Home Kitaifa Polisi haijachukua hatua kifo cha kemikali

Polisi haijachukua hatua kifo cha kemikali

by Jamhuri

Polisi wilayani Kisarawe, mkoani Pwani hawajachukua hatua yoyote kuhusiana na kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa baada ya kunywa pombe iliyotokana na kemikali.

Siku kadhaa zilizopita JAMHURI liliripoti tukio la Mwalimu Ladislaus Mkama, mtaalamu wa kemia katika Shule ya Sekondari Chole, wilayani Kisarawe kudaiwa kutengeneza kinywaji chenye kemikali ya sumu na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia.

Mwalimu huyo alikuwa anachanganya kemikali alizokuwa anaziiba kutoka katika maabara ya shule.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana, ameliambia gazeti hili kuwa bado ofisi yake haijapokea taarifa hizo za mwalimu aliyetengeneza kinywaji kwa kutumia kemikali kilichosababisha mtu mmoja kufariki dunia katika kijiji hicho.

Shana anasema atafuatilia kwa karibu suala hilo ili kujua kisa kizima.

Hata hivyo, wakati RPC Shana akisema hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Zuberi Marinda, anasema kuwa alishawahi kupigiwa simu na kamanda huyo na kumhoji kidogo na kumweleza kwamba RSO (Ofisa Usalama wa Mkoa) atampigia simu kuongea naye kwa undani.

Anadai kuwa baada ya muda kweli alipigiwa simu na RSO na kuzungumza naye kidogo, kisha akamwahidi atamtuma mtu kwenda kwenye eneo la tukio muda wowote na kumuomba ampatie ushirikiano wa kutosha.

Lakini zaidi ya wiki mbili sasa hakuna askari wa upelelezi aliyetembelea eneo la tukio huku malalamiko kutoka kwa waathirika yakizidi.

Mtendaji wa kijiji

Nasoro Mmanga, ambaye ni Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, anasema kuwa mpaka sasa mwalimu huyo bado hajarejea kazini na hana taarifa zozote zaidi ya malalamiko kutoka kwa baba wa marehemu.

“Mimi kama mtendaji nimemshauri aende kumuona Polisi John ili ikiwezekana aweze kufungua kesi ya madai dhidi ya madhara aliyokutwa nayo mtoto wake,” anasema Mmanga.

Baba wa marehemu

Baba wa marehemu, Ali Pakacha, anasema kuwa mpaka sasa haelewi kinachofanyika, hivyo amepanga kwenda kumuona Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo ili afahamishwe kinachoendelea.

Ofisa Elimu wa Wilaya

Ofisa Elimu wa Wilaya, Patrick Gwivana, anasema kuwa mwalimu huyo ambaye naye aliathiriwa na kemikali alizokuwa anachanganya anaendelea vizuri.

“Nimeongea na ndugu zake wanasema anaendelea vizuri. Inaonekana kemikali zilimsababishia madhara kooni, ni kama amechubuka kooni na bado hawezi kuongea… lakini anaendelea vizuri tunamshukuru Mungu,” anasema Gwavana.

Kaimu Mganga Mkuu

Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Greyson Mlamba, anasema taarifa za daktari aliyemfanyia uchunguzi marehemu Shaibu Pakacha wa Chole ambaye aliletwa na polisi wameshaziwasilisha kwa jeshi hilo.

Anasema alichofanya daktari huyo ni kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kwa kuchukua maini na damu na kuvipima ili kujua dawa au sumu iliyotumika kumdhuru.

Dk. Mlamba anasema kuwa daktari alipomaliza kazi hiyo aliwakabidhi polisi ripoti na tayari imekwisha kupelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi zaidi.

Anadai kuwa hawahusiki na taratibu za Ofisi ya Mkemia Mkuu, ingawa inaweza kuchukua hadi miezi miwili kupata majibu ya mwisho.

You may also like