia ya mtandao kila wiki juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri. Hakuna ripoti iliyopokewa kutoka Kurugenzi ya ICT.

c)       Maelekezo ya Bodi kwa menejimenti kutotembelea Rwanda, badala yake wafanye ziara kwenye nchi zenye bandari zinazotumia mfumo wa Electronic Single Windo System, kutokana na ukweli kuwa hakuna bandari nchini Rwanda. Ingeeleweka kwa kutembelea nchi yenye bandari inayotumia mfumo huo. Mkurugenzi wa ICT na watendaji wengine waliendelea na mpango wao, wakatembelea Rwanda licha ya kuonesha dalili kuwa walielewa kilichoagizwa na Kamati ya Bodi wakati wa mkutano. Kwa makusudi waliamua kwenda kinyume na maelekezo ya Bodi.

d)      Bodi iliagiza kuwa miradi yote ya ICT iongozwe na idara zinazohusika na matumizi ya mradi husika kwa ajili ya kuwawezesha kumiliki mfumo husika na Idara ya ICT ibaki na kazi ya uratibu na kutoa msaada. Hadi leo, miradi yote inasimamiwa na mtu mmoja, Kaimu Mkurugenzi wa ICT na kukataa maelekezo ya Bodi [Kwa sasa Phares Magesa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa ICT ni Mkurugenzi kamili tangu Januari 2014].

(v)        Kubishana na Wakurugenzi wa Bodi. Mara kadhaa na hasa Kaimu Mkurugenzi wa ICT amekuwa na mabishano na Bodi ya Wakurugenzi wakati wa mikutano ya Kamati na kusema wazi kuwa maelekezo ya Kamati ni nadharia tu na hayatekelezeki, na kwamba mifumo iliyopo inafanya kazi sawia.

5.       Hitimisho

(i)       Hali ilivyo sasa haiwezi, na haipaswa kuvumiliwa na Bodi yetu ya Wakurugenzi iliyopewa nguvu na kuaminiwa na Waziri wa Uchukuzi, akiamini kuwa tungeweza kuibadili TPA kuwa na ufanisi wa jumla na kutumia teknolojia ya kisasa katika utendaji wake.

(ii)       Bodi kushindwa kuchukua hatua sasa kutatia shaka uwezo na usafi wa Bodi mbele ya macho ya waziri na wadau wengine.

6.       Mapendekezo

Ukipitia taarifa zilizoambatanishwa (Appendix I &II) inaonekana TPA wamerejea katika utendaji wa mazoea uliokuwapo miaka 6 iliyopita, ulioifikisha Bandari hapa ilipo. Ni utendaji usio na chembe ya weledi ambao hatupaswi kuupa nafasi ikiwa tunataka kuibadili TPA hata katika kipindi cha mpito wakati tukisubiri uongozi mpya kuwekwa madarakani.

Kamati ya ICT na Usalama inapendekeza yafuatayo:-

(i)                  Kaimu Mkurugenzi wa ICT kuhamishwa mara moja kwenda idara nyingine

(ii)                Pili kupata CV za watendaji wote ndani ya Idara ya ICT isipokuwa wale tu waliotajwa katika Kamati ya Uchunguzi na wale wanaotuhumiwa na menejimenti kuwa wanahujumu mfumo kwa mujibu wa kielelezo Na. III.

(iii)               Tuteue mmoja atakayekaimu na kurejesha moyo wa kufanya kazi pamoja hadi hapo atakapopatikana Mkurugenzi wa ICT.

(iv)              Andaa mfungo (retreat) wa siku tatu na watendaji wa ICT kwa ajili ya kujadili njia bora ya kufanya kazi

(v)                Menejimenti itoe kipaumbele cha haraka katika kufanya uchambuzi wa mifumo ya ICT inayotumiwa na Bandari na utaalamu wa ICT unaohitajika. Hii itahusisha kufanya mabadiliko makubwa katika Idara ya ICT ambapo wafanyakazi wapya wenye weledi na mifumo ya kutosha wataajiriwa kuziba nafasi zilizo wazi.

(vi)              Bodi iwe inapatiwa taarifa ya maendeleo kila wiki kwa njia ya mtandao na taarifa hii itolewe na Kaimu Mkurugenzi wa ICT.

Viambatanisho vinavyotokana na Kamati ya Mbakileki:

Appendix I: Page Reference Page 151:

“ix) Kwamba kwa kukosa umakini katika kusimamia Menejimenti, Bodi [iliyovunjwa awali] imeshindwa kuweka mipango imara ya ulinzi, hasa katika Bandari ya Dar es Salaam ambako Menejimenti imekuwa ikisuasua kwa kuweka mifumo hafifu ya TEHAMA na kamera za CCTV na kupitiliza lengo la kumaliza zoezi hili mwaka 2008. Bodi imekuwa inatoa maagizo lakini hayatiliwi maanani na Menejimenti kwa kujua hakuna litalotokea.”

Kwamba uzembe wa Bodi katika kusimamia Menejimenti uliilazimu Serikali kuingilia kati na kuanzisha Kamati ya Kuboresha Utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam (Port Improvement Committee -PIC) chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi. Pamoja na Kamati hii kukosa nguvu ya kisheria ilisaidia kutatua baadhi ya mambo.

(xi) Kwamba umefika wakati kwa Serikali kuchukua hatua si tu kwa kubadili Bodi kama ilivyofanya mwaka 2006 bali pia Menejimenti, kwa sababu bila kufanya hivyo Bodi itakayoteuliwa itaathiriwa na mazoea ya Menejimenti iliyopo.

(xii) Kwamba Bodi ya Wakurugenzi haina msukumo wa kutenda wajibu wake ipasavyo, kwa kuhofia madhara ya ulegevu”

Appendix II: Page Reference 178197

3.9.1 Matumizi ya TEHAMA Katika Mamlaka ya Bandari (TPA)… Pia Kamati ilisoma na kuchambua nyaraka zifuatazo ili kukamilisha kazi yake: TPA ICT Policy, Taarifa ya Zabuni ya eSWS Vol 1 and Vol 2; Taarifa ya KPMG kwenye zabuni ya eSWS; Nyaraka za zabuni ya “Installation and commissioning of Integrated Payroll, Human Resources, Accounting and Stores System”,

Mtizamo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania ni kuongoza katika biashara za Bandari katika Bara la Afrika, maeneo ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika. Ili kufanikisha lengo na mtizamo huo ni muhimu Mamlaka ya Bandari Tanzania ikawekeza kwenye maendeleo ya teknolojia ambayo ndiyo msukumo mkubwa na maendeleo ya Bandari Tanzania.

Bandari jirani, kama vile Mombasa zimewekeza katika TEHAMA ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama kutumia teknolojia inahuishwa. TPA imekuwa ikitumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) au “Information and Communication Technology (ICT) kwa muda mrefu kwani maeneo mengi yameonekana kuwapo kwa kompyuta ingawaje hazikuingizwa kwenye mfumo/mtandao halisi wa TEHAMA (Network), ili ziweze kutoa manufaa zaidi ya kiteknolojia ya TEHAMA katika utendaji kazi.

Mamlaka ya Bandari ilianza kutumia programu aina ya “Common Business Oriented Language (COBOL)” kuanzia wakati ilipoanzishwa. Programu hii imekuwa ikitumika katika Idara ya Fedha kwa ajili ya shughuli za ukusanyaji wa mapato na kwa ajili ya kusimamia matumizi ya Mamlaka. Pia programu hii imetumika katika ulipaji mishahara. Baada ya hapo TPA walinunua mifumo mipya ya uendeshaji wa shughuli za kupakua na kupakia shehena bandarini n.k. ambayo ni pamoja na Harbour View, General Cargo, Microsoft Office Suite, Mozilla Firefox, Adobe Acrobat; (Microsoft Visco, Kapasky Anti Virus, Rexio Easy CD ) na Advance Cargo tracking system.

3.9.1.1 Historia ya Port Community System (Mfumo wa Bandari wa TEHAMA)

Port Community Systems “(PCS) ni mfumo wa Bandari unaohakikisha taarifa za utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa watu na vitu vinavyopatikana kwa wadau wote wanaotumia Mamlaka ya Bandari. Lengo kuu likiwa ni kuongeza tija na ufanisi katika upakuaji na upakiaji shehena.

(A) 1988 UNCTAD I (United Nations Conference on Trade and Development)

Mradi huu ulifadhiliwa na UNCTAD ukiwa na nia ya kuanzisha mfumo wa “Electronic Data Inter Change” (EDI) uitwao EDIFACT (Electronic Data Interchange for Commerce and Transfer). Mradi huu ulisuasua sana. Ugumu wa kuuendeleza ulijitokeza.

(B) 1997 UNCTAD II

UNCTAD wakaanza na mradi mwingine kwa ajili ya Bandari. Ukaja mradi mpya ulioanza Septemba 1997. Mradi uliitwa Advanced Cargo Tracking System (ACCESS). Mradi huu wa ACCESS ulikuwa na : (a) Harbour Master, (b) Takwimu (Statistics), (c) Manifest na (d) Gate pass.

Mfumo huu wa TEHAMA ulitumiwa kwa muda hata kuoneshwa kwenye Maonesho ya Sabasaba. Baadaye mradi huu ulikwama lakini Kamati haikupewa sababu za msingi.

(C) 2003 PHAROS

Mradi huu ambao asili yake ni Ubelgiji, ulianza vizuri kwa kuweka mifumo midogo kama; (i) Harbour view- Mfumo wa Kuingiza na Kutoa meli bandarini. Mfumo huu umeonesha tatizo la mawasiliano kati ya Harbour Master’s Office na Revenue Manager’s Office; na kumekuwa na uhaba wa mafunzo kwa wafanyakazi wa idara hizi. Aidha, meli inapobadilisha mwelekeo, mfumo huu unasumbua kuingiza taarifa zake.

(ii) Cargo System– Mfumo huu kasi yake ya kutoa maelekezo “instructions” kwa uunganishaji na utoaji wa ankara ni ndogo. Hii mara ingine husabishwa na wafanyakazi kukosa ujuzi na mtandao kasi yake ni ndogo. Mfumo huu wakati mwingine unashindwa kuusoma mfumo wa ankara. Cargo system imeshindwa kupokea manifesti ya mzigo kimtandao (electronically).

(iii) Billing System (Marine Billing, Cargo Billing container, Cargo Billing Motor Vehicle, Cargo Billing Loose cargo, Cargo Billing Liquid bulk, Cargo Billing ICD) Mfumo huu unasumbua katika utoaji wa taarifa za wiki na za mwezi. Hii inasababishwa zaidi na mtandao. Tovuti ya TPA inasumbua kuingiza taarifa, hivyo, huwalazimu wateja kwenda kwenye ofisi za Bandari. Yapo matatizo ya kuingiza taarifa za shehena kubwa aina ya vimiminika (liquid bulk cargo). Mfumo huu haujakamilika katika utoaji taarifa. Mfano taarifa zingine inabidi zitolewe na mfumo mwingine kama vile “Microsoft Excel”

(iv) Yard View -Huu ni mfumo wa ukodishaji shehena baada ya kupakuliwa kutoka kwenye meli na kabla ya kupakiwa kwa ile shehena inayosafirishwa nje ya bandari. Mfumo huu unaendelea hadi sasa huku ukizidi kuboreshwa. Maboresho yake yamechukua muda mrefu hasa maeneo ambayo yangesaidia kuonesha mwelekeo wa mapato.

Uchambuzi

i. Kuna mtizamo hasi miongoni mwa wafanyakazi na hata baadhi ya viongozi kuhusu matumizi ya mifumo ya TEHAMA. Uongozi kutoonesha nia ya kuwezesha mifumo hii kufanya kazi. Uzoefu wa Mkurugenzi wa ICT katika mambo ya meli na Bandari ni mdogo;

ii. Miradi karibu yote ya TEHAMA imeonekana kuwa ni miradi ya makao makuu, upande wa Bandari kuhusishwa kiasi kidogo sana. Ni maofisa wa ngazi ya chini ndiyo walikuwa wamepewa jukumu hilo;

iii. Kuchelewa kwa uwekaji wa miundombinu hasa upande wa mtandao wa kuunganisha mifumo hii ya ufanisi. Mfumo kutokidhi baadhi ya mahitaji ya Mamlaka katika maeneo mbali mbali, mfano, Mfumo wa Billing System kutoa invoice tu bila risiti. (Automatic issuance of receipt) Billing System na Cargo System kutokufungamanishwa (integrated) hivyo kuhitaji ‟human intervention” yaani kuingiza namba ya risiti katika Cargo System “manually” hivyo kuwa rahisi kwa mtu kuingiza risiti hata ya uongo. Idara ya TEHAMA imejitahidi kujaribu kuanzisha mfumo mbadala ili kutatua tatizo hilo.

iv. Mifumo yote kutoweza kuweka rekodi ya mtu aliyeingiza data mara ya kwanza kama data hiyo itabadilishwa. Kutomwezesha Wakala wa Meli kutoa ‟Delivery Order” kielektroniki kwa TPA hivyo kulazimika kuendelea kutumia mfumo wa karatasi kutoka kwa wenye meli. Poor control system ambapo inakuwa rahisi mtu kuingilia access ya mtu mwingine. Idara ya TEHAMA iko katika mchakato wa kuangalia hili linaondolewa.

(D) 2009 Electronic-Single Window System (eSWS)

Huu ni mradi mpya wa “Port Community” ambao Benki ya Dunia ilijitokeza kufadhili. Mradi huu uliokuwa na nia ya kuhakikisha shughuli zote za Bandari zinafanyika katika dirisha moja, yaani watumiaji wote wa Bandari hawana haja ya kufika Bandari ili kutoa au kutuma mzigo. Kwa ujumla ni matumizi ya TEHAMA katika kurahisisha utoaji wa shehena.

Nia ya mradi huu ni kuhakikisha wadau wote wa Bandari wanabadilishana taarifa na kurahisisha upakiaji na upakuaji wa shehena kwa kutumia teknohama au Tehama. Hivyo basi TPA iliamua kununua mfumo laini (software) unaoitwa eSWS. Mzabuni alitakiwa alete mfumo laini wenye viatilishi vifuatavyo;

i. Kiungo kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ili kufanikisha biashara ya ndani na ya kimataifa.

ii. Kufanikisha utaratibu wa utoaji wa vibali kwa maagenti wa shehena yote inayotumia njia ya majini na angani.

iii. Sanduku la mawasiliano kwa mfumo wa kielektroni ambalo litatunza barua pepe za mawasiliano kati ya watumiaji na jumuiya ya wafanyabiashara.

iv. Utaratibu wa malipo na gharama kwenda kwa mteja

v. Uwepo uwezo wa kufikia taarifa zote za biashara; Pia mzabuni alitakiwa atoe mafunzo na huduma ya usimamizi wa mfumo huu.

Mradi huu mpaka leo haujaanza kutokana na sababu zifuatazo;

(i) Benki ya Dunia – utaratibu

(ii) Kamati ya e-SWS

(iii) Kukubalika miongoni mwa wafanyakazi

(iv) Mchakato wa Manunuzi

(i) Benki ya Dunia

Kutokana na maelezo kutoka idara ya TEHAMA, taratibu za Benki ya Dunia zilichukua muda mrefu kiasi cha kuwafanya TPA kuamua kutenga fedha kutoka kwenye bajeti yao wenyewe.

Sehemu hii ya vitambatanisho ni Ripoti ya Kamati ya Mbakileki, ambayo ilipowasilishwa, Waziri Mwakyembe alimteua Kipande kukaimu nafasi hiyo na kumuondoa  Ephraim Mgawe, lakini kutokana na alichokiandika Dk. Jabir, hakuna kinachofanywa na Kipande zaidi ya kupiga majungu.

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa ICT, Magesa, aliyekuwa analalamikiwa na kutakiwa kuhamishwa, sasa amethibitishwa kazini ndiye Mkurugenzi wa ICT. La kushangaza, Dk. Jabir baada ya kutoa mapendekezo yaliyotangulia hapo juu, Kipande na Magesa wakampiga zengwe na Waziri Mwakyembe akamuondoa Dk. Jabir na wakurugenzi wengine watano kwenye Bodi.

Baada ya kuwaondoa wataalamu hawa ambapo Dk. Jabir ni mtaalamu wa masuala ya ICT, Dk. Mwakyembe aliteua wajumbe wengine wa Bodi akiwamo mfanyakazi wa Bandari ambaye ni mfagiaji.

2928 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!