DAR ES SALAAM

NA ALEX KAZENGA


Uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliokamilika wiki iliyopita umekipatia chama hicho safu ya uongozi katika ngazi zote huku Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, akiapa kuendeleza mapambano ya kisiasa katika mfumo mpya ili kukabiliana na changamoto ambazo chama kimezipitia katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Miaka minne iliyopita imekuwa migumu kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na mizengwe kilichopitia, ikiambatana na dhoruba zilizokielekea moja kwa moja na baadhi ya viongozi wake wakuu.
Ni miaka minne ambayo imeshuhudia viongozi kadhaa wa Chadema wakipotea na wengine kuuawa huku vifo vyao vikihusishwa na siasa.
Ni miaka minne ambayo chama hicho kimepoteza wabunge kutokana na wimbi la viongozi na wanasiasa wa upinzani kuhamia chama tawala kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuridhishwa na jinsi Rais John Magufuli anavyoendesha nchi.
Ni miaka minne ambayo imeshuhudia karibu viongozi wote wa juu wa Chadema na wale wenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama hicho wakiandamwa na kesi, huku baadhi yao akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, wakikaa mahabusu kwa kipindi kirefu.
Hadi sasa, Tundu Lissu, aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa chama hicho, analazimika kuishi nje ya nchi kwa kile anachoeleza kuwa ni kuhofia uhai wake baada ya kunusurika kifo alipomiminiwa risasi zaidi ya 16 jijini Dodoma, zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Akiuhutubia mkutano uliomchagua kuwa mwenyekiti kwa kipindi kingine cha miaka mitano wiki iliyopita, Mbowe anasema kama waliokuwa wanafanya njama hizo walidhamiria kukidhoofisha na kukiua chama hicho cha upinzani nchini, basi wamekosea, kwani badala yake kimeimarika zaidi.
Baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema waliozungumza na JAMHURI wamesisitiza kuwa licha ya kubanwa kufanya siasa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, chama chao kimeimarika zaidi.
Kile kinachotajwa kuwa sehemu ya hujuma kwa Chadema kiliendelea hadi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam pale viongozi wa serikali walipoamuru chama hicho kishushe bendera zote zilizokuwa zimetundikwa katika eneo la mkutano kama sehemu ya shamrashamra za mkutano huo.
Kwa kuonyesha dhamira ya agizo hilo, bendera hizo zilishushwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, anasema hujuma wanazofanyiwa na viongozi wa serikali haziangamizi chama chao, bali zinakiimarisha, huku akiwataka wanachama kuwa imara, hasa katika wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ubungo kupitia Chadema, Boniface Jacob, anasema vitendo vya hujuma vinavyofanyika dhidi ya chama chao vinatokana na wivu wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho amedai kuwa kimekosa uvumilivu wa kisiasa.
“Kwa kawaida mtu usiyempenda akifanikiwa lazima roho itakuuma. Hawa CCM walidhani kuzuia mikutano ya hadhara ndiyo wametumaliza, cha kushangaza wanaona sisi tunazidi kuimarika,” anasema Jacob.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, anasema CCM ina hali mbaya kisiasa, kwani kitendo cha kuanza kuhangaika kushusha bendera za chama hicho katika eneo walipofanyia mkutano mkuu ni ushahidi tosha kwamba Chadema inazidi kuimarika.
“Wameanza kuhangaika na vitambaa vyenye alama za chama chetu, hizo ni bendera tu! Wamechelewa, Chadema halisi imo mioyoni mwa watu,” anasema Mbilinyi.
Mbilinyi ni mmoja wa viongozi wa Chadema ambaye aliwahi kushitakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela. Alikaa gerezani kwa zaidi ya miezi mitatu kabla ya kuachiwa kwa msamaha wa rais.
Baadaye alishinda rufaa ambayo alikuwa ameikata kupinga hukumu na adhabu aliyopewa.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Chadema aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan, anasema mpango wa Chadema ni msingi ambao unawasumbua sana viongozi na wanachama wa CCM, na umepata nguvu kutokana na hujuma zinazofanywa dhidi ya chama hicho.
“Huu mpango wa Chadema kimsingi kama CCM wasingefanya hujuma katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulikuwa unakwenda kukiaibisha chama tawala kwa kiwango kikubwa. CCM walishituka kwamba wanakwenda kushindwa mchana kweupe, ikabidi waandae hujuma za wazi wazi na ninawaambia chama chetu kiko makini na kitazidi kuwa makini pamoja na kupitia vikwazo vyote unavyosikia tukifanyiwa,” anasema Hassan.
Hassan amewataka watawala waache mpango wa kukihujumu chama hicho, kwa sababu sera zake zinawavutia wananchi wengi, kwani zinalenga maendeleo yao binafsi kuliko maendeleo ya vitu ambayo serikali imeyakazania.
“Watu hawali barabara na ndege ambazo serikali inajisifu kutekeleza kwa kiwango kikubwa, watu wanataka mambo yanayogusa maisha yao moja kwa moja,” anasema Hassan.
Alipotakiwa afafanue mikakati ambayo chama hicho kitaitekeleza baada ya kuteuliwa katika nafasi ya ukatibu mkuu, John Mnyika, aliomba kutozungumza kwa sasa.
“Nimejizuia kuzungumzia masuala haya hadi pale nitakapoingia ofisini rasmi. Naomba kwa sasa uniache, nitawaatarifu pale nitakapokuwa tayari kuzungumza,” aliliambia JAMHURI.
Lakini katika hotuba yake muda mfupi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Mnyika alisema yuko tayari kuweka ubunge wake rehani ili afanye kazi ya kuhakikisha anaiondoa serikali ya CCM madarakani.
Katika hotuba hiyo fupi, Mnyika anasema Chadema inapitia kwenye kipindi kigumu cha kushambuliwa na serikali iliyoko madarakani, lakini wao kama viongozi wamejitahidi kukilinda chama chao, kazi ambayo anasema wameifanya kwa gharama kubwa.
 
Dhoruba kwa Chadema

Vyama vya upinzani vimepitia katika dhoruba kubwa za kisiasa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, likiwemo katazo la mikutano ya hadhara lililotolewa na Rais John Magufuli miezi kadhaa tangu aingie madarakani.
Rais Magufuli alitangaza kufuta mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge na madiwani ambao wanaruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo yao ya kuchaguliwa.
Pamoja na katazo hilo, Chadema na vyama vingine vya siasa vimeshindwa hata kufanya mikutano ya ndani ambayo imekuwa ikizuiliwa ama na Jeshi la Polisi au wakuu wa wilaya.
Misukosuko hiyo ya kisiasa ilishuhudiwa ikikisambaratisha Chama cha Wananchi (CUF) baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Seif Sharrif Hamad, kukihama chama hicho na kundi kubwa la viongozi, wanachama na wafuasi na kujiunga na ACT-Wazalendo.
Viongozi kadhaa wa Chadema, akiwemo Mbowe, hivi sasa wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyotokana na matukio ya Uchaguzi Mdogo katika Jimbo la Kinondoni ambao ulisababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji, Akwilina Akwiline, aliyepigwa risasi akiwa kwenye daladala.
Mbali ya hujuma zilizoelekezwa kwa chama moja kwa moja, Mbowe naye alishuhudia biashara zake zilizopo Dar es Salaam na Moshi zikiingia matatani kiasi cha kuvunjwa kwa jengo lililokuwa na klabu yake ya Bilicanas baada ya kuondolewa kwa nguvu kwenye jengo kwa madai ya kushindwa kulipa kodi.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani na kutangaza kusitisha mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, vimekuwa na wakati mgumu wa kuendesha shughuli za kisiasa.
Zuio hilo la mikutano ya hadhara limeathiri shughuli nyingi za kisiasa za vyama hasa Chadema ambacho kimekuwa kinalalamika kuhujumiwa waziwazi.
Viongozi wa chama hicho wanauchukulia mpango wa watawala kukidhibiti chama hicho kuwa unalenga kukwamisha juhudi zake za kujiimarisha, kwani kina mwelekeo wa kukamata dola.
Mbali ya tukio la kushushwa kwa bendera za Chadema katika eneo la Mlimani City, itakumbukwa kuwa Novemba 1, mwaka huu bendera za Chadema na CCM katika Jimbo la Moshi ziliondolewa katika barabara na mitaa mbalimbali katika Manispaa ya Moshi.
Mpango wa kushusha bendera hizo uliratibiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa hoja kwamba zimewekwa kiholela na kusababisha muonekano wa uchafu katika mji wa Moshi.
Pia, utetezi wa mkurugenzi huyo ni kwamba ziliwekwa kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019, hivyo ziliwekwa kama mabango na vipeperushi, kinyume cha sheria ndogo zinazosimamia masuala ya miji.
Katika sura ya mwonekano wa hujuma kwa chama hicho, kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengay ole Sabaya, ameingilia masuala ya ndani ya Chadema na kuzuia mikutano ya chama hicho kufanyika katika jimbo hilo linaloongozwa na Mbunge Freeman Mbowe.
Mkuu huyo wa wilaya amewahi kuwaamuru askari wa Jeshi la Polisi kuingia kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho uliokuwa ukiendeshwa na Freeman Mbowe.
Pia, amewahi kutamka hadharani kwamba amemnyanganya ofisi mbunge wa jimbo hilo wakati mbunge huyo alikuwa haitumii kutokana na ufinyu wa nafasi.
Julai 29, mwaka huu Sabaya alitoa amri kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya Mbowe katika Jimbo la Hai kwa hoja kwamba yeye (Sabaya) ana ziara katika jimbo hilo, hivyo mikutano hiyo ingeweza kuingiliana.
Mbali na Sabaya, DC wa Bariadi, mkoani Shinyanga, Festo Kiswaga, naye Oktoba mwaka jana alizuia mikutano ya ndani ya chama hicho kwa hoja kwamba ingeweza kuingiliana na ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Desemba 29, 2018 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji na viongozi wengine saba wa chama hicho walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro wakati wakiendelea na kikao cha ndani katika maeneo ya Bomangombe kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Hivi majuzi, Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ruangwa alikamatwa kwa tuhuma za kupeperusha bendera ya chama hicho cha upinzani katika barabara ambayo Rais Magufuli alipangiwa kupita akiwa ziarani wilayani humo.
Mapema mwezi huu, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Halfani Haule, aliamuru bendera za Chadema na vyama vingine vya upinzani kushushwa wilayani humo na kuziacha za CCM kwa kuwa ndicho chama tawala.
 
Tamati…… 

1944 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!