Siku ya Jumatatu, saa 6:00 mchana nimeikamilisha safari yangu ya kwenda nyumbani kwa Dk. Abdala Nyangaliyo, anayeishi Mbagala Kibondemaji A, jijini Dar es Salaam

Dk. Nyangaliyo ni maarufu na hata cheo cha udaktari amepewa tu kwa heshima, lakini siyo kwamba alikisomea.

Umaarufu wa Dk. Nyangaliyo unatokana na ulemavu alionao wa kutoona (kipofu), lakini anafanya kazi ya kushona nguo na kufundisha wengine na zaidi alishapata fursa ya kushona shati la Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Safari yangu kwenda nyumbani kwa Dk. Nyangaliyo ilianzia katika ofisi za gazeti la JAMHURI zilizopo Mtaa wa Samora, kwa usafiri wa jamii yaani daladala.

Baada ya kufika Mbagala Zakhem, kutokana na umaarufu wa mwenyeji wangu sikupata tabu kufika nyumbani kwake kwani nilipouliza ilikuwa rahisi kupelekwa.

Nilimuuliza mwendesha pikipiki kama anafahamu nyumbani kwa Dk. Nyangaliyo, akanieleza kuwa anamfahamu ikiwa ni pamoja na kunifahamisha kwamba mbali na kazi yake ya kushona nguo, lakini pia ni kiongozi wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mbagala jambo ambalo lilinivutia zaidi.

Kutoka kituo cha bodaboda hadi nyumbani kwa Dk. Nyangaliyo ni umbali unaokuchukua takribani dakika 5. Baada ya kufika tu na kubisha hodi, mara nikamuona Dk. Nyangaliyo akitoka kuja kunipokea bila kuwa na fimbo maalum ya kutembelea (white cane) kama ilivyo kwa wasioona wengi, huku akiwa amevaa shati la kitenge lenye rangi ya pinki mchanganyiko na madoa ya rangi nyeusi na usoni amevaa miwani myeusi.

Kwa ucheshi mkubwa ananifuata mahali nilipokuwa nimeketi mithili ya mtu anayeniona na kunipa mkono na mimi nampa mkono wangu tunatembea wote tumeshikana mikono kuelekea ndani kwenye ofisi yake ya ufundi.

Wakati tukitembea kuelekea kwenye ofisi yake ya ushonaji nampa pole kwa tatizo lake hilo naye ananijibu kwa kujiamini sana. “Tunapaswa kumshuru Mungu kwa kila jambo, kwani ubaya ama uzuri wa jambo husika anaujua Mungu mwenyewe aliyetuumba.”

Dk. Nyangaliyo ambaye amezaliwa miaka 58 iliyopita, mkoani Pwani, Wilaya ya Rufiji, licha ya kuwa kipofu, ni fundi mzuri anayeshona nguo mbalimbali na pia mkufunzi anayefundisha vipofu na wasio na upofu namna ya kushona nguo ili kuwawezesha kupata kipato.

 

Chanzo cha upofu wake

Akisimulia alivyopata tatizo la upofu wa macho amesema ilikuwa mwezi Mei mwaka 1989 alianza kuumwa kichwa, kiasi cha kushindwa kulala wala kupata usingizi.

Anasema kabla hajakumbana na tatizo la upofu alikuwa na uwezo mzuri wa kuona tena vizuri kama watu wengine.

“Kilianza kichwa kuuma kikapelekea usingizi kukosa kabisa, tatizo hili lilinipitisha kwenye hospitali tofauti tofauti bila mafanikio hadi nilivyokwenda Shirika la Lions Club ambalo ofisi zake zipo mtaa wa Mzizima Dar es Salaam hapo ndipo waligundua tatizo langu kuwa ni shinikizo la damu kwenye macho,” anasema Dk. Nyangaliyo.

Anasema tatizo lilipobainika, alikwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akiwa katika hospitali hiyo Daktari Saguti aliyemfanyia uchunguzi chini ya usimamizi wa Profesa Sangawe walimpima na kumshauri afanyiwe upasuaji wa macho ili apate usingizi.

“Madaktari waliniambia upasuaji nitakaofanyiwa utasababisha kupata uoni hafifu, lakini baadaye nitapofuka macho jumla,” anasema Dk. Nyangalio.

Anasema Juni 7, 1989 alifanyiwa upasuaji wa macho na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kipindi cha miezi mitatu.

Wakati amelazwa alifanikiwa kuonana na Mzungu kutoka Urusi aliyemtaja kwa jina moja la Alexander ambaye alikuwa mfanyakazi katika hospitali hiyo.

Anaongeza kuwa alijega urafiki na mzungu huyo (Alexander) ambaye alianza kumpa mbinu za kushona nguo akiwa kipofu ili kazi hiyo imsaidie kupata fedha za kujikimu na kuendesha maisha.

“Huyo Mzungu alikuwa anapenda sana kujifunza kuzungumza lugha ya Kiswahili, kila alipokuja katika wodi nilipolazwa alipenda sana kuniongelesha Kiswahili… ‘Nyangaliyo hujambo?’ Alikuwa akinisalimia hivyo, tulikuwa marafiki kipindi chote nilicholazwa hapo hospitalini,” anasema Dk. Nyangaliyo.

Siku moja akaniuliza Nyangaliyo umeshapofuka macho baada ya hapa unatarajia kufanya kazi gani? Nilimjibu nitajua nikipona vizuri… naye akaniambia nataka nikupe zawadi ambayo itakusaidia maisha yako yote… nikamuuliza zawadi gani? Akaniambia nataka nikufundishe kushona nguo. Nilishangaa sana, akaniuliza kama niko tayari, nikamjibu niko tayari.

Anasema baada ya kukubali, Alexander (Mzungu) ambaye alikuwa na cherehani ndogo ya umeme ndani kwake kila jioni alinifuata na kunichukua kwenda kwake na kuanza kunifundisha kushona.

 

Jinsi alivyofundishwa kushona

Anasema alianza kufundishwa namna ya kutumia vidole kutambua vitu vingi kwa kukariri maumbile ya vitu hivyo.

“Baadaye akanifundisha namna ya kuimiliki akili yangu ili iweze kutambua vitu ninavyovigusa kwa vidole.

“Pia alinifundisha namna ya kuishirikisha akili yangu na kile nilichokishikilia mkononi.

“Vile vile alinifundisha jinsi ya kuchukua vipimo vya mwili wa mtu kwa kumshika mkono.

JAMHURI lilitaka kujua anaijuaje saizi anayovaa mtu kwa kumshika mkono, alijibu; “Hiyo ni siri yangu binafsi na ndiyo imesababisha jopo la wasomi kutoka vyuo vikuu Norway, Kenya, Uganda na Tanzania waagize mimi nipewe cheti cha heshima na kuitwa Daktari Abdala Nyangaliyo mwaka jana,” anasema.

“Jinsi ninavyopitisha uzi kwenye sindano ni kwamba kuna kifaa mimi nakiita kitunga uzi hiki ndicho kinaniongoza kupitisha uzi kwenye sindano.”

 

Anawezaje kutumia futi kamba

Anasema; “Futi nimeiwekea alama kuanzia namba ya kwanza hadi namba ya mwisho, hizi alama nikizigusa ndo nagundua namba ya kipimo ninachokihitaji na kitambaa nikisha kipanga juu ya meza sehemu ninayohitaji kukata kwa mkasi kulingana na vipimo vyangu huwa nachomeka vipini,” anasema.

Kwa upande wake Masha Ali ambaye ni mwanafunzi anayefundishwa ufundi wa kushona nguo na Dk. Nyangalio anasema ni fundi mzuri kama walivyo mafundi wengine.

Amesema matendo yote yanayofanywa na mafundi wengine wakati wanashona hata yeye huyafanya tena kwa ufasaha, ndo maana niliamua kuja hapa kujifunza namna ya kushona.

Alipoulizwa kwanini amechagua kufundishwa na kipofu ushonaji wa nguo alijibu; “Huyu akikufundisha huwezi kusahau kwasababu yeye anafundisha kwa vitendo. Vilevile wapo watu wengi ambao wameshafundishwa na mzee huyu sio mimi tu,” Masha anasema.

 

Dk Nyangalio alivyoanza rasmi

Anasema baada ya kupewa mafunzo na yule Mzungu hakuitilia maanani kazi ya ushonaji hadi ilipofika mwaka 1994 alipoianza rasmi kazi ya ushonaji nguo. Anaseleza alianza kwa kushona vigauni na vikaptura vya watoto wadogo.

Baadaye alikata shauri na kuanza kushona nguo za watu wakubwa kwani alikuwa ameshapata uzoefu wa kushona nguo vizuri.

Anakutana na changamoto nyingi zikiwemo za kutoletewa vitambaa vya kushona na watu, masoko ya kuuza nguo anazoshona kuwa hafifu na watu wengine wakileta vitambaa washonewe nguo baadhi husema ameshona vibaya.

“Kuna mama mmoja aliniletea kitambaa nimshonee gauni. Nikampima vipimo vyangu nikamwambia siku fulani njoo uchukue gauni lako. Alivyo kuja nikampa gauni lake baadaye akalirudisha lile gauni kwamba nimelishona vibaya, nikamwambia sawa leta nitairekebisha, nikaichukua, nikaitunza wala sikuigusa nikaiacha vile vile baada ya siku tatu nikamwambia njoo uchukue nguo yako, alivyoifuata tu akaanza kusifia akisema ‘umeona sasa ulivyoishona vizuri’,” Dk. Nyangaliyo anasema.

Akieleza faida ambazo amepata kutokana na kazi yake ya ushonaji anasema imemkutanisha na watu wengi wakiwemo viongozi waliowahi kuiongoza Tanzania kama Rais wa Awamu ya Pili, Allhaj Ali Hassani Mwinyi na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, na kuongeza: “Kazi ya ushonaji haijampa manufaa makubwa sana kifedha.”

Anasema mwaka 2014 alimshonea Rais Kikwete shati la kitenge na baada ya kutoka madarakani kiongozi huyo alimtembelea kwenye banda la maonyesho ya wakulima Saba Saba jijini Dar es Salaam 2016 akiwa amevaa shati hiyo aliolomshonea.

“Aliponitembelea mwaka jana Rais Kikwete aliniletea na zawadi ya cherehani kipya ambacho hadi sasa naendelea kukitumia, namshukru sana,” anasema Dk. Nyangaliyo.

Hata hivyo, anajivunia kazi hii kumpa fursa ya kumshonea shati Rais Kikwete analosema alilivaa likamtosha kwa kiwango ambacho hakuamini iwapo fundi ni kipofu.

JAMHURI lilipomuuliza anawito gani kwa uongozi uliopo madarakani kwa sasa, anasema Rais John Magufuli kama kauli mbiu yake inavyosema “Hapa Kazi Tu” hata yeye ameamua kuitekeleza kwa vitendo kauli mbiu hiyo kwa kuanzisha kiwanda darasa kinachotoa mafunzo ya ushonaji nguo kwa vipofu.

Anasema kuanzia October 19 mwaka jana hadi June 4 mwaka huu, chini ya ufadhili wa Tantrade ametoa mafunzo kwa wanafunzi vipofu saba na wamehitimu kilichobaki ni kuwapatia vyeti.

Vilevile, anaiomba serikali impatie msaada wa gari la kutembelea, vyerehani na miundombinu mingine ili atimize azima yake ya kutoa mafunzo kwa vipofu nchi nzima.

Anamalizia kwa kutuma salamu zake kwa Rais John Magufuli katika kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” na anamkaribisha kwake Mbagala Kibondemaji A akamshonee suti.

Na ALEX KAZENGA

3144 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!