TASAC yawakumbuka walemavu Nduguni

Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) wametoa vifaa vyenye jumla ya Sh milioni 10 kwa kikundi cha watu wenye ulemavu cha Tanzanite Disabled Group Art cha Kata ya Nduguni, mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa TASAC, Emmanuel Ndomba, anasema watu wenye ulemavu waliomo kwenye jamii wana haki ya kusaidiwa kama wengine pale wanapokuwa na mahitaji.

Ndomba anasema wametoa msaada huo wa baiskeli kwa watu wenye ulemavu ili iwe chachu ya kujiwezesha kwenda katika shughuli za kutafuta kipato.

Anasema njia waliyotumia watu hao kuomba msaada wakiwa kwenye kikundi ni nzuri na inapaswa kuigwa na walemavu wengine ili iwe rahisi kwao kupata misaada.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Alex Mwisongo, anasema kata yake ina jumla ya watu wenye ulemavu 50, ambao wanahitaji misaada ya zana zitakazowawezesha kufanya shughui mbalimbali za kujiingizia kipato.

Mwisongo anadai kuwa mahitaji ya baiskeli za walemavu ni makubwa katika kata hiyo kwa sababu wengi wa walemavu ni wale wa miguu, ambao wanahitaji baiskeli kwa ajili ya kuwawezesha kwenda maeneo mbalimbali.

“Hawa walemavu wa miguu ukiwapatia baiskeli inakuwa rahisi kwao kwenda maeneo mbalimbali ambako wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji mali,” anasema.

Mwakilishi wa Diwani wa kata hiyo, Acleus Mshumbusi, anawaomba wahisani kuwa pamoja na vifaa lakini pia wawapatie walemavu hao mitaji itakayowawezesha kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.

Mshumbusi anasema ni vema jamii ikatambua kwamba walemavu mahitaji yao si vifaa peke yake, kwa sababu wanawea kuwa na vifaa hivyo lakini wakakosa shughuli za kufanya.

“Hivyo, ili kuhakikisha kuwa wanavitumia vifaa hivi vema, itafaa iwapo watapatiwa na mitaji ili waweze kuanzisha shughuli za ujasiriamali,” anasema.

Anaitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa walemavu, kwani nao ni binadamu kama wengine. Anahimiza taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi ili wasiwafungie watoto wenye ulemavu ndani.