Jopo la madaktari kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Dk. Stanford Mwakatage, wamefanya kampeni maalumu ya kutoa matibabu na upasuaji kwa gharama nafuu kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Dk. Mwakatage anasema kampeni hiyo ililenga pia kuwahamasisha watu kujiunga na mfumo wa bima ya afya ili waweze kupata matibabu endelevu wao na familia zao.

Akifafanua, anasema gharama za kufanyiwa upasuaji huo ni Sh 35,000 huku gharama za bima ya afya zikiwa ni Sh 30,000 kwa mwaka.

“Hivyo, wale waliofika tuliwashauri kama watahitaji badala ya kulipia upasuaji, walipe kwa ajili ya bima ya afya na bima zao zitakapokuwa tayari watakuja kufanya upasuaji kwa kutumia bima hizo. “Faida hapa ni kuwa kama ukilipa Sh 35,000 utafanyiwa upasuaji mara moja na fedha zitakuwa zimekwisha, lakini ukilipia bima ya afya ya Sh 30,000 utafanyiwa upasuaji, lakini bado utaendelea kutibiwa mwaka mzima, wewe na familia yako,” anafafanua.

Dk. Mwakatage anaongeza kuwa lengo la kampeni hiyo lilikuwa ni kuwahudumia wananchi wapatao 300, lakini kutokana na uhamasishaji kuwa mzuri watu takriban 500 walijitokeza.

Anasema wameamua kuipeleka kampeni hiyo mbali na hospitali ya wilaya ili kuwahamasisha na kuwafikia watu wengi zaidi ambao wako mbali na kituo hicho cha kutolea huduma za afya.

“Zamani tulikuwa tunafanya kampeni hii mjini Kisarawe, lakini tukagundua kuwa kuna wananchi wengi pembezoni ambao wanahitaji huduma hii lakini hawana uwezo wa kufika Kisarawe, tumeamua kuwafuata waliko,” anasema.

Anasema kama hamasa, wale waliokuwa wanakuja wakiwa na bima ya afya walitibiwa bure ili watu wengine nao waone umuhimu wa kuwa na bima hiyo.

Ingawa hakuwa na takwimu kamili kuhusu watu waliojiunga na bima ya afya kupitia mfumo huo lakini wengi wameonekana kuhamasika na kujiunga.

By Jamhuri