Na Christopher Gamaina

Wiki iliyopita nchi yetu, Tanzania, iliweka historia ya kipekee. Rais Jakaya Kikwete kwa mara ya kwanza alihutubia wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ikiwa ni siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha Rasimu ya Katiba mpya.

Katika hotuba za viongozi hao, suala la muundo wa Muungano ndilo lililoamsha hisia na kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa Watanzania. Hii ni kutokana na umuhimu wa pekee wa suala hilo katika mustakabali wa nchi yetu.

Jaji Warioba anasema asilimia 61 ya wananchi 27,000 waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara walipendekeza Serikali Tatu, huku asilimia 60 ya wananchi 19,000 kwa upande wa Zanzibar wakipendekeza Muungano wa Mkataba.

Kimsingi msisitizo wa Jaji Warioba ni kwamba maoni ya wananchi wengi yanahitaji muundo wa Serikali Tatu, badala ya mbili zilizopo kwa sasa.

Sambamba na hilo, Jaji Warioba anajitahidi kupinga hoja ya baadhi ya wananchi wanaohofia kuwapo kwa mzigo mkubwa wa kugharimia uendeshaji wa Serikali Tatu.

Anafafanua kwamba gharama zitakazoongezeka ni za kawaida ambazo haziepukiki pale watu wanapodhamiria kuleta ufanisi wa mfumo wa utawala.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba anatoa mfano wa utaratibu wa Serikali wa kuongeza wizara, mikoa, wilaya na taasisi mbalimbali ili kuleta ufanisi wa kiutawala hapa nchini.

“Hivyo, suala la kuongezeka kwa matumizi ni suala la lazima katika kuongeza ufanisi, hasa katika enzi hizi za ushiriki zaidi wa wananchi. Vilevile, ni suala la kawaida kuendana na kukua kwa majukumu, dhamana na ukubwa wa nchi,” anasema Jaji Warioba katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasisitiza kwamba suala la matumizi katika mfumo wa serikali zetu ni la utamaduni kuliko muundo wa Muungano. Wakati huo huo, anasema Tume imependekeza mfumo utakaodhibiti na kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma chini ya Serikali Tatu.

Binafsi ninamuunga mkono Jaji Warioba katika kipengele hicho. Kwamba tunapoamua kuongeza ufanisi katika utawala hatupaswi kuogopa na kukwepa gharama zinazohitajika.

Kama suala la kuogopa ongezeko la gharama lingezingatiwa basi Serikali isingeona haja ya kuongeza idadi ya wizara, mikoa, wilaya na taasisi za kiutawala.

Kwa upande wake, Rais Kikwete pamoja na kuonekana kupiga teke Rasimu ya Katiba kupitia hotuba yake kwa Bunge Maalum la Katiba, anasema wajumbe wa bunge hilo wana mamlaka ya kuifanyia Rasimu ya Katiba mabadiliko wanayoamini yatakubalika kwa Watanzania wengi.

Rais Kikwete amewahimiza wajumbe wa bunge hilo kuhakikisha wanakuwa makini katika kuisoma rasimu hiyo, ili waweze kutoa uamuzi sahihi unaobeba maslahi ya Taifa. Kwamba uamuzi sahihi utawezesha upatikanaji wa Katiba bora isiyonung’unikiwa na wananchi.

Hata hivyo, hotuba hiyo ya Rais Jakaya Kikwete imeonekana kujikita zaidi kwenye msimamo wa chama chake (Chama Cha Mapinduzi-CCM) ambacho kinapendekeza muundo wa Serikali Mbili.

Anafafanua kwamba rasimu hiyo inatambua mchango Serikali Mbili, kama vile kupunguza gharama za uendeshaji wa Muungano, kujenga uchumi na ushirikiano baina ya pande hizo mbili, kuimarisha umoja na amani.

Anahofia kwamba Serikali Tatu zitaleta mwanya wa kuibebesha Serikali ya Muungano majukumu makubwa ya majeshi ya ulinzi na usalama, huku ikiwa haina chanzo cha mapato ya kujiendesha.

Katika kusisitiza zaidi, Rais Kikwete amesema muundo wa Serikali Tatu hautapunguza matatizo bali utayaongeza. Kwamba matatizo yaliyopo yanaweza kutatuliwa ndani ya muundo wa Serikali Mbili zilizopo.

“Tujipe matumaini kwamba kero zilizopo tunaweza kuzimaliza. Serikali ya Muungano [ya sasa] haina kigugumizi cha kupunguza [matatizo] yanayowezekana kupunguzwa. Tunaweza kutatua hayo bila kuhitaji Serikali Tatu.

“Lakini hayo ni maoni yangu, bunge hili ndilo lenye uamuzi, ila mtakapojadili hili, hizo hoja mzifikirie,” amesisitiza kiongozi huyo wa nchi.

Hapo ndipo pia ninapomuunga mkono Rais Kikwete. Kwamba hayo anayoyahimiza ni mawazo na maoni yake, lakini wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ndiyo wenye uamuzi wa mwisho juu ya aina ya Katiba inayowafaa Watanzania.

Kadhalika, Rais Kikwete amewaasa wajumbe wa bunge hilo kuwa mahodari wa kushawishi badala kulazimisha Katiba mpya.

Kwa mtazamo wangu, Rais Kikwete na Jaji Warioba kila mmoja ameonesha umahiri wake katika kushawishi mambo mazuri juu ya Rasimu ya Katiba mpya. Sasa kazi kubwa imebaki kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Wasituangushe.

By Jamhuri